2010–2019
Msifadhaike
Oktoba 2018


2:3

“Msifadhaike”

Kuweni jasiri, akina kaka na kina dada. Ndio, tunaishi katika nyakati zenye hatari kubwa, lakini tukibaki katika njia ya agano, hatuhitaji kuogopa.

Ninaongeza ushuhuda wangu kwa ujumbe wa Rais Russell M. Nelson na Mzee Quentin L. Cook uliotolewa muda mfupi uliopita kuhusu uwiano na umoja katika Baraza la Urais wa Kwanza na Akidi ya Mitume Kumi na Wawili. Najua matangazo haya ya ufunuzi ni mapenzi na nia ya Bwana na yatabariki na kuimarisha watu binafsi, familia, na Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho kwa vizazi vijavyo.

Miaka kadhaa iliyopita, mmoja kati ya binti zetu walioolewa pamoja na mumewe walimuuliza Dada Rasband pamoja nami swali muhimu sana, swali lenye ushawishi katika maisha: “Je, bado ni salama na busara kuwaleta watoto duniani humu tunamoishi na inayoonekana imekidhiri uovu wa kuogofya?”

Sasa, hilo lilikuwa swali muhimu kwa mama na baba kulifikiria pamoja na watoto wao wapendwa walio katika ndoa. Tuliweza kusikia hofu katika sauti zao na kuhisi hofu mioyoni mwao. Jibu letu kwao lilikuwa thabiti “Ndio, ni zaidi ya SAWA,” tulipokuwa tukishiriki mafundisho ya kimsingi ya injili na mawazo yetu ya dhati na uzoefu katika maisha.

Hofu si ngeni. Wanafunzi wa Yesu Kristo, wakiwa katika Bahari ya Galilaya, waliogopa “upepo, na mawimbi” katika giza la usiku.1 Kama wanafunzi Wake leo, sisi pia tuna hofu. Vijana wetu wazima wanaogopa kufanya masharti kama vile kuoana. Vijana wanandoa, kama vile watoto wetu, wanaweza kuwa na hofu kuwaleta watoto katika dunia inayozidi kuwa ovu zaidi. Wamisionari wanaogopa vitu vingi, hasa kuwaendea watu wasiowajua. Wajane wanaogopa kusonga mbele peke yao. Vijana huogopa kutokubalika; watoto wa shule huogopa siku ya kwanza shuleni; wanafunzi wa chuo huogopa kupata matokeo ya mitihani. Tunaogopa kutofaulu, kukataliwa, kuvunja matarajio, na kile kisichojulikana. Tunaogopa vimbunga, matetemeko ya ardhi, na moto unaoteketeza dunia na maisha yetu. Tunaogopa kutochaguliwa na, kwa upande mwingine, tunaogopa kuchaguliwa. Tunaogopa kutokuwa bora vya kutosha; tunaogopa kuwa Bwana hana baraka kwetu sisi. Tunaogopa mabadiliko, na woga wetu unaweza ukaongezeka na kuwa hofu kubwa. Nimejumuisha karibu tu kila mtu?

Kuanzia nyakati za kale, woga umedhibiti mtazamo wa watoto wa Mungu. Daima naipenda hadithi ya Elisha katika 2 Wafalme. Mfalme wa Shamu amelituma jeshi kubwa “wakafika usiku, na wakauzingira mji ule pande zote.”2 Nia yao ilikuwa ni kumkamata na kumuua nabii Elisha. Tunasoma:

“Na wakati alipoamka [Elisha], na kwenda nje, tazama wamezingira jiji na jeshi la watu, na farasi na magari.” Mtumishi wake kijana akamwambia, Ole wetu! Bwana wangu, tufanyeje?”3

Hii ilikuwa hofu ikizungumza.

“[Elisha] akamjibu, Usiogope; maana walio pamoja nasi ni wengi kuliko wale walio pamoja nao.”4

Lakini hakuachia hapo.

“Elisha akaomba, akasema, Ee Bwana, nakusihi, mfumbue macho yake, apate kuona. Bwana akamfumbua macho yule mtumishi; naye akaona; na tazama, kile kilima kilikuwa kimejaa farasi na magari ya moto yaliyomzunguka Elisha pande zote.”(5).

Twaweza au hatuwezi kutumiwa magari ya moto kuondoa hofu zetu na kushinda mashetani wetu , lakini somo ni bayana. Bwana yu pamoja nasi, anatujali na anatubariki katika njia ambazo ni Yeye tu Anayeweza kufanya hivyo. Sala inaweza kushusha nguvu na ufunuo ambao tunaohitaji kulenga mawazo yetu juu ya Yesu Kristo na dhabihu Yake ya Upatanisho. Bwana alijua ya kwamba wakati mwingine tungehisi woga. Nimepitia hayo nawe pia, na hiyo ndiyo sababu maandiko yamejaa ushauri wa Bwana:

