Kuwa au Kuwahi Kuwa: Hilo Ndilo Swali
Tunatarajiwa kuhukumu. Lazima. Lakini hatupaswi kubagua au kumpachika jina mtu yeyote.
Miaka kadhaa iliyopita mimi na mke wangu tulizuru Kasri la Kronborg huko Helsingør, Denmark. Kasri hili lilikuwa limepewa umaarufu na igizo la William Shakespeare Hamlet. Tulipokuwa tukitembea kwenye kuta za kasri, mawazo yetu yalijawa na matukio na mazungumzo kutoka kwenye igizo, hususan ombi maarufu la Hamlet, “Kuwa, au kutokuwa: hilo ndilo swali.”
Lakini nilifikiria juu ya swali lenye uhusiano zaidi la kujiuliza sisi wenyewe: “Kuwa au kuwahi kuwa: hilo ndilo swali.”
Ruhusu Maboresho
Kwa bahati mbaya, mara nyingi tunabandika majina wakati tunapozungumza kuhusu wengine. Kwa mfano, tunaweza kusema mambo kama vile:
-
“Mzee Brown ni mmisionari mvivu.” Badala yake tunapaswa kusema, “Mzee Brown amekuwa hafanyi kazi kwa bidii siku za karibuni, lakini ninaamini anaweza kubadilika.”
-
“Mary siyo mtu wa dini.” Kinyume chake, tungeweza kusema, “Mary amekuwa havutiwi sana katika dini, lakini anaweza kumhisi Roho ikiwa nitatoa ushuhuda wangu kwake.”
Wakati tunaposema mtu fulani ni kitu fulani, tunaweza kuishia kupachika jina au kubagua, kuhukumu pasipo kutoa nafasi ya uwezekano wa badiliko na maboresho. Lakini tunaposema amekuwa, tunaonesha kwamba tunaamini ukuaji na uendelevu vinawezekana.
Je, ni makosa Kuhukumu?
Tafsiri nyingi za Biblia zinatoa toleo lifuatalo la fundisho la Mwokozi: “Msihukumu, msije mkahukumiwa ninyi” (Mathayo 7:1). Lakini Tafsiri ya Joseph Smith inatoa ufafanuzi: “Msihukumu ninyi pasipo haki … , bali hukumuni hukumu ya haki” (katika Mathayo 7:1, tanbihi a; msisitizo umeongezwa).
Hakika inakubalika—na hata kutegemewa—kwamba tunatoa hukumu pale tunapokadiria, kutathmini, na kutambua hali na kufanya maamuzi. Na ni muhimu hasa kwamba tufanye hukumu ya haki pale tunapochangamana na watu.
Kwa mfano, tunapaswa kutathmini kwa makini nani tunakwenda kufunga naye ndoa, kutumia ufahamu kuelewa madhumuni ya mtu, au kukadiria uwezo wa mtu wa kutimiza jukumu la kazi ya kulipwa.
Tunapaswa daima kutathmini matendo ya watu au sifa kwa kutumia viwango vya Bwana, kama vilivyo katika maandiko matakatifu na maneno ya manabii. Zaidi ya yote, tunapaswa kuwa na uhakika kwamba hukumu zetu hazijaribu kumtambulisha mtu bila ukarimu, kubagua kwa haraka, au pasipo haki kumpachika jina yeyote.
Kuweza Kubadilika
Tunatoa hukumu isiyo ya haki wakati bila usahihi tunapowaelezea wengine, hasa ikiwa kwa kufanya hivyo tunaonesha kwamba hawawezi kubadilika. Katika miingiliano yetu yote na wengine, tunapaswa kukumbuka kwamba kwa sababu ya dhabihu ya upatanisho wa Bwana, kila mmoja wetu ana uwezo wa kujiboresha. Fikiria mifano hii kutoka kwa Mwokozi:
-
Alisema kwa mwanamke aliyekamatwa kwenye uzinzi, “Enenda zako, wala usitende dhambi tena” (Yohana 8:11).
-
Alimwambia mmoja wa watu waliokuwa wamesulubiwa kando Yake, “Leo hivi utakuwa pamoja nami peponi” (Luka 23:43).
-
Kama kiumbe mfufuka, Yeye aliendelea kuuona uwezekano wa Petro na kumshauri, japokuwa Petro alikuwa amemkana mara tatu (ona Mathayo 26:34 na Yohana 21:15–17).
-
Alimwambia Sauli, ambaye alikuwa amewatesa Watakatifu, kutubu. Sauli, ambaye alikuja kuwa Paulo, alitii na kuwa mwenye haki. (Ona Matendo ya Mitume 9:3–6.)
