Mlango wa 2
Ukombozi unatokana na Masiya Mtakatifu—Uhuru wa kuamua ni muhimu kwa kuishi na kwa maendeleo—Adamu alianguka ili wanadamu wawe—Wanadamu wako huru kuchagua uhuru na uzima wa milele. Karibia mwaka 588–570 K.K.
1 Na sasa, Yakobo, ninasema nawe: Wewe ndiye mzaliwa wa kwanza wangu katika siku za taabu yangu nyikani. Na tazama, katika utoto wako umeteseka kwa masumbuko na huzuni nyingwa sababu ya ujeuri wa ndugu zako.
2 Walakini, Yakobo, mzaliwa wa kwanza wangu nyikani, wewe unajua ukuu wa Mungu; na ataweka wakfu masumbuko yako kwa faida yako.
3 Kwa hivyo, nafsi yako itabarikiwa, na wewe utaishi salama na kaka yako, Nefi; na utamtumikia Mungu wako maishani mwako. Kwa hivyo, najua kwamba wewe umekombolewa, kwa sababu ya haki ya Mkombozi wako; kwani wewe umeona kwamba katika wakati mtimilifu yeye atakuja kuwaletea wanadamu wokovu.
4 Na wewe umeona ujanani mwako utukufu wake; kwa hivyo, wewe umebarikiwa kama wale atakaowahudumia katika mwili; kwani Roho ni sawa, jana, leo, na milele. Na njia imetayarishwa tangu kuanguka kwa mwanadamu, na wokovu ni bure.
5 Na wanadamu wanashauriwa kikamilifu kwamba wajue mema na maovu. Na wanadamu wanapewa sheria. Na hakuna yeyote anayekubalika kwa sheria; au, kwa sheria wanadamu wanatengwa. Ndiyo, walitengwa kwa sheria ya muda; na pia, kwa sheria ya kiroho wanaangamizwa kutokana na yale yalio mema, na wanadhoofika milele.
6 Kwa hivyo, ukombozi unakuja kupitia Masiya Mtakatifu; kwani amejaa neema na kweli.
7 Tazama, anajitoa kuwa dhabihu ya dhambi, kutimiza masharti ya sheria, kwa wale wote wenye moyo uliopondeka na roho iliyovunjika; na hakuna mwingine yeyote anayeweza kutimiza masharti ya sheria.
8 Kwa hivyo, ni muhimu sana kuwajulisha wakazi wa dunia kuhusu vitu hivi, ili wajue hakuna binadamu anayeweza kuishi karibu na Mungu, bila fadhila, na rehema, na neema za Masiya Mtakatifu, ambaye anatoa maisha yake mwilini, na kuyachukua tena kwa uwezo wa Roho, ili alete ufufuo wa wafu, akiwa wa kwanza kufufuka.
9 Kwa hivyo, yeye ni malimbuko kwa Mungu, kwani atawaombea watoto wa watu wote; na wale watakaomwamini wataokolewa.
10 Na kwa sababu ya maombi kwa wote, watu wote wanamjia Mungu; kwa hivyo, wanasimama kwenye uwepo wake, ili kuhukumiwa na yeye kulingana na ukweli na utakatifu ulioko ndani yake yeye. Kwa hivyo, masharti ya sheria ambayo yule Mtakatifu ametoa, yatalingana na adhabu na mapigo yake, adhabu hii ni kinyume cha furaha ya kutii amri, ili kutimiza masharti ya upatanisho—
11 Kwani lazima, kuwe na upinzani katika mambo yote. Kama sio hivyo, mzaliwa wa kwanza wangu nyikani, haki haingeweza kupatikana, wala uovu, wala utakatifu au taabu, wala uzuri au ubaya. Kwa hivyo, mambo yote lazima yawe kitu kimoja; kwa hivyo, kama ni kitu kimoja lazima kikae kama kimekufa, bila uhai wala kifo, si uharibifu wala kutoharibika, si furaha wala taabu, si kufahamu wala kutofahamu.
12 Kwa hivyo, itakuwa kwamba kiliumbwa bure; kwa hivyo itakuwa kwamba hakuna kusudi la kuumbwa kwake. Kwa hivyo, kitu hiki kinaangamiza hekima ya Mungu na makusudi yake ya milele, na pia nguvu, na rehema, na haki ya Mungu.
13 Na kama mtasema hakuna sheria, mtasema pia hakuna dhambi. Kama mtasema hakuna dhambi, mtasema pia hakuna haki. Na kama hakuna haki hakuna furaha. Na kama hakuna haki wala furaha basi hakuna adhabu wala huruma. Na kama vitu hivi havipo basi hakuna Mungu. Na kama hakuna Mungu basi sisi hatupo, wala dunia; kwani hakungekuwa na uumbaji wa vitu, wala kutenda au kutendewa; kwa hivyo, vitu vyote lazima vingetokomea.
