Upatanisho wa Mwokozi: Msingi wa Ukristo wa Kweli
Kutoka katika hotuba, “The Atonement,” iliyotolewa wakati wa semina ya marais wapya wa misheni katika Kituo cha Mafunzo ya Wamisionari cha Provo mnamo Juni 24, 2008.
Sisi sote tutafufuliwa na kuishi milele kwa sababu ya dhabihu ya Yesu Kristo ya kulipia dhambi.
Nabii Joseph Smith (1805–44) aliulizwa, “Ni zipi kanuni za kimsingi za dini yako?” Yeye alijibu “Kanuni za msingi za dini yetu ni ushuhuda wa Mitume na Manabii, kuhusu Yesu Kristo, kwamba alikufa, akazikwa, na akafufuka tena siku ya tatu, na amepaa mbinguni; na mambo yote mengine ambayo yanahusiana na dini yetu ni viambatisho tu.”1
Ninataka kutoa sauti yangu juu ya kauli ya Nabii Joseph. Kitovu cha yote tunayoamini ni Mwokozi na dhabihu Yake ya kulipia dhambi zetu—“ufadhili wa Mungu” (1 Nefi 11:16) ambapo Baba alimtuma Mwana Wake duniani kutimiza Upatanisho. Kitovu cha kusudio la maisha ya Yesu Kristo lilikuwa ni kukamilisha dhabihu ya kulipia dhambi. Upatanisho ni msingi wa Ukristo wa kweli.
Ni kwa nini Upatanisho wa Mwokozi ni kanuni kuu katika Kanisa na maishani mwetu?
Makala ya Imani 1:3
Makala ya tatu ya imani inasema, “Tunaamini kwamba kwa njia ya Upatanisho wa Kristo, wanadamu wote wanaweza kuokolewa, kwa kutii sheria na ibada za Injili.”
“Kuokolewa” katika muktadha huu ina maana kufikia kiwango cha juu zaidi cha utukufu katika ufalme wa selestia. Ufufuko umetolewa kwa kila anayekuja duniani, lakini ili kupokea uzima wa milele, zile baraka kamili za makuzi ya milele, kila mtu ni lazima atii sheria, apokee ibada, na afanye maagano ya injili.
Kwa nini ni Yesu Kristo, na ni Yeye pekee, ambaye aliweza kulipia dhambi za ulimwengu? Yeye ndiye aliyekuwa na sifa zote.
Mungu Alimpenda na Kumwamini
Yesu alizaliwa kwa Wazazi wa Mbinguni katika ulimwengu wa kabla ya duniani. Yeye alikuwa Mzaliwa wa Kwanza wa Baba yetu wa Mbinguni. Yeye aliteuliwa kutoka mwanzo. Alkuwa mtiifu kwa mapenzi ya Baba Yake. Maandiko mara nyingi huzungumzia furaha ya Baba wa Mbinguni aliyo nayo kwa Mwana Wake.
Katika Mathayo tunasoma, “Na lo, akasikia sauti kutoka mbinguni, ikisema, Huyu ni Mwanangu mpendwa, ninayependezwa naye” (Mathayo 3:17).
Luka anaandika, “Sauti ikatoka katika wingu, ikisema, Huyu ni Mwanangu, mteule wangu, msikieni yeye” (Luka 9:35).
Na hekaluni katika nchi ya Neema kufuatia Ufufuko wa Mwokozi, watu waliisikia sauti ya Baba: “Tazama Mwana wangu Mpendwa ninayependezwa na yeye” (3 Nefi 11:7).
Hilo hasa linagusa moyo wangu wakati ninaposoma kwamba wakati Yesu alipokuwa akiteseka katika Bustani ya Gethsemani, Baba, kutokana na upendo Wake mkubwa na huruma kwa Mwana Wake wa Pekee, alimtuma malaika amfariji na amuimarishe (ona Luka 22:43).
