2019
Hekalu la Laie Hawaii: Karne ya Kukusanyika
Oktoba 2019


Hekalu la Laie Hawaii: Karne ya Kukusanyika

Likiwekwa wakfu miaka 100 iliyopita, Hekalu la Laie Hawaii limewaruhusu Watakatifu kukusanyika kupokea baraka za hekaluni wakati injili ilipoanza kuenea kote ulimwenguni.

Picha
Laie Hawaii Temple rendering

Utoaji wa usanifu kutoka kwa wasanifu majengo Hyrum Pope na Harold W. Burton.

Moja ya misheni kubwa ya Kanisa la Yesu Kristo katika siku za mwisho ni kutoa baraka za hekalu kwa watu wa ulimwengu, wote walio hai na walio kufa. Nabii Joseph Smith alifundisha kwamba “kusudi la kuwakusanya … watu wa Mungu katika kipindi chochote cha ulimwengu … lilikuwa ni kumjengea Bwana nyumba ambapo Yeye angeweza kufunua kwa watu Wake ibada za nyumba Yake.”1

Mwanzoni mwa karne ya 20, mahekalu manne tu yaliyofanya kazi yalikuwepo duniani, yote yakiwa Utah. Hivyo, kusanyiko la kimwili Utah ilikuwa ndiyo njia ya msingi ya kuweza kufikia baraka za hekaluni. Mnamo 1919, hilo lilibadilika. Mnamo November 27, 1919, Rais Heber J. Grant (1856–1945) aliweka wakfu Hekalu la Laie Hawaii. Hii iliweka historia katika Urejesho pale baraka za hekaluni zilipoweza kupatikana kwa mataifa mengi.

Kwa hili, Hekalu la Laie Hawaii lilikuwa hekalu la kwanza kimataifa. Mara moja lilihudumia waumini kutoka Hawaii, New Zealand, Samoa, Tonga, Tahiti, Japan, na Australia. Wakati Kanisa lilipoendelea kukua kote katika Pasifiki na Asia, idadi ya nchi zilizobarikiwa na hekalu hili iliendelea kuongezeka.

Mwaka huu unaashiria kumbukumbu ya miaka 100 ya tukio hili muhimu la kihistoria katika kukusanya Israeli pande zote za pazia.

Kusanyiko kutoka Samoa

Visiwa vya Samoa vimejinyoosha karibia maili 2,500 (4,023 km) kutoka Hawaii. Mnamo 1919, John Q. Adams, rais wa misheni katika Samoa, alisema, “Juu ya ukamilikaji wa hekalu la Laie, watu wetu walionekana kupatwa na hamu nzito ya kukusanya bidhaa za kutosha za ulimwengu huu ili kwenda hekaluni.” Aulelio Anae, kwa mfano alikuwa ametumikia kama mmisionari bila malipo kwa miaka 20. Kwa sababu ya miaka yake ya dhabihu, hakuwa na pesa za kutosha kusafiri hadi Hawaii. Hivyo kaka Anae aliuza kila kitu alichokuwa nacho na akaweza kudunduliza $ za Marekani 600 au $700.2 Kaka Anae na Wasamoa wengine walitoa dhabihu ya kila walichoweza ili kuhamia Laie mnamo miaka ya 1920s.

Familia moja, ya Leota, ilifika Hawaii Siku ya Mwaka Mpya mnamo 1923. Vailine Leota wa miaka saba anakumbuka, “[Mtazamo] wetu wa kwanza wa hekalu … ulikuwa mtazamo mzuri kuliko yote.”3 Wiki mbili tu baadaye, wazazi wa Vailine, Aivao na Matala, walipokea endaumenti zao na waliunganishwa kama wanandoa, na watoto wao waliunganishwa kwao. Aivao na Matala Leota walitumikia kwa uaminifu katika nyumba ya Bwana kwa miaka 50 na walizikwa “karibu na hekalu walilolipenda sana.”4 Leo, mamia ya vizazi vyao waaminifu wanaishi kote katika Hawaii.

Jukumu Lisilowezekana

Wakati waumini wengi huko Pasifiki waliacha ardhi zao na kuhamia Hawaii, kata na matawi mengi kutoka mataifa tofauti yalipanga safari za makundi, zilizoitwa matembezi, kwenda hekaluni. Aina hii ya kukusanyika kiroho ilitoa njia kwa waumini wa Kanisa kusafiri ili kupokea ibada za hekaluni na kisha kurudi nyumbani kujenga Kanisa katika mataifa yao wenyewe.

