Maandiko Matakatifu
Mafundisho na Maagano 10


Sehemu ya 10

Ufunuo uliotolewa kwa Joseph Smith Nabii, huko Harmony, Pennsylvania, yawezekana kuwa mnamo Aprili 1829, ingawa sehemu yawezekana kuwa zilipokelewa mapema zaidi katika kiangazi cha mwaka 1828. Ambamo ndani yake Bwana anamjulisha Joseph juu ya mabadiliko yaliyofanywa na watu waovu katika kurasa 116 za muswada kutoka kwenye tafsiri ya kitabu cha Lehi, katika kitabu cha Mormoni. Kurasa hizi za muswada ambazo zilipotea kutoka katika miliki ya Martin Harris, ambaye karatasi hizo zilikuwa zimeaminishwa kwake kwa muda. (Ona kichwa cha habari cha sehemu ya 3.) Njama ovu zilikuwa ni kusubiri tafsiri ya pili ya jambo ambalo lilikwisha tafsiriwa katika kurasa zilizoibiwa na ndipo wamwaibishe mfasiri. Kwa kuonyesha tofauti zilizosababishwa na mabadiliko hayo. Kwamba kusudio hili la uovu lilikuwa limetungwa na yule mwovu lilijulikana kwa Bwana hata wakati Mormoni, Mnefi mwanahistoria wa kale, alipokuwa akifanya ufupishaji wa mabamba yaliyokusanywa; imeonyeshwa katika kitabu cha Mormoni (ona Maneno ya Mormoni 1:3–7).

1–26, Shetani huwachochea watu waovu kupinga kazi ya Bwana; 27–33, Yeye hutafuta kuziangamiza roho za wanadamu; 34–52, Injili itaenda kwa Walamani na mataifa yote kupitia Kitabu cha Mormoni; 53–63, Bwana atalianzisha Kanisa Lake na injili Yake miongoni mwa wanadamu; 64–70, Atawakusanya wenye kutubu katika Kanisa Lake na atawaokoa watiifu.

1 Sasa, tazama, ninakuambia wewe, kwa sababu wewe ulitoa maandiko yale ambayo wewe ulipewa uwezo wa kutafsiri kwa njia ya Urimu na Thumimu, na kuyaweka katika mikono ya mtu mwovu, umeyapoteza.

2 Na pia umepoteza kipawa chako vile vile, na akili yako ikawa giza.

3 Hata hivyo, sasa kimerejeshwa tena kwako; kwa hivyo angalia kwamba uwe mwaminifu na endelea hata kumaliza mabaki ya kazi ya kutafsiri kama ulivyoanza.

4 Usikimbie haraka zaidi au kufanya kazi zaidi ya nguvu ulizonazo na nyenzo ulizopewa kukuwezesha wewe kutafsiri; bali uwe mwenye bidii hadi mwisho.

5 Omba daima, kwamba uweze kutoka mshindi; ndiyo, uweze kumshinda Shetani, na kwamba uweze kuiepuka mikono ya watumishi wa Shetani ambao hufanya kazi yake.

6 Tazama, wanatafuta kukuangamiza; ndiyo, hata mtu yule ambaye ulimwamini ametafuta kukuangamiza.

7 Na kwa sababu hii nilisema kwamba yeye ni mtu mwovu, kwani yeye ametaka kuchukua vitu ambavyo wewe umeaminiwa; na pia ametafuta kuangamiza kipawa chako.

8 Na kwa sababu wewe umeyatoa maandiko hayo na kuyaweka mikononi mwake, tazama, watu waovu wameyachukua kutoka kwako.

9 Kwa hivyo, wewe umeyatoa, ndiyo, yale yaliyokuwa matakatifu, kwa waovu.

10 Na, tazama, Shetani ameyaweka katika mioyo yao kuyabadilisha maneno ambayo wewe umeyasababisha kuandikwa, au ambayo umeyatafsiri, ambayo yamekutoka mikononi mwako.

