Maandiko Matakatifu
Mafundisho na Maagano 124


Sehemu ya 124

Ufunuo uliotolewa kwa Joseph Smith Nabii, huko Nauvoo, Illinois, 19 Januari 1841. Kwa sababu ya kuongezeka kwa mateso na taratibu zisizo za kisheria dhidi yao kutoka kwa maofisa wa serikali, Watakatifu walilazimika kuhama Missouri. Amri ya kuuawa iliyotolewa na Lilburn W. Boggs, gavana wa Missouri, 27 Oktoba 1838, iliwaacha wasiwe na uchaguzi mbadala. Katika mwaka 1841, wakati ufunuo huu ulipotolewa, mji wa Nauvoo, uliokuwa kiwanja cha kijiji cha zamani cha Commerce, Illinois, ulikuwa umejengwa na Watakatifu, na hapa ndiyo makao makuu ya Kanisa yalipoanzishwa.

1–14, Joseph Smith anaamriwa kutoa tamko la dhati la injili kwa rais wa Marekani, magavana, na watawala wa mataifa yote; 15–21, Hyrum Smith, David W. Patten, Joseph Smith Mkubwa na wengine miongoni mwa walio hai na wafu wamebarikiwa kwa sababu ya uadilifu na wema wao; 22–28, Watakatifu wanaamriwa kujenga nyumba kwa ajili ya kuwakarimu wageni na hekalu katika Nauvoo; 29–36, Ubatizo kwa ajili ya wafu lazima ufanyike hekaluni; 37–44, Watu wa Bwana daima hujenga mahekalu kwa ajili ya kufanya ibada takatifu; 45–55, Watakatifu wanasamehewa kujenga hekalu katika Wilaya ya Jackson kwa sababu ya manyanyaso ya maadui zao; 56–83, Maelekezo yanatolewa kwa ajili ya ujenzi wa Nyumba ya Nauvoo; 84–96, Hyrum Smith anaitwa kuwa patriaki, ili kupokea funguo, na kusimama mahali pa Oliver Cowdery; 97–122, William Law na wengine wanashauriwa katika kazi zao; 123–145, Viongozi wakuu na wa maeneo watajwa, pamoja na wajibu wao na akidi analoshiriki.

1 Amini, hivyo ndivyo asemavyo Bwana kwako, mtumishi wangu Joseph Smith, ninapendezwa na matoleo yako na kukubali kwako, ulikofanya; kwani kwa kusudi hili nilikusimamisha, ili nipate kuonyesha hekima yangu kwa walio wadhaifu wa dunia.

2 Sala zako zinakubalika mbele zangu; na katika kuyajibu ninakuambia kwamba sasa unaitwa haraka kufanya tangazo la dhati la injili yangu, na la kigingi hiki ambacho nimekipanda ili kuwa jiwe la kona la Sayuni, ambalo litanakishiwa kwa kusafishwa mfano wa kasri.

3 Tangazo hili litafanywa kwa wafalme wote wa ulimwengu, kwenye kona zake nne, kwa mheshimiwa rais mteule, na kwa waheshimiwa magavana wa taifa ambamo wewe unaishi, na kwa mataifa yote yaliyotawanyika duniani.

4 Acheni liandikwe katika roho ya unyenyekevu na kwa uwezo wa Roho Mtakatifu, ambaye atakuwa ndani yako wakati wa kuliandika hilo;

5 Kwani itatolewa kwako na Roho Mtakatifu kujua mapenzi yangu juu ya wafalme na wenye mamlaka hao, hata yale yatakayowapata wakati ujao.

6 Kwani, tazama, karibu nitawaita waitii nuru na utukufu wa Sayuni, kwani majira yaliyoamriwa yamewadia ya kumpendelea.

7 Waitieni, kwa hiyo, kwa tangazo la sauti kubwa, na kwa ushuhuda wenu, msiwaogope, kwani wao ni kama nyasi, na utukufu wao wote ni kama maua yake ambayo ghafla huanguka, ili nao wapate kuachwa pasipo udhuru—

8 Na ili nipate kuwatembelea siku ya kujiliwa, wakati nitakapofunua uso wa maficho yangu, kuweka fungu la mdhalimu miongoni mwa wanafiki, ndiko kutakuwako na kusaga meno, kama watawakataa watumishi wangu na ushuhuda wangu ambao nimewafunulia.

