Vitabu Vilivyo sahaulika, Ushuhuda Unao kumbukwa
Mwandishi anaishi Cagayan, Ufilipino.
Macho yote yalinitizama. Je, ninaweza kulitetea Kanisa kwa ushuhuda wangu rahisi?
Mwaka mmoja, nilikuwa na lengo la kuboresha kujifunza kwangu kiroho. Ningebeba vitabu vyangu vya Kanisa, makabrasha, vitabu vya kiada, na maandiko kila mahali, ikiwa ni pamoja na shuleni, kwa maana nilipata njaa ya neno la Mungu. Lakini juhudi zangu zilipunguka wakati nilipokuwa na kazi nyingi nikijisomea kwa ajili ya mtihani uliokuwa unakaribia.
Siku moja mwalimu wetu aliongoza majadiliano ambapo aliwauliza wanafunzi wote wasio Wakatoliki chumbani mle wasimame. Nilikuwa Mtakatifu wa Siku za Mwisho pekee yangu mle darasani. Wanafunzi wengine sita walisimama.
Kisha tukaulizwa: Nyinyi ni waumini wa kanisa gani? Ni nani alikuwa mwanzilishi wake? Kanisa lenu lilianzishwaje?
Nilikuwa wa mwisho kujibu. Nilikuwa na wasiwasi nilipogundua sikuwa nimebeba vitabu vyangu vya Kanisa, lakini nilijaribu kukumbuka yale niliyokuwa nimejifunza. Kifungu cha maandiko kilinijia akilini:
Mtumaini Bwana kwa moyo wako wote, Wala usizitegemee akili zako mwenyewe.
“Katika njia zako zote mkiri yeye, Naye atayanyosha mapito yako” (Mithali 3:5–6).
Nilisimama darasani kwa ujasiri na kusahau hofu yangu. Nilisema kwamba mimi nilikuwa muumini wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho. Nilisimulia simulizi ya mvulana mdogo, Joseph Smith, ambaye alimwona Mungu. Nilihisi moyo wangu ukiwaka, machozi yalinitoka machoni. Nilieleza ya kwamba Kanisa lilianzishwa mnamo Aprili 6, 1830, na nilishuhudia ya kwamba nabii wa Mungu alikuwa ameitwa na ukuhani kurejeshwa. Nilishuhudia ya kwamba nilijua kwamba yote haya yalikuwa ya kweli.
Muda huu mrefu wa kusoma injili ulikuwa na thamani yake. Ulikuwa umeniwezesha kutetea imani yangu na kushirikiana na wengine injili. Niliona fahari wakati, wiki kadhaa baadaye, wanne kati ya marafiki zangu walijiunga nami kanisani.
Tukio hilo lilinifundisha umuhimu wa ushuhuda. Mara ya kwanza niliwaza kwa nini Bwana hakuwa amenitia msukumo nibebe vitabu vyangu siku hiyo. Vingenisaidia kikamilifu kujibu maswali yaliyokuwa yakiulizwa. Lakini niligundua kwamba hatuhitaji kukariri kila kitu kuhusu Kanisa au kutegemea dondoo—tunapaswa kusoma, kuishi, na kushirikiana na wengine injili, tukimtegemea Roho Mtakatifu. Sikuwa na vitabu vyangu, lakini nilikuwa na ushuhuda wangu.