Marafiki Ambao Walishiriki Nuru Yao pamoja Nami
Mwandishi anaishi Baja California, Mexico.
Nilikuwa nikihisi woga na mpweke. Kisha nilihamia nchi nyingine na kwenda kanisani kwa mara ya kwanza baada ya muda mrefu.
Nilikuwa nikiishi na mama yangu kwenye mji mdogo huko Mexico ambapo watu wote walifahamiana. Nilijua mema na mabaya, lakini nilikuwa nimekanganyikiwa na nilikuwa msichana pekee anayeshiriki kikamilifu katika mji wote.
Nilitaka kuwa sehemu ya jamii, hivyo nilifanya kitu kimoja ambacho kilikuwa na maana hapo nyuma: kuwa na mpenzi. Hili lilikuwa kosa la kwanza nililoanza kufanya. Nilianza kujiingiza kwenye makundi rika na kuamini kwamba nilikuwa mkubwa vya kutosha kufikiria kwa ajili yangu mwenyewe, ambayo ilimaanisha kuwa msichana asiyeshiriki kikamilifu ambaye aliishi gizani.
Niliishi gizani kwa mwaka mmoja, kwa kila siku iliyopita kuwa yenye giza zaidi. Maamuzi yangu mabaya yalipelekea mizozo na familia yangu, na nilitambua nisingeweza kuendelea kuishi nao. Lakini haikuwa mpaka kifo cha rafiki wa karibu Mtakatifu wa Siku za Mwisho ambapo nilitambua kuna kitu kilikuwa kinakosekana. Kwa bahati mbaya, nilimlaumu Mungu pamoja na injili. Niliacha kuamini kwamba baraka zilikuja kutokana na kuwa mtiifu. Nilijua kwamba ikiwa nisingeamua kuanza kuishi injili, ningeendelea kupuuzia muunganiko wangu na Kanisa na kuendelea kuishi katika namna ya ulimwengu.
Nilikuwa nimekaa juu ya kitanda changu kwenye chumba chenye giza, nikilia na kujionea huruma mwenyewe wakati nilipotambua kwambanilikuwa na woga—woga wa kuwa pale peke yangu bila mtu wa kuzungumza naye, woga wa kutoweza kurekebisha maovu yote niliyokuwa nimetenda, woga kwamba hakuna yeyote ambaye angenisamehe, hasa Mungu.
Hatimaye, nilihamia Minnesota, Marekani, pamoja na babu na bibi yangu, ambao si waumini wa Kanisa. Baba yangu wa kambo alisafiri pamoja nami, na Jumapili yangu ya kwanza huko, tulikwenda Kanisani, lakini kwa ajili ya mkutano wa sakramenti tu. Kuelekea hitimisho la mkutano nilikuwa tayari nimekwisha amua kuondoka Kanisani, lakini kwa mshangao wangu, wakati tulipokuwa tukielekea kwenye gari, tulimwona askofu akitukimbilia. Alituuliza maswali machache na kutualika kuhudhuria tena Jumapili iliyofuata—na tulifanya hivyo.
Jumapili iliyofuata, wakati mkutano wa sakramenti ulipokuwa ukimalizika, kabla sijasimama, nilikuwa nimezungukwa na wasichana kutoka kwenye kata—wasichana ambao wangenisaidia kubadili maisha yangu.
Ghafla nilikuwa nimeingia kwenye ulimwengu tofauti kabisa: ulimwengu uliokuwa na askofu na rais wa Wasichana ambao walinijali na, zaidi ya yote, wasichana ambao walijaribu kuishi injili kila siku, waliojitahidi kuishi viwango vya juu na kusimamia kilicho sahihi. Waling’ara sana kiasi kwamba wangeweza kuangaza njia mbele yangu.
Hapo ndipo nilipotambua kile nilichopaswa kufanya: “Nuru [yangu] na iangaze mbele ya watu, wapate kuyaona matendo [yangu] mema, wamtukuze Baba [yangu] aliye mbinguni” (ona Mathayo 5:16). Na hivyo nilianza kwa kwenda kanisani na kwenye shughuli za Mutual kila wiki, kusoma Kitabu cha Mormoni na kuomba kila siku, kuvaa kwa staha, kutumia lugha nzuri, kwenda hekaluni, na kujiandaa kupata baraka yangu ya baba mkuu.
Nilikuwa nimebadilika kikamilifu, lakini sikutambua hilo mpaka kwenye kambi ya Wasichana, ambapo nilihisi Roho Mtakatifu na kugundua kwamba nilikuwa na ushuhuda—ushuhuda ambao ungenikumbusha kwamba Mungu ananipenda, kwamba ana mpango kwa ajili yangu, na kwamba hataki mimi niwe peke yangu. Ushuhuda angavu na imara kwamba ulinibadili. Ushuhuda wa kushiriki na kuangaza si tu njia yangu bali ya wengine. Ushuhuda ambao hauna woga kung’ara kwenye giza.