9 Na tena, nitawajilia na kulainisha mioyo yao, wengi wao kwa faida yenu, ili mpate neema machoni mwao, ili waweze kuja kwenye nuru ya kweli, na Wayunani kwa kuipandisha au kuinuliwa kwa Sayuni.

10 Kwani siku ya kuwajilia yaja haraka, katika saa msiyodhania; na wapi kutakuwa usalama wa watu wangu, na kimbilio kwa wale watakaoachwa nao?

11 Amkeni, enyi wafalme wa dunia! Njooni ninyi, enyi njooni, pamoja na dhahabu na fedha zenu, ili muwasaidie watu wangu, hata kwenye nyumba ya mabinti wa Sayuni.

12 Na tena, amini ninakuambia, acha mtumishi wangu Robert B. Thompson akusaidie kuliandika tangazo hili, kwani Mimi ninapendezwa naye, na kwamba awe pamoja nawe;

13 Acheni yeye, kwa sababu hiyo, atasikiliza ushauri wako, na mimi nitambariki kwa wingi wa baraka; acheni awe mwaminifu na mkweli katika mambo yote tangu sasa na kuendelea, naye atakuwa mkuu machoni pangu;

14 Lakini acheni akumbuke kwamba usimamizi wake nitaudai kutoka kwake.

15 Na tena, amini ninakuambia, amebarikiwa mtumishi wangu Hyrum Smith; kwani Mimi, Bwana, ninampenda kwa sababu ya uadilifu wa moyo wake, na kwa sababu yeye hupenda yaliyo ya haki mbele zangu, asema Bwana.

16 Tena, acha mtumishi wangu John C. Bennett akusaidie katika kazi zako katika kupeleka neno langu kwa wafalme na watu wa dunia, na asimame pamoja nawe, hata wewe mtumishi wangu Joseph Smith, katika saa ya mateso; na thawabu yake haitakosekana kama ataupokea ushauri.

17 Na kwa sababu ya upendo wake atakuwa mkuu, kwani atakuwa wangu kama atafanya hili, asema Bwana. Nimeiona kazi aliyoifanya, ambayo ninaikubali kama ataendelea, na nitamvika taji la baraka na utukufu mkuu.

18 Na tena, ninakuambia kwamba ni mapenzi yangu kuwa mtumishi wangu Lyman Wight aendelee katika kuhubiri kwa ajili ya Sayuni, katika roho ya unyenyekevu, akinikiri mimi mbele ya ulimwengu; nami nitamnyanyua juu kama vile mbawa za tai; naye atajipatia utukufu na heshima kwake yeye mwenyewe na kwa jina langu.

19 Ili atakapomaliza kazi yake nipate kumpokea kwangu, hata kama nilivyomfanya mtumishi wangu David Patten, ambaye yupo pamoja nami hivi sasa, na pia mtumishi wangu Edward Partridge, na pia mtumishi wangu mzee Joseph Smith, Mkubwa, ambaye hukaa pamoja na Ibrahimu mkono wake wa kuume, na yeye yu mtakatifu na mbarikiwa, kwa kuwa yeye ni wangu.

20 Na tena, amini ninawaambia, mtumishi wangu George Miller hana hila; aweza kuaminiwa kwa sababu ya uadilifu wa moyo wake; na kwa mapenzi aliyonayo kwa ushuhuda wangu Mimi, Bwana, ninampenda yeye.

21 Kwa hiyo ninawaambia, ninatia muhuri juu ya kichwa chake ofisi ya uaskofu, kama kwa mtumishi wangu Edward Partridge, ili apate kupokea vilivyowekwa wakfu kwa nyumba yangu, ili apate kutoa baraka juu ya vichwa vya maskini wa watu wangu, asema Bwana. Acheni mtu yeyote asimdharau mtumishi wangu George, kwani yeye ataniheshimu Mimi.

22 Acha mtumishi wangu George, na mtumishi wangu Lyman, na mtumishi wangu John Snider, na wengineo, wajenge nyumba kwa jina langu, kama vile mtumishi wangu Joseph atakavyowaonyesha, juu ya mahali ambapo yeye pia atawaonyesha.

23 Nayo itakuwa kwa ajili ya nyumba ya kuishi, nyumba ambayo wageni wanaweza kuja kutoka mbali na kuishi ndani yake; kwa hiyo acheni iwe nyumba nzuri, yenye kustahili kukubalika kote, ili mgeni aliyechoka aweze kupata afya na usalama wakati atakapokuwa akitafakari neno la Bwana; na jiwe la kona nililolichagua kwa ajili ya Sayuni.

