Sauti za Watakatifu wa Siku za Mwisho
Kurasa Mbili Zilizojaa Shukrani
Elise Dahlen
Utah, Marekani
Baba yangu aliteseka maisha yake yote kutokana na kutokujiamini na hisia za kutokua na thamani. Alilelewa na baba mlevi ambaye mara kwa mara alimwambia jinsi alivyodhani hakuwa na thamani. Nashukuru, baba yangu kamwe hakuwahi kuwa mlevi, lakini hakuwahi kuniambia mimi na ndugu zangu kwamba alikuwa akijivuna kwa ajili yetu au kutusifu kwa mambo tuliyofanya vizuri. Nilipokuwa nikikua, nilijaribu kumfurahisha, lakini daima nilihisi nisingeweza kufua ndafu. Hii ilitusababisha kuwa na uhusiano usio mzuri.
Mwaka mmoja, nilidokeza hili kwa askofu wangu mwenye hekima. Alinishauri nimwandikie baba yangu barua nikimwambia sababu zote za kuwa na shukrani juu yake. Hili lingekuwa tendo la ujasiri kwangu. Majeraha yangu yalikuwa makubwa, na sikutaka barua yangu ya shukrani kuwa moja ya maudhi. Hivyo niliomba. Nikiwa na Roho akiniongoza, sababu kwamba nilikuwa na shukrani kwa ajili ya baba yangu zilianza kutiririka. Ilichukua muda, lakini nilipomaliza, nilikuwa nimejaza kurasa mbili.
Nilipeleka barua yangu, bila kujua baba yangu angejibu nini. Lakini nilijua kwamba sikupaswa kuchagua jinsi atakavyojibu. Nilihitaji tu kujiangalia ndani ya moyo wangu mwenyewe na kukumbuka kwa nini niliandika barua.
Asubuhi iliyofuata, nilipokea simu kutoka kwa mama yangu wa kambo. Alikuwa akilia. Aliniambia kuwa baba yangu alikuwa amesoma barua tena na tena na tena. Alisema asingeweza kuzungumza na mimi kwa sababu alikuwa analia sana.
“Asante!” mama alisema. “Baba yako alihitaji hili.”
Baadaye siku ile, baba yangu alipiga simu kunishukuru. Alinipigia kila siku kwa siku kadhaa kuelezea jinsi gani barua ilikuwa na maana kwake.
Natamani ningeweza kusema kwamba uhusiano wetu ulikuwa umeponywa kimiujiza, lakini tulikua bado na kazi kubwa ya kufanya. Baada ya muda, moyo wangu ulianza kupona, na uhusiano wetu uliimarika. Hatimaye, niliweza kumsamehe.
Miaka michache baadaye, baada ya vita kali dhidi ya saratani, baba yangu alifariki. Nina uhakika sasa anapata uzoefu wa shangwe kuu pale Mwokozi anapomsaidia kupona kutokana na miaka ya uonevu. Ninajua kwamba nimepata uzoefu wa uponyaji kupitia nguvu ya Upatanisho ya Yesu Kristo. Mwokozi anaelewa mahitaji yetu na anaweza kutusaidia kuondoa sumu ya maumivu na chuki kutoka kwenye nafsi zetu. Ninajua kwamba shukrani, msamaha, na upendo ni tiba zenye nguvu.