2015
Lazima Tuende Hekaluni Sasa!
Aprili 2015


Lazima Twende Hekaluni Sasa!

Mary Holmes Ewen, California, USA

drawing of elderly woman sitting and talking to another woman

Vielelezo na Bradley H. Clark

Jumapili moja asubuhi muumini aliye batizwa hivi karibuni alitambulishwa kwenye kata. Jina lake lilikuwa Lydia. Alikuwa amezikonga nyoyo zetu mara moja.

Lydia alikuwa mzee na kipofu kutokana na miaka mingi ya kupambana na kisukari. Kwa haraka aliwajua waumini wa kata kwa sauti zao na vishindo vya hatua zao. Aliyataja majina yetu na kutushika mikono, na hatukudokezwa hata kidogo kwamba alikuwa kipofu.

Baada ya subira ya mwaka mmoja kama inavyotakiwa, Lydia alikutana na askofu na raisi wa kigingi kupokea kibali chake cha hekaluni. Katika Muungano wa Usaidizi wa Kina mama Jumapili moja, alinivuta karibu naye na kuniambia, “Raisi wa kigingi aliniambia lazima niende hekaluni haraka iwezekanavyo. Utanipeleka?”

Ilikuwa ni wiki ya kwanza ya Desemba—wakati wa shughuli nyingi ulikuwa umetukaribia. Nilijaribu kutoa sababu za kawaida na kusema, “Hatuwezi kusubiri hadi Januari?”

“Hapana, lazima tuende sasa!”

Kundi la wanawake toka kwenye kata yetu walikwenda hekaluni kila mwezi, hivyo nikawaendea ili waende pamoja na Lydia. Nao pia walikuwa na shughuli nyingi. Lakini Lydia, akiwa na machozi machoni mwake, akatuambia tena raisi wa kigingi amemwambia aenda haraka iwezekanavyo.

Kwa hilo wote tulikubaliana kusafiri maili 150 (241 km) wiki iliyofuata. Tukiwa njiani, gari lilijaa wanawake wanane wenye kubwabwaja na urafiki. Lydia alikuwa na furaha isiyo na kifani kwa tukio lake la kwenda hekaluni na baraka ya kupokea endaumenti yake.

Wiki ya kwanza ya Januari, hali ya Lydia ikazidi kuwa mbaya na akapelekwa hospitali kwa ajili ya uangalizi wa dharura. Wiki moja baadaye akafariki. Lakini Lydia alikwenda na baraka za milele alizozipokea katika hekalu wiki chache zilizopita.

Baadaye nikaielezea ile habari kwa raisi wa kigingi juu ya safari yetu na nikamwambia jinsi nilivyo furahishwa kwa jinsi alivyoongozwa kumwambia Lydia lazima aende hekaluni mara moja.

“Hakika sikuwa na maana lazima aende sasa,” alijibu. “Mara nyingi nawaambia wanaothibitishwa kwenda hekaluni haraka. Roho aliongea na Lydia, siyo mimi!”

Lydia alitufundisha sisi wote kumsikiliza Roho na kutenda hayo mara moja. Nina shukuru kwa kukumbuka kwake kuisikiliza sauti ndogo, nyororo.