24 Nyumba hii itakuwa makazi yenye afya ikiwa itajengwa kwa jina langu, na kama gavana ambaye atateuliwa kwa ajili yake hataruhusu uchafu wowote kuja juu yake. Itakuwa takatifu, au kama sivyo Bwana Mungu wenu hatakaa ndani yake.

25 Na tena, amini, ninawaambia, acheni watakatifu wangu wote waje kutoka mbali.

26 Na wapelekeni wajumbe upesi, ndiyo, wajumbe walioteuliwa, na waambieni: Njooni, pamoja na dhahabu zenu zote, na fedha zenu, na mawe yenu ya thamani, na pamoja na vitu vyenu vyote vya kale; na pamoja na wale wote wenye ujuzi wa vitu vya kale, watakao kuja, na waje, na leteni mtidhari, mberoshi, na mteshuri, pamoja na miti yote mizuri ya dunia;

27 Na pamoja na chuma, na shaba nyekundu, na shaba nyeupe, na zinki, pamoja na vitu vyenu vyote vya thamani vya duniani; na jengeni nyumba kwa jina langu, ili Aliye Juu Sana akae ndani yake.

28 Kwani hakuna mahali palipopatikana juu ya dunia ambapo yeye aweza kuja na kurejesha tena kile ambacho kilipotea kwenu, au kile alichokiondolea mbali, hata utimilifu wa ukuhani.

29 Kwani kisima cha ubatizo hakiko juu ya dunia, ili wao, watakatifu wangu, waweze kubatizwa kwa ajili ya wale waliokufa—

30 Kwani ibada hii ni mali ya nyumba yangu, na haiwezi kukubaliwa kwangu, isipokuwa tu katika siku ya ufukara wenu, ambapo hamna uwezo wa kunijengea nyumba.

31 Lakini ninawaamuru ninyi, ninyi watakatifu wangu wote, kunijengea nyumba; na ninatoa kwenu muda wa kutosha kunijengea nyumba; na kwa wakati huo ubatizo wenu nitaukubali.

32 Lakini tazama, muda huu ukiisha ubatizo wenu kwa ajili ya wafu hautakubaliwa kwangu; na kama hamkufanya mambo haya mwishoni mwa muda huu mtakataliwa kama kanisa, pamoja na wafu wenu, asema Bwana Mungu wenu.

33 Kwani amini ninawaambia, kwamba baada ya kupata muda wa kutosha kunijengea nyumba, ambamo ndani yake ibada ya kubatizwa kwa ajili ya wafu itafanyika, na kwa ajili hiyo hii iliwekwa tangu kabla ya kuwekwa msingi wa ulimwengu, ubatizo wenu kwa ajili ya wafu wenu hautaweza kukubalika kwangu;

34 Kwani ndani yake funguo za ukuhani mtakatifu zimewekwa, ili mpate kupokea heshima na utukufu.

35 Na baada ya wakati huu, ubatizo wenu kwa ajili ya wafu, kwa wale ambao wametawanyika mbali, hautakubalika kwangu, asema Bwana.

36 Kwani imeamuriwa kwamba katika Sayuni, na katika vigingi vyake, na katika Yerusalemu, sehemu zile ambazo nimeziteua kwa ajili ya kimbilio, zitakuwa ndizo sehemu zenu kwa ajili ya ubatizo wa wafu wenu.

37 Na tena, amini ninawaambia, ni namna gani uoshwaji wenu utakubaliwa kwangu, isipokuwa tu mmeufanya katika nyumba ambayo mmeijenga kwa jina langu?

38 Kwani, kwa ajili hii, nilimwamuru Musa kwamba lazima ajenge hema takatifu, kwamba waibebe pamoja nao huko nyikani, na wajenge nyumba katika nchi ya ahadi, ili ibada zile zipate kufunuliwa zile ambazo zilifichwa kabla ya ulimwengu kuwako.

39 Kwa hiyo, amini ninawaambia, kwamba kupakwa kwenu mafuta, na kuoshwa kwenu, na ubatizo wenu kwa ajili ya wafu, na makusanyiko yenu ya kiroho, na kumbukumbu zenu za dhabihu kwa wana wa Lawi, na kwa ajili ya mafunuo yenu katika mahali penu patakatifu zaidi ambamo ndani yake mnapokea maagizo, na sheria na hukumu zenu, kwa ajili ya kuanza kwa mafunuo na msingi wa Sayuni, na kwa ajili ya utukufu, heshima, na endaomenti kwa manispaa zake zote, zimefanywa kuwa thabiti kwa ibada ya nyumba yangu takatifu, ambayo watu wangu daima wanaamriwa kuijenga kwa jina langu takatifu.

