“Kumsaidia Mdogo Wangu Wa Kiume,” Rafiki, Nov. 2023, 16–17.
Kumsaidia Mdogo Wangu Wa Kiume
Hakuna mtu yeyote aliyekuwa na muda kwa ajili ya Lashia sasa.
Hadithi hii ilitokea huko Afrika Kusini.
Lashia alikuwa na mdogo wake mpya wa kiume. Jina lake lilikuwa Liam. Alikuwa na nywele nyeusi na mikono na miguu midogo. Alikuwa mzuri sana.
Lakini wakati mwingine kuwa na mtoto mpya katika familia kunaleta wakati mgumu. Mama na baba daima walikuwa na kazi nyingi. Na Liam alilia sana.
“Mama, unaweza kunisomea hadithi?” Lashia aliuliza.
“Ninahitaji kumwosha Liam,” Mama alisema. “Pengine unaweza kusoma na Ariana.”
Lashia aliketi chini sakafuni na mdogo wake wa kike. Walipekua pekua kurasa za kitabu. Lakini haikuwa sawa bila mama.
“Baba, utacheza mchezo na mimi?” Lashia aliuliza.
“Ninahitaji kumsaidia Mama kumshughulikia mtoto kabla sijaondoka kwenda kazini,” Baba alisema.
Laisha alikunja uso. Mama na Baba hawakuwa na muda sasa. Mara zote walikuwa wakimsaidia Liam.
Punde Baba aliondoka kwenda kazini. Mama alimweka Liam kitandani ili alale. Mama alikaa na Lashia na Ariana kwenye kochi. Alionekana amechoka.
“Tumekuwa na shughuli nyingi na Liam,” Mama alisema. “Je, umekuwa ukihisi mpweke kidogo?”
Lashia alikubali kwa kichwa. Alihisi kama vile anataka kulia.
Mama aliwapa kumbatio Lashia na Ariana. “Liam anahitaji msaada mkubwa kwa sasa kwa sababu yeye ni mdogo sana. Hawezi kufanya chochote yeye mwenyewe.
“Najua,” Lashia alisema.
“Lakini kama unataka, unaweza kunisaidia kumwangalia Liam.” Mama alitabasamu.
“Kweli?” Lashia aliuliza. Alilipenda wazo hilo.
“Mimi pia?” aliuliza Ariana.
“Wewe pia,” alisema Mama.
Mara Liam alianza kulia. Wakati Mama alipokuwa akimbadilisha nep, Lashia alimletea vitambaa vya kufutia.
“Asante,” Mama alisema,
Siku iliyofuata, Liam alipokuwa anaogeshwa, Lashia na Ariana walichagua nguo safi ya yeye kuvaa. Ilikuwa na wanyama wadogo wazuri juu yake! Waliileta kwa mama ili amvalishe Liam.
“Asante,” Mama alisema,
Lashia na Ariana walifikiria njia zingine za kusaidia. Walitandika vitanda vyao kila asubuhi bila ya kuambiwa. Wakati mwingine walitandika kitanda cha Mama na Baba! Na wakati wa chakula, walimsaidia Baba jikoni.
“Asanteni,” Mama na Baba walisema,
Liam alipolia, Lashia alimsaidia ahisi vizuri. Alimshika na kuzungumza naye kwa sauti ya utulivu. Liam hakuweza bado kusema asante. Lakini siku moja alitoa tabasamu pana kwa Lashia!
Lashia alirudisha tabasamu. Alikuwa na furaha kwamba ameweza kumsaidia mdogo wake wa kiume na mama na baba pia!