Sehemu ya 136
Neno na mapenzi ya Bwana, yaliyotolewa kupitia Rais Brigham Young huko katika Makazi ya Winter Quarters, ya kambi ya Israeli, Nchi ya Omaha, juu ya kingo za magharibi za Mto Missouri, karibu na Council Bluffs, Iowa.
1–16, Namna kambi ya Israeli inavyopaswa kuundwa kwa ajili ya safari ya kuelekea magharibi yaelezwa; 17–27, Watakatifu wanaamriwa kuishi kulingana na kanuni nyingi za injili; 28–33, Watakatifu yawapasa kuimba, kucheza, kuomba, na kujifunza hekima; 34–42, Manabii wanauawa ili wapate kuheshimiwa na waovu wahukumiwe.
1 Neno na Mapenzi ya Bwana juu ya Kambi ya Israeli katika safari zao za kwenda Magharibi:
2 Acheni watu wote wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho, na wale wanaosafiri pamoja nao, wawekwe katika makundi, kwa agano na ahadi ya kuzishika amri zote na sheria za Bwana Mungu wetu.
3 Acheni makundi yaundwe kwa maakida wa mamia, maakida wa hamsini, na maakida wa makumi, pamoja na rais na washauri wake wawili juu ya vichwa vyao, chini ya maelekezo ya Mitume Kumi na Wawili.
4 Na hili litakuwa agano letu—kwamba tutatembea katika maagizo yote ya Bwana.
5 Acheni kila kundi lijitegemee lenyewe kwa mafahari wote, magari ya kukokota mizigo, vyakula, mavazi, na mahitaji mengine muhimu kwa safari, yale wawezayo kupata.
6 Wakati makundi hayo yawapo tayari na waondoke kwa nguvu zao, kuwaandalia wale watakaosalia.
7 Acheni kila kundi, pamoja na maakida wao na marais, waamue ni wangapi wanaweza kwenda wakati wa majira ya kuchipua yajayo; halafu chagueni idadi ya kutosha ya watu wenye nguvu na wataalamu, kuchukua mafahari wa kulima, mbegu, na zana za kulimia, kwenda kama watangulizi wa kutayarisha kwa ajili ya kupanda mazao ya majira ya kuchipua.
8 Acheni kila kikundi kibebe uzito sawa, kulingana na mgawanyo wa mali zao, katika kuwachukua maskini, wajane, wasio na baba, na familia za wale ambao wameenda vitani, ili vilio vya wajane na wasio na baba visije masikioni mwa Bwana dhidi ya watu hawa.
9 Acheni kila kikundi kitengeneze nyumba, na mashamba kwa ajili ya kuotesha nafaka, kwa ajili ya wale ambao watabakia nyuma majira haya; na haya ndiyo mapenzi ya Bwana juu ya watu wake.
10 Acheni kila mtu atumie uwezo wake wote na mali yake kuwapeleka watu hawa mahali ambapo Bwana atapachagua kuwa kigingi cha Sayuni.
11 Na kama mtafanya hili kwa moyo safi, katika uaminifu wote, mtabarikiwa; mtabarikiwa katika mifugo yenu, na katika wanyama wenu, na katika mashamba yenu, na katika nyumba zenu, na katika familia zenu.
12 Acheni watumishi wangu Ezra T. Benson na Erastus Snow waunde kikundi.
13 Acheni watumishi wangu Orson Pratt na Wilford Woodruff waunde kikundi.
14 Pia, acheni watumishi wangu Amasa Lyman na George A. Smith waunde kikundi.
15 Na wateueni marais, na maakida wa mamia, na wa hamsini, na wa makumi.
16 Acheni watumishi wangu ambao nimewatuma na waende na kufundisha haya, mapenzi yangu, kwa watakatifu, ili wapate kuwa tayari kwenda kwenye nchi ya amani.
17 Enendeni zenu na mkafanye kama nilivyowaambia, na msiwaogope maadui zenu; kwani hawatakuwa na uwezo wa kuisimamisha kazi yangu.
18 Sayuni itakombolewa katika wakati wangu mwenyewe.
19 Na kama mtu yeyote atatafuta kujijenga mwenyewe, na hatafuti ushauri wangu, hatakuwa na uwezo, na upumbavu wake utadhihirishwa.
20 Tafuteni; na timizeni ahadi zenu wenyewe kwa wenyewe; na usitamani kile kilicho cha ndugu yako.
21 Msifanye uovu kwa kulitamka ovyo jina la Bwana, kwani Mimi ndiye Bwana Mungu wenu, hata Mungu wa baba zenu, Mungu wa Ibrahimu na wa Isaka na wa Yakobo.