11 Na tazama, ninakuambia, kwamba kwa sababu wao wameyabadilisha maneno, yanasomeka kinyume na yale ambayo ulitafsiri na ukasababisha yaandikwe;

12 Na, kwa jinsi hii, ibilisi ametafuta kuweka mpango wa hila, ili apate kuiharibu kazi hii;

13 Kwani yeye ameweka katika mioyo yao kufanya hili, kwamba kwa kudanganya waweze kusema kwamba wamekukamata wewe katika maneno ambayo wewe mwenyewe umedai kuyatafsiri.

14 Amini, ninakuambia, kwamba sitakubali kwamba Shetani atimilize mpango wake huu mwovu katika jambo hili.

15 Kwani tazama, ameyaweka haya katika mioyo yao kukukamata wewe ili unijaribu Bwana Mungu wako, katika kuomba kuyatafsiri hayo tena.

16 Na halafu, tazama, wanasema na kuwaza mioyoni mwao—Tutaona kama Mungu amempa yeye uwezo wa kutafsiri; kama ndivyo, pia atampa tena yeye uwezo;

17 Na kama Mungu atampa yeye uwezo tena, au atatafsiri tena, au, katika maneno mengine, kama atayaleta maneno haya haya, tazama, sisi tunayo, na tumeyabadilisha;

18 Kwa hiyo hawatakubaliana, na tutasema kwamba amesema uwongo katika maneno yake, na kwamba yeye hana kipawa, na kwamba yeye hana uwezo;

19 Kwa hivyo tutamwangamiza, na pia kazi; na tutafanya haya ili tusije aibika mwishoni, na ili tuweze kupata utukufu wa ulimwengu.

20 Amini, amini, ninakuambia, kwamba Shetani ana mshiko mkubwa katika mioyo yao; yeye huwachochea wao kufanya uovu dhidi ya kile kilicho chema;

21 Na mioyo yao imepotoka, na imejaa uovu na machukizo; na wanapenda giza kuliko nuru, kwa sababu matendo yao ni maovu; kwa hivyo wao hawataniomba Mimi.

22 Shetani huwachochea, ili kwamba aweze kuwaongoza nafsi zao kwenye maangamizo.

23 Na hivyo yeye ametega mpango huu wa ulaghai, akifikiria kuharibu kazi ya Mungu; lakini nitayadai haya kutoka kwao, na itageuka kuwa aibu na hukumu yao katika siku ya hukumu.

24 Ndiyo, huwachochea katika mioyo yao kuikasirikia dhidi ya kazi hii.

25 Ndiyo yeye huwaambia: Danganyeni na mvizieni, ili mpate kumwangamiza; tazama, hii haina madhara. Na hivyo huwalaghai, na kuwaambia kwamba siyo dhambi kudanganya ili kwamba waweze kumkamata mtu katika uongo, ili wapate kumwangamiza.

26 Na hivyo huwalaghai, na kuwaongoza wao, hata kuzikokota roho zao hadi chini jehanamu; na hivyo kusababisha hao kujinasa katika mtego wao wenyewe.

27 Na hivyo ndivyo aendavyo juu na chini, mbele na nyuma katika ulimwengu, akitafuta kuziangamiza roho za wanadamu.

28 Amini, amini, ninakuambia, ole na iwe kwake yeye ambaye husema uongo ili kudanganya kwa sababu yeye adhani kwamba mtu mwingine pia husema uongo ili kudanganya, kwani mtu wa namna hiyo hatasamehewa kutokana na hukumu ya Mungu.

29 Sasa, tazama, wameyabadilisha maneno haya, kwa sababu Shetani amewaambia wao hivyo: Amekudanganyeni ninyi—na hivyo ndivyo yeye anavyowalaghai wao kufanya uovu, ili kuwapateni ninyi ili mumjaribu Bwana Mungu wenu.

30 Tazama, ninakuambia, kwamba usitafsiri tena maneno yale ambayo yamekwishatoka mikononi mwako;

31 Kwani, tazama, hawatatimiza njama zao hizo za uovu katika kudanganya dhidi ya maneno yale. Kwani, tazama, kama wewe utayatoa tena maneno yale yale watasema kwamba umedanganya na ya kwamba unajidai kuwa unatafsiri kumbe umejichanganya mwenyewe.

