“Tutalifanya Hili kwa Pamoja,” Rafiki, Nov. 2023, 40–41.
Tutalifanya Hili kwa Pamoja
Annie alikuwa anaogopa kuanza darasa la Wasichana.
Hadithi hii ilitokea huko Marekani.
Annie alisugua nyuzi za gauni lake. Alijaribu kuwasikiliza wazungumzaji. Lakini alikuwa na wasiwasi, hisia za woga tumboni.
Leo ilikuwa ni siku ambayo Annie angeanza kwenda katika darasa la Wasichana. Angeenda darasani mara baada ya mkutano wa sakramenti kumalizika. Kila mmoja alimwambia kwamba angefurahia, lakini badala yake, yeye aliogopa.
Alimtazama Tami, dada yake mkubwa. Tami amekuwa katika darasa la Wasichana kwa miaka mitatu, na alilipenda. Tami daima alimwambia Annie jinsi gani lilivyo zuri. “Utakuwa na marafiki wengi,” Tami alisema. “Ni tofauti na darasa la Msingi. Ni kama umekuwa mkubwa vya kutosha.”
Lakini Annie hakuwa kama dada yake. Tami alipenda kukutana na watu wapya, na ilikuwa rahisi kwake kupata marafiki. Annie alikuwa mkimya na aliona bora kusoma au kuchora kuliko kuzungumza na wengine.
Annie pia alikuwa na chunusi, na aliona aibu kuhusu jinsi alivyoonekana. Alikuwa akitumia krimu maalumu, ambayo ilikuwa inamsaidia. Lakini madoa mekundu juu ya ngozi hayakuweza kupotea.
Baada ya mkutano wa sakramenti, Annie alikuwa akivuta miguu yake ukumbini. “Siwezi kwenda katika darasa la Wasichana leo,” alimwambia mama na Tami.
Mama alionekana mwenye wasiwasi. “Nilidhani unayo shauku kuhusu kwenda katika darasa la Wasichana. Nini kimetokea?”
Simjui yeyote kati ya hao wasichana wakubwa.” Annie aliugusa uso wake. “Na pengine watanicheka watakaponiona.”
Mama alimpa Annie kumbatio kubwa. “Kumbuka kwamba Tami atakuwepo huko pia.”
“Mimi siyo kama Tami,” Annie alisema. Alimtazama dada yake. “Wewe ni mzuri katika kuzungumza na watu.”
“Ninajua ni vigumu kwenda katika darasa jipya,” Tami alisema. “Lakini tutalifanya hili kwa pamoja. Nilihisi kuogopa pia nilipoanza darasa la Wasichana.”
Annie alimwangalia Tami kwa kumkazia macho. Tami daima alionekana kuwa jasiri! Amewahi hata kujaribu katika muziki wa shule na akachaguliwa kuwa sehemu ya kuongoza. Annie hakufanya vitu kama hivyo. Alijaribu tu kuwa mtu asiyetambulika.
“Lakini wewe siyo mwoga,” Annie alisema.
Tami alitabasamu. “Ukweli ni kwamba mimi ni mwoga! Niliogopa nilipojaribu kwenye muziki. Unajua nilichokifanya?”
Annie alitikisa kichwa chake.
“Niliomba na nikafanya nilichoweza. Na nikawasaidia watoto wengine pia. Ilionekana kama wengi wao walikuwa wanaogopa kama mimi. Kuwasaidia wengine kuwa majasiri kulinisaidia mimi kuwa jasiri.”
Annie aliwaza kuhusu hilo. Je, angeweza kufanya kile Tami alichofanya na kuwasaidia wasichana wengine katika darasa lake wasiogope?
“Je, unadhani unaweza kwenda darasa la Wasichana leo?” Mama aliuliza.
Annie alivuta pumzi ndefu. Kisha akaitika kwa kichwa. Angeweza kufanya hilo.
Annie na Tami walitembea kwenda darasa la Wasichana. Annie aliwaangalia wale wasichana wengine. Baadhi yao walionekana wenye wasiwasi kama yeye alivyokuwa. Julie alikunja nywele kidoleni pake wakati Erica akitafuna kucha za vidole vyake.
Annie alifikiria kuhusu jinsi anavyoweza kuwasaidia. Alienda na akaketi pembeni ya Julie. “Je, wewe unaogopa pia?” Annie alinong’ona. “Itakuwa SAWA.”
Julie alitabasamu, na Annie alirudisha tabasamu. Annie alihisi uoga unapungua sasa. Pengine darasa la Wasichana hakika linaweza kuwa zuri.