2017
Vita Vinaendelea
April 2017


Vita Vinaendelea

Vita ambavyo vilianza mbinguni bado vinaendelea hadi siku hii ya leo. Kwa kweli, vita vinakuwa vikali kadiri Watakatifu wanapojitayarisha kwa ajili ya kurudi kwa Mwokozi.

clouds

Picha na Katarina Stefanovic © iStock/Getty Images; Moment/Getty Images

Mtu yeyote anayefuata habari za kimataifa atakubali ya kwamba tunaishi katika nyakati za “vita na minong’ono ya vita” (M&M 45:26). Kwa bahati nzuri, kila mtu duniani ni mkongwe wa vita. Tumekuwa tukipigana na majeshi ya uovu katika vita vinavyoendelea ambavyo vilianza katika ulimwengu wa kabla ya kuzaliwa duniani.

Kwa sababu hatukuwa tumepokea miili, tulipigana Vita hivyo vya Mbinguni bila sime, au bunduki, au mabomu. Lakini mapigano hayo yalikuwa makali tu kama vita vya kisasa, na kulikuwa na mabilioni ya majeruhi.

Vita vya kabla ya kuzaliwa vilipiganwa kwa maneno, mawazo, mijadala, na ushawishi (ona Ufunuo 12:7–9, 11). Mbinu ya Shetani ilikuwa ni kuwatisha watu. Alijua kwamba hofu ni mbinu bora ya kuharibu imani. Anaweza kuwa alitumia hoja kama hizi: “Ni ngumu sana.” “Haiwezekani kurudi ukiwa msafi.” “Kuna hatari kubwa sana.” “Unajuaje kama unaweza kumwamini Yesu Kristo?” Alimwonea wivu sana Mwokozi.

Kwa shukrani, Mpango wa Mungu uliushinda uongo wa Shetani. Mpango wa Mungu ulishirikisha haki ya maadili ya kujiamulia kwa ajili ya binadamu na dhabihu kuu. Jehova, anajulikana kwetu kama Yesu Kristo, alijitolea kuwa dhabihu hiyo—ili ateseke kwa ajili ya dhambi zetu. Alikuwa radhi kufa kwa niaba ya kaka zake na dada zake ili wale ambao wangetubu wangerudi wakiwa wasafi na hatimaye kuwa kama Baba yao wa Mbinguni. (Ona Musa 4:1–4; Ibrahimu 3:27.)

Faida nyingine ambayo ilimsaidia Jehova kushinda mioyo ya watoto wa Mungu ni ushuhuda wa nguvu uliotolewa na wafuasi Wake, wakiongozwa na Mikaeli, malaika mkuu (ona Ufunuo 12:7, 11; M&M 107:54). Katika maisha ya kabla ya kuja duniani, Adamu aliitwa Mikaeli, na Shetani aliitwa Lusiferi, linalomaanisha “mbeba nuru.”1 Hilo laweza kuonekana kama jina la ajabu kwa mfalme wa giza (ona Musa 7:26), lakini maandiko yanafundisha ya kwamba Shetani alikuwa “malaika wa Mungu aliyekuwa mwenye mamlaka katika uwepo wa Mungu” kabla ya kuanguka (ona M&M 76:25–28).

Ni namna gani roho mwenye elimu na uzoefu mwingi angeanguka mbali hivyo? Ilikuwa kwa sababu ya kiburi chake. Lusiferi aliasi dhidi ya Baba yetu wa Mbinguni kwa sababu aliutaka ufalme wa Mungu uwe wake.

Katika hotuba yake maarufu “Jihadhari na Kiburi,” Rais Ezra Taft Benson (1899–1994) alifundisha ya kwamba Lusiferi “alitaka kuheshimiwa zaidi ya wengine wote” na hiyo “hamu ya kiburi chake ilikuwa ni kumpindua Mungu.”2 Umesikia pia kwamba Shetani alitaka kuharibu haki ya mwanadamu ya kujiamulia, lakini hiyo sio sababu pekee iliyomfanya aanguke kutoka kwenye neema ya Mungu. Alifukuzwa kutoka mbinguni kwa sababu ya uasi dhidi ya Baba na Mwana (ona M&M 76:25; Musa 4:3).

