Chagueni Hivi Leo
Ukubwa wa furaha yetu ya milele hutegemea kumchagua Mungu aliye hai na kujiunga Naye katika kazi Yake.
Mhusika wa kubuni Mary Poppins ni yaya mwenye asili ya Uingereza—ambaye anatokea kuwa wa kichawi.1 Anajivumisha kwenye upepo wa mashariki kuisaidia familia ya Banks yenye matatizo ya Namba 17, Cherry Tree Lane, huko Edwardian London. Anapewa jukumu la watoto, Jane na Michael. Katika namna imara lakini yenye huruma, anaanza kuwafundisha masomo ya thamani kwa mguso wa kimazingaombwe.
Jane na Michael wanafikia maendeleo makubwa, lakini Mary anaamua kwamba ni muda kwake kusonga mbele. Katika uzalishaji wa jukwaani, rafiki wa Mary msafisha dohani, Bert, anajaribu kumshawishi asiondoke. Anatoa hoja, “Lakini ni watoto wazuri, Mary.”
Mary anajibu, “Ningekuwa nahangaika nao kama wasingekuwa? Lakini siwezi kuwasaidia kama hawataniruhusu, na hakuna mtu mgumu kufundisha kama mtoto anayejua kila kitu.”
Bert anauliza, “Kwa hiyo?”
Mary anajibu, “Kwa hiyo wanapaswa kufanya sehemu inayofuata wao wenyewe.”2
Akina kaka na kina dada, kama Jane na Michael Banks, sisi ni “watoto wazuri” ambao tuna thamani kuhangaikiwa. Baba yetu wa Mbinguni anataka kutusaidia na kutubariki, lakini si mara zote tunamruhusu. Wakati mwingine, tunajifanya kana kwamba tayari tunajua kila kitu. Na sisi pia tunahitaji kufanya “sehemu inayofuata” wenyewe. Hiyo ndiyo sababu tulikuja duniani kutoka nyumbani mbinguni. “Sehemu” yetu inajumuisha kufanya chaguzi.
Lengo la Baba yetu wa Mbinguni katika malezi siyo kufanya watoto Wake kutenda yale yaliyo mema; ni kufanya watoto Wake kuchagua kufanya yale yaliyo mema na hatimaye kuwa kama Yeye. Kama Yeye angetaka tu sisi tuwe watiifu, Angetumia zawadi na adhabu za papo hapo kushawishi tabia zetu.
Lakini Mungu hapendezwi na watoto Wake kuwa tu “wanyama” waliofunzwa na watiifu ambao hawatawezi kutafuna kwenye ndala Zake katika sebule ya selestia.3 Hapana, Mungu anataka watoto Wake wakue kiroho na kujiunga Naye katika kazi ya familia.
Mungu aliweka mpango ambapo tunaweza kuwa warithi katika ufalme Wake, njia ya agano ambayo hutuongoza sisi kuwa kama Yeye, kuwa na aina ya maisha aliyonayo, na kuishi pamoja kama familia kwenye uwepo Wake.4 Uchaguzi binafsi ulikuwa—na ni—muhimu kwenye mpango huu, ambao tulijifunza kuuhusu katika maisha kabla ya dunia kuwapo. Tuliukubali mpango na kuchagua kuja duniani.
Kuhakikisha kwamba tungeonyesha imani na kujifunza kutumia haki yetu ya kujiamulia vizuri, pazia la kusahau liliwekwa juu ya akili zetu ili tusikumbuke mpango wa Mungu. Bila pazia hilo, malengo ya Mungu yasingefikiwa kwa sababu tusingeendelea na kuwa warithi walioaminiwa anaotaka tuwe.
Nabii Lehi alisema: “Kwa hivyo, Bwana Mungu amemruhusu mwanadamu kujitendea mwenyewe. Kwa hivyo, mwanadamu hangeweza kujitendea mwenyewe bila kuvutiwa na moja au nyingine.”5 Katika hatua ya msingi, uchaguzi mmoja unawakilishwa na Yesu Kristo, Mzaliwa wa Kwanza wa Baba. Uchaguzi mwingine unawakilishwa na Shetani, Lusiferi, ambaye anataka kuharibu haki na nguvu ya kujiamulia.6
Katika Yesu Kristo, “tuna mtetezi kwa Baba.”7 Baada ya kumaliza dhabihu Yake ya upatanisho, Yesu “alipaa mbinguni … kudai kwa Baba haki zake za neema ambazo anazo juu ya watoto wa watu.” Na, baada ya kudai haki za neema, “yeye anatetea teto la watoto wa watu.”8
Utetezi wa Kristo kwa Baba kwa niaba yetu sio wa kiadui . Yesu Kristo, ambaye aliruhusu mapenzi Yake kumezwa na mapenzi ya Baba,9 asingetetea chochote zaidi ya kile Baba alichotaka wakati wote. Baba wa Mbinguni bila shaka hushangilia na kuunga mkono mafanikio yetu.