32 Na, tazama, wao watayachapisha haya, na Shetani itaishupaza mioyo ya watu kwa kuwachochea wakukasirikie wewe, kiasi kwamba hawatayaamini maneno yangu.

33 Na hivyo ndivyo Shetani awazavyo ili kuushinda ushuhuda wako katika kizazi hiki, kwamba kazi hii isije katika kizazi hiki.

34 Lakini tazama, hii ndiyo hekima, na kwa sababu ninakuonyesha wewe hekima, na kukupa amri kuhusu mambo haya, nini yakupasa kufanya, usiyaonyeshe kwa walimwengu mpaka utakapomaliza kazi ya kutafsiri.

35 Usishangae kwamba nimeyasema haya kwako: Hapa ndipo penye hekima, usiyaonyeshe kwa walimwengu—kwani nilisema, usiyaonyeshe kwa ulimwengu, kwamba uweze kulindwa.

36 Tazama, mimi sisemi kwamba hutaonyesha kwa wenye haki;

37 Bali, kwa vile huwezi daima kuwahukumu wenye haki, au kama vile wewe usivyoweza daima kuwatambua waovu na wenye haki, kwa hivyo ninakuambia, nyamaza mpaka nitakapoona inafaa kuyafanya mambo yote yajulikane kwa ulimwengu kuhusu jambo hili.

38 Na sasa, amini ninakuambia, kwamba historia ya mambo yale ambayo uliyaandika, ambayo yametoka mikononi mwako, yamechorwa katika mabamba ya Nefi.

39 Ndiyo, na unakumbuka kwamba ilisemwa katika maandiko yale kwamba historia zaidi juu ya mambo haya yametolewa katika mabamba ya Nefi.

40 Na sasa, kwa sababu historia ambayo imechorwa juu ya mabamba ya Nefi ambayo ni sahihi zaidi mambo ambayo, katika hekima yangu, nitayaleta kwenye ufahamu wa watu katika historia hii—

41 Kwa hivyo utatafsiri michoro ambayo ipo juu ya mabamba ya Nefi, kwenda chini mpaka ufike kwenye utawala wa mfalme Benjamini, au hadi ufike kwa yale ambayo umekwisha yatafsiri, ambayo uliyabakisha;

42 Na tazama, utachapisha hiyo kama kumbukumbu ya Nefi; na hivyo nitawashinda wao ambao wameyabadilisha maneno yangu.

43 Sitakubali kwamba waiharibu kazi yangu; ndiyo, nitawaonyesha wao kwamba hekima yangu ni kuu kuliko hila ya ibilisi.

44 Tazama, wamepata sehemu tu, au ufupisho wa historia ya Nefi.

45 Tazama, kuna mambo mengi yaliyochorwa juu ya mabamba ya Nefi ambayo huonyesha ufahamu mkubwa wa injili yangu; kwa hivyo, ni hekima kwangu kwamba wewe utafsiri sehemu hii ya kwanza ya michoro ya Nefi, na itokee katika kazi hii.

46 Na tazama, mabaki yote ya kazi hii yanayo sehemu zile zote za injili yangu ambayo manabii wangu watakatifu, ndiyo, na pia wanafunzi wangu, walitamani katika sala zao yaweze kutolewa kwa watu hawa.

47 Na mimi niliwaambia wao, kwamba itakubaliwa kwao kulingana na imani yao katika sala zao;

48 Ndiyo, na hii ndiyo ilikuwa imani yao—kwamba injili yangu, ambayo niliwapa wao kwamba waweze kuihubiri katika siku zao, iweze kuja kwa ndugu zao Walamani, na wale pia wamekuwa Walamani kwa sababu ya mafarakano yao.

