UJUMBE WA URAIS WA ENEO
‘Enenda zako nawe Ukafanye Vivyo Hivyo’
Ni upi ungekuwa uzoefu wako ikiwa ungejikuta kwenye njia ya Yeriko hivi leo?
Mwokozi na Mkombozi wetu Yesu Kristo alielewa misheni Yake ya kuwaokoa watoto wa Mungu, kama vile Yeye alivyotangaza: “Mwana wa Adamu alikuja kukiokoa kilichopotea . . .
“[Vivyo hivyo] haipendezi mbele za Baba yenu aliye mbinguni kwamba mmoja wa wadogo hawa apotee” (Mathayo 18:11; 14).
Katika sala ya kutuombea iliyoelekezwa kwa Baba Yake na Baba Yetu, ili kutusaidia tuelewe thamani ya kila nafsi, Yesu Kristo alisema, “Nilipokuwapo pamoja nao, mimi naliwalinda kwa jina lako: wale ulionipa, nikawatunza, wala hapana mmojawapo wao aliyepotea” (Yohana 17:12). Yeye anatoa amri katika ufunuo wa siku za leo kwamba “hakuna hata mmoja wao wale ambao baba amenipatia atakayepotea” (M&M 50:42).
Ni muhimu sana kama wafuasi wa Yesu Kristo tufuate mfano wa upendo na huruma Yake katika kukuza uwezo wetu binafsi wa kusikia sauti za wengi wa akina kaka, akina dada, vijana na watoto ambao wanaomba ili kuokolewa na wanaita kila siku kuomba msaada.
Naomba sasa niwapeleke kwenye safari chini ya njia ambayo wakati wa Mwokozi iliitwa “njia nyekundu” au “njia ya damu.” Ilishuka futi 3,400 (zaidi ya kilomita moja) katika usawa wa bahari na ilijawa na wanyang’anyi na majambazi. Hii ni njia ambayo ilishuka kutoka Yerusalemu kwenda Yeriko. Katika kujibu swali la mwanasheria, “Na jirani yangu ni nani?” (Luka 10:29), Mwokozi alitoa mfano wa Msamaria mwema (ona Luka 10:30–37). Kulikuwa na uadui mkubwa kati ya Wayahudi na Wasamaria wakati wa kipindi cha Kristo. Katika hali ya kawaida, makundi haya mawili yaliepuka michangamano kati yao.
Katika sheria iliyoandikwa ya Musa, makuhani na Walawi walipewa jukumu la kumtumikia Mungu na jirani zao, kote ndani ya hekalu na kama walimu na vielelezo kwa sheria ya Mungu. Wenye ukuhani hawa walielewa kikamilifu amri ya “mpende jirani yako kama nafsi yako” (Mambo ya Walawi 19:18).
Kiuhalisia, Walawi walikuwa na jukumu mahususi la kuwasaidia wasafiri kiuchumi na katika njia zingine (ona Mambo ya Walawi 25:35–36). Katika mfano wa Mwokozi, hata hivyo, kuhani na Walawi walienda kinyume na amri hizi—wote walimwona mtu aliyejeruhiwa na bado “walipita kando” (Luka 10:31–32). Msamaria, hata hivyo, alijawa na upendo na huruma. Hebu tujiulize maswali yafuatayo tukijiweka sisi wenyewe kwenye mfano huu wa Msamaria mwema na tuzingatie jinsi ambavyo tungeitikia kwa wale wanaohitaji msaada wetu.
Ni upi ungekuwa uzoefu wako ikiwa ungejikuta kwenye njia ya Yeriko hivi leo? Je, ungeshindwa kumwona mtu aliyeanguka kati ya wanyang’anyi na akihitaji msaada wako? Je, ungekuwa mtu ambaye unamwona aliyejeruhiwa na kusikia ombi lake, na bado unapita kando? Au utakuwa mtu anayeona, anayesikia, anayesimama na anayesaidia?
