Daraja la kwenda kwenye Matumaini na Uponyaji
Kwa usaidizi unaofaa, waathiriwa wa unyanyasaji wa kijinsia wanaweza kupata uponyaji wanaotamani kwa dhati.
Hebu fikiria unasimama kwenye ukingo wa korongo na unataka kuvuka kwenda upande ule mwingine wa korongo kuu, ulikoelezwa kwamba kuna furaha kubwa inayokusubiri. Wakati unatafuta njia ya kuvuka, unaona rundo la vifaa ambavyo, ikiwa vitawekwa pamoja kwa njia inayofaa, vitajenga daraja la kuvuka korongo hilo.
Ikiwa haujui jinsi ya kujenga daraja, vifaa vile vitakuwa havina maana kwako kabisa nawe utajiona unachanganyikiwa na kukata tamaa. Lakini ikiwa utapata usaidizi kutoka kwa mtu aliye na uzoefu katika kujenga madaraja, ufahamu wako na kuelewa kwako kwaweza ongezeka na kwa pamoja kazi hiyo inaweza kukamilika.
Kwa muda wa miaka 18 iliyopita, kazi yangu imekuwa kutoa vifaa na mwongozo ili kuwasaidia watu kuvuka ghuba la mateso ya kihisia na kiakili. Kati ya wale watu wote ambao nimekwisha kuwashauri, hakuna wateja wengine ambao huja wakiwa wamejeruhiwa sana kama wale ambao wamekuwa waathirika wa unyanyasaji wa kijinsia. Nimeona athari ambayo changamoto hii inayo juu ya uwezo wa mtu huyo katika kuvumilia hadi mwisho.
Hata hivyo, nimekuja pia kujua ya kwamba msaada wa kudumu kutokana na mapambano na mateso yetu inawezekana kupitia kwa Mwokozi wetu. Upendo wake unawainua watu kutoka gizani na kuwaingiza katika nuru.
Ni Kwa nini Unyanyasaji wa Kijinsia Unasababisha Madhara Kama Haya?
Waathirika wa unyanyasaji hunielezea kuhusu maisha yaliyojawa na msongo wa mawazo, kutojiamini, na uchungu mwingine mkubwa wa kihisia. Rais Gordon B. Hinckley (1910–2008) alitusaidia kuelewa ni kwa nini unyanyasaji wa kijinsia husababisha maumivu makubwa hivi:
“Kuna tabia ya kutisha, na kutatanisha ya unyanyasaji wa kijinsia. Ni zaidi ya uwezo wa kuelewa. Ni fedheha kwa heshima ambayo inastahili kuwepo ndani ya kila mwanaume na mwanamke. Ni ukiukaji wa sheria ya kile kilicho kitakatifu na cha kiungu. Ni uharibifu katika maisha ya watoto. Ni ya kukemewa na yenye kustahili kulaaniwa vikali kabisa.
“Aibu kwa mwanaume au mwanamke yeyote anayemnyanyasa mtoto kijinsia. Kwa kufanya hivyo, mnyanyasaji hajeruhi tu katika njia mbaya zaidi. Yeye pia huwa na hatia mbele ya Bwana.”1
Uwezo wa kuumba maisha ni uwezo uliotukuka na ambao Mungu amewapa watoto Wake. Mzee David A. Bednar wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili alifundisha: Uwezo wa kuumba maisha ni muhimu kiroho. Baba yetu wa Mbinguni na Mwanawe Mpendwa ni waumbaji na wamemkabidhi kila mmoja wetu sehemu ya uwezo Wao wa kuumba.2 Si ajabu, hasa, kwamba kukiukwa kwa uwezo huu mtukufu kunastahili kushutumiwa vikali sana” na kunasababisha “majeraha makali zaidi ya aina hiyo i.”
