2023
Safari Yangu kwenye njia ya agano
Septemba 2023


Wasifu wa Muumini: Dumazedier Kabasele

Jina langu ni Dumazedier Kabasele, na ninaishi Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Nimeoa mke mzuri aitwaye Choudelle Kazadi, na sisi ni wazazi wa watoto 2 wa kiume waitwao Bryan na Khalis Kabasele.

Nilipata kuwa mmisionari niliyetumikia katika Misheni ya lugha ya Kifaransa ya Kongo Lubumbashi. Kitabu cha mwongozo cha mmisionari cha Hubiri Injili Yangu kilinipa msukumo nijifunze Kingereza kwa sababu ingekuwa ni baraka kwangu, kwa familia yangu na kwa kanisa. Sikujua ni kiasi gani baraka hii ingeleta matokea katika maisha yangu. Uamuzi wangu wa kujifunza Kingereza wakati wa misheni yangu uliungwa mkono na Philip na Joy McMullin ambao ni rais wangu wa misheni na mke wake. Nilijifunza Kingereza kwa saa mbili kila siku na hii ilinisaidia niendelee kupata maarifa zaidi.

Nilipata shahada yangu ya kwanza (ya udaktari) katika madawa katika nchi yangu ya kuzaliwa ya Kongo. Nikivutiwa na kujifunza zaidi kuhusu ubongo, nilifanya masomo zaidi ya chuo huko Bangalore, India ili kupanua maarifa yangu kupitia ufadhili uliokuwa unahusu mambo ya neurolojia na elekrofiziologia.

Mara ya kwanza nilisikia kuhusu Programu ya BYU PathwayConnect nikiwa India. Waumini wengi wa Kanisa walikuwa wakijiunga na programu hii. Nilishangaa kwamba Kanisa lilitoa programu hii katika nchi zigine lakini siyo nchini kwangu Kongo. Lakini sikujiunga na Pathway kwa muda huo kutokana na masomo yangu magumu, lakini sala yangu ilikuwa kwamba siku moja programu ingetolewa katika nchi yangu na kwamba ningejiunga na kujifunza zaidi kuihusu.

Niliporejea DRC mnamo 2018, sala yangu ilikuwa kwamba Pathway ingeruhusiwa katika nchi yangu na kwamba ningekuwa na fursa ya kujifunza zaidi kuihusu. Mnamo 2019 programu ilikuwa imeruhusiwa, na nilikuwa miongoni mwa kizazi cha kwanza cha wanafunzi wa Kinshasa kuandikishwa. Mwanzo ulikuwa mgumu kwangu, kwa sababu nilikuwa nafanya kazi na kuishi eneo tofauti na mahali pa kukutania kwa ajili ya programu. Lakini niliungwa mkono na familia yangu na rafiki yangu Patrick Kalambayi. Sote tulitembea umbali mrefu kuhudhuria vikao na kurejea nyumbani usiku sana. Wakati mwingine hatukuwa na umeme. Tulitafuta sehemu zenye umeme ili kuchaji kompyuta zetu.

Wakati mmoja, mamlaka za serikali zilizuia intaneti kutokana na sababu za kisiasa. Mimi pamoja na rafiki yangu tulikwenda kwenye ofisi za Umoja wa Mataifa (UN) za eneo letu kwa ajili ya msaada, tukiwaambia tunapaswa kutuma kazi zetu za shule na tulihitaji intaneti ili kufanya mazoezi yetu ya nyumbani. Nina ushuhuda kwamba Baba wa Mbinguni huwaweka watu katika safari yetu ili kutusaidia katika nyakati za dhiki, kama uhaba wa umeme na intaneti.

Baada ya kumaliza PathwayConnect, Niliamua kujiandikisha katika programu ya Afya ya Umma katika Chuo Kikuu cha BYU-Idaho. Nilihitimu ngazi ya cheti katika kipengele cha Kupanga na kutekeleza Afya ya Umma, Tathmini ya Njia ya Afya na Epidemiolojia. Nimejifunza kuisaidia dunia katika kuzuia ugonjwa na kuandaa mpango wa afya wa magonjwa yanayosambaa kwa kasi. Nilikuwa na furaha kuisaidia nchi yangu wakati wa mlipuko wa Uviko 19 huko Kinshasa. Watu walikuwa wa kupendeza. Nilijifunza ujuzi zaidi kuhusu jinsi ya kuzuia ugonjwa huu katika eneo langu.

Programu ya BYU PathwayConnect ilinisaida nielewe kwamba tunapaswa kuwa waaminifu na kukuza ujuzi wetu ili kujenga ufalme wa Mwokozi wetu hapa duniani. Programu hii iliongeza ufahamu wangu wa Mwokozi na ilinihamasisha kupata ujuzi zaidi na kuwa mwaminifu zaidi.

Badala ya kubakia katika magumu na kuhangaika, nimejifunza kumtumainia Bwana na kusonga kielimu katika vyuo maarufu ulimwenguni. Leo ninayo furaha kusema nimejifunza shahada tatu za chuo kikuu: moja kutoka nchini kwangu, moja kutoka India na moja kutoka Marekani. Na kama matokeo yake, nimeongeza kipato changu, imani yangu katika Yesu Kristo na ujuzi wangu upande wa afya ya umma.

Ujuzi niliojifunza wakati wa safari yangu umenisaidia kuanzisha taasisi ya afya isiyo ya kiserikali inayojishughulisha na elimu ya afya ya akili huko DRC. Uzoefu wangu wa hivi karibuni, nilipokuwa nikiomba kazi mpya kwenye shirika la Center for Disease Control kama mtaalamu wa afya ya umma huko DRC, timu ya maafisa rasilimali watu walishangaa kwamba nina shahada ya Marekani na ninaishi Kongo na ilikuwa rahisi kwao kuhakiki hili kutokana na cheti changu cha astashahada.

Mchakato wa kuajiri ulikuwa wa kuvutia na kila hatua niliyopita, nilijifunza kuwa tayari kwa sababu ya programu ya BYU PathwayConnect, kuandaa wasifu wangu binafsi (CV) na barua, nikifurahia usaili na kuwaonyesha watu sifa zangu za msingi. Nina shukrani kwa Baba yangu wa Mbinguni kwa fursa aliyonipa ya kujiunga na timu hiyo ya Center for Disease Control huko DRC ili kuzuia, kutambua na kudhibiti magonjwa katika nchi yangu.

Kama Mwafrika, tumebarikiwa kuwa na shahada ya Amerika, tukitumikia katika jamii zetu na kuliimarisha Kanisa katika eneo letu. BYU PathwayConnect imebariki maisha yangu, familia yangu na nchi yangu katika wakati huu muhimu. Programu ilinisaidia nielewe kanuni ya kufanya kazi kwa bidii kimya kimya na kuruhusu mafanikio yako yawe kelele zako.

Bila kujali kiwango ulichopo katika maisha na kama una shahada au huna, tafadhali jiunge na programu na fanyia kazi kwa bidii, Bwana anajua jitihada zako na atakusaidia kupata shahada mpya na ujuzi zaidi na ulimwengu utakulipa kulingana na elimu na ujuzi wako.