“Changamkeni, na msiogope.”6

“Nitegemeeni katika kila wazo; msitie shaka, msiogope.”7

“Msiogope, enyi kundi dogo.”8 Ninapenda upole wa “kundi dogo.” Katika Kanisa hili tunaweza tukawa wachache kwa idadi kulingana na jinsi dunia inavyofafanua ushawishi, lakini tunapofungua macho yetu ya kiroho, “maana walio pamoja nasi ni wengi kuliko wale walio pamoja nao.”9 Mchungaji wetu mpendwa, Yesu Kristo, kisha anaendelea, Acha dunia na jahanamu ziungane dhidi yenu, kwani kama mmejengwa juu ya mwamba wangu, haziwezi kuwashinda.”10

Hofu inaondolewa vipi? Kwa mvulana huyo, alikuwa amesimama kando ya Elisha, nabii wa Mungu. Tunayo ahadi hiyo hiyo. Wakati tunapomsikiliza Rais Russell M. Nelson, wakati tunapotii ushauri wake, tunasimama pamoja na nabii wa Mungu. Kumbuka maneno ya Joseph Smith: “Na sasa, baada ya ushuhuda mwingi uliokwisha kutolewa juu yake, huu ni ushuhuda, wa mwisho wa zote, ambao tunautoa juu yake: Kwamba yu hai!”11 Yesu Kristo yu hai. Upendo wetu Kwake na Injili Yake huondoa woga.

Tamaa yetu “daima Roho wake apate kuwa”12 nasi itaondoa woga kwa ajili ya mtazamo wa milele wa maisha yetu ya muda. Rais Nelson ameonya, “Katika siku zijazo, haitawezekana kunusurika kiroho bila uzoefu wa kuongoza, kuelekeza, kufariji na ushawishi daima wa Roho Mtakatifu.”13

Bwana Amesema, kuhusu mabaa ambayo yatafunika dunia na kushupaza mioyo ya wengi: “wafuasi wangu watasimama katika mahali pa takatifu, na wala hawataondoshwa.”14

Na kisha ushauri huu mtakatifu: “Msifadhaike, kwani haya yote yatakapokuja kutokea, ili ninyi muweze kujua kwamba ahadi ambazo zimefanywa kwenu zitatimizwa.”15

Simama katika mahali patakatifu—usifadhaike—na ahadi zitatimizwa. Acha tuangalie kila moja ya hizi kuhusiana na hofu yetu.

Kwanza, simama katika mahali patakatifu. Wakati tunaposimama katika mahali patakatifu—nyumba zetu takatifu, majengo yetu ya mikutano yaliyowekwa wakfu, mahekalu yaliyowekwa wakfu—tunahisi Roho wa Bwana pamoja na nasi. Tunapata majibu ya maswali yanayotusumbua au amani ya kuyaweka tu kando. Huyo ndiye Roho akitenda. Sehemu hizi takatifu katika ufalme wa Mungu Duniani zinahitaji staha yetu, heshima yetu kwa wengine, nafsi zetu bora katika kuishi injili, na matumaini yetu kuweka kando woga wetu na kutafuta nguvu za uponyaji wa Yesu Kristo kupitia Upatanisho Wake.

Hakuna nafasi ya woga katika hizi sehemu takatifu za Mungu au katika mioyo ya watoto Wake. Kwa nini? Kwa sababu ya upendo. Mungu anatupenda sisi—daima—na tunampenda. Upendo wetu kwa Mungu nikinyume na woga wetu wote, na upendo wake unasheheni katika sehemu takatifu. Fikiria kuhusu hilo. Wakati hatuko imara katika kuweka ahadi zetu kwa Bwana, wakati tunapopotea kutoka kwenye njia Yake inayoelekeza kwenye maisha ya milele, wakati tuna shaka au wasiwasi kuhusu umuhimu wetu katika mpango Wake Mtakatifu, wakati tunaporuhusu woga kufungua mlango kwa wandani wake wote—kuvunjika moyo, hasira, kukata tamaa, masikitiko—Roho anatuacha, na tunabaki bila Bwana. Kama unajua hicho kinafananaje, unajua si mahali pazuri kuwepo. Kinyume cha hayo, wakati tunaposimama katika sehemu takatifu, tunaweza kuhisi upendo wa Mungu, na “upendo ulio kamili huitupa nje hofu.”16

Ahadi ifuatayo ni “Msifadhaike.”17 Bila kujali kiasi gani uovu na ghasia zinazokithiri duniani, tunaahidiwa kwa ajili ya uaminifu wetu wa kila siku katika Yesu Kristo “amani ya Mungu, ipitayo akili zote.”18 Na wakati Kristo atakapokuja kwa uweza wote na utukufu mkuu, uovu, uasi, na udhalimu vyote vitaisha.

Muda mrefu uliopita Mtume Paulo alitabiri kuhusu nyakati zetu, akimwambia kijana Timotheo:

“Lakini ufahamu neno hili, kwamba siku za mwisho kutakuwako nyakati za hatari.

