SAUTI ZA WAUMINI
Kanuni tukufu ya kujitegemea
Kile tukifanyacho leo ili kutekeleza kanuni ya kujitegemea kitatubariki sisi na familia zetu—leo na kesho.
Mzee Bednar wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili amesema, “Kuchukua hatua ni tendo la imani”.1 Hatua ya muhimu zaidi katika kujitegemea ni kuanza. Hata katikati ya changamoto ya Uviko-19, tunaweza kufanya kitu! Rais Russell M. Nelson alisema, katika Mkutano Mkuu wa Aprili 2020, “Bwana anapenda juhudi.”2 Na ahadi ni kwamba “Bwana atakuza juhudi zetu ndogo lakini za dhati.”3
Hatua ndogo katika kujitegemea sasa itapelekea hatua kubwa baadaye.
Dada Puati Odile kutoka Kinshasa, DRC, aliona kanuni hii ikifunuka katika maisha yake. Baada ya kuhitimu mafunzo ya kujitegemea, anasema “nilikuwa na wazo la kupanua mgahawa wangu wa Kikongo.” Aliamua kuhudhuria mafunzo ya upishi. “Niliongeza maarifa yangu ya sayansi ya mapishi, hivyo nilijifunza zaidi kuhusu mapishi ya kimataifa. Sasa naweza kupika mapishi ya Kiasia, Kiamerika, Kiulaya na Kiafrika,” anasema Dada Odile. “Darasa lilitusaidia kwa sababu tunaweza kupata pesa zaidi.” Sasa, “Tunajitegemea wenyewe; hakuna tunachokikosa. Tunalipa zaka zetu na matoleo na kusaidia familia zetu zote,” anasema.
Kaka Berhane Belay Wendem, anashiriki kwamba kupitia programu ya kutoa mbegu bila malipo, aliandaa shamba, akapanda na kuitunza mimea ambayo ilikua ana kuzaa chakula kwa ajili ya familia yake. Aliandaa kwa ajili ya mahitaji ya kiafya ya familia yake.
Dada Marceline Kukalukila Kunangika, kutoka Kinshasa, DRC, ni mke wa Patriaki wa Kigingi cha Kinshasa, Simon Lendo Vandam Wamande. Alipoulizwa kile familia yake ilifanya ili kuwa waaminifu, wenye kujiandaa na wenye kustahili ili kupokea wito mtakatifu wa Patriaki kutoka kwa Bwana, alisema, “Siku zote tunamuweka Bwana katika nafasi ya kwanza katika maisha yetu. Tulikubali wito wote kutoka kwa Bwana na kukuza wito huo katika njia zote tulizoweza. Tuliifundisha familia yetu kuishi kanuni za injili bila kujali chochote na kuwa mifano ya kustahili kwa kila mmoja na kwa jamii.” Hivyo, wito ulipokuja, familia ilikuwa imejijenga kujitegemea kiroho. Walikuwa wamejiandaa.
Ingawa anatoka kwenye familia yenye rasilimali chache, Dada Patience Ngalula, kutokea Kananga, DRC, alikuwa na ndoto ya kuwa mwandishi wa habari. Alihitimu masomo yake ya upili na kisha kujitolea kufanya kazi bila malipo katika kituo cha redio/televisheni. Alijifunza mambo mengi, na baada ya mwaka mmoja aliajiriwa katika kituo hicho cha redio. Alipata pesa ya kuisaidia familia yake na kufanikisha masomo yake ya weledi. “Sasa nina kazi nzuri katika kituo cha redio hapa Kinshasa ambapo maudhui yake yanalenga watoto. Ninabakia chanya, aliye tayari kutumikia na kujali ustawi wa wengine.”
Dada Elysee Buzangu na mumewe, Jean Claude, wanaishi Kinshasa. Wote wawili ni wamisionari walimaliza muda wao; waliamua kuanza kujiandaa kifedha mapema katika maisha yao ya ndoa. “Sote tulikuwa na kazi, na tulikuwa na nyumba mbili za kupangisha,” anasema Dada Buzangu. “Kwa miaka 20 ya ndoa, tumetoa dhabihu kubwa sana ili kwamba watoto wetu waweze kupata elimu na kuweza kutumikia misheni. Siri ya baraka zetu za kimwili na kiroho ni kulipa zaka zetu kila mara na kufanya kazi kwa bidii.”
Kama Watakatifu hawa walivyoshuhudia, juhudi zetu leo, iwe kubwa ama ndogo, hutusaidia sisi sote kuwa na furaha baadaye pale tunapokuwa watiifu kwa kanuni hii tukufu ya Kujitegemea.