2023
“ Usafi Bustanini
Julai 2023


“Usafi Bustanini,” Rafiki, Julai 2023, 4–5.

Usafi Bustanini

“Nani tunaweza kumwalika asaidie pamoja nasi?”

Hadithi hii imetokea huko Uingereza.

Picha
Mama na mvulana wakiwa wamevalia glavu za bustanini na wakiwa wameshikilia mikasi.

Jonah alikula kiasi chake cha mwisho cha chakula na akatabasamu. Chakula cha jioni mara zote kilikuwa chenye kuburudisha wakati wamisionari walipokuja.

“Tunataka kushiriki nanyi ujumbe kuhusu huduma,” alisema Dada Kearl. “Kwa nini kuwahudumia wengine ni jambo muhimu?”

“Kwa sababu inamfanya Yesu awe na furaha!” alisema Eliza, dada mdogo wa Jonah.

“Uko sahihi! Inamfanya awe na furaha sana. Na tunapowasaidia wengine, inatufanya tuwe na furaha pia,” alisema Dada Christensen. “Je, mnamjua yeyote anayehitaji usaidizi?”

Jonah aliwaza kwa dakika. “Sina mtu yeyote ninayemfikiria, lakini bustani yetu shuleni ingeweza kupata usaidizi.”

“Wazo zuri,” alisema Mama.

Shule ya Jonah ina bustani ambapo wangeweza kufanya shughuli. Lakini hakuna aliyeshughulikia bustani kwa muda mrefu. Vichaka vilikuwa vimekua na kuyapita mazao. Palikuwa na magugu mengi pia.

“Tungependa kukusaidia katika hilo!” alisema Dada Kearl. “Nani tunaweza kumwalika asaidie kuisafisha pamoja nasi?”

“Binamu zetu!” alisema Jacob, kaka wa Jonah.

“Na darasa letu la Msingi,” alisema Jonah.

Siku iliyofuata, Mama alizungumza na mtu shuleni ili kupata ruhusa. Walichagua siku ya kusafisha bustani. Kisha Mama alimsaidia Jonah na ndugu zake kuwapigia simu binamu zao na darasa la Msingi.

Wiki chache baadaye, Jonah na familia yake walikutana na wamisionari shuleni. Binamu zao na marafiki wa Msingi walikuwepo pia. Ulikuwa muda wa kufanya kazi!

Jonah alivalia jozi ya glavu kubwa za mpira za bustanini. “Tazama, Mama Mikono yangu ni mikubwa!”

Mama alicheka. “Unaweza kutumia mikono hiyo mikubwa kusaidia kupunguza vichaka.”

Alimpa Jonah kifaa cha kukatia ambacho kilionekana kama mkasi mkubwa. Kisha alimsaidia kukata matawi yaliyokauka.

“Hii inafurahisha,” Jonah alisema.

Picha
Msichana na akina dada wamisionari wakiwa wameshikilia makoleo

Wakati Jonah akikata, Eliza alisaidia kulima kuzunguka bustani. Jacob alimsaidia Baba kujenga kiota kipya cha ndege. Wengine waling’oa magugu na kukusanya vijiti. Waliviweka kwenye mfuko wa plastiki wa rangi ya samawati. Hata kaka mdogo wa Jonah, Ezra, alisaidia kwa kuokota mawe.

Punde bustani ilikuwa safi. Jonah alihesabu mifuko waliyokuwa wameijaza. “Ona kuna mifuko 13!” alisema. “Tumesafisha uchafu mwingi sana.”

Dada Christensen alitabasamu. “Sasa tunahitaji nguvu ya kila mmoja kutusaidia kupeleka mifuko hii kwenye gari.”

Jonah, Jacob na Eliza kila mmoja alichukua mfuko. Jonah alihisi furaha pale aliponyanyua mfuko wa mwisho kuuweka kwenye gari. Kuwasaidia wamisionari ilikuwa ya kufurahisha. Alitaka pia kuwa mmisionari siku za baadaye. Hadi wakati huo, kulikuwa na njia nyingi ambazo kupitia hizo angeweza kuhudumu. Alisubiri kwa shauku kufikiria mradi wake ambao ungefuatia!

Picha
Alt text

Kielelezo na Samara Hardy

Chapisha