2019
Kutoka kwenye Uonevu mpaka Kubatizwa
Oktoba 2019


Kutoka kwenye Uonevu mpaka Kubatizwa

Urafiki wako na mfano wa uadilifu utawabariki rafiki zako na vizazi vijavyo.

young men tempting Hugo to smoke

Kielelezo na Brooke Smart

Nilipokuwa na umri wa miaka 17, nilikutana na shinikizo kubwa la kundi rika kwenye shule yangu ya upili. Marafiki niliokuwa nao hawakuwa na viwango sawa na vyangu. Mimi na rafiki zangu tulishiriki pamoja kwenye shughuli nyingi za kufaa kama kucheza mpira wa kikapu au mpira wa miguu. Lakini pia walikunywa pombe na kuvuta sigara—shughuli mbili ambazo sikufanya pamoja nao.

Siku moja kundi letu lilikuwa nje ya shule yetu tukisoma kwa ajili ya jaribio ambalo tungefanya baadaye siku hiyo. Pamoja nami walikuwa ni rafiki zangu wa karibu sana, Juan na Francisco (majina yamebadilishwa). Ghafla, mmoja akatoa kiberiti na sigara. Nilidhani rafiki zangu walikuwa wamechoka kusoma na walikuwa wamesahau kwamba nilikuwa pale. Niligundua sikuwa sahihi pale waliponigeukia na kusema, “Sasa ni wakati wa Hugo kujifunza jinsi ya kuvuta.”

Kabla hata sijapata nafasi ya kujibu, Juan na Francisco walinirukia na kunishika mikono yangu, mmoja kila upande. Walishusha mikono yangu pale mmoja aliposukuma sigara katikati ya midomo yangu. Mwili wangu haraka ulikataa hili, na nilitema sigara chini, mbali na mimi. Punde baada ya hilo, nilihisi mvumo wa ngumi iliyokazwa ikiungana kwa pembe mraba na mfupa wangu wa shavu. Walinitishia, wakisema, “Tunawasha sigara tena, na utajifunza jinsi ya kumeza moshi. Usiiteme chini. Ukiitema, hatma yake haitakuwa nzuri.”

Dakika ile, nilijua nilikuwa matatizoni. Nilifumba macho na kusema sala ya haraka nikiomba aina fulani ya usaidizi. Punde tu nilipohitimisha sala, gari ya mwalimu wetu ilifunga breki na kusimama karibu yetu. Mwalimu wetu alitoka nje ya gari na kutuuliza kile tulichokuwa tukifanya. Rafiki zangu waliniachia. “Tunajiandaa kwa ajili ya jaribio,” walimhakikishia mwalimu. Tulikwenda shuleni na kufanya jaribio, na suala hilo liliisha.

Licha ya uzoefu huo kuwa mgumu, niliwasamehe rafiki zangu kwa kile walichofanya. Nilijua hawakuelewa viwango vyangu na uamuzi wangu kuishi Neno la Hekima, hivyo niliwasamehe na kuchagua kutokuwa na hisia mbaya juu yao. Nilipohitimu shule, nilienda misheni lakini niliendelea kuwasiliana na Juan na Francisco. Niliwaandikia barua mara kwa mara nikishiriki nao injili na ushuhuda wangu wa Yesu Kristo. Niliwaalika watubu na wahudhurie kanisani. Kwa mshangao wangu mkubwa, mmoja wao alihudhuria.

Nilikuwa nimewaalika rafiki zangu mara kwa mara kwenye mikutano ya Jumapili kabla, lakini hakuna aliyekubali mpaka sasa. Japokuwa sikuweza kuhudhuria pamoja na Juan, kaka zangu na baba yangu walikuwepo kumsaidia na kumpa urafiki. Familia yangu walimkubali, na Juan alijihisi vizuri kanisani. Alianza kubadilika kidogo kidogo mpaka alipofanya uamuzi wa kubatizwa. Nilikuwa na msisimko kwa ajili yake na hata kuwa na msisimko zaidi wakati aliponiambia kwamba alikuwa amejifunza kumpenda Yesu Kristo kwa sababu ya barua zangu. Niliporudi nyumbani kutoka misheni yangu, nilikuwa karibu pia na Francisco, na baada ya muda, yeye na mke wake pia walibatizwa. Leo, Juan na Francisco bado ni rafiki zangu wa karibu.

Matukio haya yamewekea alama maisha yangu. Nimejifunza kwamba njia nzuri zaidi ya kuleta ushawishi katika maisha ni kuishi kwa uadilifu, kuwapenda wengine, na kufikia. Kijitabu cha Kwa Nguvu ya Vijana kinasema, “Ili kuwa na marafiki wema, kuwa rafiki mwema. Onyesha nia ya kweli kwa wengine; tabasamu na acha wajue kuwa unawajali.”1 Hiki ndicho Bwana alichonisaidia mimi kufanya kwa Juan na Francisco. Kwa sababu ya hilo, nina marafiki wakuu wawili ambao nimewahi kuwajua, na sasa tunafanya kazi pamoja kuunga mkono ufalme wa Mungu kama waumini wa Kanisa.

Daima inua juu viwango vya Kanisa, hata kama upo katika hali ngumu kama niliyokuwa nayo. Kwa Nguvu ya Vijana inaelekeza, “Unapojitahidi kuwa rafiki kwa watu wengine, usipuuze viwango vyako. Kama rafiki zako wanakuomba kufanya mambo ambayo si sahihi, kuwa wa kwanza kusimamia ukweli.”2 Hata kama inaonekana kama kila mmoja anafanya kile kilicho tofauti na amri, baki imara kwa sababu mfano wako una nguvu. Kuwa aina ya mfano ambao rafiki zako wanaweza kuufikiria wakati wa nyakati zao za uhitaji. Katika baadhi ya matukio kama langu, urafiki wako waweza kuwa jambo ambalo linawasaidia wao kujifunza, kutubu, na kuongoka.

Muhtasari

  1. Kwa Nguvu ya Vijana (2011), 16.

  2. Kwa Nguvu ya Vijana, 16.