Ni kwa nini wewe na mimi tulipigana dhidi ya ibilisi? Tulipigana kutokana na utiifu. Tulimpenda na kumuunga mkono Baba yetu aliye Mbinguni. Tulitaka kuwa kama Yeye. Lusiferi alikuwa na lengo tofauti. Alitaka kuchukua nafasi ya Baba (ona Isaya 14:12–14; 2 Nefi 24:12–14). Hebu fikiria jinsi usaliti wa Shetani ulivyowaumiza Wazazi wetu wa Mbinguni. Katika maandiko, tunasoma ya kwamba, “mbingu zililia juu yake” (M&M 76:26).

Baada ya kampeni kali, Mikaeli na majeshi yake walishinda. Theluthi mbili ya majeshi ya mbinguni walichagua kumfuata Baba (ona M&M 29:36). Shetani na wafuasi wake walifukuzwa kutoka mbinguni, lakini hawakupelekwa mara moja nje gizani. Kwanza, walitumwa hapa duniani (ona ufunuo 12:7–9), ambapo Yesu Kristo angezaliwa na ambapo dhabihu yake ya upatanisho ingetendeka.

Ni kwa nini majeshi ya Shetani yaliruhusiwa kuja duniani? Walikuja kutoa upinzani kwa wale waliokuwa wakijaribiwa hapa (ona 2 Nefi 2:11). Je hatimaye watatupwa nje gizani? Ndiyo. Baada ya Milenia, Shetani na majeshi yake watatupwa nje milele.

Shetani anajua siku zake zimehesabiwa. Wakati wa Ujio wa Pili wa Yesu, Shetani na malaika wake watafungwa kwa kipindi cha miaka 1000 (ona Ufunuo 20:1–3; 1 Nefi 22:26; M&M 101:28). Wakati tarehe hiyo ya mwisho inapokaribia, majeshi ya uovu yanapigana mno ili kuteka nafsi nyingi iwezekanavyo.

Yohana Mfunuzi alionyeshwa Vita vya Mbinguni kama sehemu ya maono makubwa. Alionyeshwa jinsi Shetani alivyotupwa duniani kuwajaribu wanadamu. Hii ndilo itikio la Yohana: “Ole kwa wakazi wa nchi na wa bahari! Kwa maana yule Ibilisi ameshuka kwenu mwenye ghadhabu nyingi, akijua ya kuwa ana wakati mchache tu” (Ufunuo 12:12).

Kwa hiyo ni namna gani Shetani anatumia wakati wake, akijua hana wakati wa kupoteza? Mtume Petro aliandika “ibilisi, kama simba angurumaye, huzunguka-zunguka, akitafuta mtu ammeze” (1 Petro 5:8).

family kneeling in prayer

Ni kipi kinamchochea Shetani? Kamwe hatawahi kuwa na mwili, hatawahi kuwa na mke au familia, na hatawahi kuwa na ukamilifu wa shangwe, kwa hivyo anataka kuwafanya wanaume na wanawake wote “wawe na huzuni kama yeye” (2 Nefi 2:27).

Shetani huwalenga wanadamu wote, lakini hasa wale walio na uwezo mkubwa wa kuwa na furaha ya milele. Ni wazi kuwa anamwonea wivu mtu yeyote aliye katika njia ya kuinuliwa. Mafundisho yanatufundisha ya kwamba Shetani “hufanya vita na watakatifu wa Mungu, na kuwazingira” (M&M 76:29).

