“Njoo, Unifuate”
Yesu Kristo anatualika kufuata njia ya agano kurejea nyumbani kwa Wazazi wetu wa Mbinguni na kuwa na wale tunaowapenda.
Akina kaka na dada zangu wapendwa, mke wangu Wendi pamoja nami tunafurahi kuwa pamoja nanyi asubuhi hii ya Sabato. Mengi yametendeka tangu mkutano mkuu uliopita. Mahekalu mapya yamewekwa wakfu huko Concepción, Chile; Barranquilla, Colombia; na Roma, Italia. Tulihisi uwepo mkubwa wa Roho katika matukio haya matakatifu.
Ninawapongeza wanawake wengi (na wanaume) ambao hivi karibuni wamesoma Kitabu cha Mormoni na kugundua shangwe na hazina zilizofichika. Ninatiwa moyo sana na ripoti za miujiza iliyopokewa.
Ninashangazwa na wavulana wa umri wa miaka 11 ambao, sasa kama mashemasi, kwa kustahili wanapitisha sakramenti kila Jumapili. Wanaenda hekaluni pamoja na wasichana wetu wa umri wa miaka 11, ambao sasa kwa hamu kubwa wanajifunza na kutumikia kama Beehives. Wote wavulana na wasichana wanahubiri kweli za injili kwa uwazi na Ushawishi.
Ninafurahi pamoja na watoto na vijana wanaosaidia kufundisha injili nyumbani mwao pale wanapofanya kazi na wazazi wao kufuata mtaala unalenga nyumbani na kusaidiwa na Kanisa.
Tulipokea picha hii ya Blake mwenye umri wa miaka minne, ambaye, Jumamosi moja asubuhi na mapema, alichukua kitabu cha Kanisa na kusema kwa msisimko, “Ninahitaji kulisha roho yangu!”
Blake, tunafurahia pamoja nawe na wengine wanaochagua kulisha roho zao kwa kusheherekea kweli za injili iliyorejeshwa ya Yesu Kristo. Na tunafurahia kujua kuwa wengi wanapokea uwezo wa Mungu maishani mwao wanapoabudu na kuhudumu hekaluni.
Kama wengi wenu mjuavyo, familia yetu ilipitia uzoefu wa utengano miezi mitatu iliyopita wakati binti yetu Wendy alipoondoka kutoka maisha haya ya duniani. Katika siku za mwisho za mapambano yake dhidi ya saratani, nilibarikiwa kwa nafasi ya kuwa na mazungumzo ya buriani ya baba na bintiye.
Nilishika mikono yake na nilimwambia jinsi gani ninampenda na kwa kiasi gani nilikuwa na shukrani kuwa baba yake. Nilisema: “Ulifunga ndoa hekaluni na kuheshimu maagano yako. Wewe na mume wako mlipokea watoto saba nyumbani kwenu na kuwalea kuwa wafuasi wa dhati wa Yesu Kristo, washiriki shupavu wa Kanisa, na wananchi wema. Na wamechagua wenzi wa sifa hiyohiyo. Baba yako anajivunia sana, sana juu yako. Umeniletea shangwe kuu!”
Alijibu kwa upole, “Asante Baba.”
Ulikuwa wakati mtulivu wa machozi kwetu. Kwa muda wa miaka yake 67, tulifanya kazi pamoja, tuliimba pamoja, na mara kadhaa tuliteleza juu ya theluji pamoja. Lakini jioni hiyo, tulizungumza kuhusu mambo ya muhimu zaidi, kama vile maagano, ibada, utiifu, imani, familia, uaminifu, upendo, na uzima wa milele.