Yesu Alitumia Haki yake ya Kujiamulia Kutii
Yesu Alihitajika kutoa uhai Wake kwa hiari Yake kwa ajili yetu.
Katika Baraza kuu la Mbinguni, Lusiferi, “mwana wa asubuhi” (Isaya 14:12; M&M 76:26–27), alisema:
Tazama, niko hapa, nitume mimi, nitakuwa mwanao, nami nitawakomboa wanadamu wote, ili hata nafsi moja isipotee, na hakika nitatenda hivyo; kwa sababu hiyo nipe mimi heshima yako.
“Walakini, tazama, Mwanangu Mpendwa, ambaye alikuwa Mpendwa na Mteule tangu mwanzo, aliniambia—Baba, mapenzi yako na yatimizwe, na utukufu uwe wako milele na milele” (Musa 4:1–2; ona pia Ibrahimu 3:27).
Kwa sababu ya upendo mkubwa Mwana alio nao kwa Baba Yake na kwa kila mmoja wetu, Alisema, “Nitume mimi. Wakati Aliposema “nitume mimi, Alitumia haki Yake ya kujiamulia.
Kama vile Baba anijuavyo, nami nimjuavyo Baba. Nami nautoa uhai wangu kwa ajili ya kondoo.
“Ndiposa Baba anipenda, kwa sababu nautoa uhai wangu ili niutwae tena.
“Hakuna mtu aniondoleaye, bali mimi nautoa mwenyewe. Nami ninao uweza wa kuutoa, ninao na uweza wa kuutwaa tena. Agizo hilo nalilipokea kwa Baba yangu.” (Yohana 10:15, 17–18).
Kama Mwokozi angelitaka, majeshi ya malaika wangeweza kumtoa msalabani na kumpeleka moja kwa moja hadi kwa Baba Yake. Lakini alitumia haki Yake ya kujiamulia ili kujitoa dhabihu kwa ajili yetu, kukamilisha misheni Yake katika mwili wenye kufa, na kustahmili hadi mwisho, akikamilisha dhabihu ya kulipia dhambi.
Yesu alitaka kuja duniani, na Alikuwa mwenye sifa zilizostahili. Na wakati Alipokuja, Alisema, “Kwa kuwa mimi sikushuka kutoka mbinguni ili niyafanye mapenzi yangu, bali mapenzi yake aliyenipeleka.” (Yohana 6:38).
Yesu Aliteuliwa Kabla
Petro alifundisha kwamba Yesu “naye amejulikana kweli tangu zamani, kabla haijawekwa misingi ya dunia” (ona 1 Petro 1:19–21).
Manabii katika vipindi vyote vya maongozi ya Mungu walitabiri kuhusu kuja kwa Yesu Kristo na lengo la Misheni Yake. Kwa njia ya imani kubwa, Henoko alionyeshwa maono ya ajabu kuhusu kuzaliwa, kufa, Kupaa, na Ujio wa Pili wa Mwokozi:
Na tazama, Henoko aliiona siku ile ya kuja kwa Mwana wa Mtu, hata katika mwili; na roho yake ilifurahia, akisema: Mwenye haki ameinuliwa juu, na Mwanakondoo amechinjwa tangu kuwekwa kwa msingi wa ulimwengu.
“Na Bwana akamwambia Henoko: Angalia, naye akaangalia na akamwona Mwana wa Mtu ameinuliwa juu ya msalaba, kwa jinsi ya wanadamu;
Naye akasikia sauti kubwa; na mbingu zikafunikwa kwa pazia; na viumbe wote wa Mungu waliomboleza; nayo dunia ikiugulia; na miamba kupasuka; na watakatifu wakiamka, na kuvikwa taji mkono wa kuume wa Mwana wa Mtu, kwa mataji ya utukufu.
Na Henoko akamwona Mwana wa Mtu akapaa juu kwa Baba.