Utetezi wa Kristo ni, angalau kwa sehemu, kutukumbusha kwamba Yeye amelipia dhambi zetu na kwamba hakuna yeyote aliyetengwa kutoka kwenye ufiko wa neema ya Mungu.10 Kwa wale wanaoamini katika Yesu Kristo, wanatubu, wanabatizwa, na kuvumilia hadi mwisho—mchakato unaopelekea kwenye upatanisho11—Mwokozi husamehe, huponya, na kutetea. Yeye ni msaidizi wetu, mfariji, na mwombezi—akithibitisha na kudhamini kwa ajili ya upatanisho wetu na Mungu.12
Katika utofauti bayana, Lusiferi ni mshitaki au mwendesha mashitaka. Yohana Mfunuzi alielezea anguko la Mwisho la Lusiferi: “Nikasikia sauti kuu mbinguni ikisema, Sasa kumekuwa wokovu, na nguvu, na ufalme wa Mungu wetu, na mamlaka ya Kristo wake.” Kwa nini? Kwa maana “ametupwa chini mshitaki wa ndugu zetu, yeye awashitakiye mbele za Mungu wetu mchana na usiku. Nao wakamshinda kwa damu ya Mwanakondoo, na kwa neno la ushuhuda wao.”13
Lusiferi ndiye huyu mshitaki. Alizungumza dhidi yetu katika maisha kabla ya dunia kuwapo, na anaendelea kutushutumu katika maisha haya. Anatafuta kutuvuta chini. Anataka sisi tupate huzuni isiyo na mwisho. Ni yeye anayetuambia kwamba hatufai, yule anayetuambia kwamba hatuwezi vya kutosha, yule anayetuambia hakuna uponyaji kutoka kwenye kosa. Yeye ni mdhalimu mkuu, yule ambaye hutupiga mateke tunapokuwa chini.
Kama Lusiferi angekuwa anamfundisha mtoto kutembea na mtoto akajikwaa, angemgombeza mtoto, angempa adhabu, na kumwambia aache kujaribu. Njia za Lusiferi huleta kukata tamaa na huzuni—mwishowe na daima. Huyu baba wa uongo ni mlishaji mkuu wa uongo14 na kwa ujanja hutafuta kudanganya na kutuvuruga, “kwani anataka wanadamu wote wawe na dhiki kama yeye.”15
Kama Kristo angekua anamfundisha mtoto kutembea na mtoto akajikwaa, Yeye angemsaidia mtoto kunyanyuka na kutia moyo hatua zinazofuata.16 Kristo ni msaidizi na mfariji. Njia zake huleta furaha na tumaini—mwishowe na daima.
Mpango wa Mungu hujumuisha maelekezo kwa ajili yetu, yaliyotajwa katika maandiko kama amri. Amri hizi siyo kundi la vitu vilivyopitwa na wakati wala mkusanyiko usio na mantiki wa sheria zilizowekwa kwa kusudi tu la kutufunza sisi kuwa watiifu. Zimeunganishwa kwenye kujenga kwetu sifa za kiungu, kurudi kwa Baba yetu wa Mbinguni, na kupokea furaha ya kudumu. Utiifu kwa amri Zake siyo upofu; kwa kujua tunamchagua Mungu na njia Yake ya kurudi nyumbani. Mpangilio kwetu ni sawa na ilivyokuwa kwa Adamu na Hawa , ambapo “Mungu aliwapa amri, baada ya kuwafahamisha mpango wa ukombozi.”17 Japo Mungu anatutaka tuwe kwenye njia ya agano, Yeye anatupatia heshima ya kuchagua.
Hakika, Mungu anatamani, anatarajia, na anategemea kwamba kila mmoja wa watoto Wake ajichagulie mwenyewe. Yeye hatatulazimisha. Kupitia zawadi ya haki ya kujiamulia, Mungu huruhusu watoto Wake “kujitendea wenyewe na siyo kutendewa.”18 Haki ya kujiamulia inaturuhusu kuchagua kwenda kwenye njia, au la. Inaturuhusu kuacha, au la. Kama vile ambavyo hatuwezi kulazimishwa kutii, hatuwezi kulazimishwa kutotii. Hakuna anayeweza, bila ushirikiano wetu, kutuondoa kwenye njia. (Hii haipaswi kukanganywa na wale ambao haki yao ya kujiamulia imekiukwa. Hawako nje ya njia; wao ni wahanga. Wanapokea uelewa wa Mungu, upendo, na huruma.)
Tunapotoka kwenye njia, Mungu anahuzunishwa kwa sababu Yeye anajua hili mwishowe, lakini siku zote, hupelekea kwenye kufifia kwa furaha na upotezaji wa baraka. Katika maandiko, kutoka kwenye njia kunatajwa kama dhambi, na matokeo ya kufifia kwa furaha na upotezaji wa baraka huitwa adhabu. Katika hali hii, Mungu hatuadhibu; adhabu ni matokeo ya chaguzi zetu, siyo Zake.