Katika kuweka wakfu, Rais Grant aliomba kwa ajili ya Bwana kufungua njia kwa Watakatifu huko New Zealand na visiwa vyote vya Pasifiki na kupata vizazi vyao ili waweze kuja hekaluni na kuwa waokozi kwa mababu zao.

Matembezi kwenda hekaluni yalianza na kundi la Watakatifu wa Maori huko New Zealand miezi sita tu baada ya kuwekwa wakfu. Japokuwa ni maili 5,000 (8,045 km) mbali na Hawaii, Watakatifu hawa walishangilia kwa taarifa ya kuwekwa wakfu.

Waimate na Heeni Anaru walitamani kuwa sehemu ya kundi la kwanza kwenda hekaluni. Bado jukumu lilionekana kutowezekana kwa sababu ya umasikini wa familia na gharama zilizohitajika za paundi 1,200 za New Zealand kwa ajili ya safari—kiasi kikubwa sana. Wangehitaji muujiza.

Kwa miaka, familia ya Anaru ilifuata ushauri wa nabii na kukusanya kumbukumbu za vizazi. Kumbukumbu hizo kisha zilikaa kwenye rafu wakati familia ya Anaru wakisubiri muujiza utokee. Kijana wao, Wiwimi, alijua kuhusu imani ya wazazi wake: “Mama kamwe hakukata tamaa kwamba [asingeweza] siku moja kupiga magoti na Baba kwenye madhabahu ya hekalu.”

Muujiza ulitendeka. Waimate alishinda mkataba kutoka serikali ya New Zealand kwa ajili ya mradi mkubwa wa kuendeleza-ardhi. Kipato chake kutokana na mradi huu kilitoa kiasi cha kutosha kulipia kabla ili kukidhi gharama ya safari kwenda Hawaii. Waimate na Heeni walishinda hofu yao ya kusafiri baharini na kufika Hawaii pamoja na kundi la Watakatifu 14 mnamo Mei 1920. Walipokea endaumenti yao na kuunganishwa. Kisichowezekana kilikuwa kimewezekana.

Hadithi ya Anaru ni moja kati ya maelfu kuhusu Watakatifu wa Siku za Mwisho ambao walisafiri kwenda hekalu la Laie Hawaii kupokea ibada na kudai ahadi zilizotolewa na Bwana katika nyumba Yake. Hii ilihitaji dhabihu kubwa, lakini ilizalisha Watakatifu imara ambao walirudi katika nchi zao wakiwa wamejiandaa kuongoza Kanisa.5

Kujenga Laie

Juhudi za Kanisa za kujenga Laie ya kisasa ziliendelea kuwabariki Watakatifu wa Siku za Mwisho kote katika Pasifiki. Mnamo miaka ya 1950 na 1960, wamisionari kutoka Hawaii, Tonga, Samoa, New Zealand, Tahiti, visiwa vya Cook, Fiji, na Amerika ya Kaskazini waliitwa kusaidia kutoa talanta zao za kiutamaduni na ujuzi wa kujenga ili kusaidia kujenga Chuo cha Kanisa cha Hawaii (sasa Chuo Kikuu cha Brigham Young–Hawaii), Kituo cha Sanaa cha Polinisiani, na kituo kipya cha wageni cha hekalu. Wamisionari arobaini na saba kutoka Tonga na Samoa walipokea ibada zao za hekaluni mnamo Mei 3, 1960—mfano wa baraka za kiroho ambazo zilisindikiza kazi yao ya maisha haya (ona Kujenga Wamisionari katika Hawaii, 1960–1963, Maktaba ya Historia ya Kanisa, Jiji la Salt Lake, 100).

Mmisionari mmoja, Matte Teʻo, alichomeka vibaya kabla ya kuondoka Samoa, lakini alikuja Hawaii vivyohivyo. Madaktari walihofia mkono wake ulioungua na mweusi ungeweza kuhitaji kukatwa. Wengi wa wamisionari wenzake waliomba kwa ajili yake. Wakati wakiwa hekaluni, Kaka Teʻo alilia kwa sauti kwa Bwana, “Gusa mkono huu.” “Rekebisha mkono huu ili niweze kusaidia kidogo vyovyote niwezavyo.” Alianza kupona mara moja. Leo mkono wake hauna makovu. Sasa anatumikia kama muunganishaji katika Hekalu la Laie Hawaii na anasema, “Hekalu hili … lina ushawishi mkubwa kote katika jamii hizi si tu hapa, bali kote katika Pasifiki” (katika hadithi za Christensen, za Hekalu huko Lāʻie, Hawaiʻi, 328–330).