22 Mimi ndiye niliye waongoza wana wa Israeli kutoka nchi ya Misri; na mkono wangu umenyooshwa katika siku hizi za mwisho, kuwaokoa watu wangu wa Israeli.
23 Acheni kugombana ninyi kwa ninyi; acheni kuneneana vibaya.
24 Acheni ulevi; na acheni maneno yenu yawe ya kujengana.
25 Kama ukiazima cha jirani yako, wewe utakirejesha kile ulichoazima; na kama huwezi kulipa basi nenda moja kwa moja na kumwambia jirani yako, asije akakuhumu.
26 Kama utakiona kitu cha jirani yako alichokipoteza, wewe fanya bidii ya kumtafuta mwenyewe na kumrudishia tena.
27 Utafanya bidii katika kutunza kile ulichonacho, ili upate kuwa mtumishi mwenye busara; kwani hiyo ni zawadi kutoka kwa Bwana Mungu wako, nawe ni mtumishi wake.
28 Kama mmefurahi, msifuni Bwana kwa kuimba, kwa kinubi, kwa kucheza, na kwa sala ya kusifu na kutoa shukrani.
29 Kama mna huzuni, mlinganeni Bwana Mungu wenu, kwa maombi ya dhati, ili mioyo yenu ipate kufurahi.
30 Msiwaogope maadui zenu, kwa kuwa wapo mikononi mwangu na nitawafanya nipendavyo.
31 Watu wangu ni lazima wajaribiwe katika mambo yote, ili wapate kutayarishwa kupokea utukufu ule nilionao kwa ajili yao, hata utukufu wa Sayuni; naye yule ambaye hatastahimili kurudiwa haustahili ufalme wangu.
32 Acheni yule ambaye hana maarifa ajifunze hekima kwa kujinyenyekeza mwenyewe na kumlingana Bwana Mungu wake, ili macho yake yapate kufunguliwa ili apate kuona, na masikio yake kufunguliwa ili apate kusikia;
33 Kwani Roho yangu imetolewa ulimwenguni kuwaangaza wanyenyekevu na waliopondeka, na kwa kuwahukumu wasio mcha Mungu.
34 Ndugu zenu wamewakataa ninyi na ushuhuda wenu, hata taifa lile lililowafukuzeni;
35 Na sasa yaja siku ya msiba wao, hata siku za huzuni, kama mwanamke ambaye amechukuliwa katika utungu; na huzuni yao itakuwa kuu isipokuwa watubu haraka, ndiyo, haraka sana.
36 Kwani waliwaua manabii, na wale waliotumwa kwao; nao wamemwaga damu isiyo na hatia, ambayo hulia kutoka ardhini dhidi yao.
37 Kwa hiyo, msishangazwe na mambo haya, kwani ninyi bado hamjawa safi; bado hamwezi kustahimili utukufu wangu; lakini mnaweza kuuona kama mtakuwa waaminifu katika kuyashika maneno yangu ambayo nimeyatoa kwenu, kutoka siku za Adamu hadi Ibrahimu, kutoka Ibrahimu hadi Musa, kutoka Musa hadi Yesu na mitume wake, na kutoka Yesu na mitume wake hadi kwa Joseph Smith, ambaye nilimwita kupitia malaika zangu, watumishi wangu wahudumu, na kwa sauti yangu mimi mwenyewe kutoka mbinguni, kuianzisha kazi yangu;
38 Msingi ambao aliuweka, naye alikuwa mwaminifu; nami nimemchukua kwangu.
39 Wengi wamestaajabu kwa sababu ya kifo chake; lakini ilikuwa muhimu kwamba lazima atie muhuri ushuhuda wake kwa damu yake, ili apate kuheshimiwa na waovu wapate kuhukumiwa.
40 Je, sijawakomboa ninyi kutokana na maadui zenu, katika hilo tu nimeacha ushahidi wa jina langu?
41 Sasa, kwa hiyo, sikilizeni, Enyi watu wa kanisa langu; nanyi wazee sikilizeni kwa pamoja; mmeupokea ufalme wangu.
42 Kuweni na bidii katika kuzishika amri zangu zote, isije hukumu ikaja juu yenu, na imani yenu ikawatindikia, na maadui zenu wakapata ushindi juu yenu. Hivyo hakuna la zaidi kwa sasa. Amina na Amina.