“Maana watu watakuwa wenye kujipenda wenyewe, wenye kupenda fedha, wenye kujisifu, wenye kiburi, wenye kutukana, wasiotii wazazi wao, wasio na shukrani, wasio safi, …

“… wapendao anasa kuliko kumpenda Mungu.”19

Kumbuka, “walio pamoja nasi” pande zote za pazia, wale wanaompenda Bwana kwa moyo wao wote, uwezo, akili, na nguvu zao zote, “ni wengi kuliko wale walio pamoja nao.”20 Kama tutamwamini Bwana na njia Zake, kama tutashiriki katika kazi Yake, hatutaogopa mitindo ya dunia au kutishwa nayo. Ninawasihi muweke kando ushawishi na mashinikizo ya kidunia na kutafuta vitu vya kiroho katika maisha ya kila siku. Penda kile anachokipenda Bwana—ikijumuisha amri Zake, nyumba Zake takatifu, maagano yetu matakatifu pamoja Naye, sakramenti kila siku ya Sabato, mawasiliano yetu kupitia sala—na hautafadhaika.

Hoja ya mwisho: mwamini Bwana na ahadi Zake. Ninajua kwamba ahadi Zake zote zitatimizwa. Ninajua kwa uthabiti kama ninanvyosimama mbele yenu katika huu mkutano mtakatifu.

Bwana amefunua: “Kwani wale walio na hekima na kupokea ukweli, na kumchukua Roho Mtakatifu kuwa kiongozi wao, na hawajadanganyika—amini ninawaambia, hawatakatiliwa chini na kutupwa katika moto, bali watastahimili siku ile.”21

Hii ndio sababu hatupaswi kufadhaishwa na ghasia za siku hizi, na wale walio katika jengo kubwa na pana, na wale wanaofanyia mzaha juhudi za kweli na huduma ya kujitolea kwa Bwana Yesu Kristo. Msimamo wa kutegemea mema, ujasiri, hata hisani huja kutoka katika moyo usiolemewa na shida na ghasia. Rais Nelson, ambaye ana “msimamo wa kutegemea mema katika siku zijazo,” ametukumbusha, “Kama tunatakiwa kuwa na matumaini yoyote ya kupekua kupitia sauti nyingi sana na falsafa za watu ambazo zinashambulia ukweli, lazima tujifunze kupokea ufunuo.”22

Kupokea ufunuo wa kibinafsi, ni lazima tuweke mbele kuishi injili na kutia moyo uaminifu na mambo ya kiroho kwa wengine pamoja na sisi wenyewe.

Spencer W. Kimball alikuwa mojawapo ya manabii katika ujana wangu. Miaka hii michache iliyopita, baada ya kuitwa kama Mtume, nimepata amani katika ujumbe wake wa kwanza katika mkutano mkuu mnamo Oktoba mwaka wa 1943. Alikuwa anahisi amezidiwa na mwito wake; ninajua jinsi inavyohisi. Mzee Kimball alisema: “Niliwaza na kusali kwa muda mrefu, na kufunga na kusali. Kulikuwa na mawazo yaliyokuwa yanagongana akilini mwangu—sauti zilizoonekana kusema: ‘Huwezi kufanya kazii hii. Wewe si mstahiki. Hauna uwezo’—na daima hatimaye lilikuja wazo la ushindi: ‘Ni lazima ufanye kazi uliyopangiwa—ni lazima ujiwezeshe, kuwa mstahiki, na mwenye kuhitimu.’ Na mapambano yakaendelea.”23

Najipa moyo kutokana na ushuhuda wa dhati wa Mtume huyu ambaye aliweza kuwa Rais wa 12 wa Kanisa hili kuu. Alitambua alikuwa ameziwacha hofu zake “kufanya kazi aliyopangiwa” na kwamba alihitaji kumtegemea Bwana kwa ajili ya nguvu za kumfanya “awe na uwezo, mstahiki, na mwenye kuhitimu. Nasi pia tunaweza. Mapambano yatazidi kuwa, lakini tutakabiliana nayo pamoja na Roho wa Bwana. “Hatutafadhaika” kwa sababu wakati tunaposimama na Bwana na kutetea kanuni Zake na mpango Wake wa Milele, tunasimama mahali patakatifu.

Sasa, ni nini kuhusu yule binti na mkwe ambao waliuliza swali la dhati na undani, lililotokana na hofu miaka mingi iliyopita. Walizingatia kwa makini sana mazungumzo yetu usiku huo; walisali na kufunga na wakafikia mahitimisho yao wenyewe. Kwa furaha na shangwe kwa ajili yao na kwetu sisi, akina babu, sasa wamebarikiwa na watoto saba wazuri wakisonga mbele kwa imani na upendo.

Saba kati ya wajukuu wa Mzee na Dada Rasband

Kuweni jasiri, akina kaka na kina dada. Ndio, tunaishi katika nyakati zenye hatari kubwa, lakini tukibaki katika njia ya agano, hatuhitaji kuogopa. Ninawabariki kuwa mnapofanya hivyo, hamtatishwa na nyakati ambamo tunaishi au na shida zinazowakabili. Ninawabariki muweze kusimama katika sehemu takatifu na wala msiondoshwe. Ninawabariki muamini katika ahadi za Yesu Kristo, kuwa Yu hai, Anatulinda, anatujali na anasimama pamoja nasi. Katika jina la Bwana na Mwokozi wetu, Yesu Kristo, amina.