2010–2019
Kuitwa katika Utumishi
Aprili 2017


16:13

Kuitwa katika Utumishi

Jukumu la kuhudumu katika sehemu mahususi ni la msingi na muhimu, lakini linafuata baada ya wito katika utumishi.

Rais Monson, tunafurahia sana kusikia sauti yako na kupokea maelekezo yako. Tunakupenda, tunakukubali, na daima tunakuombea.

Naomba usaidizi wa Roho Mtakatifu tunapofikiria pamoja kanuni zihusuzo kazi kuu ya kuhubiri injili kwa kila taifa, kabila, ndimi, na watu.1

Kuitwa katika Utumishi na Kupangiwa Kazi.

Kila mwaka makumi elfu ya vijana wa kiume na wa kike na wanandoa wengi wazee, kwa hamu hutarajia kupokea barua maalumu kutoka Jijini Salt Lake. Yaliyomo katika barua milele humwathiri mtu ambaye ametumiwa vile vile wana familia na idadi kubwa ya watu wengine. Inapofika, bahasha yaweza kufunguliwa kwa uangalifu na subira au kuchanwa kwa furaha na kwa haraka kubwa. Kusoma barua hii maalumu ni tukio lisilo sahaulika kamwe.

Barua husainiwa na Rais wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho, na sentensi mbili za mwanzo husomeka kama ifuatavyo: “Umeitwa kutumikia kama mmisionari wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho. Umepangiwa kutumikia katika Misheni ya_________________.”

Tafadhali kumbuka kwamba sentensi ya kwanza ni wito wa kutumikia kama mmisionari katika Kanisa la Bwana lililorejeshwa. Sentensi ya pili huonyesha kazi ya kufanya na sehemu mahususi ya misheni. Tofauti muhimu inayoonyeshwa katika sentensi hizi mbili ni muhimu kwetu sote kuelewa.

Katika utamaduni wa Kanisa, mara kwa mara tunaongea kuhusu kuitwa kutumikia katika nchi kama vile Argentina, Uholanzi, Korea na Marekani. Lakini mmisionari haitwi mahali, bali huitwa kutumikia. Kama Bwana alivyotangaza kwa Nabii Joseph Smith mnamo 1829, “Kama unayo tamaa ya kumtumikia Mungu umeitwa kwenye kazi hiyo.”2

Kila wito wa misheni na upangiwaji mahali pa kazi, au baadaye kupangiwa upya mahali, ni matokeo ya ufunuo kupitia watumishi wa Bwana. Wito katika utumishi huja kutoka kwa Mungu kupitia kwa Rais wa Kanisa. Kupangiwa mahali pa kazi kwenye mojawapo ya zaidi ya misheni 400 zinazofanya kazi kwa sasa kote ulimwenguni huja kutoka kwa Mungu kupitia kwa mmoja wa washiriki wa Akidi ya Mitume Kumii na Wawili, akitenda kwa kupewa mamlaka na Nabii wa Bwana anayeishi. Vipawa vya kiroho vya unabii na ufunuo hutumika katika miito yote ya misheni na upangaji wa maeneo ya kazi.

Sehemu ya 80 ya Mafundisho na Maagano ni kumbukumbu ya wito wa misheni kwa Stephen Burnett uliotolewa na Nabii Joseph Smith mnamo 1832. Kujifunza wito huu wa kaka Burnett kunaweza kutusaidia (1) kuelewa kwa uhakika tofauti kati ya “kuitwa katika utumishi” kama mmisionari na “kupangiwa kufanya kazi” katika sehemu husika na (2) kuelewa vyema kwa ukamilifu kabisa jukumu letu binafsi na uteuzi wa kiungu wa kutangaza injili.

