2022
Safari ya Mfuasi
Julai/Agosti 2022


UJUMBE WA URAIS WA ENEO

Safari ya Mfuasi

Kujifunza kuwa mfuasi ni kujiingiza kwenye safari inayodumu maisha yote. Ni safari ambayo huleta shangwe kuu kwenye moyo ikiwa itachukuliwa kwa bidii—licha ya vikwazo ambavyo mara zote hujificha njiani.

Kila safari huanza kwa hamu ya moyo kwa ajili ya jambo ambalo litapatikana pale safari inapomalizika. Vivyo hivyo, kila juhudi huanza na msimamo imara kwamba matokeo mazuri yataonekana kazi itakapokuwa imekamilika. Akiwa amejazwa tumaini kwa siku zijazo, msafiri hufanya haraka kwenye safari yake na mfanyakazi kwa bidii zote hushughulikia jukumu moja baada ya jingine.

Safari yangu ya ufuasi kwa Kristo ilianza kwa hamu ya kuwa na muunganiko na nguvu kubwa kuliko mimi. Ndani ya kina cha moyo wangu, nilijua nguvu ilikuwepo. Lakini sikufahamu jinsi ya kufanya muunganiko. Pasipo ufahamu kamili, nilianza kutafuta. Mara kwa mara nilitazama kwa mshangao na kupendezewa na ukuu wa anga la usiku pamoja na nyota zake zisizo na idadi. Nilistaajabu jinsi mifumo mbalimbali ya maisha duniani ilivyotokea na jinsi kila kiumbe hai kinavyohusiana kiuhalisia na akili ambayo huwezesha uwepo wake na ulinzi binafsi. Niligundua kwamba hata baadhi ya mimea ilifahamu jinsi ya kuwalaghai ndege na wanyama wale matunda yake na mingine jinsi ya kufungua maganda yake na kutoa mbegu zake zenye mbawa ilipofika wakati wa kiangazi—na upepo ulikuwa mkali ili kusambaza mbegu zake kwenye ardhi mpya na kuzaa miti mipya. Antena yangu kwa mambo ya Mungu iliinuliwa na ilikuwa tayari kupokea.

Hivyo, wakati, ilipoonekana ni kwa bahati nasibu, tulikutana na wamisionari wanandoa wazee walioniambia mimi na mke wangu Gladys kuhusu Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho—na kutualika kuungana na kusanyiko nyumbani kwao siku iliyofuata ili tujionee wenyewe—tuliitikia haraka. Niliketi katika lile kusanyiko dogo la takriban watu ishirini kwa mara ya kwanza , kile nilichosikia kikifundishwa kilisikika kuwa kweli na kilileta hisia nzuri. Nilitaka hilo liwe sehemu ya maisha yangu. Nilishiriki hisia hizi kwa mke wangu na kugundua kwamba yeye pia alihisi hivyo. Tuliamua kwamba tungeungana na kusanyiko tena Jumapili iliyofuata. Tuliendelea kufanya hivyo, na punde ukawa utamaduni wa familia yetu kuwepo Kanisani kila Jumapili. Tuliposhiriki kwenye ibada ya sakramenti, nilihisi na mpaka leo, ninaendelea kupata hisia ya kina ya amani wakati ninapokumbuka maneno ya Mwokozi:

“Basi Yesu akawaambia, Amin, amin, nawaambieni, Msipoula mwili wake Mwana wa Adamu na kuinywa damu yake, hamna uzima ndani yenu.

Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu anao uzima wa milele; nami nitamfufua siku ya mwisho.

Kwa maana mwili wangu ni chakula cha kweli, na damu yangu ni kinywaji cha kweli.

Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu hukaa ndani yangu, nami hukaa ndani yake.

Kama vile Baba aliye hai alivyonituma mimi, nami ni hai kwa Baba: kadhalika naye mwenye kunila atakuwa hai kwa mimi” (Yohana 6:53–57).

Dhana kuu ya badiliko (au toba) ilitokea kwangu pale nilipojifunza kuhusu msisitizo mkubwa kwenye familia katika mafundisho ya Kanisa. Nilikuja kupenda ushauri ambao Bwana aliutoa kupitia manabii Wake kote katika vipindi vya maongozi ya Mungu ikiwa ni pamoja na maelekezo na ahadi zilizotolewa kupitia Musa:

“Na maneno haya ninayokuamuru leo, yatakuwa katika moyo wako:

Nawe uwafundishe watoto wako kwa bidii, na kuyanena uketipo katika nyumba yako, na utembeapo njiani, na ulalapo, na uondokapo.

Yafunge yawe dalili juu ya mkono wako, nayo yatakuwa kama utepe katikati ya macho yako.

Tena yaandike juu ya miimo ya nyumba yako, na juu ya malango yako” (Kumbukumbu la Torati 6:6–9).

“Sikiza basi, Ee Israeli, ukaangalie kuzitenda; upate kufanikiwa, mpate kuongezeka sana, kama Bwana, Mungu wa baba zako, alivyokuahidi, katika nchi ijaayo maziwa na asali” (Kumbukumbu la Torati 6:3).