Bwana Yesu Kristo ni shujaa wa nafasi za pili—na za tatu na za nne pia. Alitufunza kusamehe “hata saba mara sabini” (Mathayo 18:22). Yeye ni mtu pekee aliyeishi maisha makamilifu kwenye dunia hii, lakini kwa sababu ya maisha Yake, mafundisho Yake, dhabihu Yake ya upatanisho, na Ufufuo Wake, na kupitia ibada za injili Yake, sisi pia tunaweza kuwa wakamilifu siku moja. Kuwarejelea akina kaka na dada zetu katika njia ambayo huelezea kutokuwa na imani katika uwezo wao wa kubadilika kungeelezea pia kutokuwa na imani katika nguvu ya Mwokozi na Upatanisho Wake.
Nje na Ndani
Ni uhalisia wa maisha kwamba mara nyingi tunahukumu (na tunahukumiwa) kwa muonekano wa kwanza. Tuko katika hatari ya kuhukumu pasipo haki, hata hivyo, wakati tunapohukumu tunategemea tu muonekano wa kwanza na kushindwa kutathmini sifa ya kweli ya mtu.
“Bwana haangalii kama binadamu aangaliavyo; maana wanadamu huitazama sura ya nje, bali Bwana huutazama moyo” (1 Samweli 16:7). Yesu aliwarejelea wanafiki katika siku Yake kama “makaburi yaliyopakwa chokaa, nayo kwa nje yaonekana kuwa mazuri, bali ndani yamejaa … uchafu wote” (Mathayo 23:27).
Mwokozi alikuwa hafundishi kwamba mwonekano chanya na wa kupendeza wa nje si kitu kizuri bali kwamba sifa ya ndani ya mwanaume au mwanamke (hali ya kimwili na kiroho) ni muhimu zaidi. Fikiria mahekalu yetu ya kupendeza, lakini muhimu zaidi ni ibada ambazo hufanywa ndani.
Wamisionari pia wanahitajika kuendeleza viwango vya uvaaji na maadili. Kwa kuwa wasafi, kuvaa kwa staha, na kutumia lugha inayofaa, wanaweka mfano mzuri kwa wale ambao kutambulishwa kwao kwenye injili ya Yesu Kristo kutakuja kupitia kile wanachoona na kusikia kutoka kwa wamisionari.
Kutumia Utambuzi
Tunapojaribu kufanya hukumu za haki, ni muhimu kutumia utambuzi. Mwongozo kwenye Maandiko unasema utambuzi ni “kuelewa au kujua jambo kupitia nguvu ya Roho. … Unajumuisha kutambua sifa ya kweli ya mtu na chanzo na maana ya onyesho la kiroho” (“Utambuzi, Kipawa cha”).
Wakati mwingine watu ambao ni waovu ndani hutumia muonekano wa kidunia kujaribu kutuhadaa katika kudhani wanastahili kuigwa. Wao ni “wenye hekima katika macho yao wenyewe, na wenye busara katika fikira zao wenyewe” (Isaya 5:21; 2 Nefi 15:21). Mwokozi aliweza kuona zaidi ya uongo huu, na aliweza kutambua nguvu na sifa na kusudi la uaminifu la moyo kati ya hata wale waliokuwa wanyenyekevu na kutupiliwa mbali.
Alma alitumia utambuzi kama huo wakati alipozungumza na wale waliokuwa “wametupwa nje kwa sababu ya umasikini wao” na bado walibarikiwa kwa sababu walikuwa wamejishusha na “wanyenyekevu mioyoni (ona Alma 32:5–8).
Tunapaswa kukumbuka kwamba “mambo ya Roho wa Mungu … yatambulikana kwa jinsi ya rohoni” (1 Wakorintho 2:14). Tunapowaona wengine kama Baba yetu wa Mbinguni anavyowaona, utambuzi unaturuhusu kutoa hukumu ya haki.
Hukumu ya Haki
Kila siku ya maisha yetu tunahukumu kwa kukadiria, kutathmini, na kutambua. Hata hivyo, Bwana anatutarajia kufanya hivyo kwa haki. Kama wafuasi wa Bwana Yesu Kristo, maneno na matendo yetu, yanapaswa kuonesha kwamba sisi ni wenye huruma, upendo, na tuko radhi kusaidia.
Kama waamuzi wa haki, tunahitaji kuhakikisha kwamba tunakuwa makini zaidi kwenye sifa ya mtu badala ya muonekano wao. Wakati huo huo, tunapaswa kukumbuka kwamba kila siku tunatengeneza mwonekano wa kwanza kwa jinsi tunavyoonekana na maneno tunayotumia. Watu wengi watavutwa kujua zaidi kuhusu sifa na ujumbe wa injili ikiwa mwonekano wetu unaakisi thamani kubwa ya ujumbe wetu.
Bwana wetu, Yesu Kristo, ametuonyesha mfano mkamilifu wa kufuata pale tunapojitahidi kuhukumu kwa haki. Tunapaswa—kama Yeye anavyofanya—kuwekea usawa kile tunachoona kwenye umbo la nje na kile kinachoendelea ndani ya kila mtu.