Kuelewa Majeraha
Unyanyasaji wa kijinsia ni uhusiano bila idhini unaoshirikisha tabia za kugusa au tabia zisizo za kugusa ambapo mtu anatumika kwa kumridhisha mwingine kijinsia. Mara nyingi sana, waathirika wa unyanyasaji wa kijinsia huachwa na fikra za kuchanganyikiwa vile vile na hisia za kutokuwa wenye kustahili na aibu ambayo inaweza kufikia kuwa nzito zaidi kuvumilika. Uchungu na mateso ambayo waathiriwa hupitia mara nyingi huzidishwa na maoni ya watu wengine yanayotokana na kutoelewa unyanyasaji wa kijinsia na athari zake. Waathiriwa wengine hutuhumiwa kuwa wanadanganya au wanaambiwa kuwa unyanyasaji huo ulikuwa ni makosa yao wenyewe. Wengine kimakosa wanaongozwa kuamini ya kwamba ni lazima watubu, kama kwamba kwa njia fulani walikuwa wametenda dhambi kwa kuwa waathirika.
Wateja wengi ambao nimefanya kazi nao ambao walinyanyaswa kijinsia utotoni au ujanani mwao huambiwa “waachane na hayo,” au “samehe tu na usahau.” Matamshi ya aina hii—hasa wakati yanapotoka kwa marafiki wa karibu, wana familia, au viongozi wa Kanisa—yanaweza kumfanya mwathirika kuwa msiri zaidi na kuaibika badala ya kupona na kuwa na amani. Sawa tu na jeraha kubwa la kimwili au maambukizi, majeraha haya ya kihisia hayapotei tuu kwa kuyapuuza. Bali, kuchanganyikiwa kunakoanza wakati wa unyanyasaji kunazidi kuongezeka, na pamoja na hisia za uchungu zinazo fuaatia, fikra za mtu zaweza kubadilika, hatimaye kusababisha kuwepo kwa tabia zisizo bora. Sio ajabu kwa waathirika wa unyanyasaji kutojua kwamba kilicho watokea ilikuwa ni unyanyasaji, na wanaweza kuwa na tabia zisizo nzuri na hisia chungu.
Hannah (jina limebadilishwa) alinyanyaswa kijinsia mapema utotoni mwake. Kama waathiriwa wengine, alikua akijihisi kwamba alikuwa mtu mbaya asiye na thamani. Alitumia sehemu kubwa ya maisha yake akijaribu kuwahudumia wengine kiasi cha kufidia hisia zake za kutokuwa “mzuri vya kutosha” kwa Baba wa Mbinguni au mtu mwingine ye yote kumpenda. Katika uhusiano wake, aliogopa kwamba ikiwa mtu yeyote angejua kabisa ukweli juu yake, wangefikiria kuwa yeye ni mbaya kama vile yeye mwenyewe alivyoamini. Alihisi hofu kubwa sana ya kukataliwa ambayo ilimsababisha kuwa na uoga kujaribu mambo mapya maishani au kufanya majukumu madogo kama kumpigia mtu simu. Alikuwa amebarikiwa kwa kipaji cha sanaa lakini akakata tamaa kwa kuogopa kwamba hangeweza kustahimili kukosolewa.
Kwa zaidi ya miaka 50 hisia zake za unyonge, udhaifu, hofu, hasira, kuchanganyikiwa, aibu, upweke, na kujitenga ziliongoza maamuzi yake ya kila siku.
Kubadilisha Uchungu kuwa Amani
Mwokozi aliteseka maumivu na mateso na majaribu ya kila aina. Alifanya hivi ili kwamba Yeye “ajue kulingana na mwili jinsi ya kuwasaidia watu wake” (Alma 7:11–12). Mateso yake hayakuwa tu kwa ajili ya dhambi zetu lakini pia kwa ajili ya uponyaji wakati dhambi za mwingine zinapo sababisha kuteseka kwetu.
Ikiwa Yeye angekuwa hapa leo hii, ninafikiri Mwokozi angelia na kuwabariki wale walionyanyaswa kijinsia, kama vile alivyolia na kuwabariki Wanefi (ona 3 Nefi 17). Wakati Yeye hayuko hapa kimwili, Roho Wake anaweza kuwa nasi, na ametuandalia njia ya kupona, kujisikia amani, na kusamehe.