Vita ambavyo vilianza mbinguni vinaendelea hadi hii leo. Kwa kweli, vita vinakuwa vikali kadiri Watakatifu wanapojitayarisha kwa ajili ya kurudi kwa Mwokozi.

Rais Brigham Young (1801–77) alitabiri “kwamba Kanisa lingeenea, fanikiwa, kukua na kupanuka, na kuwa kwa uwiano na ueneaji wa Injili kwa mataifa ya ulimwengu, pia nguvu za Shetani zingeongezeka.”3

Ninafikiri sisi sote tutakubali kwamba utabiri huu unatimizwa huku tukiona uovu ukipenya katika jamii za dunia. Rais Young alifundisha kwamba tunahitaji kujifunza mbinu za adui ili tuweze kumshinda. Ninashirikiana nanyi mbinu nne za Shetani ambazo zimethibitika na mawazo kadhaa kuhusu jinsi unavyoweza kumpinga.

Mbinu za Shetani

1. Majaribu. Shetani hana haya ikija katika kuweka mawazo maovu akilini mwetu. Kitabu cha Mormoni kinafundisha kwamba Shetani hunong’ona mawazo machafu na ya uhasama na kupanda fikra za mashaka. Yeye hutusumbua ili tuitikie haja za kutawaliwa na tukubali uchoyo na ulafi. Hataki tutambue kule ambapo mawazo haya yanatoka, kwa hivyo ananong’ona, “Mimi sio ibilisi, kwani ibilisi hayupo” (2 Nefi 28:22).

Ni namna gani tunaweza kupinga majaribu haya ya moja kwa moja? Moja ya zana yenye mafanikio zaidi ni kumfukuza. Hivyo ndivyo Yesu angefanya.

Hadithi moja ya Mwokozi katika Agano Jipya akiwa juu ya mlima wa majaribu ni ya kuelimisha. Baada ya kila jaribu ibilisi alijitokeza Kwake, Yesu alitumia mbinu ya hatua mbili ili kujikinga: kwanza, alimwamuru Shetani aondoke; kisha akanukuu maandiko.

Wacha nikupe mfano: “Nenda zako, Shetani,” aliamuru Yesu, “kwa maana imeandikwa, Msujudie Bwana Mungu wako, umwabudu yeye peke yake” (Mathayo 4:10). Aya inayofuata inaandika, “Kisha Ibilisi akamwacha; na tazama, wakaja malaika wakamtumikia” (Mathayo 4:11). Kinga ya Mwokozi ilikuwa ya ufanisi mno!

Wasifu wa Rais Heber J. Grant (1856–1945) unatupa maarifa jinsi Rais Grant, kama mvulana mdogo alivyompinga ibilisi. Wakati Rais Grant alipotambua kwamba Shetani alikuwa akimnong’oneza, akijaribu kupanda shaka ndani ya moyo wake, alisema tu kwa sauti kubwa, “Bwana Ibilisi, nyamaza.”4

Una haki ya kumwambia Shetani aondoke wakati unapokabiliwa na jaribu. Maandiko yanafundisha, “Mpingeni Shetani, naye atawakimbia” (Yakobo 4:7).

Sehemu nyingine ya kinga ya Mwokozi ilikuwa kunukuu maandiko. Kuna nguvu kubwa katika kukariri maandiko, jinsi Yesu alivyofanya. Aya za kimaandiko zaweza kuwa ghala la silaha za kiroho.

Unapojaribiwa, unaweza kutamka amri kama hizi kama vile “Ikumbuke siku ya Sabato uitakase,” “Wapendeni adui zenu,” au “na wema uyapambe mawazo yako bila kukoma” (Kutoka 20:8; Luka 6:27; M&M 121:45). Nguvu za maandiko hazimtishi tu Shetani, lakini pia zinaleta Roho ndani ya moyo wako, ambaye anakuthibitishia, na kukuimarisha dhidi ya majaribu.