Kukusanyika Kiroho kutoka Asia

Kufuatia Vita vya pili vya Dunia na kujengwa upya kwa Kanisa huko Japani, Watakatifu huko waliunda matembezi ya kwanza ya hekaluni ya Asia. Mnamo 1965 ndege iliyojaa Watakatifu wenye kujitolea 165 walisafiri kutoka Tokyo mpaka Hawaii ili kupokea ibada za hekaluni. Safari hii ilileta nguvu ya ajabu kwa Kanisa huko Japani. Asilimia tisini na tano ya waumini hawa walibaki hai Kanisani. Watano baadaye walikuwa marais wa hekalu katika nchi zao, ikiwa ni pamoja na Mzee Yoshihiko Kikuchi, Kiongozi Mkuu mwenye Mamlaka wa kwanza kutoka Japani.6

Mnamo 1970 kundi la waumini wa Kikorea walisafiri kwenda Laie. Choi Wook Whan, rais wa tawi, alisema, “Tulikwenda hekaluni na ilifungua akili zetu na kutufahamisha jinsi tunavyoweza kupokea wokovu. Mpango wa milele ulikuwa halisi; shuhuda zetu zimekuwa zikiimarishwa kiasi kwamba ni vigumu kuelezea. Ni baraka kuu iliyoje kwa watu wa Korea kuwa na fursa ya kuhudhuria hekaluni.”7

Picha
Laie Hawaii Temple at night

Picha ya nakshi ya Hekalu la Hawaii kwa heshima ya Maktaba ya Historia ya Kanisa; picha ya jioni ya Hekalu la Laie Hawaii na Carla Johnson

Kukusanya Vizazi Vyetu Vilivyokufa

Wakati ibada za hekalu zinapopatikana kwa taifa, zinaleta baraka za Bwana si tu kwa wale walio hai katika nchi ile bali pia kwa wale kutoka katika taifa lile walio upande mwingine wa pazia. Baraka hii imehisiwa na waumini wa nchi za Asia, ambapo utamaduni wao kwa umakini umeweka kumbukumbu ya vizazi kwa karne nyingi.

Wazazi wa Kwai Shoon Lung walihama kutoka China kwenda Hawaii. Alizaliwa huko Kauai mnamo 1894 na kubatizwa mnamo 1944 kwenye siku yake ya kutimiza miaka 50. Kaka Lung alifundisha historia ya familia kanisani na kuliambia darasa lake, “nilipata ndoto usiku mmoja ambapo niliona wengi wa uzao wangu waliokufa wakiniita niwafanyie kazi.” Siku tatu baadaye alipokea nasaba kutoka kwa shangazi yake huko China: kurasa 22 za muswada wa Kichina ukionyesha uzao wake wa nyuma mpaka 1221 BK. Pamoja na mwanawe Glenn na mkwewe Julina, wamekamilisha maelfu ya ibada hekaluni kwa ajili ya familia yao. Glenn na Julina Lung baadaye walitumikia kwa uaminifu kama rais na mlezi wa Hekalu la Laie toka 2001 hadi 2004.8

Hati ya Kukunja Ambayo Haikuweza Kuungua

Michie Eguchi alikuja Hawaii kutoka Japani mapema miaka ya 1900 na alibeba pamoja naye hati ya hariri ya kukunja ya Kijapani. Mjukuu wake Kanani Casey alitumikia misheni Japani na baadaye aligundua kwamba hati ya kukunja ya bibi yake ilinakili uzao wa familia yake kurudi nyuma takriban miaka elfu moja.

Mnamo 2013, nyumba ya Kanani iliungua yote. Yeye na familia yake walipoteza karibu kila kitu kwenye moto. Walikuwa wametunza nasaba yao ndani ya mabeseni ya plastiki chini ya kitanda chao. Baada ya moto, walirudi kwenye nyumba, walichokuta ni mlima wa majivu na moshi.

“Kitu pekee ambacho hasa nilitumaini kupata ilikuwa ni nakala ya hati ya kukunja na tafsiri yake na historia,” Kanani alisema. “Nilihakikishiwa tena kwamba kazi yote ya hekaluni ilikuwa imekwisha fanywa kwa ajili ya mababu zangu wa Kijapani, lakini nakala ya hati ya kukunja ilikuwa na thamani kubwa kwangu.”