Nefi aliona katika ono Kanisa la Mwanakondoo wa Mungu katika siku za Mwisho. Alisema kwamba waumini wa Kanisa la Yesu Kristo wangezungukwa kwa haki na nguvu. Nguvu ya kuwapenda, kuwabadili, kuwatii, kuwatumikia na kuwahudumia wale wanaohitaji msaada na uokozi wetu, tukifuata mfano wa upendo msafi wa Kikristo wa Kristo kama ulivyoelezwa katika mfano wa Msamaria.
Rais Thomas S. Monson alisema: “Yesu alitoa neno letu la angalizo: ‘Enenda zako, nawe ukafanye vivyo hivyo.’ Tunapotii tamko hilo, kunafunguka katika uoni wetu mtazamo wa shangwe kuu. . . .
“Tunapotembea kwenye hatua za yule Msamaria mwema, tunatembea kwenye njia iongozayo kwenye ukamilifu”.1
Msamaria alikuwa na huruma wakati alipokuwa na jukumu la kusaidia, kwani alihisi huruma kwa matatizo ya mtu aliyejeruhiwa. Hisia hii ya ukarimu huletwa ndani ya moyo wa kila mmoja ambaye ameguswa na Roho wa Bwana. Hisia hizi za huruma zinapaswa kuhisiwa na kila mmoja wetu kumuelekea kila mmoja wetu. Hakika, Mwokozi amesema kwamba Israeli ya agano inapaswa kujulikana na kutofautishwa kwa upendo wanaouonesha kwa kila mmoja (ona Yohana 13:35).
Msamaria “alimkaribia.” Hakusubiri kufikiwa na mtu mwenye uhitaji, bali alitambua hitaji na akasonga karibu bila kuombwa kufanya hivyo.
Msamaria “alimfunga jeraha zake, akizitia mafuta na divai.” Alitoa uangalizi wa kitabibu na kupoza kiu cha mtu aliyeteseka. Msaada huu wa haraka yawezekana pia uliokoa maisha ya mtu yule.
Msamaria “alimpandisha juu ya mnyama wake”—hiyo ni kwamba, alitoa usafiri na “alimpeleka kwenye nyumba ya wageni,” mahali pa pumziko na uangalizi. Kwa kutoa malazi haya sahihi alihakikisha mazingira ya kufaa kwa ajili ya uponaji kuchukua nafasi.
Msamaria “alimtunza.” Gundua kwamba wakati wa kipindi kigumu cha uponaji, Msamaria hakuacha jukumu la uangalizi wa mtu aliyejeruhiwa kwa watu wengine bali alitoa dhabihu ya muda wake na nguvu zake ili kutoa huduma hii ya uponaji yeye mwenyewe.
Msamaria “hata siku ya pili . . . alitoa dinari mbili, akampa mwenye nyumba ya wageni.” Alichukua pesa yake mwenyewe, si ya mtu mwingine na kulipia huduma ambazo hakuweza kuzitoa yeye mwenyewe.
Msamaria, akihitaji kuendelea kutafuta pato lake, alimwambia mwenye nyumba ya wageni “amtunze.” Katika njia hii aliwahusisha wengine—rasilimali watu—wasaidie na kuendeleza uangalizi.
Msamaria kisha aliahidi kwamba “chochote utakachogharimiwa zaidi, mimi nitakaporudi nitakulipa.” Hapa kilele cha huruma kimeoneshwa! Haweki ukomo kwenye kiwango cha yeye kusaidia. Na, pengine hata muhimu zaidi, haachii tu pale na kusahau, lakini anajiwekea sharti la kurejea na kuhakikisha kwamba yote ambayo yangeweza kufanyika yamefanyika.
Nikihudumu katika Urais wa Kigingi, niliguswa na uzoefu alioshiriki Mzee Mervyn B. Arnold wa wale Sabini katika Mkutano Mkuu wa Aprili 2004 wakati aliposhiriki hadithi ya Kaka Marques ambaye alimwokoa Kijana aliyeitwa Fernando aliyekuwa hashiriki kikamilifu na hakuhudhuria mikutano ya Kanisa ya Jumapili.
