2017
Kujitayarisha kwa ajili ya Safari Mpya
April 2017


Kujitayarisha kwa ajili ya Safari Mpya

Mwandishi anaishi Paraná, Brazili.

Kama vile Nefi alivyosafiri kwa meli kuelekea asiko kujua, vivyo hivyo mimi nilihitaji kuwa na imani kwa Bwana kuhusu kuanzisha familia.

sail boat on the water

Picha © Getty Images

Katika wiki zilizotangulia ndoa yangu na kuunganishwa hekaluni, nilianza kuwa na wasi wasi kidogo kuhusu mambo yote ambayo nilihitaji kufanya kabla ya kuanzisha familia yangu mpya. Licha ya furaha hiyo yote ya wakati huo, nilijihisi nimefadhaika kuhusu kuandaa utaratibu wetu mpya, kupanga hali yetu ya kifedha, kutafuta sehemu ya kuhifadhi mali yetu, na majukumu yangu mapya kama mke. Nilitaka kuhakisha ya kwamba tulianza ndoa yetu kwa njia sahihi kwa kutengeneza nafasi katika maisha kwa ajili ya shughuli muhimu kama vile kushika amri na kupata muda wa kuwa pamoja kama mume na mke licha ya maisha yetu yenye shughuli nyingi mno.

Kadiri siku ya harusi ilivyokuwa ikikaribia, nilishangazwa na mfululizo wa majinamizi yaliyohusu aina zote za matatizo ambayo yangeweza kuiathiri familia. Kwa sababu ninatoka katika familia yenye upendo lakini iliyoteseka sana, iliyotishiwa na mabishano makali na ya kila mara na mioyo iliyovunjika, ndoto hizo mbaya ziliniathiri zaidi ya vile ilivyonipasa. Kwa hivyo usiku mmoja, baada ya nyingine kadhaa kama hiyo, niliamka nikitokwa na jasho na nikaamua kufuata ushauri ambao Dada Neill F. Marriot, Mshauri wa Pili katika Urais Mkuu wa Wasichana, alitoa katika hotuba yake “Yielding Our Hearts to God” (Liahona, Nov. 2015, 30–32). Nilifunga macho yangu na kuomba, “Baba Mpendwa wa Mbinguni, ni nini naweza kufanya ili kuzuia mambo haya mabaya mbali na familia yangu?

Jibu lilinijia upesi na kwa nguvu kana kwamba mtu fulani alikuwa amefungua mlango kichwani mwangu na kuweka wazo lile hapo. Ile sauti ndogo, tulivu ilinishawishi, “Fanya kile tu unachopaswa kufanya. Kuwa mwaminifu katika kila hatua.” Roho alinong’ona ushauri fulani maalum, na nilihisi kwamba ikiwa ningefanya mambo hayo, kila kitu kingekuwa sawa.”

Nilitabasamu na kuhisi kifua changu kikiwa kimejaa upendo. Wasiwsi wote ulisahaulika ghafla, kwa sababu nilijua ilikuwa ni kweli. Nilikuwa nimewahi kumsikia Roho Mtakatifu hapo awali, lakini kamwe sio jinsi nilivyomsikia kwa nguvu usiku ule. Nilihisi upendo wa Baba yetu wa Mbinguni na Mwokozi ukinizingira, na nilijua ya kwamba faraja na wokovu wa familia yangu ilikuwa muhimu kwao kama vile ilivyokuwa kwangu.

Kama nyongeza ya uhakikisho, hadithi kutoka kwenye maandiko ilinijia katika fahamu zangu—wakati Bwana alipomuamuru Nefi kujenga Meli: “Na ikawa kwamba Bwana akanizungumzia, na kusema: Wewe utajenga merikebu, kulingana na vile nitakavyo kuonyesha, ili niwavushe watu wako haya maji” (1 Nefi 17:8; imetiliwa mkazo).

Nefi na familia yake walikuwa nyikani kwa muda wa miaka mingi, wakivumilia aina zote za dhiki. Angeweza kuhisi hofu ya kuanza safari ya kuvuka bahari na kuruhusu hofu zake kuwa na nguvu zaidi kuliko imani yake. Lakini hakufanya hivyo. Alikubali na kutii maelekezo kutoka kwa Mungu. Alikuwa na imani ya kwamba ahadi zake Bwana zingetimizwa. Bwana hakumwambia Nefi kwamba tufani hazingetokea au kwamba mawimbi hayangeipiga meli. Lakini Yeye alimwambia Nefi ikiwa angefuata maelekezo Yake, angeweza kuiongoza familia yake kwa usalama kuvuka bahari hadi katika nchi ya ahadi.

Niligundua ya kwamba mimi pia nilikuwa nimesafiri kupitia katika nyika kwa muda wa miaka mingi, lakini sasa nilikuwa mbele ya bahari, nikijitayarisha kwa safari mpya: ndoa. Nimepewa wito—na nafikiri hiyo ndiyo hali ilivyo kwa familia zote za Watakatifu wa Siku za Mwisho—kujenga meli kwa kufuata maelekezo ya Mungu.

Mara tu mume wangu na mimi tulipooana, matatizo yalijitokezea. Niliugua, na tulihangaika kuweka hali yetu ya kifedha katika uwiano na kufanya yale mazoea mazuri yote tuliyokuwa tumeamua kuyafuata.

Lakini ushauri ambao nilikuwa nimeupokea usiku ule ulisalia moyoni mwangu. Tulijaribu kila siku kujifunza na kulihifadhi neno la Mungu mioyoni mwetu, kufuata mifano mizuri ya viongozi wetu wapendwa—ikiwa ni pamoja na Kristo—na kuboresha tabia yetu. Nilipata ushuhuda imara kuhusu maombi na kwa kweli nikaonja upendo wa Baba kwetu sisi. Nilianza kuamini zaidi na kupunguza hofu. Tuligundua kwamba shida ambazo tulikabiliana nazo zilikuja kuwa ngazi za kujiboresha. Leo nyumba yetu huonekana kama mbingu ndogo.

Bado tupo mwanzoni mwa safari yetu, lakini kufunga ndoa na kuanzisha familia ulikuwa uchaguzi bora zaidi ambao niliwahi kufanya. Moyo wangu unajawa na furaha wakati ninapofikiria kuhusu ibada ya hekaluni tuliyopokea na kujua ya kwamba iliunganishwa kwa Mamlaka ya Mungu. Kadiri ninavyozidi kuelewa kuhusu umuhimu wa familia katika mpango wa Baba wa Mbinguni na utukufu wa agano tulilofanya, ndivyo ninavyotaka kusaidia familia zingine kupokea ibada hiyo.

Nilijifunza ya kwamba hatuhitaji kuwa na wasi wasi juu ya kile kitakacho tendeka, kwa sababu “Mungu hakutupa roho ya woga, bali ya nguvu na ya upendo, na ya moyo wa kiasi” (2 Timotheo 1:7). Tunahitaji tu kuwa watiifu, kufuata maelekezo yaliyotolewa katika maandiko na maneno ya manabii wa siku zetu, na kuomba katika maombi maelekezo zaidi ya kibinafsi. Ikiwa tutafanya vitu hivi, tunaweza kuvuka bahari ya hizi siku za mwisho na tukijiamini kwamba bila kujali ni aina gani ya matatizo yatatupiga, wapendwa wetu watakuwa salama.