2. Uongo na Udanganyifu. Maandiko yanadhihirisha kuwa Shetani ni “baba wa uwongo” (2 Nefi 9:9). Usimwamini anaponong’ona uwongo ujumbe kama “Hakuna unalofanya sawa,” “Wewe ni mwovu sana kiasi cha kutosamehewa,” “Hutaweza kubadilika,” “Hakuna anayekujali,” na “Hauna vipaji vyovyote.”

Moja kati ya uongo wake anaotumia sana ni ufuatao: “Unahitaji kujaribu kila kitu angalau mara moja—ili tu upate uzoefu. Mara moja haitakuumiza.” Siri ndogo chafu asiyotaka ufahamu ni kuwa dhambi inalevya.

Uongo mwingine utumikao ambao Shetani ataujaribu juu yako ni: “Kila mtu anafanya hivyo. Ni SAWA.” Si SAWA! Kwa hivyo mwambie Shetani kwamba hutaki kwenda katika ufalme wa telestia—hata ikiwa watu wengine wote wanaenda huko.

father teaching his family

Ingawa Shetani atakudanganya, unaweza kumtegemea Roho akueleze ukweli. Hiyo ndiyo sababu kipawa cha Roho Mtakatifu ni muhimu.

Ibilisi ameitwa “mdanganyifu mkuu.”5 Yeye hujaribu kutengeneza vitu vya bandia vya kila kanuni ambayo Bwana huleta.

Kumbuka vitu vya bandia sio sawa na vitu vilivyo kinyume chake. Kinyume cha nyeupe ni nyeusi, lakini kitu cha bandia cheupe chaweza kuwa nyeupe kiasi au kijivu. Vitu vya bandia hufanana na vitu halisi ili kuwadanganya watu wasiotia shaka. Ni toleo la udanganyifu kinyume na kitu kizuri, kama vile pesa bandia, haina thamani. Wacha niwaonyeshe.

Mojawapo ya kitu bandia cha Shetani kwa imani ni ushirikina. Kitu bandia cha upendo ni tamaa. Yeye hutengeneza ukuhani bandia kwa kuanzisha ukuhani wa uongo, na huigiza miujiza ya Mungu kwa kutumia uchawi.

Ndoa kati ya mwanamume na mwanamke imetakaswa na Mungu, lakini ndoa ya jinsia moja ni ya bandia. Haileti watoto wala kuinuliwa. Ingawaje vitu vyake vya bandia huwadanganya watu wengi, sio vya kweli. Haiwezi kuleta furaha ya kudumu.

Bwana altuonya kuhusu vitu bandia katika Mafundisho na Maagano. Alisema, “Kile kisichojenga siyo cha Mungu, nacho ni giza” (M&M 50:23).

3. Ubishi. Shetani ndiye baba wa ubishi. Mwokozi anafundisha, “Huchochea mioyo ya watu kubishana na hasira mmoja kwa mwingine” (3 Nefi 11:29).

Ibilisi amejifunza kutokana na karne nyingi za uzoefu kwamba mahali ambapo pana ubishi, roho wa Bwana ataondoka. Kutoka alipomshawishi Kaini kumuua Habili, Shetani amewashawishi ndugu kugombana. Yeye pia huchochea matatizo katika ndoa, miongoni mwa washiriki wa kata, na baina ya wamisionari. Anafurahia kuona watu wazuri wakigombana. Yeye hujaribu kuanzisha ugomvi katika familia Jumapili kabla ya kanisa, kabla ya jioni ya familia nyumbani Jumatatu usiku, na kila mara wana ndoa wanapanga kuhudhuria kikao cha hekaluni. Majira yake ni ya kutabirika.

Wakati kunapokuwa na ubishi nyumbani kwako au kazini, mara moja wacha unachofanya na utafute kuleta amani. Bila kujali nani alianzisha.