40 Na amini ninawaambia, acheni nyumba hii na ijengwe kwa jina langu, ili nipate kuzifunua ibada zangu ndani yake kwa watu wangu;

41 Kwani nimekubali kulifunulia kanisa langu mambo ambayo yalifichwa tangu kabla ya kuwekwa kwa msingi wa ulimwengu, mambo yale yahusuyo kipindi hiki cha utimilifu wa nyakati.

42 Na Mimi nitamwonyesha mtumishi wangu Joseph mambo yote yahusuyo nyumba hii, na ukuhani wake, na mahali ambapo juu yake itajengwa.

43 Nanyi mtaijenga juu ya mahali ambapo mmefikiria kuijenga, kwani hapo ndipo mahali sahihi nilipowachagulia ninyi kuijenga.

44 Kama mtafanya kazi kwa nguvu zenu zote, nitapaweka wakfu mahali pale ili pafanywe kuwa patakatifu.

45 Na kama watu wangu wataisikiliza sauti yangu, na sauti ya watumishi wangu ambao nimewateua kuwaongoza watu wangu, tazama, amini ninawaambia, wao hawataondoshwa kutoka mahali pao.

46 Lakini kama hawataisikiliza sauti yangu, wala sauti ya watu hawa ambao nimewateua, wao hawatabarikiwa, kwa sababu wanachafua ardhi yangu takatifu, na ibada zangu takatifu, na katiba, na maneno yangu matakatifu ambayo nayatoa kwao.

47 Na itakuwa kwamba kama mtaijenga nyumba kwa jina langu, na msifanye mambo yale nisemayo, mimi sitafanya kiapo ambacho ninakifanya kwenu, wala kutimiza ahadi ambazo ninyi mnazitegemea kutoka kwangu, asema Bwana.

48 Kwani badala ya baraka, ninyi, kwa matendo yenu wenyewe, hujiletea laana, ghadhabu, uchungu wa hasira, na hukumu juu ya vichwa vyenu wenyewe, kwa upumbavu wenu, na kwa machukizo yenu yote, ambayo mnayafanya mbele zangu, asema Bwana.

49 Amini, amini, ninawaambia kwamba nitoapo amri kwa wana wa watu wowote kuifanya kazi kwa jina langu, na wana wale wa watu wakienda kwa nguvu zao zote na vile vyote walivyonavyo kuifanya kazi ile, na bila kuacha juhudi yao, na adui zao wakaja juu yao na kuwazuia kufanya kazi ile, tazama, ninakuwa sina budi kuacha kuidai kazi ile kutoka mikononi mwa wanadamu, lakini huyapokea matoleo yao.

50 Na uovu na uvunjaji wa sheria na amri zangu takatifu nitawajilia juu ya vichwa vya wale waliozuia kazi yangu, hadi kizazi cha tatu na cha nne, endapo hawatatubu, na kunichukia mimi, asema Bwana Mungu.

51 Kwa hiyo, kwa sababu hii nimekubali matoleo ya wale ambao niliwaamuru kuujenga mji na nyumba kwa jina langu, katika wilaya ya Jackson, Missouri, na wakazuiliwa na maadui zao, asema Bwana Mungu wenu.

52 Nami nitajibu hukumu, ghadhabu, na uchungu wa hasira, maombolezo, na machungu, na kusaga meno juu ya vichwa vyao, hata kizazi cha tatu na cha nne, ilimradi kama hawatatubu, na hawatanichukia, asema Bwana Mungu wenu.

53 Na hii naifanya mfano kwenu, kwa ajili ya kuwafariji ninyi kuhusu wale wote ambao wameamriwa kufanya kazi na wakazuiliwa kwa mikono ya maadui zao, na kwa ukandamizaji, asema Bwana Mungu wenu.

54 Kwani Mimi ndimi Bwana Mungu wenu, nami nitawaokoa ndugu zenu wale wote ambao wamekuwa wasafi moyoni, na wakauawa katika nchi ya Missouri, asema Bwana.

