2022
Kuishi Sheria ya Kufunga
Julai/Agosti 2022


UJUMBE WA KIONGOZI WA ENEO

Kuishi Sheria ya Kufunga

Kupitia imani, kufunga na sala, tulipata muujiza wetu.

Mnamo 2020, mimi na mume wangu tulikuwa tukitafuta pesa za kuwarejesha wana wetu wawili, Aaron na Musa nyumbani. Walikuwa punde wamemaliza masomo yao huko Bangalore (India), lakini juhudi zetu za kupata pesa za kuwarejesha nyumbani zilithibitisha kutokuwa na mafanikio. Hivyo, tuliamua kuliweka suala hili mikononi mwa Bwana.

Katika kipindi hicho kwa mwaka huo, janga la ulimwengu la Uviko-19 lilikuwa likienea Bangalore, kwa ongezeko la kasi ya maambukizi. Tulikuwa na hofu nyingi kuhusu wanetu.

Katika jioni ya Jumatano moja, baada ya kusali, nilihisi msukumo wa kufunga. Niliwaomba wana wangu wawili kuwa nami katika sala wakati nikiwa kwenye kufunga. Niliwaambia, “Wanangu, usiku wa leo tunakwenda kuomba muujiza ambao utamweka mjaribu kwenye aibu, kama vile Farao alivyowekwa kwenye aibu pale alipowashuhudia Waisraeli wakivuka kupita Bahari ya Shamu kwenye nchi kavu. Saa sita usiku, tutaamka, tutajiweka tayari na kuanza kusali.” Kwa upole nilimwambia mume wangu aniamshe saa 5:00 usiku kwa maelekezo kwamba nilikuwa na jambo la kufanya. Usiku ule, nilisoma maandiko, nikiimimina nafsi yangu katika sala nyingi na kutafakari juu ya maajabu ya Baba yetu wa Mbinguni. Siku iliyofuata, Bwana alijibu ombi letu kwa kutuma mtu kununua sehemu ya ardhi yetu. Tulikuwa tumemtafuta mnunuzi kwa miezi kumi na miwili iliyopita ili kupata pesa za kuwasafirisha wana wetu. Muujiza wetu ulikuwa umetendeka!

Mzee Joseph B. Wirthlin (1917–2008) alifundisha: “Bila sala, kufunga hakujakamilika kufunga; kunakuwa kushinda njaa tu. Ikiwa tunataka kufunga kwetu kuwe zaidi ya kushinda njaa tu, lazima tuiinue mioyo yetu, akili zetu na sauti zetu katika kuwasiliana na Baba yetu wa Mbinguni. Kufunga, kukiambatana na sala ya dhati, kunakuwa na nguvu. Kunaweza kujaza akili zetu kwa ufunuo wa Roho. Kunaweza kutuimarisha dhidi ya nyakati za majaribu.”1

Misheni ya wana wa Mosia ilikuwa yenye mafanikio kwa sababu walikuwa wamejitoa kwa sala na kufunga (ona Alma 17:3).

Isaya anatuambia leo jinsi tunavyopaswa kufunga, “Je! Saumu niliyoichagua, siyo ya namna hii? Kufungua vifungo vya uovu, kuzilegeza kamba za nira, kuwaacha huru walioonewa, na kwamba mvunje kila nira?” (Isaya 58:6).

Bwana Yesu Kristo anatushauri tusionekane na wanadamu kuwa tumefunga (ona Mathayo 6:18). Yeye pia aliwaambia Wanefi, “msiwe kama wanafiki, wenye nyuso za kuhuzunika, kwani hukunja nyuso zao ili waonekane wanafunga.Amin ninawaambia, wanayo thawabu yao” (3 Nefi 13:16).

Ninajua kwamba Yesu Kristo yu hai. Yeye ni Mkombozi na Mwokozi wetu. Analiongoza Kanisa Lake leo kupitia nabii aliye hai, Russell M. Nelson. “Tunapochagua kumwacha Mungu ashinde katika maisha yetu, tutapata uzoefu wetu wenyewe kwamba Mungu ni ‘Mungu wa Miujiza.’”2

Dada Delphine Marie Beatrice Mawang-Luko Muzama alizaliwa Kikwit (Bandundu, Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo). Yeye na mumewe ni wazazi wa watoto wanne na aliitwa kama Mshauri wa Taasisi wa Eneo mnamo Julai 2021.

Muhtasari

  1. Joseph B. Wirthlin, “Sheria ya Kufunga,” Mkutano Mkuu, Aprili 2001.

  2. Russell M. Nelson, “Acheni Mungu Ashinde,” Mkutano Mkuu, Oktoba 2020.