14 Na sasa, wana wangu, nawaambia vitu hivi kwa faida yenu na elimu; kwani kuna Mungu, na ameumba vitu vyote, mbingu na dunia, na vitu vyote vilivyomo, vitu vya kutenda na vitu vya kutendewa.
15 Na kutimiza makusudio yake ya milele katika kikomo cha mwanadamu, baada ya kuumba wazazi wetu wa kwanza, na wanyama wa porini na ndege wa hewani, na mwishowe, vitu vyote vilivyoumbwa, ilibidi lazima kuwe na upinzani, hata tunda lililokataliwa kinyume cha mti wa uzima; mmoja ukiwa mtamu na mwingine ukiwa chungu.
16 Kwa hivyo, Bwana Mungu amemruhusu mwanadamu kujitendea mwenyewe. Kwa hivyo, mwanadamu hangeweza kujitendea mwenyewe bila kuvutiwa na moja au nyingine.
17 Na mimi, Lehi, kulingana na mambo ambayo nimesoma, lazima niwaze kwamba malaika wa Mungu, kulingana na lile lililoandikwa, alianguka kutoka mbinguni; kwa hiyo, akawa ibilisi, kwani alitafuta kile ambacho kilikuwa ni uovu mbele za Mungu.
18 Na kwa sababu alianguka kutoka mbinguni, na kuhuzunika milele, aliwatakia wanadamu nao pia wahuzunike. Kwa hivyo, akamwambia Hawa, ndiyo, hata yule nyoka wa zamani, ambaye ni ibilisi, ambaye ni baba wa uwongo wote, kwa hivyo akasema: Kuleni tunda lililokatazwa, na hamtakufa, lakini mtakuwa kama Mungu, mkifahamu mema na maovu.
19 Na baada ya Adamu na Hawa kula tunda lililokatazwa walifukuzwa kutoka bustani ya Edeni, ili walime ardhi.
20 Na wamezaa watoto; ndiyo, hata jamii ya dunia yote.
21 Na maisha ya watoto wa watu yaliongezewa, kulingana na nia ya Mungu, ili waweze kutubu wakiwa hai; kwa hivyo, hali yao ikawa hali ya majaribio, na wakati wao ukaongezewa, kulingana na amri ambazo Bwana Mungu aliwapatia watoto wa watu. Kwani alitoa amri kwamba lazima wanadamu wote watubu; kwani alionyesha wanadamu wote kwamba walipotea, kwa sababu wazazi wao walivunja sheria.
22 Na sasa, tazama, kama Adamu hangevunja sheria hangeanguka, bali angeishi katika bustani ya Edeni. Na vitu vyote vilivyoumbwa vingebaki katika hali yao ya kwanza baada ya kuumbwa; na vingebaki vivyo hivyo milele, na kuwa bila mwisho.
23 Na hawangezaa watoto; na hivyo wangeishi katika hali ya kitoto, bila shangwe, kwani hawakufahamu dhiki; bila kutenda mema, kwani hawakujua dhambi.
24 Lakini tazama, vitu vyote vimetendwa kwa hekima ya yule ajuaye vitu vyote.
25 Adamu alianguka ili wanadamu wawe; na wanadamu wapo, ili wapate shangwe.
26 Na Masiya anakuja katika wakati mtimilifu, ili awakomboe watoto wa watu kutokana na mwanguko. Na kwa sababu wamekombolewa kutokana na mwanguko wamekuwa huru milele, wakielewa mema na maovu; kujitendea wenyewe na sio kutendewa, ila tu katika kuadhibiwa na sheria katika siku ile kuu ya mwisho, kulingana na amri ambazo Mungu amezitoa.
27 Kwa hivyo, wanadamu wana uhuru wanapoishi; na wamepewa vitu vyote ambavyo ni muhimu kwa mwanadamu. Na wana haki kuchagua uhuru na uzima wa milele, kupitia yule Mpatanishi mkuu wa wanadamu wote, au kuchagua utumwa na kifo, kulingana na utumwa na nguvu za ibilisi; kwani anataka wanadamu wote wawe na dhiki kama yeye.
28 Na sasa, wana wangu, ningetaka mtazame yule Mpatanishi mkuu, na msikilize amri zake kuu; na muwe waaminifu kwa maneno yake, na mchague uzima wa milele, kulingana na mapenzi ya Roho Mtakatifu wake.
29 Na msichague kifo cha milele, ambacho ni kulingana na nia ya mwili na uovo ulio ndani yake, ambayo inaipatia roho ya ibilisi nguvu za kuteka nyara, na kukuleta jehanamu, ili awatawale katika ufalme wake.
30 Nimewazungumzia ninyi nyote, wana wangu, maneno haya machache, katika siku zangu za mwisho za majaribio; na nimechagua sehemu njema, kulingana na maneno ya nabii. Na sina lengo lingine lolote ila ustawi wenu usio na mwisho wa nafsi zenu. Amina.