Na ikawa kwamba Henoko aliiona siku ya kuja kwa Mwana wa Mtu, katika siku za mwisho, kukaa juu ya dunia katika haki kwa kitambo cha miaka elfu (Musa 7:47, 55–56, 59, 65).
Takriban miaka 75 kabla ya kuzaliwa kwa Kristo, Amuleki alishuhudia: “Tazama, nawaambia, kwamba najua kwamba Kristo atakuja miongoni mwa watoto wa watu, kujitwalia makosa ya watu, na kwamba atalipia dhambi za ulimwengu; kwani Bwana Mungu amesema” (Alma 34:8).
Yesu Alikuwa na Sifa za Kipekee
Ni Yesu Kristo pekee ambaye angeweza kutekeleza dhabihu ya kulipia dhambi—akiwa amezaliwa na mama mwanadamu, Maria, na akiwa amepokea nguvu za uzima kutoka kwa Baba Yake (ona Yohana 5:26). Kwa sababu ya nguvu hizi za uzima, Alishinda mauti, nguvu za kaburi zilibatilishwa, na akawa Mwokozi na Mpatanishi na Bwana wa Ufufuko—njia ambayo kwayo tunapata wokovu na uwezo wetu sisi sote wa kuishi milele. Tutafufuliwa na kuishi milele kwa sababu ya dhabihu ya Yesu Kristo ya kulipia dhambi.
Yesu kwa Hiari Yake Alilipia Dhambi ya Asili
Makala ya pili ya imani inasema, “Tunaamini kwamba wanadamu wataadhibiwa kwa ajili ya dhambi zao wenyewe, na siyo kwa ajili ya uvunjaji sheria wa Adamu.”
Kupitia matumizi ya haki yetu ya kujiamulia, sisi tunachagua kutumia imani yetu. Kwa bidii, tunaweza kutubu; bila Upatanisho, hatuwezi.
Katika Musa tunafundishwa, “Kuanzia hapa ukaenea msemo miongoni mwa watu, kwamba Mwana wa Mungu amelipia hatia ya asili, ambayo ni kuwa dhambi za wazazi haziwezi kujibiwa juu ya vichwa vya watoto” (Musa 6:54).
Katika 2 Nefi tunapewa mafunzo muhimu sana:
“Kwani kifo kimekuja juu ya wanadamu wote, ili kutimiza mpango wa huruma wa Muumba mkuu, inahitajika lazima pawe na nguvu ya ufufuko, na inahitajika lazima ufufuko umfikie mwanadamu kwa sababu ya anguko; na anguko lilitokana na uvunjaji sheria; na kwa sababu hiyo mwanadamu akawa ameangukaa wakawa wametengwa mbali na uwepo wa Bwana.
“Kwa sababu hivyo, unahitajika kuwe na upatanisho usio na kipimo—bila huu upatanisho usio na kipimo huu uharibifu hauwezi kuvaa kutoharibika. Kwa sababu hivyo, hukumu ya kwanza iliyompata mwanadamu lazima ingekuwa kwa muda usio na mwisho. Na kama ni hivyo, miili hii lazima ingelala chini kuoza na kurudi mavumbini ilikotoka, bila kufufuka tena” (2 Nefi 9:6–7).
Yesu Alikuwa Kiumbe Pekee Mkamilifu
Katika Mafundisho na Maagano, Mwokozi Anasema, “Baba, tazama mateso na kifo chake yeye ambaye hakutenda dhambi, ambaye ulipendezwa naye; tazama damu ya mwanao iliyomwagika; damu yake yeye ambaye ulimtoa ili upate kutukuzwa” (M&M 45:4).
Yesu ni binadamu wa pekee ambaye alikuwa mkamilifu, bila dhambi. Dhabihu katika Agano la Kale ilikuwa na maana dhabihu ya damu—ikionyesha mbele hadi dhabihu ya Bwana na Mwokozi wetu akiwa msalabani akitimiza dhabihu ya kulipia dhambi. Wakati dhabihu za damu zilizokuwa zikifanywa katika mahekalu ya kale, makuhani walitoa kafara kondoo asiye na ila, mkamilifu katika kila njia. Mwokozi mara nyingi anasomwa katika maandiko kama mwana kondoo wa Mungu kwa sababui ya usafi Wake (ona, kwa mfano, Yohana 1:29, 36; 1 Nefi 12:6; 14:10; M&M 88:106).