Tunamkosa sana binti yetu. Hata hivyo, kwa sababu ya injili iliorejeshwa ya Yesu Kristo, hatuna wasiwasi kumhusu yeye. Tunapoendelea kuheshimu maagano yetu na Mungu, tunaishi kwa matarajio ya kuwa naye tena. Kwa sasa, tunamtumikia Bwana hapa na yeye anamtumikia huko—paradiso.1
Tena, mimi na mke wangu tulitembelea Paradiso mwanzoni mwa mwaka huu—Yaani Paradiso, California. Wakati ilipotokea, ratiba yetu ya kutembelea huko ilikuja chini ya saa 40 baada ya binti yetu kuondoka duniani. Mke wangu pamoja na mimi, pamoja na Mzee Kevin W. Pearson na mkewe, June, tuliimarishwa na Watakatifu wa Kigingi cha Chico California. Tulijifunza kuhusu imani yao kuu, kuhudumu kwao, na miujiza iliyotokea hata katikati ya hasara kubwa kutokana na uharibifu mkubwa wa moto katika historia ya California.
Tulipokuwa pale, tulizungumza kwa muda na afisa kijana wa Polisi, John, ambaye alikuwa mmoja wa wenye ujasiri kati ya wengi waliofika kwanza kwenye tukio. Alikumbuka giza zito lililoshuka huko Paradiso mnamo Novemba 8, 2018, wakati ndimi na miale ya moto kama janga ilipozunguka mji, ikimeza mali na hazina kama laana na kuacha jivu tu na dohani za matofali.
Kwa saa 15, John aliendesha gari kupita giza lisiloweza kupenyeka likiwa na miale ya moto ya kutisha akisaidia mtu mmoja baada ya mwingine, familia moja baada ya nyingine kwenda kwenye usalama—yote akihatarisha maisha yake. Hata hivyo katika juhudi zake, kilichomwogopesha zaidi John kilikuwa ni swali: “iko wapi familia yangu?” Baada ya saa nyingi, saa za kuogofya na huzuni, hatimaye alijua kuhusu kutoka kwao salama.
Simulizi ya wasiwasi wa John kwa familia yake imenipa msukumo kuzungumza leo na wale kati yenu ambao mnaweza kuuliza mnapokaribia mwisho wa maisha yenu ya duniani, “iko wapi familia yangu?” Katika siku hiyo ijayo wakati utakapokamilisha jaribio la hapa duniani na kuingia ulimwengu wa roho, utakumbana uso kwa uso na swali hili la kuvunja moyo: “iko wapi familia yangu?”
Yesu Kristo anafundisha njia ya kurudi kwenye nyumba yetu ya milele. Anaelewa vyema mpango wa Baba Yetu wa Mbinguni wa Maendeleo ya milele kuliko yeyote kati yetu. Hata hivyo, Yeye ni jiwe la katikati la tao la mpango wote. Ni Mkombozi, mponyaji, na Mwokozi wetu.
Tangu Adamu na Eva walipofukuzwa kutoka kwenye Bustani ya Edeni, Yesu Kristo ametoa mkono Wake wenye nguvu kuwasaidia wote wanaochagua kumfuata Yeye. Mara nyingi, maandiko husema kwamba, licha ya aina zote za dhambi kutoka kwa watu wa kila aina, bado mikono Yake imenyooshwa.2
Roho ndani ya kila mmoja wetu inatamani kwa asili upendo wa familia kudumu milele. Nyimbo za mapenzi huendeleza tumaini la uongo kwamba upendo ndio kila kitu mnachohitaji kama manataka kuwa pamoja milele. Na wengine kimakosa huamini kuwa Ufufuo wa Yesu Kristo hutoa ahadi kuwa watu wote watakuwa na wapendwa wao baada ya kifo.
Kwa kweli, Mwokozi Mwenyewe alisema dhahiri kabisa kuwa wakati Ufufuo Wake unahakikisha kwamba kila mtu aliyewahi kuishi kweli atafufuliwa na kuishi milele,3 mengi zaidi yanahitajika tukitaka kupata fursa kuu ya kuinuliwa. Wokovu ni jambo la kibinafsi, lakini kuinuliwa ni jambo la kifamiia.
