Maswali na Majibu
“Ninawezaje kuridhika vya kutosha kuzungumza na askofu wangu kuhusu mambo au mashaka yangu?”
Unaweza kujisikia mwenye wasiwasi kumzungumzia askofu wako kuhusu mambo unayosumbuka nayo, na hiyo ni kawaida. Kila mara tunapata wasiwasi kabla ya matukio mapya au kabla ya kuzungumza na mtu mzima.
Lakini Askofu wako ameitwa na Mungu. Aliitwa kwa sababu ni mfuasi wa dhati wa Yesu Kristo. Atafanya juhudi kuwa mkarimu na muelewa. Dhamira yake ni kukusaidia kuja kwa Mwokozi ili upate amani. Mwanzoni, unaweza kuona soni kumzungumzia kuhusu maswali yako au dhambi, lakini hatakufikiria kuwa wewe ni mpungufu. Kwa hakika, atafurahi kuwa una hamu ya kuwa bora Na atatunza mazungumzo yenu ya siri.
Hupaswi kubeba mizigo yako pekee yako. Askofu wako anaweza kukusaidia kupata majibu ya maswali yako na ikibidi, kukusaidia kutubu na kushinda, kupitia Upatanisho wa Kristo, hisia za hatia, kuvunjika moyo, au kutostahili.
Unapozungumza na askofu wako utahisi upendo wake kwako. Ingawa ana jukumu la kata au tawi lote, lengo lake ni hali njema ya wavulana na wasichana. Humsumbui kwa kumwomba usaidizi.
Unaweza kusali kwa Baba wa Mbinguni akupe nguvu na ujasiri wa kuzungumza na askofu wako. Amemwidhinisha askofu wako kukusaidia na askofu wako ana hamu ya kufanya hivyo. Ukienda na moyo ulio wazi na hamu ya kuwa bora, utaona kwamba unapoondoka katika ofisi yake utakuwa unajisikia vyema zaidi ya ulivyokuwa hapo awali.
Hatakufikiria Kuwa Mpungufu
Askofu wa kata yako amepewa mamlaka kukuongoza kupitia hatua za toba. Mara nyingine kumgeukia askofu wako ni njia ya pekee kwako kutubu kikamilifu kupitia kwa Mwokozi. Nilipohitaji kumzungumza na askofu wangu, alinisaidia kumpata Mwokozi na kushinda kidonda kikuu nilichowahi kuwa nacho. Askofu wako anataka kukuasaidia. Wito wake ni kukulinda, na hatakufikiria kuwa mpungufu kwa sababu ya kitu unachohitaji kumwona.
Madison D., umri 18, Utah, Marekani
Askofu Wako Yu Tayari Kukusaidia
Nilikuwa nahisi vibaya katika mahojiano, lakini hatimaye niligundua kuwa askofu wangu alikuwa tayari kila wakati kunisaidia kutatua matatizo yangu. Mwamini askofu wako, yeye ni mchungaji na kata ni kundi lake.
Jaime R., umri 19, Cochabamba, Bolivia
Hataisaliti Imani Yako
Nimekuja kujua kuwa askofu ni mtu mzima pengine anayeaminika zaidi ambaye kijana anaweza kutafuta usaidizi kutoka kwake. Hataweza kamwe kusaliti imani yako—kila kitu unachomsimulia husalia pale ofisini mwake Wakati mwingine ni vigumu sana kusimulia matatizo yako, lakini kuzungumza ana kwa ana na mtu anayekupenda na kukujali na anayetaka mema zaidi kwako hufanya kuwa rahisi zaidi.
Nicole S., umri 18, Idaho, USA
Unaweza Kumtegemea
Askofu wako au rais wa tawi ni mtumishi wa kweli wa Bwana. Unaweza kumtegemea kwa maelekezo unapotafuta maongozi kutoka kwa Roho Mtakatifu na maandiko. Ni lazima uelewe kuwa askofu yuko pale ili kusaidia, na kwamba anaongozwa na Mungu.
Stanislav R., umri 19, Donetsk, Ukraine
Kumbuka Kwamba Anakupenda
Ikiwa una kitu unachotaka kweli kujadiliana na askofu, inaweza kuwa rahisi kuzungumza naye kuhusu shule na mambo mengine ya kawaida kwanza. Ikiwa una wasiwasi kwa sababu unahitaji kuzungumza naye mambo ya toba, kumbuka kwamba anakupenda. Huhitaji kuwa na wasi wasi kuhusu kile atakachofikiria juu yako, kwa sababu, kwa nini akubeze kwa kutaka kuwa karibu na Kristo?
Ashley D.,umri 17, Arizona, Marekani
Sali ili Ufahamu
Jiulize kwa nini unasikia vibaya ukizungumza na askofu. Unafikiri hataweza kutatua matatizo yako? Sali ili ujue kuwa askofu anakupenda na ameitwa ili kukusaidia.
Adam H., umri 13, California, USA
Hata Kama Utafanya Makosa
Inaweza kuwa vigumu na aibu kukiri mambo kwa askofu wako lakini unapotoka katika ile ofisi, utahisi kupata nafuu, na utajua kuwa Baba wa Mbinguni anakupenda. Anataka uwe na furaha hata ukifanya kosa.
Amanda W., umri 16, Utah, USA
Yuko Hapa Ili Kusaidia
Askofu ni mchungaji wa kata yako. Kumbuka kwamba atafanya awezalo kukusaidia na ana uwezo wa Bwana uko upande wake. Ukihisi uoga, unaweza kusali kwa ajili ya kuomba nguvu ili kuweza kuzungumza na askofu wako. Hatimaye, utafurahi kuwa ulimwendea—na itakuwa ya kustahili.
Samuel H., umri 14, Idaho, USA
Mwamini yeye
“Tafuta ushauri kutoka kwa viongozi wako wa ukuhani, hasa askofu wako. Anajua viwango, na anajua cha kukufunza. Tafuta fursa za kuwa naye. Unaweza kutarajia akuulize maswali ya moja kwa moja, ya upekuzi. Mwamini. Mwamini yeye. Muombe akusaidie kuelewa kile Bwana anachotarajia kutoka kwako. Dhamiria kuishi kulingana na viwango vya Kanisa vya maadili. Uhusiano wenye maana na mtu mzima kiongozi ni muhimu kukusaidia kuwa msafi kimaadili na mwenye kustahili.”
Mzee M. Russell Ballard wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili, “Usafi Huja kabla ya Uwezo,” Ensign, Nov. 1990, 37.
Swali Linalokuja
“Ninakejeliwa shuleni kwa kuwa MSM. Ninajua ninapaswa kutetea ninachoamini lakini ni vigumu sana! Nitakuwaje jasiri ya kutosha kuwaambia wale watu wakome?
Wasilisha majibu yako, na ukipenda, picha ya ubora wa hali ya juu kabla ya Mei 1, 2015, katika liahona.lds.org, kwa barua pepe liahona@ldschurch.org, au kwa posta (Ona anwani katika ukurasa wa 3).
Taarifa ifuatayo na ruhusa lazima ijumuishwe katika barua pepe yako au barua: (1) jina kamili, (2) tarehe ya kuzaliwa, (3) kata au tawi, (4) kigingi au wilaya, (5) ruhusa yako uliyoandika, na kama u chini ya miaka 18, ruhusa iliyoandikwa na mzazi wako (barua pepe inakubalika) ili kuchapisha majibu yako na picha.
Majibu yanaweza kuhaririwa kwa ajili ya urefu au ufafanuzi.