UJUMBE WA KIONGOZI W ENEO HUSIKA
Kumwokoa Asiyeshiriki Kanisani Kikamilifu
Tunapotimiza majukumu yetu ya kuwafikia wale wanaohangaika, tunaweza kuzishinda changamoto na dhiki tutakazokutana nazo.
Kuwa muumini wa Kanisa kwa miaka 13 iliyopita, ninapenda kuwatembelea waumini wasioshiriki kikamilifu ili kuona wanaendeleaje na kushiriki pamoja nao upendo wa Yesu Kristo kwa ajili ya watoto wake. Ninakumbuka Jumamosi moja nikiwa nimepiga magoti na kumwomba Baba wa Mbinguni anisaidie kuwafikia wale wanaohitaji faraja yangu na kuelewa upendo wa Kristo kwa ajili yao. Nilipohitimisha sala yangu nilihisi msukumo wa roho kumtembelea dada mmoja asiyeshiriki kikamilifu. Hajapata kuwepo kanisani kwa muda mrefu sasa. Nilipompigia simu aliniambia kwamba alikuwa hospitali akiwa amebainika kuwa na ugonjwa mbaya. Niliamua kwenda mwenyewe kumtembelea dada huyo, hata ikiwa sikupata msaada wa kunifikisha hospitalini (kwa sababu mimi ni kipofu).
Aliponiona alijawa na shangwe na kusema, “wewe ni mtu wa kwanza kunitembelea”. Nilishiriki naye hadithi ya Lazaro, na jinsi, kwa sababu ya imani yake, Kristo alimfufua kutoka kwa wafu (ona Yohana 11:1–44).
Wiki chache baadaye dada huyu alikuja kanisani na kutoa ushuhuda wake kuhusu kutembelewa kwake kwa mara ya kwanza na muumini wa kanisa. Alishiriki jinsi matembezi hayo yalivyoimarisha ushuhuda wake na kumpa tumaini jipya katika maisha la kuelewa mpango wa Baba yetu wa Mbinguni kwa watoto wake.
Tunapowatembelea waumini wasioshiriki kikamilifu, tunafuata mfano wa Yesu Kristo wa kumtafuta kondoo aliyepotea (Mathayo 18:12–14). Tunapofanya hivi, si tu tunawasaidia wengine, ushuhuda wetu sisi wenyewe pia utaimarika.
Kuwahudumia watoto Wake ambao hawashiriki kikamilifu katika shughuli za kanisani ni moja ya amri za Baba yetu wa Mbinguni. Tunapotimiza majukumu yetu, tunaweza kushinda changamoto na dhiki tutakazokutana nazo. Tutapata baraka zilizoahidiwa katika Alma 37:16: “Lakini kama utatii amri za Mungu, na ufanye vitu hivi ambavyo ni vitakatifu kulingana na yale ambayo Bwana amekuamuru ufanye, (kwani lazima uombe msaada wa Bwana kwa vitu vyote ambavyo unataka kuvitumia) tazama, hakuna nguvu za ardhini au jehanamu, zinazoweza kuvichukua kutoka kwako, kwani Mungu ni mwenye uwezo kwa kutimiza maneno yake yote.”