Wakati Kanani na mumewe, Billy, walipopita katikati ya majivu, hatimaye walipata mfuko wa plastiki wa samawati. Ndani ya mfuko, walipata nakala ya hati ya kukunja, sambamba na tafsiri na kitabu cha historia ya familia, kwa mshangao ikiwa salama. Hati ya kukunja ilikuwa imeungua kidogo kuzunguka pembezoni, lakini ilikuwa ndicho kitu pekee katika chumba chao cha kulala ambacho kilinusurika.

Kanani anahisi Bwana alihifadhi hati ya kukunja “kwa manufaa ya uzao wangu kama ushahidi wa upendo wake kwetu na kuonyesha umuhimu wa kufanya kazi ya historia ya familia na hekalu” (katika Christensen, Hadithi za Hekalu huko Lāʻie, Hawaiʻi, 172–74).

Kukusanyika kupitia Elimu

Baraka za Hekalu la Laie Hawaii zimenyooshwa pia kwa wale ambao wamekusanyika Laie kupata elimu ya juu. Tangu miaka ya 1950, makumi elfu ya wanafunzi wamekuja kwenye kile ambacho sasa ni Chuo Kikuu cha Brigham Young–Hawaii kutoka kote Polinisia na Asia. Wengi wa wanafunzi hawa wamefanya ubatizo kwa ajili ya wafu na kutumikia kama wafanyakazi wa ibada za hekaluni. Hekalu la Laie limesaidia wanafunzi kujenga upendo kwenye kazi ya historia ya familia na hekalu na limewabariki kujiandaa vyema kutumikia wakati mahekalu yanapokuja kwenye nchi zao.

Choon Chua James, mzaliwa wa Singapore, alikuja Chuo Kikuu cha Brigham Young–Hawaii mnamo miaka ya 1970 akiwa na dada yake. Wote wawili waliolewa na wanaume kutoka nchi zingine mnamo 1978. Dada James alikumbuka,”Ndoa yetu ndani ya hekalu la Laie ilileta waongofu wawili na tamaduni mbili pamoja kwa muda na milele yote—mwanzo wa kile tunachotumaini kitakuwa urithi wa muda mrefu wa baraka za hekalu katika familia yetu. Zetu ni mbili tu kati ya mamia mengi ya ndoa za milele zinazohusisha wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Brigham Young–Hawaii ambazo zimefungwa ndani ya hekalu la Laie, pengine moja ya urithi wake mkubwa kwa zaidi ya miaka sitini iliyopita ya kuwepo kwa chuo kikuu” (katika Christensen, Hadithi za Hekalu katika Lāʻie, Hawaiʻi, 236).

Kukusanyika Kunaendelea

Likiwa kwenye njia panda ya Pasifiki kati ya Amerika na Asia, Hekalu la Laie Hawaii limefungua mlango wa baraka za hekalu kwa mataifa mengi. Hivyo, kukusanyika kwa Israeli kukawa kimsingi kukusanyika kiroho wakati waumini wanapoweza kupokea baraka za hekalu na kisha kurudi ili kujenga Kanisa katika nchi zao za asili. Fursa hii imesaidia kuenea kwa injili ya urejesho kwa tamaduni nyingi na watu wengi katika pande zote za pazia.

Tunaposherehekea maadhimisho ya miaka 100 ya Hekalu la Laie Hawaii, tunapata fursa ya kushuhudia tukio muhimu katika Urejesho na kutimia kwa unabii wa nabii Yakobo katika Kitabu cha Mormoni: “Kubwa ni ahadi za Bwana kwa wale walio kwenye visiwa vya bahari” (2 Nefi 10:21).

Muhtasari

  1. Mafundisho ya Marais wa Kanisa: Joseph Smith (2007), 416.

  2. Ona James Adams Argyle, comp., “The Writings of John Q. Adams,” 14, FamilySearch.org.

  3. Vailine Leota Niko, katika Clinton D. Christensen, comp. Stories of the Temple in Lāʻie, Hawaiʻi (2019), 70–71.

  4. Aivao Frank Leota (1878–1966), FamilySearch.org.

  5. Ona Christensen, Stories of the Temple in Lāʻie, Hawaiʻi, 64–65.

  6. Ona Christensen, Stories of the Temple katika Lāʻie, Hawaiʻi, 114–17.

  7. Choi Wook Whan, katika “Going to the Temple Is Greatest Blessing,” Church News, Apr. 17, 1971, 10.

  8. Ona Christensen, Stories of the Temple in Lāʻie, Hawaiʻi, 166.

Chapisha