Sauti za Watakatifu wa Siku za Mwisho
Pochi Iliyopotea
Hivi karibuni nilihamia kwenye nyumba mpya na nikawaomba baadhi ya waumini wa Kanisa kunisaidia kazi maalumu katika nyumba yangu. Katikati ya mradi, niliondoka kwenda kununua vifaa tulivyohitaji kumalizia kazi. Baada ya kumaliza mradi, niligundua sikuwa na pochi yangu. Nilitaharuki kwa sababu ndani ya pochi yangu kulikuwa na nyaraka zangu binafsi pamoja na pesa ambazo nilikuwa nimepokea kutoka kwa mteja asubuhi ile. Nikarudi kufuatilia hatua zangu kwenda kule niliko nunua vitu lakini sikuwa na bahati. Nikaenda nyumbani na kutafuta kuona kama niliiangusha sehemu, lakini bado sikuiona. Nikaanza kufikiria uwezekano kwamba nianze kupata nakala mpya za nyaraka zote. Ndipo kabla ya kuondoka nyumbani, rafiki yangu aliniuliza “Je umeshaomba tayari?”
Mara moja nikafikiria, “Ndio tayari nimekwisha omba!”
Lakini kwa kweli, sikuwa nimeomba kwa dhati. Badala yake, nilitaka kulazimisha mapenzi yangu kwa Baba wa Mbinguni na kwa namna fulani kuifanya kuwa ni kazi Yake kunisaidia mimi kutafuta pochi yangu. Lakini kisha nikakumbuka maandiko katika Isaya 55:8: “Maana mawazo yangu si mawazo yenu, wala njia zenu si njia zangu; asema Bwana.”
Jumapili nilikwenda Kanisani, na muumini aliyekuwa na mimi jana aliniambia kwamba ameomba sana kwa Baba wa Mbinguni ili niweze kuipata pochi yangu. Alisema amehisi kwamba nitaipata. Baadaye, nikiwa nimekaa kwa ajili ya mafunzo binafsi, nikaanza kusoma Kupokea Majibu ya Maombi Yetu na Mzee Gene R. Cook, mshiriki wa heshima wa Sabini. Ukurasa wa kwanza ulielezea habari sawa na ya kwangu: Mwana wa Mzee Cook alipoteza pochi, hivyo familia ilikusanyika pamoja na kuomba kwa Bwana ili waweza kuipata.
Baada ya kusoma juu ya tukio lile, mimi niliyaweka katika vitendo yale niliyojifunza na kuwakusanya mke na watoto wangu pamoja. Tukatengeneza duara, na kila mtu alitoa maombi, tukimwomba sana Bwana kutusaidia kuipata pochi kama yalikuwa ni mapenzi yake.
Nimewahi kushuhudia nguvu za maombi, lakini baadaye, nikiwa ninaomba kwa siri, nilimwomba Baba wa Mbinguni kujibu maombi yetu ili kuimarisha imani ya mke na watoto wangu.
Siku iliyofuata mtu akanipigia simu. Alisema ameipata pochi yangu, pamoja na pesa. Nikalia kama mtoto kwa sababu maombi yangu yalijibiwa na imani ya familia yangu iliimarishwa.
Ninajua kwamba Baba wa Mbinguni, hata pamoja na kuwa na watoto wengi wa kuwahudumia, anamjibu kila mmoja wetu kulingana na muda Wake na katika njia Yake.