55 Na tena, amini ninawaambia, ninawaamuru tena kuijenga nyumba kwa jina langu, hata katika mahali hapa, ili mpate kujithibitisha wenyewe kwangu kwamba mu waaminifu katika mambo yote yale nitayowaamuru, ili nipate kuwabariki, na kuwavika kwa heshima, kutokufa, na uzima wa milele.

56 Na sasa ninawaambia, kwa kuhusiana na nyumba yangu ya kuishi ambayo nimewaamuru kuijenga kwa ajili ya kuishi wageni, acheni ijengwe kwa jina langu, na acheni jina langu litajwe juu yake, na mtumishi wangu Joseph na nyumba yake wapate nafasi ndani yake, kutoka kizazi hadi kizazi.

57 Kwani mpako huu wa mafuta nimeuweka juu ya kichwa chake, ili baraka zake pia ziwekwe juu ya uzao wake baada yake.

58 Na kama vile nilivyosema kwa Ibrahimu kuhusu makabila za dunia, hivyo ndivyo ninavyosema kwa mtumishi wangu Joseph: Katika wewe na katika uzao wako kabila zote za dunia zitabarikiwa.

59 Kwa hiyo, acheni mtumishi wangu Joseph na uzao wake baada yake yeye wapate nafasi katika nyumba hiyo, kutoka kizazi hadi kizazi, milele na milele, asema Bwana.

60 Na acheni jina la nyumba hiyo iitwe Nyumba ya Nauvoo; na acheni iwe makazi ya kupendeza kwa mwanadamu, na mahali pa kupumzika kwa msafiri aliyechoka, ili apate kutafakari utukufu wa Sayuni, na utukufu wa hili, jiwe lake la kona;

61 Ili apate pia kupokea ushauri kutoka kwa wale ambao nimewaweka kuwa kama mimea ijulikanayo, na kama walinzi juu ya kuta zake.

62 Tazama, amini ninawaambia, acheni mtumishi wangu George Miller, na mtumishi wangu Lyman Wight, na mtumishi wangu John Snider, na mtumishi wangu Peter Haws, wajipange wenyewe, na kumteua mmoja wao kuwa rais juu ya akidi yao kwa madhumuni ya kuijenga nyumba hiyo.

63 Nao watunge katiba, ambayo kwayo wapate kupokea hisa kwa ajili ya ujenzi wa nyumba hiyo.

64 Nao wasipokee chini ya dola hamsini kama fungu la hisa katika nyumba hiyo, na wataruhusiwa kupokea dola elfu kumi na tano kutoka kwa mtu mmoja kama fungu la hisa katika nyumba hiyo.

65 Lakini hawataruhusiwa kupokea zaidi ya dola elfu kumi na tano kama fungu la ubia kutoka kwa mtu yeyote.

66 Na hawataruhusiwa kupokea chini ya dola hamsini kwa ajili ya fungu la ubia kutoka kwa mtu yeyote katika nyumba hiyo.

67 Na hawataruhusiwa kumpokea mtu yeyote, kama mwenye hisa katika nyumba hii, isipokuwa mtu huyo amelipa hisa yake mikononi mwao wakati anapopata hisa hiyo;

68 Na kwa idadi sawa na kiwango cha hisa anacholipa mikononi mwao atapokea hisa katika nyumba hiyo; lakini kama hakulipa chochote mikononi mwao asipewe hisa yoyote katika nyumba hiyo.

69 Na kama yeyote atalipa hisa mikononi mwao itakuwa kwa ajili ya hisa katika nyumba hiyo, kwa ajili yake, na kwa ajili ya kizazi chake baada yake, kutoka kizazi hadi kizazi, ilimradi tu yeye na warithi wake wataendelea kuishikilia hisa hiyo, na hawaiuzi au kuitoa hisa hiyo kutoka mikononi mwao kwa ridhaa yao wenyewe na kutenda, kama mtafanya mapenzi yangu, asema Bwana Mungu wenu.

70 Na tena, amini ninawaambia, kama mtumishi wangu George Miller, na mtumishi wangu Lyman Wight, na mtumishi wangu John Snider, na mtumishi wangu Peter Haws, watapokea hisa yoyote mikononi mwao, katika fedha, au katika mali ambayo kwayo watapata thamani halisi ya fedha, wasiigawe sehemu yoyote ya hisa hiyo kwa dhumuni jingine lolote, isipokuwa katika nyumba hiyo tu.

