Albamu ya Zamani ya Familia: Nguvu ya Hadithi za Kifamilia
Mwandishi anaishi New York, Marekani.
Urithi wa mababu zangu unaendelea kuishi kupitia mimi, daima ukishawishi maisha yangu kuwa bora.
Asubuhi moja wakati wa kiangazi kabla ya Vita vya Pili vya Dunia, baba wa babu yangu aliamka kama afanyavyo siku zote—kabla ya jua kuchomoza. Alitoka nje ya nyumba yake kwenye kilima kilichokuwa juu ya bonde la kijani kibichi la kijiji chake kule Romania, na akaketi kwenye nyasi zilizo funikwa na umande wa asubuhi mapema, akiwa amezama katika mawazo yake— mawazo yale yale ambayo yalikuwa akilini mwake kwa muda sasa. Mwanaume aliyeelimika mwenye moyo mkarimu na akili dadisi, alipendwa na kuheshimiwa na kila mtu katika kijiji.
Baada ya jua kuchomoza, alienda nyumbani na kukiri kwa mkewe kwamba amekuwa na hamu ya kutaka kujua mazishi yake yangekuwa ya aina gani, na alitaka kufanya mazoezi ya mavazi yake ya mazishi. Alipanga tarehe, akanunua jeneza, akakodisha kuhani na waombolezaji wenye taaluma, na akapata vifaa vingine vyote vinavyohitajika katika tamaduni Halisi ya Kiothodoksi ya Kigiriki. Kisha siku ya mazishi ya kuigiza ikafika. Meza ziliandaliwa katikati ya kijiji kwa ajili ya karamu ya makumbusho, familia yote ilikuwa imevalia nguo nyeusi, kuhani akaja, baba wa babu yangu akajilaza ndani ya jeneza, akigeuza mto ili aweze kuonekana vizuri, na kisha maandamano ya mazishi yakaanza. Wakati sherehe ilipokamilika, kijiji kizima kilialikwa kwenye karamu, na baba wa babu yangu alitimiza ndoto yake ya kucheza ngoma katika mazishi yake. Aliishi miaka mingine 20, mara kwa mara akichunguza kuona ikiwa jeneza lake bado lilimtosha.
Siyo tu Majina na Tarehe
Sijawahi kukutana na baba wa babu yangu , lakini simulizi yake siku zote imekuwa yenye kunipendeza zaidi ambayo niliambiwa na babu na bibi yangu. Kila siku babu na bibi zangu wangetueleza ndugu zangu na mimi simulizi kuhusu mababu zetu wa kale: kule walikotoka, jinsi walivyokuwa, maadili yao, ndoto na matumaini. Baada ya mlo wa kila Jumapili, babu na bibi yangu wangechukuwa albamu ya familia, na kwa kufungua kila ukurasa, simulizi zilitolewa na mioyo iliunganishwa pamoja katika pambo la upendo kwa muda wa vizazi sita. Hazikuwa tu ni picha kuu kuu zilizokuwa zimeandikwa majina na tarehe upande wa nyuma. Nyuma ya kila sura kulikuwa na baba au mama, mwana au binti, ndugu au dada, na hivyo basi ukawa urithi wao, ikiwa ni pamoja na tamaduni nyingine za familia, nilizorithishwa.
Nguvu Katika Nyakati za Majaribu
Wakati nilipokuwa nafika umri wa miaka 19, wazazi wangu na wengi kati ya wana familia wangu wa karibu walikuwa wameaga dunia na mali nyingi niliyokuwa nimerithi ilipotea au kuibiwa. Na bado kuna kitu kimoja ambacho muda, majanga ya asili, au hata kifo hakiwezi kuharibu: daraja linalounganisha siku zilizopita, wakati wa sasa, na siku zijazo ambazo kila mmoja wa wana familia wangu walijenga. Kwa sababu ya bidii yao, nyuzi zinazounganisha mioyo ya familia yangu pamoja imenipa nguvu ya kushinda hali ngumu.
Wakati wazazi wangu na babu na bibi zangu walpoikufa, nilihisi huzuni kubwa sana kiasi cha kwamba niliwaza kama nitakuwa na nguvu za kutosha kuendelea kuishi. Nilibarikiwa kuhisi ushawishi wao kutoka upande huo mwingine wa pazia, na hiyo ilinisaidia kupata ushuhuda wa nguvu kuhusu mpango wa wokovu, kuhusu maisha baada ya kifo, na kisha baadaye, kuhusu ibada za hekaluni ambazo ni muhimu sana kwa ajili ya wokovu wetu. Kamwe sikuwahi kukutana na mababu zangu wakuu au wengi wa mashangazi na wajomba zangu, lakini kila wakati ninapoichukuwa albamu kongwe ya familia iliyo na picha zao, ninajiona mimi mwenyewe machoni mwao. Niko jinsi nilivyo kwa ajili ya wale walionitangulia. Uzoefu wao na hekima yao vimesaidia kujenga tabia yangu na kuniongoza maishani.
Mojawapo ya zawadi kubwa ambayo familia yangu ilinipa tangu mapema utotoni ni ufahamu wa historia ya familia yangu na imani ya kwamba mimi ni kiungo baina ya siku zilizopita na siku zijazo. Pia ninajua ya kwamba nilikuja duniani kuishi maisha yangu—kuchunguza na kujifunza na kuyathamini. Ni ufahamu huu wa historia ya familia yangu ambao unanisaidia kupitia majaribu yote ya maisha.
Mimi hufikiria mara kwa mara kuhusu familia yangu iliyo upande mwingine wa pazia na dhabihu ambazo walifanya kwa niaba yangu ili niweze kuwa na maisha bora. Ninafikiria kuhusu ibada za hekaluni ambazo zinatuwezesha kuwa pamoja tena kama familia siku moja. Na ninafikiria kuhusu Upatanisho wa Mwokozi wangu, aliyefanya kuwezekana kwa haya yote. Alilipa fidia ili tuweze kuishi. Kwa sababu hii tunampenda na kumwabudu Yeye kwa shukrani leo na milele.