Nafasi Yetu
Jeshi la Zimamoto na Ngao ya Mungu
Ilikuwa siku tulivu kazini kwangu nikiwa kama mwana zimamoto wa kujitolea, hivyo nikaamua kusoma Kitabu cha Mormoni. Wakati mmoja wa wafanyakazi wenzangu aliponiona nikisoma, aliuliza kama nilijua jinsi gani tunaweza kuvaa ngao ya Mungu siku hizi. Tulipokuwa tukiongea, king’ora kikalia. Kulikuwa na moto kwenye duka la jirani.
Kwa haraka tukavaa magwanda yetu ya zimamoto na kuelekea huko. Miali ya moto ilikuwa mikubwa, na tulipolikaribia duka, kitu kikalipuka katika upande tuliokuwepo. Miali ya moto ikatuzingira. Mlipuko uliwakanganya wafanya kazi wenzangu na mimi kwa sekunde chache. Lakini asante kwa vyombo vyetu na nguo za kujikinga, hatukuumia.
Tuliporudi kituoni baada ya kupambana na moto, nilimwuliza mfanyakazi mwenzangu kama alikumbuka swali lake juu ya ngao ya Mungu. Alisema alikumbuka, na nikamwelezea kwamba ngao ya Mungu ni kama nguo za kujikinga za zimamoto. Lazima tuzivae mara zote ili tuweze kuhimili mashambulio ya nguvu ya adui. Kama tutatii amri, tutabarikiwa kwa nguvu za kujikinga za ngao ya Mungu, na Roho Mtakatifu atakuwa mwongozi wetu.
Fernando de la Rosa Marrón, Mexico
Andiko Langu Nilipendalo
1 Samweli 16:7. “Bwana haangalii kama aangaliavyo mwanadamu; kwani mwanadamu huangalia muonekano wa nje, lakini Bwana huangalia kwenye moyo.”
Kabla sijajiunga na Kanisa, mara nyingi nimejiona kama mtu wa kawaida nikiwa na uwezo wa kawaida. Nilijiona kwamba sikuwa na chochote cha thamani ninachoweza kutoa. Nilikuwa naogopa kuwaonyesha watu kuwa mimi ni nani kwasababu ya kuogopa kukataliwa na kuumizwa. Nilifikiri kwamba kila mtu aliyenizunguka alikuwa imara, mwenye akili, na mzuri zaidi yangu,
Lakini haya matarajio yote yalibadirika pale nilipokuwa muumini wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho. Nilijifunza kwamba sisi wote ni watoto wa Mungu na tulirithi tabia takatifu. Sasa ninaelewa kwamba hakuna mashindano ya nani mwenye akili, tajiri, au mwenye sura nzuri. Machoni pa Bwana, sisi wote tupo sawa, na Yeye ndiye anaye hukumu—siyo kwa kuangalia sifa za mwili wetu bali kwa utii wetu na kwa kutamani kwetu kufuata njia Alizoziweka.
Joan Azucena, Philippines
Utafanya kazi Jumapili?
Nilipokuwa na miaka 15, nilipata ushuhuda mkubwa wa injili ya Yesu Kristo na nilikuwa na furaha tele kujiunga na Kanisa. Wakati huo, nilikuwa nafanyakazi kuisaidia familia yangu. Si muda mrefu baada ya kubatizwa Hata hivyo, nilipoteza kazi yangu.
Nilitakiwa kutafuta kazi mpya haraka kwa sababu familia yangu ilinitegemea, lakini kila kazi niliyoomba ilihitaji nifanye kazi Jumapili. Nilikataa ofa za kazi nyingi kwasababu nilijua kwamba nilihitaji kuwa kanisani Jumapili (ona M&M 59:9–10).
Baada ya miezi miwili ya kutafuta, bado sikupata. Mama yangu hakuwa muumini wa Kanisa, na japokuwa alimwamini Mungu, alikuwa mwenye hasira sana kwa sababu nilikataa kazi nyingi sana.
Usiku mmoja aliniangalia akiwa na machozi machoni mwake na akauliza, “Kwa nini Mungu anayaacha haya yatokee kwetu wakati wewe ni mwaminifu sana katika kutenda kile kilicho cha haki?”
Nikajibu, “Mama, sijui ni kwanini hili linatokea kwetu, lakini ninajua kwamba ninafanya kitu sahihi, na ninajua kwamba Mungu atatubariki kwa hilo.”
Asubuhi iliyofuata mtu mmoja alinipa kiasi kikubwa cha pesa ili nikitumie kwa siku mbili kuhamisha mizigo mizito toka nyumba moja hadi nyingine. Kazi ilikuwa ya kuchosha, lakini nilipopata pesa, nilikwenda moja kwa moja nyumbani na kutoa sala ya shukrani. Mara nikapata kazi nzuri ambayo iliniruhusu kupumzika Jumapili, na sijawahi kukosa kazi toka hapo.
Nina furaha kwamba nilichagua kuifanya takatifu siku ya sabato. Kuna changamoto nyingi katika maisha, lakini ninajua kwamba kama tutajitahidi kuwa imara licha ya changamoto hizo, Bwana atatubariki.
Sahil Sharma, India