Sitaki Kuwa Tofauti!
Mwandishi anaishi Utah, Marekani.
“Thamani ya nafsi ni kubwa mbele za Mungu” (Mafundisho na Maagano 18:10).
Mika siku zote alitazamia darasa la dansi. Alipenda kusikiliza muziki. Alipenda kufanyia mazoezi mruko wake wa kipepeo na kufanya hivyo kwa usahihi. Na alipenda hasa wakati darasa lote lilipopiga hatua pamoja. Wakati walipofanya hivyo, ilikuwa ni kama wacheza dansi wote walikuwa wanafanana. Ilikuwa ni kama hakuwa pekee mwenye Down syndrome.
Leo walikuwa wakijifunza hatua mpya ya dansi. Mika alimtazama mwalimu wake akiruka hewani. Aliwatazama wasichana wengine wakijaribu. Baadhi walipatia mara moja. Baadhi walijaribu mara kadhaa. Mika alijaribu tena na tena, lakini hakuweza kupatia.
“Unaweza kunisaidia, mwalimu?” Mika aliuliza.
Msichana pembeni yake alimtazama Mika. Kisha akamgeukia rafiki yake aliyekuwa pembeni. “Kwa nini anazungumza hivyo?” alinong’ona. Wasichana wote wawili waligeuka na kumtazama Mika.
Njiani kuelekea nyumbani baada ya darasa, Mika alikuwa kimya njia nzima.
Walipofika nyumbani, Mama alikuwa akikanda kinyunya jikoni. Alikuwa na unga kwenye shavu. Wakati mwingine hilo lilimfanya Mika acheke. Lakini leo alidondosha tu mkoba wake sakafuni na kuzama ndani ya kiti mezani.
“Dansi ilikuwaje?” Mama aliuliza.
“Mbaya,” Mika alisema. “Niliomba kusaidiwa, na msichana akasema nazungumza vya kuchekesha. Kisha akanitazama kwa mshangao.” Mika alitazama chini. “Sitaki kwenda tena kwenye dansi.”
“Jamani, Mika!” Mama alisema. “Pole. Mimi na baba tunapenda kukutazama ukidansi. Tunaona fahari kwa juhudi yako kubwa!”
Mika alihisi machozi yakimlenga. “Sipendi Down syndrome ndani yangu. Sipendi kwamba uso wangu uko tofauti. Natamani isingekuwa vigumu kwangu kujifunza mambo mapya. Napaswa kufanyia mazoezi hata kuzungumza!”
Baba aliketi pembeni ya Mika na kuweka mkono wake kumzunguka. “Mika, tunakupenda sana. Hatungeweza kubadili kitu kimoja kuhusu wewe.”
Lakini Mika alitikisa tu kichwa chake na kuficha uso wake kwa mikono yake. “Sitaki kuwa tofauti. Nataka Down syndrome yangu iondolewe kwangu!”
Mama na Baba walikuwa kimya kwa muda.
“Nina wazo,” Mama alisema. Mika alichungulia kupitia upenyo wa mikono yake. “Kwa nini usiombe na kumuuliza Baba wa Mbinguni jinsi Yeye anavyohisi kuhusu wewe?”
Mika alifikiria kuhusu hilo. Alipenda kuomba. Taratibu, alikubali kwa kichwa. “Unaweza kuandika swali ili niweze kukumbuka nini cha kuomba?”
Mama aliandika swali. Kisha Mika alichukua karatasi na kwenda chumbani kwake kuomba.
Wakati aliporudi jikoni dakika chache baadaye, uso wa Mika ulikuwa uking’aa kama mwanga wa balbu. “Baba wa Mbinguni amejibu!” alisema.
“Amesema nini?” Mama aliuliza.
“Amesema, Mika, nakupenda jinsi ulivyo,’” Mika alisema. “Na Yeye amesema hivyo kwa sauti KUBWA!”
Wiki iliyofuata kwenye dansi, Mika hakuhofia kile wasichana wengine walichofikiria kuhusu Down syndrome yake. Badala yake, alimwona msichana mwingine, Sara, ambaye alionekana mwenye huzuni. Sara alikuwa na wakati mgumu kujifunza hatua mpya pia.
Mika aliporudi nyumbani, aliamua kumuandikia Sara ujumbe. Alichora picha nyingi za moyo. Mama alimsaidia kwenye matamshi.
“Mpendwa Sara,” Mika aliandika. “Wewe ni mcheza dansi mzuri. Ninataka kuwa rafiki yako. Ninafurahi upo kwenye darasa langu la dansi.”
Mika hakutaka kuchelewa kumpa Sara ujumbe. Alitaka Sara ahisi furaha na kupendwa kwenye dansi pia.