Tulifanya kazi pamoja—mke wangu Gladys pamoja nami—kuanzisha utamaduni wa kila siku wa sala ya familia na kusoma na kujadili kutoka kwenye mafundisho ya Kitabu cha Mormoni. Tulifanya juhudi za kukutana pamoja mara kwa mara kadiri tulivyoweza kila wiki kwa ajili ya jioni ya familia nyumbani. Wakati Familia: Tangazo kwa Ulimwengu lilipopokelewa mnamo 1995, nilifurahi kwamba ningeweza kutoa ushuhuda binafsi wa kweli ambazo manabii na mitume walio hai walizitangaza kwenye tangazo kwa sababu nilikuwa nimeshuhudia zikitokea kwenye familia yangu mwenyewe:

“Furaha katika maisha ya familia itapatikana kwa urahisi ikiwa imejengwa katika mafundisho ya Bwana Yesu Kristo. Ndoa na familia zenye ufanisi zimejengwa na kukuzwa katika misingi ya imani, maombi, toba, msamaha, heshima, upendo, huruma, kazi na matendo mazuri ya maburudisho”.1

Imani yangu iliathiri maisha yangu ya kazi vilevile. Siku moja, msambazaji wa bidhaa kwa mwajiri wangu aliingia ofisini kwangu na kuniambia kwamba alikuwa ameniletea “zawadi ndogo” kama shukrani kwa ajili ya manunuzi ambayo kampuni yake ilikuwa imeyapokea mwaka ule. Wakati huo nilikuwa nikisimamia idara ya manunuzi kwa vifaa vyote vya kutumika mara kwa mara. Nilimuuliza ikiwa yeyote kati ya wafanyakazi wangu alikuwa ameomba “zawadi ndogo” kutoka kwake. Alisema hakuna yeyote aliyefanya hivyo lakini ilikuwa ni tendo la kawaida kwa makampuni mengine aliyofanya nayo kazi. Nilimwomba abadili thamani ya “zawadi yake ndogo” kuwa bidhaa za ziada na kuzileta bila gharama kwenye stoo ya kampuni siku iliyofuata. Alishtuka waziwazi kwa jibu hili lakini alienda na kufanya vile.

Jaribu la imani yangu lilikuja katika hatua tofauti tofauti za maendeleo kwenye safari na lilikuwa moto wa kweli wa kusafisha. Katika tukio moja, nikihisi kukosewa na kuumizwa, nilijikuta nikizama kwenye kubadilishana maneno yasiyo ya kirafiki na mwanafamilia yangu hasa. Nilipotambua kile kilichokuwa kikiendelea niliamua kunyamaza na kuondoka eneo lile. Nilipoanza kuondoka, nilihisi kukemewa na Roho, hivyo nilirudi na kuomba msamaha kwa dhati kwa sehemu yangu katika kusababisha tukio. Kilichofuata kilikuwa ni machozi ya pamoja ya majuto kwa kile kilichokuwa kimetokea na msamaha wa dhati kwa kila mmoja.

Baada ya uzoefu wa kuishi injili nyumbani, fursa zilizofuata kwa ajili ya ukuaji wa kiroho zimekuja kutokana na kuwahudumia wengine kupitia miito ya Kanisa. Nilijifunza kwamba shangwe ya kudumu ya injili ipo katika kuwasaidia wengine kuipata na kurejea kwenye njia ya agano. Swali lililotolewa na Baba kwenye baraza kabla ya kuja duniani: “Nimtume nani” (Ibrahimu 3:27), ni la msingi katika kutambua baraka za milele za mbinguni. Nilipata shangwe tele katika kuwahudumia watakatifu isivyo rasmi katika nyumba zao na rasmi katika mikutano ya Kanisa.

Kwa muda mrefu nimetafakari picha ya Bwana mwishoni mwa huduma Yake duniani, akiwa amepigiliwa misumari msalabani angali akiwa hai, ikimsababisha Yeye kulia kwa Baba kwa uchungu. Ulikuwa wakati wa maumivu makali ya mwili kuliko ilivyowahi kufikirika kwa akili ya binadamu yaliyosababishwa na mkono wa mwanadamu. Ni wachache tu walioishi wakati huo waliweza kupata uzoefu kama huo. Kufikiria kwamba Bwana, wakati akivumilia hali hiyo, aligeuza fikra zake kutoka kwenye maumivu yake ya kutisha ili badala yake afokasi kwenye ustawi wa kiroho wa wasulubishaji wake—ni ushuhuda wa unyenyekevu Wake kamili kwa Baba na sheria Yake, na kwenye wokovu wa wanadamu Wenzake. Muda kitambo baadaye, sasa akiwa amefufuka na mshindi wa maumivu yote ya duniani daima nyuma Yake, Yeye alitangaza “Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani” (Mathayo 28:18).

Kupitia uzoefu Wake, nimetembea njia ambayo imenileta kwenye kujua mimi mwenyewe kwamba kupitia upatanisho wa Kristo aliye Bwana, ili kuwa mfuasi Wake, lazima niwe “kama mtoto, mtiifu, mpole, mnyenyekevu, mvumilivu, mwenye upendo tele, aliye tayari kukubali vitu vyote ambavyo Bwana ananipatia [mimi], hata kama vile mtoto hunyenyekea kwa baba yake” (Mosia 3:19), kwani Yeye alijinyenyekeza kwa Baba wa ulimwengu na wa uhai wote na alivishwa utukufu.

Kujifunza kuwa mfuasi ni kujiingiza kwenye safari inayodumu maisha yote. Ni safari ambayo huleta shangwe kuu kwenye moyo ikiwa itachukuliwa kwa bidii—licha ya vikwazo ambavyo mara zote hujificha njiani. Ni safari ambayo humleta mtu kwenye kumjua na kumpenda Bwana Yesu Kristo na kushangilia ndani Yake.

Joseph W. Sitati aliidhinishwa kama Sabini Mkuu mwenye Mamlaka mnamo Aprili 2009. Amemuoa Gladys Nangoni; wao ni wazazi wa watoto watano.

Muhtasari

  1. “The Family: A Proclamation to the World” (Tangazo kwa Familia), ChurchofJesusChrist.org.

Chapisha