Petro alifundisha kwamba tunakombolewa kwa damu ya thamani, kama ya mwana-kondoo asiye na ila, asiye na waa, yaani, ya Kristo (1 Petro 1:19).
Yesu Kristo Aliziondoa Dhambi za Dunia
Aya zifuatazo zinaonyesha wazi kwamba kwa njia ya Upatanisho Wake, Mwokozi alilipia dhambi zetu:
Sisi sote, kama kondoo, tumepotea; kila mmoja wetu amegeukia njia yake; na Bwana amemwekea maovu yetu sisi sote (Mosia 14:6).
Bali Mungu aonyesha pendo lake yeye mwenyewe kwetu sisi, kwa kuwa Kristo alikufa kwa ajili yetu, tulipokuwa tungali wenye dhambi.
Kwa maana ikiwa tulipokuwa adui tulipatanishwa na Mungu kwa mauti ya Mwana wake; zaidi sana baada ya kupatanishwa tutaokolewa katika uzima wake.
Wala si hivyo tu, ila pia twajifurahisha katika Mungu kwa Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye kwa yeye sasa tumeupokea huo upatanisho.
Kwa sababu kama kwa kuasi kwake mtu mmoja watu wengi waliingizwa katika hali ya wenye dhambi, kadhalika kwa kutii kwake mmoja watu wengi wameingizwa katika hali ya wenye haki. (Warumi 5:8, 10–11, 19).
Ili litimie lile neno lililonenwa na nabii Isaya, akisema, Mwenyewe aliutwaa udhaifu wetu, Na kuyachukua magonjwa yetu (Mathayo 8:17).
Lakini Mungu hakomi kuwa Mungu, na rehema hudai wanaotubu, na rehema huja kwa sababu ya upatanisho; na upatanisho huleta ufufuo wa wafu; na ufufuo wa wafu huwarudisha watu kwenye uwepo wa Mungu; na hivyo wanarudishwa kwenye uwepo wake, kuhukumiwa kulingana na matendo yao, kulingana na sheria na haki.
Na hivyo Mungu hutimiza kusudi lake kubwa na la milele, ambalo lilitayarishwa kutokea msingi wa dunia. Na hivyo huja wokovu na ukombozi wa binadamu, na pia maangamizo yao na taabu. (Alma 42:23, 26).
Yesu Alivumilia hadi Mwisho
Yesu Alivumilia majaribu, mateso, dhabihu, na dhiki za Gethsemani, pamoja na kuteseka kwake kule Golgotha msalabani. Kisha, hatimaye, Aliweza Kusema, Imekwisha (Yohana 19:30). Alikuwa amekamilisha kazi Yake akiwa katika hali ya mauti na kuvumilia hadi mwisho, hivyo basi kukamilisha dhabihu ya kulipia dhambi.
Katika bustani Alisema, Baba yangu, ikiwezekana, kikombe hiki kiniepuke; walakini si kama nitakavyo mimi, bali kama utakavyo wewe. (Mathayo 26:39).
Katika Mafundisho na Maagano tunafundishwa:
Mateso ambayo yalisababisha Mimi mwenyewe, hata Mungu, mkuu kuliko wote, kutetemeka kwa sababu ya maumivu, na kutoka damu kwenye kila kinyweleo, na kuteseka mwili na roho—na kutamani nisinywe kikombe kichungu, na kusita—
Hata hivyo, utukufu na uwe kwa Baba, na Mimi nikachukua na kukamilisha maandalizi yangu kwa wanadamu” (M&M 19:18–19).