Mstari  wa 1 wa sehemu hii ni wito wa kutimikia: “Amini, Bwana asema hivi kwako wewe mtumishi wangu Stephen Burnett: Nenda wewe, nenda wewe ulimwenguni na ukahubiri injili kwa kila kiumbe kitakachokuwa chini ya sauti yako.”3

Cha kushangaza, mstari  wa 2 unamwelezea Ndugu Burnett kuhusu mwenzi mmisionari aliyepangiwa: “Na kwa vile unataka mwenza, nitakupa mtumishi wangu Eden Smith.”4

Mstari wa 3 huonyesha wapi hawa wamisionari wawili wangefanya kazi: “Kwa hivyo enendeni na mkaihubiri injili yangu, iwe kaskazini au kusini, mashariki au magharibi, si kitu Kwa hiyo nendeni, kwani hamwezi kukosea.”5

Siamini kifungu cha maneno “si kitu” kama yalivyotumiwa na Bwana katika maandiko haya, humaanisha kwamba Hajali wapi watumishi wake hufanya kazi. Kwa kweli, Hujali kiundani. Lakini kwa sababu kazi ya kuhubiri injili ni kazi ya Bwana, hushawishi, huongoza na kuelekeza watumishi wake aliowapa mamlaka. Kadiri wamisionari wanavyojitahidi kuwa zaidi wenye kustahili na kuweza kuwa vifaa vinavyofaa katika mikono yake na kufanya kwa uwezo wao wote kutimiza majukumu yao, kwa uaminifu, ndipo kwa msaada Wake “hawawezi kukosea”—popote wanapohudumu. Pengine moja ya masomo Mwokozi anatufundisha katika ufunuo huu ni kwamba jukumu la kutumikia katika sehemu mahususi ni la msingi na muhimu lakini linafuatia baada ya wito katika utumishi.

Mstari unaofuata huonyesha wazi sifa muhimu kwa wamisionari wote: “Kwa sababu hiyo, yatangazeni mambo ambayo mmeyasikia, na hakika kuyaamini, na kujua ni ya kweli.6

Mstari wa mwisho humkumbusha Ndugu Burnett na sisi sote ambao kutoka kwake wito wa kutumikia huja: “Tazama, haya ndiyo mapenzi yake yeye aliyewaita ninyi, Mkombozi wenu, hata Yesu Kristo. Amina.”7

Kushinda Kutokuelewa.

Baadhi yenu mnaweza kujiuliza kwa nini nimechagua kujadili katika kipindi cha ukuhani cha mkutano mkuu hii inayoonekana tofauti ya kawaida kati ya kuitwa katika utumishi na kupangiwa eneo la kufanya kazi. Jibu langu kwa swali lenu ni dhahiri kabisa: uzoefu wangu umenifundisha kwamba kanuni hizi hazieleweki vizuri kwa waumini wengi wa kanisa.

Sababu moja kuu ya kuongelea suala hili ni kile nilichojifunza kwa muda mrefu kuhusu dukuduku, hofu na hata hisia ya hatia iliyohisiwa na wamisionari wengi ambao kwa sababu mbalimbali walipangiwa upya maeneo tofauti ya kazi wakati wa kipindi chao cha kutoa huduma. Kupangiwa upya huko wakati mwingine ni muhimu kwa sababu ya matukio na hali kama vile ajali za kimwili na madhara, kucheleweshwa na changamoto za kupata viza, hali mbaya ya kisiasa, kuanzishwa na kujaza misheni mpya au mzunguko na mabadiliko ya mahitaji ulimwenguni kote katika kazi ya kutangaza injili.8

Wakati mmisionari anapopangiwa upya kwenye eneo tofauti la kazi, mchakato ni sawasawa kama upangaji wa kwanza. Washiriki wa Akidi ya wale Kumi na Wawili hutafuta mwongozo wa kiungu na mwongozo mwingine katika kufanya yote yahusuyo kupanga upya.

Hivi karibuni nimeongea na mwanaume mwaminifu aliyenishiriki hisia za ndani ya moyo wake. Katika mkutano fulani, nilikuwa nimeelezea tofauti kati ya kuitwa katika utumishi na kupangiwa kazi. Kaka huyu mzuri alinipa mkono na kwa machozi machoni mwake aliniambia, “mambo uliyonisaidia kujifunza leo yameinua mzigo kutoka mabegani mwangu mzigo ambao nimeubeba kwa zaidi ya miaka 30. Kama mmisionari kijana, eneo nililopangiwa mwanzo lilikuwa ni kutumikia katika eneo la Amerika ya Kusini. Lakini sikuweza kupata viza, hivyo eneo langu la kazi lilibadilishwa kuwa katika Marekani. Miaka yote hii nimejiuliza kwa nini sikuweza kutumikia mahali ambapo nilikuwa nimeitwa. Sasa najua niliitwa kwenye kazi na siyo mahali. Siwezi kuelezea jinsi gani uelewa huu umenisaidia.