Fernando alijiingiza kwenye mashindano ya kuteleza baharini Jumapili asubuhi na aliacha kwenda kwenye mikutano ya Kanisa. Mnamo Jumapili asubuhi Kaka Marques alibisha mlangoni kwa Fernando na kumuuliza mama yake Fernando ambaye hakuwa muumini ikiwa angeweza kuzungumza na Fernando. Alimwambia kwamba Fernando alikuwa amelala, hivyo Kaka Marques aliomba ruhusa ya kumwamsha. Alimwambia “Fernando, unachelewa kanisani!” Bila kujali kujitetea kwake, alimpeleka kanisani.
“Jumapili iliyofuata jambo lilelile lilifanyika, hivyo Jumapili ya tatu Fernando aliamua kuondoka mapema ili kumkwepa. Fernando alipofungua geti, alimkuta Kaka Marques ameketi ndani ya gari lake, akisoma maandiko matakatifu. Alipomwona alisema, Vyema! Umeamka mapema. Leo tutaenda na kumtafuta kijana mwingine!’ Fernando alihitaji kuruhusiwa haki yake ya kujiamulia, lakini Kaka Marques alisema, ‘Tunaweza kuzungumza kuhusu hilo baadaye.’
“Baada ya Jumapili nane Fernando hakuweza kumuepuka, hivyo aliamua kulala nyumbani kwa rafiki. Fernando alikuwa ufukoni mwa bahari asubuhi iliyofuata wakati alipomwona mtu aliyevalia suti na tai akitembea kumwelekea. Wakati alipoona kwamba alikuwa Kaka Marques, alikimbilia ndani ya maji. Mara ghafla, alihisi mkono wa mtu juu ya bega lake. Alikuwa Kaka Marques, ndani ya maji yaliyofika kifuani pake!Alimwinua kwa mkono na kusema, ‘Umechelewa! Twende.’ Wakati Fernando alipolalamika kwamba hakuwa na nguo yoyote ya kuvaa, Kaka Marques alijibu, ‘Ziko ndani ya gari.’”
Siku ile wakati wakitembea kutoka ufukoni mwa bahari Fernando aliguswa na upendo wa dhati na hofu ya Kaka Marques kwake. Hakika alielewa maneno ya Mwokozi: ‘Nami nitawatafuta waliopotea, nitawarudisha waliofukuzwa, nitawafunga waliovunjika, nitawatia nguvu wagonjwa’ (Ezekieli 34:16).’”2
Wapendwa akina Kaka na akina Dada, tunapokwenda kwenye kuokoa, Mungu hutupatia nguvu, kututia moyo na baraka, ili tuweze kuwasaidia wengine.
Naomba niwaalike tusichelewe kwenda kwenye kuokoa kwani wengi wapo katika uhitaji lakini hawajui wapi pa kugeukia kupata msaada. Usikate tamaa kwani kamwe hakuna kuchelewa kwenye kufanya mema kwa ajili ya mtu. Tafuta shangwe katika kuwaokoa wengine, ukiwa na mwisho akilini (M&M 18:15–16). Bila kujali umri wetu, sote tumealikwa kwenda na kuokoa.
Rais Henry B. Eyring alitangaza, “Licha ya umri wetu, wito wa Kanisa au mahali, sisi ni wamoja tulioitwa kwenye kazi ya kumsaidia [Mwokozi] katika mavuno Yake ya nafsi hadi Yeye atakapokuja tena.”3
Ninaomba kwamba kwa dhati, uaminifu na kwa moyo wote tuitikie mwaliko wa Mwokozi wa kwenda na kufanya vivyo hivyo. Ninashuhudia kwamba Yesu Kristo anawaokoa wote wanaohitaji usaidizi. Yeye ana huruma na huponya majeraha ya kiroho ya dhambi. Yeye hutuokoa kutoka kifo. Ninashuhudia kwamba kupitia Upatanisho Wake, Yesu Kristo yeye binafsi alilipa gharama kwa ajili ya sisi kurudi kwa Baba.