Yesu Alimwambia Baba Yake, “Mimi nimekutukuza duniani, hali nimeimaliza kazi ile uliyonipa niifanye” (Yohana 17:4).
Kisha, msalabani, “basi Yesu alipokwisha kuipokea ile siki, alisema, Imekwisha. Akainama kichwa, akaisalimu roho yake” (Yohana 19:30).
Yesu alikuja duniani, akasalia na Uungu Wake ili Yeye aweze kutekeleza ile dhabihu ya kulipia dhambi, na kuvumilia hadi mwisho.
Mkumbukeni Yeye kwa njia ya Sakramenti
Leo tunakumbuka dhabihu ya Mwokozi ya kulipia dhambi kwa kutumia ishara za maji na mkate—ishara ya mwili na damu Yake—kama ilivyoanzishwa wakati wa Karamu ya Mwisho ya Bwana akiwa na Mitume Wake.
“Akatwaa mkate, akashukuru, akaumega, akawapa, akisema, Huu ndio mwili wangu unaotolewa kwa ajili yenu; fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu.
“Kikombe nacho vivyo hivyo baada ya kula; akisema, Kikombe hiki ni agano jipya katika damu yangu, inayomwagika kwa ajili yenu” (Luka 22:19–20).
Katika Yohana 11:25–26 tunasoma:
“Mimi ndimi huo ufufuo, na uzima. Yeye aniaminiye mimi, ajapokufa, atakuwa anaishi:
“Naye kila aishiye na kuniamini hatakufa kabisa hata milele.”
Tunasoma pia: “Mimi ndimi chakula chenye uzima kilicho shuka kutoka mbinguni; mtu akila chakula hiki, ataishi milele. Na chakula nitakacho toa mimi ni mwili wangu, kwa ajili ya uzima wa ulimwengu” (Yohana 6:51).
“Uzima wa ulimwengu” ina maana uzima wa milele
Tunahitaji kujitayarisha pamoja na familia zetu kila wiki ili kuwa wenye kustahili kushiriki sakramenti na kujazwa na Roho Mtakatifu.
Baba na Mwana Wanatupenda Sisi
Baba alimtuma Mwanawe duniani—ufadhili—kumruhusu Yeye kusulubiwa na kupitia yale yote ambaye Yeye aliyohitaji kuyapitia. Katika Yohana tunasoma:
Yesu akamwambia, Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi.
Kama mngalinijua mimi, mngalimjua na Baba; tangu sasa mnamjua, tena mmemwona (Yohana 14:6–7).
Hili ndilo pendo, si kwamba sisi tulimpenda Mungu, bali kwamba yeye alitupenda sisi, akamtuma Mwanawe kuwa kipatanisho kwa dhambi zetu (1 Yohana 4:10).
Kipatanisho inamaanisha maridhiano au kuridhisha.
Hitimisho
Kila anayekuja duniani na kupokea mwili wenye kufa atafufuliwa, lakini ni lazima tufanye bidii ili tupate baraka ya kuinuliwa kupitia uaminifu wetu, haki yetu ya kujiamulia, utiifu wetu, na toba yetu. Huruma itatolewa pamoja na haki, kuruhusu toba.
Kwa sababu tumechagua kumfuata na kumkubali Yesu Kristo kama Mkombozi, tunajichukulia jina Lake juu yetu tunapobatizwa. Tunajichukulia sheria ya utiifu. Tunaahidi ya kwamba tutamkumbuka daima na kushika amri Zake. Tunaweka upya maagano yetu wakati tunapopokea sakramenti.
Kwa kufanya upya maagano yetu, tunapewa ahadi ya Roho Wake kuwa pamoja nasi daima. Ikiwa tutamruhusu Roho Wake aje maishani mwetu na atuongoze, tunaweza kurudi katika uwepo wa Baba wa Mbinguni na Mwanawe, Yesu Kristo, ambao huu ni mpango Wao kwa ajili ya furaha yetu sisi—ule mpango wa wokovu.