Ubishi mara nyingi huanza na kutafuta makosa. Joseph Smith alifundisha ya kwamba “ibilisi hutusifu sana kwamba sisi ni wenye haki sana, wakati tunapozungumzia makosa ya wengine.”6 Wakati unapofikiria juu ya hilo, kujiona mwenye haki ni bandia ya haki ya ukweli.

Shetani anapenda kueneza ubishi Kanisani Ana utaalamu katika kuonesha dosari za viongozi wa Kanisa? Joseph Smith aliwaonya Watakatifu ya kwamba mwanzo wa ukengefu ni kupoteza imani katika viongozi wa Kanisa.7

Karibu fasihi zote za kupinga uMormoni msingi wake ni uongo kuhusu tabia ya Joseph Smith. Adui hufanya bidii kumfedhehesha Joseph kwa sababu ujumbe wa Urejesho unategemea historia ya Nabii kuhusu yale yaliyotendeka katika KisituKitakatifu. Shetani anafanya bidii zaidi siku hizi kuliko awali kuwafanya waumini watie shaka ushuhuda wao juu ya Urejesho.

Katika siku za mwanzoni mwa kipindi chetu hiki cha maongozi ya Mungu, ndugu wengi katika uongozi wa ukuhani, kwa majuto yao, hawakubaki waaminifu kwa Nabii. Mmoja wao alikuwa Lyman E. Johnson, ambaye alitengwa na Kanisa kwa mienendo yake ambayo haikuwa ya haki. Baadaye aliomboleza akiwa ameliasi Kanisa: “Ningekubali mkono wangu wa kulia ukatwe, ikiwa ningeamini tena. Kisha nilikuwa nimejawa na shangwe na furaha. Ndoto zangu zilikuwa nzuri. Wakati nilipoamka asubuhi roho yangu ilikuwa yenye furaha. Nilikuwa mwenye furaha mchana na usiku, nikiwa nimejawa na amani na shangwe na shukrani. Lakini sasa ni giza, uchungu, majonzi, mateso yaliyokithiri. Tangu wakati huo sijaona kipindi cha furaha.”8

Tafakari juu ya maneno hayo. Yanasimama kama onyo kwa waumini wote wa Kanisa.

Mimi ni mwongofu kwa Kanisa. Nilibatizwa wakati nikiwa na miaka 23 kijana mzima ambaye hajaoa nikisoma katika shule ya udaktari kule Arizona, Marekani. Ninajua moja kwa moja jinsi Shetani anavyofanya kazi juu ya wachunguzi katika kuwachanganya na kuwakatisha tamaa wakati wanapotafuta ukweli.

Katika ujana wangu wote, nilikuwa nikitazama mifano ya marafiki zangu Watakatifu wa Siku za Mwisho. Nilivutiwa na namna walivyo yaongoza maisha yao. Nilifanya uamuzi wa kujifunza zaidi juu ya Kanisa, lakini sikutaka kumwambia yeyote nilikuwa najifunza Umormoni. Ili kuepuka kusumbuliwa na marafiki zangu, niliamua kufanya uchunguzi wangu kuwa wa kibinafsi.

Hii ilikuwa miaka mingi kabla ya tovuti, kwa hiyo nilienda katika maktaba ya umma. Nilipata nakala ya Kitabu cha Mormoni na kitabu kinachoitwa A Marvelous Work and a Wonder, na Mzee LeGrand Richards (1886–1983) wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili. Nilianza kuvisoma vitabu hivi kwa hamu kubwa, na vilinitia msukumo.

Wakati roho yangu ilipokuwa ikitaka kujifunza zaidi, Shetani alianza kunong’oneza sikioni mwangu. Aliniambia kwamba ili niweze kuwa mkweli kabisa, nilihitaji kusoma yale yaliyoandikwa na wakosoaji wa Kanisa pia. Nilirudi kwenye maktaba ya umma na kuanza kuangalia kote. Hakika, nilipata kitabu kilichomfedhehesha Nabii Joseph.