71 Na kama wataigawa sehemu yoyote ya hisa hiyo kwenda sehemu nyingine yoyote, isipokuwa katika nyumba hiyo tu, bila ya kauli ya mwenye hisa, na hawalipi mara-nne kwa hisa ambayo waliigawa kokote kwingineko, isipokuwa katika nyumba hiyo, watalaaniwa, nao wataondolewa kutoka katika nafasi zao, asema Bwana Mungu; kwani Mimi, Bwana, ndiye Mungu, na siwezi kudhihakiwa katika mambo haya.

72 Amini ninawaambia, acheni mtumishi wangu Joseph alipe hisa mikononi mwao kwa ajili ya ujenzi wa nyumba hiyo, kama aonavyo yeye kuwa vyema; lakini mtumishi wangu Joseph hawezi kulipa zaidi ya dola elfu kumi na tano kama hisa katika nyumba hiyo, wala chini ya dola hamsini; wala haiwezekani kwa mtu mwingine yeyote, asema Bwana.

73 Na kuna wengine pia wanaotaka kujua mapenzi yangu juu yao, kwani wameomba kutoka kwangu.

74 Kwa hiyo, ninawaambia juu ya mtumishi wangu Vinson Knight, kama atafanya mapenzi yangu, na aweka hisa ndani ya nyumba hiyo kwa ajili yake mwenyewe, na kwa ajili ya kizazi chake baada yake, kutoka kizazi hadi kizazi.

75 Naye msiache apaze sauti yake kubwa na ndefu, katikati ya watu, ili kuwatetea teto za maskini na wenye shida; na ashindwe, wala moyo wake ukate tamaa; nami nitapokea matoleo yake, kwani hayatakuwa kwangu kama matoleo ya Kaini, kwani atakuwa wangu, asema Bwana.

76 Acheni familia yake na ifurahi na kuigeuza mioyo yao kutoka kwenye mateso; kwani nimemteua yeye na kumpaka mafuta, naye ataheshimika katikati ya nyumba yake, kwani nitazisamehe dhambi zake zote, asema Bwana. Amina.

77 Amini ninawaambia, acheni mtumishi wangu Hyrum aweke hisa ndani ya nyumba hiyo kama aonavyo yeye kuwa ni vyema, kwa ajili yake na kizazi chake baada yake, kutoka kizazi hadi kizazi.

78 Acheni mtumishi wangu Isaac Galland aweke hisa ndani ya nyumba hiyo; kwani Mimi, Bwana, ninampenda kwa ajili ya kazi alizozifanya, na nitamsamehe dhambi zake zote; kwa hiyo, acheni akumbukwe kuwa alikuwa mwenye hisa katika nyumba hiyo kutoka kizazi hadi kizazi.

79 Acheni mtumishi wangu Isaac Galland ateuliwe miongoni mwenu, na kutawazwa na mtumishi wangu William Marks, na abarikiwe naye, kwenda pamoja na mtumishi wangu Hyrum kumalizia kazi ile ambayo mtumishi wangu Joseph atawaonyesha, nao watabarikiwa sana.

80 Acheni mtumishi wangu William Marks na alipe hisa katika nyumba hiyo, kama aonavyo yeye kuwa vyema, kwa ajili yake mwenyewe na kizazi chake, tangu kizazi hadi kizazi.

81 Acheni mtumishi wangu Henry G. Sherwood na alipe hisa katika nyumba hiyo, kama aonavyo yeye kuwa ni vyema, kwa ajili yake na uzao wake baada yake, tangu, kizazi hadi kizazi.

82 Acheni mtumishi wangu William Law alipe hisa ndani ya nyumba hiyo, kwa ajili yake na uzao wake baada yake, tangu kizazi hadi kizazi.

83 Kama atafanya mapenzi yangu msimwache aichukue familia yake kwenda nchi za mashariki, hata Kirtland; hata hivyo, Mimi, Bwana, nitaijenga Kirtland, lakini Mimi, Bwana, ninalo baa nililolitayarisha kwa ajili ya wakazi wake.

84 Na pamoja na mtumishi wangu Almon Babbit, yapo mambo mengi ambayo sijapendezwa nayo; tazama, anatamani kuweka baraza lake badala ya baraza ambalo nimelitawaza, hata lile la Urais wa Kanisa langu, naye humweka ndama wa dhahabu kwa ajili ya kuabudu watu wangu.