Moyo wangu uliumia kwa ajili ya mwanaume huyu mzuri. Kadiri nilivyofundisha kanuni hizi muhimu ulimwenguni kote, watu wasio na idadi wamenieleza kwa siri hisia sawa kama za mwanaume niliyemwelezea punde. Ninashughulikia mada hii leo kwa sababu hakuna hata muumini mmoja wa kanisa hili anapaswa kubeba mzigo usio wa lazima wa kutokuelewa, shaka, maumivu ya moyo au hatia kuhusu eneo la kufanya kazi.

“Kwa hivyo enendeni na mkaihubiri injili yangu, iwe kaskazini au kusini, mashariki au magharibi, si kitu Kwa hiyo nendeni, kwani hamwezi kukosea.”9 Mnapotafakari maneno ya andiko hili na kufungua mioyo yenu, natumaini na kuomba mtamwalika Roho Mtakatifu kupeleka ndani kabisa ya nafsi zenu uelewa, uponyaji, na urejesho mnaoweza kuhitaji.

Sababu moja ya ziada ninajisikia kuvutiwa kujadili mada hii ni uzoefu wangu binafsi wa kuwapangia maeneo wamisionari kwa miaka mingi. Kwa Kumi na Wawili, hakuna kinachothibitisha uhalisia wa muendelezo wa ufunuo wa siku za mwisho kwa nguvu zaidi ya kutafuta kujua mapenzi ya Bwana wakati tunapotimiza majukumu yetu ya kuwapangia wamisionari maeneo yao husika ya kazi. Ninatoa ushahidi kwamba Mwokozi anajua na anamjali kila mmoja wetu “mmoja mmoja” na jina kwa jina.

Kujiandaa kwa ajili ya Wito katika Utumishi.

Sasa ninataka kujadili kwa ufupi kipengele muhimu lakini mara nyingi kisichootiliwa maanani cha kujiandaa kwa ajili ya wito katika utumishi.

Maneno matatu yanayohusiana yanaelezea mpangilio wa maandalizi na maendeleo kwa wana wa Mungu: ukuhani, hekalu, misheni. Wakati mwingine kama wazazi, marafiki na waumini wa Kanisa, tunajikita kwa undani sana kwenye maandalizi ya umisionari kwa wavulana kiasi kwamba tunapuuzia kwa kiwango fulani hatua zingine muhimu katika njia ya agano ambazo ni lazima zitimizwe kabla ya kuanza huduma ya umisionari. Kutumikia kama mmisionari ni kitu kimoja lakini sio tofali pekee muhimu la kujengea katika mchakato wa kutengeneza msingi imara wa maisha yote ya ukuaji wa kiroho na huduma. Baraka za ukuhani na hekalu, zote ambazo hutangulia kabla ya kufika kwenye eneo la kazi lililopangwa , pia ni muhimu kutuimarisha na kutukuza kiroho kwa maisha yetu yote.

Wavulana, kadiri mnavyotimiza majukumu yenu na kuheshimu Ukuhani wa Haruni au ukuhani mdogo, mnajiandaa kupokea na kukuza kiapo na agano la Melkizedeki au ukuhani mkubwa.10 Ustahili binafsi ni sifa moja muhimu sana inayohitajika katika kupokea ukuhani mkubwa. Huduma ya maisha isiyo na ubinafsi ya ukuhani ipo mbele yenu. Jiandaeni sasa kwa kutoa huduma yenye maana kila mara. Tafadhali jifunzeni kupenda kuwa na kubaki wenye kustahili. Muwe wenye kustahili. Mbaki wenye kustahili.