Kukisoma kitabu hiki dhidi ya Mormoni kulinichanganya. Nilipoteza yule roho mzuri na ushawishi uliokuwa umeongoza upelelezi wangu. Nilikata tamaa na nilikuwa karibu kuacha uchunguzi wangu wa ukweli. Nilikuwa naomba nipate jibu huku nikisoma fasihi dhidi ya Mormoni!

Kwa mshangao wangu, nilipokea simu kutoka kwa rafiki yangu mmoja aliyekuwa akisoma Chuo Kikuu cha Brigham Young. Alinialika niende nikamtembelee kule Utah, akiahidi kwamba ningefurahia safari hiyo ya kuvutia macho. Hakuwa anajua nilikuwa nikichunguza Kanisa lake kwa siri.

Nilikubali mwaliko wake. Rafiki yangu alipendekeza twende Jijini Salt Lake tukatembee Temple Square. Alishangazwa na mwitikio wangu wa shauku. Hakujua ni namna gani nilikuwa na hamu ya kujifunza ukweli juu ya Joseph Smith na Urejesho.

Kina dada wamisionari katika Temple Square walikuwa wenye usaidizi mkubwa. Bila ya kujua, walijibu maswali yangu mengi. Ushuhuda wao ulinishawishi “kujibu [zangu] tuhuma,”9 na imani yangu ilianza kukua. Thamani ya ushuhuda wa kutoka moyoni haiwezi kupuuzwa.

Rafiki yangu pia alishirikiana nami ushuhuda wake na kunialika niombe na nimwulize Mungu ikiwa Kanisa lilikuwa la kweli. Katika safari hiyo ndefu kurudi Arizona, nilianza kusali kwa imani—kwa mara ya kwanza “na kwa moyo wa kweli, na kusudi halisi” (Moroni 10:4). Wakati fulani katika safari hiyo, ilionekana kama kuwa gari langu lilikuwa limetiwa nuru na mwanga. Nilijifunza kuwa mwanga unaweza ukaondoa giza.

Baada ya kuamua kubatizwa, Shetani alianza mapambano ya mwisho. Alijaribu familia yangu, ambao walifanya kila kitu katika uwezo wao kunikatisha tamaa, na walikataa kuhudhuria ubatizo wangu.

Nilibatizwa hata hivyo, na pole pole mioyo yao ilifanywa kuwa laini. Walianza kunisaidia kuchunguza historia ya familia yangu. Miaka michache baadaye, nilimbatiza ndugu yangu mdogo. Rafiki ambaye alinialika nimtembelee kule Utah sasa ni mke wangu.

4. Kuvunjika Moyo. Shetani hutumia kifaa hiki kwa ufanisi kwa Waaminifu wakati mengine yote yanapokuwa yameshindwa. Kwangu mimi, wakati ninapoanza kuhisi kuvunjika moyo, ni ya manufaa kwangu kutambua ni nani anajaribu kuniangusha. Hili linanifanya nikasirike kiasi cha kuchangamka—ili tu nimchukize ibilisi.

Miaka kadhaa iliyopita, Rais Benson alitoa hotuba iliyoitwa “Msikate Tamaa.” Katika hiyo hotuba ya kugusa hisia, alionya, “Shetani anazidi kujitahidi kuwashinda watakatifu na kukata tamaa, kuvunjika moyo, kufa moyo, na huzuni.”10 Rais Benson aliwahimiza waumini wa Kanisa kuwa macho, na akawapa mapendekezo 12 ya kweli ya kukabiliana na kuvunjika moyo.

