Mwezi Huu katika Historia ya Kanisa
Wamisionari Wanawasili Lesotho
Mnamo tarehe 18 Septemba 1989, Marc Modersitzki na Bradley Saunderson waliingia Lesotho, wamisionari wa kwanza vijana waliopangiwa kufundisha injili katika ufalme huu mdogo wenye milima. Familia tatu za waumini kwa shauku zilisubiria ujio wao: Familia ya Massey, ya Scott na ya Daffendols. Familia hizi tatu ziliunda kikundi pamoja na Kaka Massey akiwa kama kiongozi wa kikundi. Familia zote zilikuwa na shauku ya kuanza kufanya kazi ya umisionari na wazee wapya. Mwishoni mwa wiki mbili za mwanzo, wamisionari walikuwa na familia 18 katika orodha yao ya kufundisha.
Mzee Saunderson aliandika kwenye shajara yake, “Ninafurahishwa na uwezo ambao eneo linao: mavuno yake ni mengi.” Katika mwezi wa kwanza wa kutafuta watu walikataliwa mara nne tu.
Dada Scott, mama wa moja ya familia aliyekutana na wazee wakati wa kufika kwao, alikuwa na furaha sana kuhusu ubatizo wa kwanza wa waongofu kiasi kwamba alitaka ufanyikie nyumbani kwake. Hata hivyo, familia ya Scott haikuwa na bwawa la ubatizo hivyo Kaka Scott alinunua bwawa la kupachika. Tatizo jingine lilikuwa kwamba hakukuwa na sehemu tambarare katika eneo lao la kuweza kutosha bwawa. Hilo halikuondoa shauku yao. Kwa msaada wa Kaka Lawrence Van Tonder, mmoja wa wawili wa mwanzo waliopaswa kubatizwa, walisawazisha upande wa nyuma wa uwanja wa Scott ili kuweka bwawa.
Shukrani kwa jitihada nyingi za waumini na wamisionari, sasa Lesotho ina zaidi ya waumini 1,300.