Yasikilize maneno haya yaliyosemwa na Bwana Yesu Kristo kwa Nabii wake: “Maagano yote, mikataba, mapatano, ahadi, viapo, nadhiri, utendaji, mahusiano, ushirika, au matarajio, ambayo hayakufanyika na kuingiwa na kufungwa na yule Roho Mtakatifu wa ahadi … maagano hayo hayataleta matokeo yanayofaa, uwezo, au nguvu katika ufufuko na baada ya ufufuko kutoka kwa wafu; kwani mikataba yote ambayo haifanywi kwa madhumuni haya inakoma watu wanapokufa.”4
Hivyo, ni nini kinahitajika kwa familia ili kuinuliwa milele? Tunastahili kupata hiyo fursa kwa kufanya maagano na Mungu, kutunza maagano hayo, na kupokea ibada muhimu.
Hii imekuwa kweli tangu mwanzo wa nyakati. Adamu na Eva, Noah na mkewe, Ibrahimu na Sara, Lehi na Saria, na wafuasi wengine waliojitolea wa Yesu Kristo—tangu ulimwengu ulipoumbwa—wamefanya maagano sawa na hayo na Mungu. Wamepokea ibada sawa na zile ambazo sisi kama waumini wa Kanisa la Bwana lililorejeshwa hivi leo tumefanya: maagano yale tunayopokea wakati wa ubatizo na hekaluni.
Mwokozi anatualika sote kumfuata kwenye maji ya ubatizo na, kwa wakati, kufanya maagano ya ziada na Mungu kwenye hekalu na kupokea na kuwa waaminifu kwa ibada hizo muhimu za ziada. Haya yote yanahitajika kama tunataka kuinuliwa pamoja na familia zetu na Mungu milele.
Uchungu wa moyo wangu ni kuwa watu wengi niwapendao, ninaovutiwa nao na kuwaheshimu hukataa mwaliko Wake. Wanapuuza maombi ya Yesu Kristo wakati Anapoita “Njoo, Unifuate.”5
Ninaelewa kwa nini Mungu hulia.6 Mimi pia hulia kwa ajili ya marafiki na ndugu kama hawa. Ni wanaume na wanawake wazuri, wanaojitolea katika majukumu ya familia na nchi yao. Wanatoa kwa ukarimu wakati wao, nguvu, na mali. Na ulimwengu ni bora kwa sababu ya juhudi zao. Lakini wamechagua kutofanya maagano na Mungu. Hawajapokea ibada zitakazowainua pamoja na familia zao na kuwaunganisha pamoja milele.7
Ni jinsi gani ninatamani ningewatembelea na kuwaalika kufikiria kwa kina amri za Mungu zinazowezesha. Nimejiuliza juu ya kile ambacho ningeweza kusema ili wahisi jinsi mwokozi anavyowapenda na wajue ni kiasi gani ninawapenda na wajue jinsi wanaume na wanawake wenye kutunza maagano wanavyoweza kupokea “Utimilifu wa shangwe.”8
Wanahitaji kufahamu kwamba japokuwa kuna sehemu kwa ajili yao baada ya hapa—pamoja na wanaume na wanawake wema ambao pia hawakuchagua kufanya maagano na Mungu—hiyo si sehemu ambapo familia zitaungana tena na kupewa fursa ya kuishi na kuendelea milele. Huo si ufalme ambapo watapata uzoefu wa utimilifu wa shangwe—wa maendeleo yasiyo na kikomo na furaha.9 Baraka hizi timilifu zinaweza kuja tu kwa kuishi katika ulimwengu ulioinuliwa wa selestia pamoja na Mungu, Baba yetu wa Milele; Mwanaye, Yesu Kristo; na wanafamilia wetu wema na wenye kustahili.