Tunapogundua kwamba hatuko kwenye njia, tunaweza kubaki nje, au kwa sababu ya Upatanisho wa Yesu Kristo, tunaweza kuchagua kugeuza hatua zetu na kurudi kwenye njia. Katika maandiko, mchakato wa kuamua kubadilika na kurudi kwenye njia unatajwa kama toba. Kushindwa kutubu humaanisha kwamba tunachagua kutojistahilisha wenyewe kutoka kwenye baraka Mungu anazotamani kutoa. Kama “hatuko tayari kufurahia kile ambacho [sisi] tungeweza kupokea,” sisi “[tutarejea] … mahali [petu], ili kufurahia kile ambacho [sisi] tuko tayari kukipokea”19—uchaguzi wetu, siyo wa Mungu.
Haijalishi kwa muda gani tumetoka kwenye njia au mbali kiasi gani tumetangatanga, wakati tunapoamua kubadilika, Mungu hutusaidia kurudi.20 Kutoka kwenye mtazamo wa Mungu, kupitia toba ya dhati na kusonga mbele kwa uimara katika Kristo, tunaporudi tena kwenye njia, itakuwa kama vile hatukuwahi kutoka.21 Mwokozi analipia dhambi zetu na anatuweka huru kutokana na kupungua katika furaha na baraka. Hili limetajwa katika maandiko kama msamaha. Baada ya ubatizo, waumini wote huteleza na kuacha njia—baadhi yetu hata huzama nje. Kwa hivyo, kuonyesha imani katika Yesu Kristo, kutubu, kupokea usaidizi kutoka Kwake, na kusamehewa, siyo matukio ya mara moja bali mchakato wa maisha yote, hatua ambazo ni za kujirudia na zenye msisitizo. Hivi ndivyo tunavyo “vumilia hadi mwisho.”22
Tunahitaji kuchagua yule tutakayemtumikia.23 Ukubwa wa furaha yetu ya milele hutegemea kumchagua Mungu aliye hai na kujiunga Naye katika kazi Yake. Tunapojitahidi “kufanya sehemu inayofuata” sisi wenyewe, tunafanyia mazoezi kutumia haki yetu ya kujiamulia kwa usahihi. Kama Marais Wakuu wawili waliopita wa Muungano wa Usaidizi wa Kina Mama walivyosema, hatupaswi kuwa “watoto wanaohitaji malezi na sahihisho wakati wote.”24 Hapana, Mungu anatutaka tupevuke kuwa watu wazima na kujisimamia wenyewe.
Kuchagua kufuata mpango wa Baba ndiyo njia pekee tunayoweza kuwa warithi katika ufalme Wake; ndipo hapo tu anaweza kutuamini hata kutoomba kile kilicho kinyume na mapenzi Yake.25 Lakini tunapaswa kukumbuka kwamba “hakuna mtu mgumu kufundisha kama mtoto anayejua kila kitu.” Hivyo tunahitaji kuwa tayari kufundishwa katika njia za Bwana na Bwana pamoja na watumishi Wake. Tunaweza kuamini kwamba sisi ni watoto wapendwa wa Wazazi wa Mbinguni26 na tuna thamani “kuhangaikiwa” na kuwa na hakikisho kwamba “peke yetu” kamwe haimaanishi “wapweke.”
Kama Yakobo nabii wa Kitabu cha Mormoni alivyosema, ninasema pamoja naye:
“Kwa hivyo, changamsheni mioyo yenu, na kumbukeni kwamba mko huru kujitendea—kuchagua njia ya kifo kisicho na mwisho au njia ya uzima wa milele.
“Kwa hivyo, ndugu zangu wapendwa [na akina dada], jipatanisheni na nia ya Mungu, na sio kwa nia ya ibilisi … ; na kumbukeni, baada ya kupatanishwa na Mungu, kwamba ni kwa na kupitia neema ya Mungu pekee mnaokolewa.”27
Hivyo, chagueni imani katika Kristo; chagueni toba; chagueni kubatizwa na kupokea Roho Mtakatifu; chagueni kwa bidii kujiandaa kwa na kupokea sakramenti kwa kustahili; chagueni kufanya maagano hekaluni; na chagueni kumtumikia Mungu aliye hai na watoto Wake. Chaguzi zetu huamua jinsi tulivyo na vile tutakavyokuwa.
Ninahitimisha na baraka ya Yakobo iliyosalia: “Kwa hivyo, Mungu awafufue kutoka … kifo kisicho na mwisho kwa nguvu za upatanisho, kwamba mpokelewe katika ufalme wa milele wa Mungu.”28 Katika jina la Yesu Kristo, amina.