Kwa wengi ambao wameumizwa, dhana ya kuwa uchungu walio nao unaweza kubadilishwa na kuwa na amani ni kana kwamba haiwezekani kuaminika. Mara nyingi vidonda vya walionyanyaswa huwa havionekani na havitambuliwi na wengine kwa miaka mingi. Majeraha yanafunikwa na nyuso zenye tabasamu, utayari wao wa kuwasaidia wengine, na kuishi maisha kana kwamba hakuna chochote kibaya kilichofanyika, lakini bado uchungu ungalipo.
Wacha tulinganishe mchakato wa uponyaji wa kihisia na kuhudumia na kutibu jeraha la kimwili. Tuseme kwa mfano wakati ulipokuwa mchanga, ulivunjika mguu wako. Badala ya kwenda kwa daktari kupata matibabu, ulichechemea hadi uchungu huo mkubwa ulipo potea, lakini siku zote kuna uchungu kidogo kwa kila hatua unayochukua. Miaka kadhaa baadaye unahitaji uchungu huo uondoke kabisa, kwa hivyo unaenda kumwona daktari. Ni lazima daktari aupange upya mfupa, asafishe sehemu yoyote iliyokuwa imekua vibaya, aikate, na akupeleke kwa tabibu wa viungo vya mwili ili kuimarisha mguu wako.
Mchakato wa kupona kutokana na unyanyasaji ni sawa sawa na huu kwa vile muathirika ni lazima kwanza atambue kwamba uchungu ni wa kweli na kwamba kuna jambo linaloweza kufanyika juu ya uchungu huo. Mchakato unajumuisha kukiri kile kilichofanyika na kuruhusu hisia za kujeruhiwa, hofu, na huzuni lazima uzisikie, zitambuliwe, na kuthibitishwa. Mara nyingi inasaidia kufanya kazi na mtaalamu mwenye uzoefu katika mchakato huu wa uponyaji. (Mwulize kiongozi wako wa ukuhani ikiwa LDS Family Services inapatikana katika eneo lako.)
Muathirika awe au asiwe na uwezo wa kupata usaidizi wa mtalaamu, ni vyema kuomba, soma kuhusu maisha ya Mwokozi na Upatanisho Wake, na kuonana mara kwa mara na kiongozi wako wa ukuhani. Anaweza kusaidia kupunguza mizigo na kupokea maongozi ya kumsaidia mwathirika kuelewa thamani yake tukufu na uhusiano wake na Baba wa Mbinguni na Mwokozi. Dada Carole M. Stephens, Mshauri wa Kwanza katika Urais Mkuu wa Muungano wa Usaidizi wa Wakina Mama hivi karibunu alifundisha “Uponyaji waweza kuwa mchakato mrefu. Itakuhitaji kwa maombi utafute mwongozo na usaidizi unaofaa, ikiwa ni pamoja na kushauriwa na wenye ukuhani waliotawazwa ipasavyo. Unapojifunza kuwasiliana wazi wazi, weka mipaka inayofaa na pengine tafuta ushauri nasaha. Kudumisha afya ya kiroho katika mchakato huo wote ni muhimu!”3
Kwa Hannah, maisha yake yalikuwa yamekosa faraja kiasi cha kwamba alitafuta usaidizi. Alijua kutokana na ushuhuda wake ya kwamba angeweza kujisikia amani na kuridhika maishani mwake lakini hakujisikia hivyo katika hali endelevu. Kupitia maombi na kuzungumza na askofu wake, alielekezwa kupata ushauri nasaha, ambapo aliweza kupata vifaa alivyohitaji ili kutoa ukweli kutoka gizani na kushirikiana na mnasihi mzigo mbaya aliokuwa akibeba pekee yake. Katika kufanya hivyo, aliweza kuachilia uchungu na kupata amani iliyo ahidiwa na Mwokozi (ona Yohana 14:27). Pamoja na amani hii na faraja kulikuja hamu na uwezo wa kusamehe.