Baada ya kupokea Ukuhani wa Melkizedeki na wito wa kutumikia, kijana wa kiume anaweza kujikinga kwa nguvu11 kupitia maagano na ibada za hekalu takatifu. Kwenda hekaluni na kufanya roho wa hekalu aje kwenu hutangulia huduma yenye weledi kama mmisionari wa muda wote. Ustahili binafsi ni mojawapo ya kigezo kikuu cha kupokea baraka za hekalu kwenu ninyi wavulana na kwa waumini wote wa Kanisa. Kadiri mnavyoishi kulingana na viwango vya injili, mnaweza kuingia nyumba ya Bwana na kushiriki katika maagano matakatifu kipindi chote cha ujana wenu. Upendo wenu na uelewa wenu wa ibada za hekaluni utawaimarisha na kuwabariki maisha yenu yote. Tafadhali jifunzeni kupenda kuwa na kubaki wenye kustahili. Muwe wenye kustahili. Mbaki wenye kustahili.

Wavulana na wasichana wengi tayari wana kibali cha hekalu cha matumizi ya muda. Kama wenye Ukuhani wa Haruni mnatafuta majina ya familia zenu na kufanya ubatizo na kuthibitishwa kwa ajili ya wanafamilia wenu hekaluni. Kutunza vibali vyenu vya hekaluni huonyesha kustahili kwenu, na kuwatumikia wengine ndani ya hekalu ni sehemu muhimu ya kujiandaa kwa Ukuhani wa Melkizedeki.

Wavulana, kila mmoja wenu ni mmisionari sasa. Wote wanaowazunguka kila siku, ni marafiki na majirani “ambao tu wamezuiliwa kwenye ukweli kwa sababu hawajui wapi pa kuupata.”12 Kadiri mnavyoongozwa na Roho, mnaweza kushiriki wazo, mwaliko, ujumbe mfupi au tweet ambayo itatambulisha kweli za injili iliyorejeshawa kwa marafiki zenu. Hamhitaji na hampaswi kungojea wito rasmi ndiyo mjihusishe kwa bidii katika kazi ya ummisonari.

Kadiri baraka za ukuhani, hekalu na misheni zinavyokusanywa “pamoja … katika Kristo”13 na kuingiliana katika moyo, mawazo na nafsi ya mmisionari kijana, na anaweza kustahili kwa kazi.14 Uwezo wake unaongezwa kutimiza majukumu ya kumwakilisha kwa mamlaka Bwana Yesu Kristo. Muunganiko wenye nguvu wa kiroho wa kuheshimu ukuhani na maagano ya hekaluni, kupokea “nguvu ya uungu”15 kupitia ibada za ukuhani,16 kutumikia bila ubinafsi, na kutangaza injili isiyo na mwisho kwa watoto wa Mungu humuwezesha mvulana kuwa ” imara na asiyetingishika katika imani”17 na “aliyeota mizizi na kujengwa katika [Kristo].18

Katika nyumba zetu na kanisani, tunapaswa kutoa msisitizo sawa kwa vipengele vyote vitatu vya mpangilio wa Bwana wa kuandaa na kuendeleza kwa wana waaminifu wa Mungu: ukuhani, hekalu, misheni. Vyote vitatu vinahitaji sisi kupenda kuwa na kubaki wenye kustahili. Muwe wenye kustahili. Mbaki wenye kustahili.

Ahadi na Ushuhuda

Ndugu zangu wapendwa, ninaahidi zawadi ya kiroho ya ufunuo atashughulikia wito wenu kwenye kazi ya kutangaza injili na majukumu yenu katika eneo au maeneo mahususi ya kazi. Kadiri mnavyojiandaa kwa bidii sasa kupitia ukuhani usio na ubinafsi na huduma ya hekaluni, ushahidi wenu wa uhalisia wa Bwana anayeishi utaimarishwa. Upendo kwake na kwa kazi yake utaijaza mioyo yenu. Kadiri mnavyojifunza kupenda kuwa wastahili, mnaweza kuwa chombo kikuu katika mikono ya Bwana ili kubariki na kuwatumikia watu wengi.

Kwa furaha, ninatoa ushahidi kwamba Baba yetu wa Mbinguni na Mwanae Mpendwa, Yesu Kristo, wanaishi. Kujikita katika huduma yao ni mojawapo ya baraka kuu tunazoweza kupokea. Ninashuhudia hivyo katika jina takatifu la Yesu Kristo, amina.