“Klabu ya Kuwasaidia Watu,” Rafiki, Julai 2023, 20–21.
Klabu ya Kuwasaidia Watu
Josie alijua jinsi ambavyo angeweza kufuata mfano wa Yesu Kristo.
Hadithi hii ilitokea huko Marekani.
Josie aliketi pamoja na binamu yake chini ya mti nje ya nyumba yake.
“Natamani kungekuwa na jambo la kuburudisha ambalo tungeweza kufanya ili tupate pesa,” Josie alisema.
“Pengine tunaweza kupata pesa kwa kufanya mambo kwa ajili ya watu,” alisema Ashlyn.
“Itakuwa vipi ikiwa tutaifanya iwe klabu?” Josie aliruka kwa furaha. “Kama vile klabu ya kuwalea wanyama au klabu ya kuwatembeza mbwa.”
“Tunaweza kufanya mambo ya kila aina,” alisema Ashlyn. “Watu mara zote wanahitaji usaidizi. Na watatulipa.”
Ashlyn alikuwa sahihi. Kila siku Josie aliwaona watu waliohitaji usaidizi.
Ghafla Josie akapata wazo jingine. Alihisi vizuri moyoni. Lilimkumbusha kuhusu ubatizo wake mwaka jana. Aliahidi daima kumkumbuka Yesu na kufuata mfano Wake. Alifahamu njia moja ya kufanya hivyo.
“Vipi ikiwa tutakuwa na klabu inayowasaidia watu bila malipo?” Josie aliuliza. Hisia nzuri ziliongezeka.
Macho ya Ashlyn yalikuwa makubwa. “Hiyo hakika itakuwa burudani,” alisema. “Tunaweza kuwasaidia watu shuleni na kanisani—na popote pale.”
“Tunaweza kuiita Klabu ya Kuwasaidia Watu!” Josie alisema. “Ngoja tuanze kesho shuleni.”
Siku iliyofuata wakati wa mapumziko, Ashlyn na Josie walikimbia kwenye ukingo wa uwanja wa michezo.
“Je, unamwona yeyote tunayeweza kumsaidia?” Ashlyn alisimamia vidole vyake na kutazama kuelekea sehemu ya kutelezea yenye rangi ya upinde wa mvua yenye matuta.
“Hapana sijamwona.” Josie alitafuta kwenye vyuma vya bembea na kwenye bembea. Watoto walikuwa wakiteleza na kubembea. Walikuwa wakirusha mipira na kuchezea kamba za kurukia. Hakuna yeyote aliyeonekana kama alihitaji usaidizi. Kila mmoja alionekana kuwa na rafiki. Kisha alimwona msichana mdogo akiwa peke yake na kamba ya kurukia.
Josie aliushika mkono wa Ashlyn. “Tazama pale!”
Josie na Ashlyn walitafuta kamba za kurukia na walitembea kumuelekea msichana.
“Habari. Mimi ni Josie.”
“Na mimi ni Ashlyn. Jina lako ni nani?”
Msichana alionekana kushangazwa. “Naitwa Leslie.”
“Je, unataka kucheza nasi?” Josie aliinua juu kamba ya kurukia.
Leslie alitabasamu. “Ndiyo!”
Ashlyn na Josie walimfundisha Leslie baadhi ya njia mpya za kuruka kamba. Wakati kengele ilipogonga, waliagana. Josie alihisi vizuri moyoni. Alijua alikuwa ni Roho Mtakatifu.
Baada ya hilo, wakati wowote Josie na Ashlyn walipomwona Leslie ukumbini, walimsalimia.
Josie na Ashlyn waliwatafuta watu zaidi wa kuwasaidia. Wakati mwingine walisema mambo mazuri kwa watu na kujaribu kuwachangamsha. Wakati mwingine waliwaalika watoto wacheze pamoja nao.
Siku moja, Josie alimtabasamia mvulana nje ya shule. “Nimeipenda tisheti yako ya mjusi mkubwa,” alisema.
Mvulana alitabasamu na kutazama chini kwenye tisheti yake. “Asante.”
Josie alipoketi, alitambua hakuwa hata amefikiria kuhusu kufanya hilo kwa ajili ya klabu! Alikuwa amelifanya tu.
Josie aliwafikiria marafiki wote aliowapata tangu yeye na Ashlyn waanzishe klabu yao. Josie alipenda hasa kuwasaidia watu. Ilimfanya atake zaidi kufanya mambo mazuri kwa ajili ya wengine. Klabu ya Kuwasaidia Watu ilikuwa ikimfanya awe bora. Na hiyo ilikuwa hisia nzuri sana.