Ni Ukubwa Sahihi Tu
Trina hakutaka kuwa tofauti.
“Wewe ni mdogo sana!” Sasha alisema. “Tunapaswa kukuita Trina Mdogo.”
Trina alijaribu kutabasamu. Watoto wengine shuleni walimtania sana kwa kuwa yu mdogo. Amezaliwa na umbile dogo, na hajakua kwa haraka kama watoto wengine. Lakini hakulipenda jina la Trina Mdogo. Yeye hakutaka kuwa tofauti.
“Wewe ni mdogo sana yawezekana usikue,” Max alisema walipokuwa wakitoka nje kwa mapumziko.
“Najua mimi ni mdogo,” Trina alisema. “Lakini hakuna lolote ninaloweza kufanya juu ya hili” Twende zetu tukacheze.”
Trina akakimbia kwenda kucheza soka na watoto wengine. Walipigiana mpira huo. Wote walikuwa wakiburudika kwa pamoja.
Lakini kitambo kifupi Trina akawa amechoka sana. Pole pole alitembea akiacha kucheza na kwenda kukaa kwenye nyasi.
Muda mfupi rafiki yake Josie akaja. Josie alikuwa katika darasa lake la Msingi la Kanisani pia.
“Je, uko sawa?” Josie alimwuliza.
“Ndio,” Trina alisema. “Ninahitaji tu kupumzika. Mapafu yangu yanachoka ninapokimbia sana. Hayako imara sana.”
Josie akakaa chini karibu na Trina. Walichuma nyasi na kutengeneza pete ndogo ndogo na bangili. Walizungumza kuhusu shule na marafiki na kazi za shule wafanyazo nyumbani.
“Nilisikia kile Sasha alichokisema,” Josie alisema. “Ninasikitika kwa kukuita wewe Trina Mdogo.”
Trina aliitikia kwa kichwa tu.
“Lakini mimi ninadhani wewe una ukubwa ulio sahihi tu!” Josie alisema.
Trina alitabasamu. Akampatia Josie mkononi bangili ya nyasi aliyokuwa ameitengeneza.
Jumapili iliyofuata, Trina alikuwa tayari kwa ajili ya kanisa. Alivaa gauni lake na kuchana nywele zake. Kisha akachukia alipoviangalia viatu vyake vidogo kabatini. Alikuwa na uhakika hakuna mtu mwingine katika darasa lake la Msingi aliyevaa viatu vidogo kama vyake.
Trina aliikokota miguu yake alipokuwa akitembea kushuka chini katika ukumbi wa kanisa. Alifika kwenye darasa lake la Msingi, Josie alikuwa akimsubiri nje.
“Tunayo zawadi ya kushangaza kwa ajili yako!” Josie alisema. “Njoo uone!”
Wakati Trina alipoingia katika chumba cha darasa, watoto wengine na mwalimu wao, Dada Bott, walikuwa wakiunyoshea vidole ubao angavu uliopambwa. Ubao ulikuwa na mioyo iliyobandikwa kote ubaoni. Kulikuwa na maandishi juu ya mioyo hiyo ambayo yalisema, “Trina ana tabasamu kubwa! Trina ana moyo mkubwa!”
“Je, unaipenda?” aliuliza Josie. “Dada Bott alitusaidia kuitengeneza.”
“Ninaipenda!” alisema Trina. “Asanteni.”
“Tulitaka kukukumbusha wewe juu ya ukweli mmoja mkubwa,” Dada Bott alisema. “Baba wa Mbinguni anampenda kila mmoja wetu. Mfupi, mrefu, mkubwa, mdogo, hilo siyo muhimu Kwake. Sisi sote ni watoto Wake na Yeye anampenda kila mmoja.”
Trina aliiangalia ile mioyo juu ya ubao na akatoa tabasamu—kubwa.