family walking on Boston Massachusetts Temple grounds

Mapendekezo yake yanajumuisha kuwahudumia wengine; kufanya kazi kwa bidii na kuepukana na kuwa wavivu; kuwa na tabia nzuri za kiafya, hii ikiwa ni pamoja na kufanya mazoezi na kula vyakula katika hali yake halisi; kutafuta baraka za ukuhani; kusikiliza muziki unaotia msukumo; kuhesabu baraka zako; kuweka malengo. Na juu ya yote, jinsi maandiko yanavyotufundisha, tunapaswa kusali siku zote ili tuweze kumshinda Shetani (ona M&M 10:5).11

Shetani hutetemeka wakati anapomwona

Mtakatifu mdhaifu kabisa akiwa amepiga magoti.12

Ni muhimu kujua ya kwamba kuna mipaka ya nguvu za uovu. Uungu huweka mipaka hiyo, na Shetani hajaruhusiwa kuivuka. Kwa mfano, maandiko yanatuhakikishia ya kwamba “kwani uweza haujatolewa kwa Shetani wa kuwajaribu watoto wadogo” (M&M 29:47).

Kizuizi kingine kikubwa ni kwamba Shetani hajui mawazo yetu hadi tumwambie. Bwana alieleza, “Hapana yeyote ila Mungu ambaye hujua mawazo yako na dhamira ya moyo wako” (M&M 6:16).

Pengine hii ndiyo maana Bwana ametupa amri kama vile “Usinung’unike” (M&M 9:6) na “Usimseme jirani yako uovu, wala usimdhuru” (M&M 42:27). Ikiwa unaweza jifunza kuuzuia ulimi wako kwa hatamu (ona Yakobo 1:26), mwishowe hutampa shetani maelezo mengi sana. Wakati anaposikia kunung’unika, kulalamika, na kukosoa, yeye kwa uangalifu huandika. Maneno yako hasi yanafichua udhaifu wako kwa adui.

Nina habari njema kwenu. Majeshi ya Mungu ni mengi zaidi kuliko ya Lusiferi. Unaweza ukaangalia kote na ufikirie wewe mwenyewe, “Dunia inageuka kuwa ovu na ovu zaidi. Shetani ni lazima anashinda vita.” Usidanganywe. Ukweli ni kwamba, tunamshida adui kwa idadi. Kumbuka, theluthi mbili ya watoto wa Mungu walichagua mpango wa Bwana.

Kaka zangu na dada zangu, hakikisheni ya kwamba mnapigana katika upande wa Bwana. Hakikisha ya kwamba umebeba upanga wa Roho.

Ni ombi langu kwamba mwishoni mwa maisha yenu, mweze kusema pamoja na Mtume Paulo, “Nimevipiga vita vilivyo vizuri, mwendo nimeumaliza, Imani nimeilinda” (2 Timotheo 4:7).

Muhtasari

  1. Mwongozo wa Maandiko, “Lusiferi,” scriptures.lds.org.

  2. Ezra Taft Benson, “Beware of Pride,” Ensign, Mei 1989, 5.

  3. Discourses of Brigham Young, sel. John A. Widtsoe (1954), 72.

  4. Ona Francis M. Gibbons, Heber J. Grant: Man of Steel, Prophet of God(1979), 35–36.

  5. Ona, kwa mfano, Dieter F. Uchtdorf, “You Matter to Him,” Liahona, Nov. 2011, 20; Gordon B. Hinckley, “The Times in Which We Live,” Liahona, Jan. 2002, 86.

  6. Teachings of Presidents of the Church: Joseph Smith (2007), 369

  7. Ona Teachings: Joseph Smith, 318.

  8. Lyman E. Johnson, in Brigham Young, Deseret News, Aug. 15, 1877, 484.

  9. Dieter F. Uchtdorf, Njoo, Jiunge Nasi, Liahona, Nov. 2013, 23.

  10. Ezra Taft Benson, “Do Not Despair,” Ensign, Nov. 1974, 65.

  11. Ona Ezra Taft Benson, “Do Not Despair,” 65–67.

  12. William Cowper, in Robert Andrews, comp., The Concise Columbia Dictionary of Quotations (1987), 78.