49 Sasa, haya siyo yote—imani katika sala zao ilikuwa kwamba injili hii iweze kujulikana pia, kama ingewezekana kwamba mataifa mengine yangekuja kumiliki nchi hii;

50 Na hivyo waliacha baraka juu ya nchi hii katika sala zao, kwamba yeyote atakayeamini katika injili hii katika nchi hii apate uzima wa milele;

51 Ndiyo, kwamba iwe bure kwa wote na wa taifa lolote, kabila, lugha, au watu wowote watakaokuwa.

52 Na sasa, tazama, kulingana na imani yao katika sala zao nitaileta sehemu hii ya injili kwenye ufahamu wa watu wangu. Tazama, siileti kuja kuharibu kile ambacho wamekwisha kipokea, bali kwa kukijenga.

53 Na kwa sababu hiyo mimi nimesema: Kama kizazi hiki hakitaishupaza mioyo yao, nitalianzisha kanisa langu miongoni mwao.

54 Sasa sisemi hili ili kuliangamiza kanisa langu, bali nasema hili ili kulijenga kanisa langu;

55 Kwa hivyo, yeyote aliye wa kanisa langu hahitaji kuogopa, kwani huyo ataurithi ufalme wa mbinguni.

56 Lakini ni wao ambao hawaniogopi Mimi, wala kuzishika amri zangu bali wanajijengea makanisa yao wenyewe ili kujinufaisha, ndiyo, na wale wote ambao hufanya maovu na kujenga ufalme wa ibilisi—ndiyo, amini, amini, ninakuambia, kwamba ndiyo wao ambao nitawavuruga, na kusababisha watetemeke na kutikisika hadi kitovuni.

57 Tazama, Mimi ni Yesu Kristo, Mwana wa Mungu. Nilikuja kwa walio wangu, na walio wangu hawakunipokea.

58 Mimi ni nuru ingʼaayo gizani, na wala giza halikuiweza.

59 Mimi ndiye yule aliyesema—Kondoo wengine ninao ambao si wa zizi hili—kwa wanafunzi wangu, na wengi walikuwepo ambao hawakunielewa.

60 Na nitaonyesha kwa watu hawa kwamba nilikuwa na kondoo wengine, na kwamba walikuwa tawi la nyumba ya Yakobo;

61 Na mimi nitazileta katika nuru kazi zao za ajabu, ambazo walizifanya katika jina langu;

62 Ndiyo, na pia nitaileta katika nuru injili yangu ambayo walihudumiwa wao, na, tazama, wao hawataweza kukikataa kile ambacho wewe umekipokea, bali wao watazijenga, na watazileta nuruni sehemu muhimu za kweli za mafundisho yangu, ndiyo, na fundisho pekee lililoko ndani yangu.

63 Na hii ninafanya ili kwamba niweze kuanzisha injili yangu, ili pasiwepo na ubishi mwingi; ndiyo, Shetani huchochea mioyo ya watu kwenye ubishi kuhusu mambo ya mafundisho yangu; na katika mambo haya wanakosea, kwani wanayapindisha maandiko na wala hawayaelewi.

64 Kwa hivyo, nitafunua kwao siri hii kubwa;

65 Kwani, tazama, nitawakusanya wao kama vile kuku avikusanyavyo vifaranga vyake chini ya mabawa yake, kama hawataishupaza mioyo yao;

66 Ndiyo, kama wanatakakuja, wao wanaweza, na kunywa maji ya uzima bure.

67 Tazama, hili ni fundisho langu—yeyote atubuye na kuja kwangu, huyo ndiye kanisa langu.

68 Yeyote atangazaye zaidi au pungufu kuliko hili, huyo siye wangu, bali ni adui yangu; kwa hivyo siyo wa kanisa langu.

69 Na sasa, tazama, yeyote aliye wa kanisa langu, na alivumiliaye kanisa langu hadi mwisho, huyo nitamweka juu ya mwamba wangu, na milango ya jehanamu haitamshinda.

70 Na sasa, kumbuka maneno yake yeye aliye uzima na nuru ya ulimwengu, Mkombozi wako, Bwana wako na Mungu wako. Amina.