Ninahisi kuwaambia marafiki zangu wanaosita:
“Katika maisha haya, hamjawahi kuwa kwenye nafasi ya pili kwa ubora. lakini, wakati mnapokataa kukumbatia kikamilifu injili iliyorejeshwa ya Yesu Kristo, mnachagua kuwa kwenye nafasi ya pili kwa ubora.
“Mwokozi alisema, ‘Nyumbani mwa Baba Yangu mna makao mengi.’10 Hata hivyo, mnapochagua kutofanya maagano na Mungu, mnakubali paa duni juu ya vichwa vyenu kwa milele yote.”
Ningewashawishi zaidi rafiki zangu wanaosita kwa kusema:
“Toa moyo wako kwa Mungu. Muulize kama mambo haya ni ya kweli. Tenga muda kujifunza maneno yake. Jifunze hasa! Ikiwa kweli unaipenda familia yako na unatamani kuinuliwa pamoja nao milele yote, lipa gharama hivi sasa—kupitia kusoma kwa dhati na sala ya dhati—kujua kweli hizi za milele na kisha kuziishi.
“Ikiwa huna hata hakika kama unamwamini Mungu, anza hapo hapo. Elewa kuwa katika ukosefu wa uzoefu kuhusu Mungu, mtu anaweza kushuku uwepo wa Mungu. Kwa hivyo, jiweke katika nafasi ambapo utaanza kupata uzoefu Naye. Jinyenyekeze. Sali kupata macho ya kuona mkono wa Mungu katika maisha yako na katika dunia inayokuzunguka. Muulize kama kweli Yupo—Kama Anakufahamu. Muulize jinsi Anavyohisi kuhusu wewe. Na kisha sikiliza.”
Rafiki yangu mmoja alikuwa na uzoefu haba kuhusu Mungu. Lakini alitamani kuwa na mkewe aliyekuwa amefariki. Hivyo aliniomba nimsaidie. Nilimhimiza kukutana na wamisionari wetu ili kuelewa mafundisho ya Kristo na kujifunza juu ya maagano, ibada, na baraka za injili.
Na alifanya hivyo. Lakini alihisi kuwa njia waliyoshauri ingemhitaji kufanya mabadiliko mengi maishani mwake. Alisema “Hizo amri na maagano ni ngumu sana kwangu. Pia, siwezi kulipa fungu la kumi, na sina muda wa kutumikia Kanisani.” Kisha akaniomba, “Mara nitakapokufa tafadhali fanya kazi ya hekalu inayohitajika ili mimi na mke wangu tuwe pamoja tena.”
Nashukuru, mimi si hakimu wa mtu huyu. Lakini nina shaka kuhusu ufanisi wa kazi ya hekalu kwa mtu aliyekuwa na nafasi kubatizwa katika maisha haya—kutawazwa kwenye ukuhani na kupokea baraka za hekaluni katika maisha haya ya duniani—lakini akafanya uamuzi kwa kufahamu kuikataa njia hiyo.
Akina Kaka na dada zangu wapendwa, Yesu Kristo anatualika kufuata njia ya agano kurejea nyumbani kwa Wazazi wetu wa Mbinguni na kuwa na wale tunaowapenda. Anatualika “Njoo, Unifuate.”
Sasa, kama Rais wa Kanisa Lake, ninawaomba sana wale ambao mmejitenga na Kanisa na ninyi ambao bado hamjatafuta kwa dhati kujua kuwa Kanisa la Mwokozi limerejeshwa. Fanya kazi ya kiroho ili kujua wewe mwenyewe, na tafadhali fanya hivyo sasa. Wakati unakwisha.
Ninashuhudia kwamba Mungu anaishi! Yesu ndiye Kristo. Kanisa Lake na utimilifu wa Injili Yake vimerejeshwa ili kubariki maisha yetu kwa shangwe, hapa na baada ya hapa. Ninashuhudia hivyo katika jina la Yesu Kristo, amina.