Haja ya Kusamehe
Dhana ya kusamehe mara nyingi huwa ngumu kwa waathirika wa unyanyasaji kusikia na mara nyingi huwa inaeleweka vibaya. Ikiwa watafikiria kwamba kusamehe ni kama kumwachilia mkosaji aende zake au kusema ya kwamba kile walichokifanya kwa sasa si tatizo tena, muathirika atajiona hatambuliki. Huku tukiwa tumeamriwa kusamehe (ona M&M 64:10), katika hali ambazo majeraha ni makubwa, uponyaji kawaida lazima uanze kabla ya muathirika hajaweza kumsamehe mnyanyasaji kikamilifu.
Wale ambao wanateseka kwa uchungu ulio sababishwa na unyanyasaji wanaweza kupata faraja katika ushauri huu kutoka Kitabu cha Mormoni: “Mimi, Yakobo, nitawazungumzia wale walio safi moyoni. Mtegemeeni Mungu kwa mawazo yaliyo imara, na mwombeni kwa imani kubwa, na Yeye atawafariji katika mateso yenu, na atatetea teto zenu, na kuwateremshia hukumu wale wanaotaka kuwaangamiza” (Yakobo 3:1). Haja ya haki na haki ya kurejeshewa vyaweza kuachwa kwa Bwana ili Yeye aweze kubadilisha majeraha yetu kuwa amani.
Hannah hatimaye aligundua ya kwamba angeweza kumwachia Mwokozi kutaka kwake haki na kama malipo angepata hisia ya amani maishani mwake kwa jinsi ambavyo hajawahi kujisikia hivyo hapo awali. Mwanzoni alikuwa anaogopa kuhudhuria mikutano ya familia ambapo alijua mnyanyasaji wake angekuwepo. Sasa, kwa sababu ya kuwa kwake tayari kukabiliana na majeraha magumu ya kihisia akiwa njiani kuelekea uponyaji, sasa hana hofu tena ya kuwa katika uwepo wake na anaweza hata kumhurumia yeye katika umri wake wa uzee.
Huru kutokana na Mizigo Isiyohitajika
Mzee Richard G. Scott (1928–2015) wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili alisema ya kwamba “uponyaji kamili utakuja kupitia imani yako katika Yesu Kristo na nguvu Zake na uwezo Wake, kupitia Upatanisho Wake, kuponya makovu ya kile kisicho cha haki na kisichostahili. …
“Anakupenda. Alitoa uhai Wake ili uwe huru na mizigo isiyohitajika. Yeye atakusaidia kufanya hivyo. Ninajua kwamba anao uwezo wa kukuponya.”4
Adui anataka kuwashikilia watu wakiwa wamefungwa kwa uchungu na mateso kwa sababu yeye ni mwenye huzunii (ona 2 Nefi 2:27). Kwa usaidizi wa Mwokozi, Yesu Kristo, uchungu waweza hakika kubadilishwa na kuwa amani, kama vile tu Mwokozi anavyoweza kutoa, nasi tunaweza kuishi kwa shangwe. “Adamu alianguka ili wanadamu wawe; na wanadamu wapo, ili wapate shangwe” (2 Nefi 2:25). Kuishi kwa shangwe kutatuwezesha nyakati za majaribu kuvumilia zaidi na kutuwezesha kujifunza na kukua na kuzidi kuwa kama Baba wa Mbinguni.
Nimenyenyekezwa na baraka niliyokuwa nayo maishani mwangu kuketi na wale wote waliojeruhiwa na unyanyasaji na kuona muujiza wa uponyaji unaokuja tu kupitia kwa Mwokozi. Ikiwa unateseka, tafadhali kwa maombi geuka upate usaidizi. Hauhitaji kubeba mzigo huo mzito pekee yako. Ninajua Yeye huponya, kwani nimeshuhudia haya mara nyingi sana.