Sala na Makanisa Makuu
Mwandishi anaishi Utah, Marekani.
“Kama mkipendana ninyi kwa ninyi, ninyi ni wanafunzi Wangu” (Yohana 13:35).
Dani alitazama juu lakini bado hakuweza kuona kilele cha kanisa lile kubwa. Watu wa makanisa tofauti walikuja pale. Dani hakuelewa kwa nini familia yake ilikuwa inatembelea kanisa hili siku ya Ijumaa lakini Baba alisema walikuwa wanahudhuria kitu kilichoitwa Wimbo wa Jioni.
“Hiyo ni nini?” Dani akauliza.
“Ni mkutano ambapo watu wanaimba, kusoma maandiko na kusali pamoja” Baba alisema. “Kama familia kubwa mwishoni mwa siku.”
Dani alipenda jinsi hilo lilivyosikika. Yeye na familia yake walikuwa wanatembelea Uingereza. Jumapili iliyopita walikwenda katika kata iliyoitwa York. Katika darasa la Watoto, watoto wote waliyajua maandiko yale yale ambayo Dani aliyajua. Alijua kata aliyotembelea ilikuwa sehemu ya Kanisa la Kweli la Kristo, kama kata yake nyumbani.
Lakini hili kanisa kubwa lilikuwa tofauti sana na kile alichokizoea. Aliona meza ndogo iliyojaa mishumaa. Dani alimtazama mvulana akiwasha mshumaa.
“Kwa nini unawasha mishumaa?” Dani akamwuliza.
Yule mvulana akatabasamu. “Ninawasha mshumaa ninapoomba kwa ajili ya mambo maalum. Mradi mwale unaendelea kuwaka, ninatumaini kuwa sala itaendelea kusikilizwa na Mungu.”
Ilionekana kama mishumaa ya kawaida kwa Dani Alikanganyikiwa kidogo lakini alitaka kuwa mpole. Alitabasamu kwa yule mvulana.
Dani na familia yake walikaa, na mara Wimbo wa jioni ulianza. Alimwona mvulana yule yule safu chache kutoka alipokuwa. Kisha akagundua kuwa hakujua wimbo wowote kati ya nyimbo ambazo kila mtu alikuwa akiimba. Walipoomba, walisoma kutoka katika kijitabu kidogo. Kila kitu kilionekana tofauti na kile alichozoea.
Lakini muziki ulikuwa mzuri, hata ingawa haukufahamika. Kisha mtu akasimama kusoma maandiko. Alikuwa amevaa kanzu, badala ya suti na tai kama vile askofu wa Dani. Lakini mara alipoanza kusoma, Dani aligundua kuwa aliifahamu hadithi hii! Alikuwa akisoma kuhusu Yesu akiponya wakoma 10.
“Baba.” Dani alinong’oneza, “Ninaipenda hadithi hii.”
Baba akatabasamu. “Pia mimi.”
Kisha mtu aliyekuwa amevaa kanzu akatoa sala. Alimwomba Mungu kuwabariki waliokuwa wagonjwa na waliokuwa na shida. Kama Vile Dani alivyofanya! Aliomba pia baraka maalumu kwa viongozi wa Kanisa lake. Dani akakumbuka jinsi familia yake kila mara ilivyomwomba Baba wa Mbinguni kumbariki Rais Thomas S. Monson na washauri wake.
Hisia ya joto ikaja ndani ya moyo wa Dani. Alijua kwamba Baba wa Mbinguni alikuwa akimwambia kuwa Aliwapenda watoto wake wote na Alisikiliza sala zao zote hata kama walienda kwenye kanisa tofauti na hawakuwa na utimilifu wa injili
Walipoamka ili kuondoka, Baba aliangalia simu yake. Alionekana kuwa na huzuni alipokuwa akisoma ujumbe wake. “Dada ameaga dunia,” alisema.
“La hasha!” Dani akatoa sala ya haraka moyoni mwake kwamba Rais Monson awe SAWA.
“Je u mzima?” mtu akauliza. Ilikuwa yule mvulana wa hapo awali. Alikuwa amemsikiliza Dani na alionekana kuwa na wasiwasi.
“Dada Monson ameaga dunia,” Dani akasema. “Ni mke wa nabii wetu, Rais Monson.”
“Pole,” alisema kwa upole. “Nitawasha mshumaa kwa ajili yake.”
Dani akatabasamu na kumshukuru. Alifikiri ilikuwa vyema kwa mvulana yule kutoa sala maalum kwa ajili ya Rais Monson. Alijua kuwa Baba wa Mbinguni angesikiliza ile sala aliyosema moyoni mwake na ile ambayo yule mvulana alitoa.