85 Msiache mtu yeyote aende kutoka mahali hapa ambaye amekuja hapa akitafuta kushika amri zangu.

86 Kama wao wanaishi hapa acheni waishi kwangu; na kama watakufa acheni watakufa kwangu; kwani watapumzika kutokana na kazi zao zote za hapa, na wataendelea na kazi zao.

87 Kwa hiyo, acheni mtumishi wangu William anitumaini Mimi, na akome kuogopa juu ya familia yake, kwa sababu ya maradhi ya nchi. Kama wanipenda, shika amri zangu; na maradhi ya nchi yatakuletea utukufu wako.

88 Acheni mtumishi wangu William aende na kutangaza injili yangu isiyo na mwisho kwa sauti kubwa, na kwa shangwe kuu, kama vile atakavyoongozwa na Roho wangu, kwa wakazi wa Warsaw, na pia kwa wakazi wa Carthage, na pia kwa wakazi wa Burlington, na pia kwa wakazi wa Madison, na kusubiri kwa uvumilivu na bidii kwa maelekezo zaidi kwenye mkutano wangu mkuu, asema Bwana.

89 Kama atafanya mapenzi yangu mwacheni kutoka sasa na kuendelea asikilize ushauri wa mtumishi wangu Joseph, na kwa faida yake awasaidie maskini, na kuchapisha ile tafsiri mpya ya neno langu takatifu kwa wakazi wa dunia.

90 Na kama atafanya hili nitambariki yeye kwa wingi wa baraka, kwamba yeye hatasahaulika, wala uzao wake hautaonekana ukiomba mkate.

91 Na tena, amini ninawaambia, acheni mtumishi wangu William ateuliwe, atawazwe na kupakwa mafuta, kama mshauri kwa mtumishi wangu Joseph, mahali pa mtumishi wangu Hyrum, ili mtumishi wangu Hyrum apate kuchukua ofisi ya Ukuhani na patriaki, ambayo ilichaguliwa kwake na baba yake, kwa kubarikiwa na pia kwa haki;

92 Ili kutoka sasa yeye atashikilia funguo za baraka za kipatriaki juu ya vichwa vya watu wangu wote;

93 Ili yeyote atakaye mbariki atabarikiwa, na yeyote atakayemlaani atalaaniwa; ili lolote atakalolifunga duniani litakuwa limefungwa mbinguni; na lolote atakalolifungua duniani litakuwa limefunguliwa mbinguni.

94 Na tangu wakati huu na kuendelea ninamteua yeye aweze kuwa nabii, na mwonaji, na mfunuzi kwa kanisa langu, kama vile mtumishi wangu Joseph;

95 Ili apate kutenda katika umoja pia pamoja na mtumishi wangu Joseph; na kwamba yeye atapokea ushauri kutoka kwa mtumishi wangu Joseph, ambaye atamwonyesha yeye funguo ambazo kwa hizo aweze kuomba na kupokea, na kuvikwa taji la baraka hizo hizo, na utukufu, na heshima, na ukuhani, na vipawa vya ukuhani, ambavyo wakati mmoja viliwekwa juu yake yeye aliyekuwa mtumishi wangu Oliver Cowdery;

96 Ili mtumishi wangu Hyrum apate kushuhudia mambo nitakayomwonyesha yeye, ili jina lake lipate kukumbukwa kwa heshima tangu kizazi hadi kizazi, milele na milele.

97 Acheni mtumishi wangu William Law pia apokee funguo ambazo kwa hizo apate kuomba na kupokea baraka; na awe mnyenyekevu mbele zangu, na pasipo hila, naye atampokea Roho wangu, hata Mfariji, ambaye atamwonyesha yeye ukweli wa mambo yote, naye atampa, katika saa ile ile, kile atakachosema.

98 Na ishara hizi zitafuatana naye—atawaponya wagonjwa, atawatoa pepo wabaya, na ataokolewa kutoka kwa wale watakaomywesha sumu;

99 Naye ataongozwa katika njia ambazo nyoka wenye sumu hawatamshika kisigino chake, naye atapaa katika dhana za mawazo yake kama vile juu ya mbawa za tai.

100 Na kama itatokea kwamba nikataka amfufue mtu aliyekufa, msimwache aizue sauti yake.

101 Kwa hiyo, acheni mtumishi wangu William alie kwa sauti na asiache, kwa shangwe na furaha, na pamoja na hosana kwa yeye aketiye juu ya kiti cha enzi milele na milele, asema Bwana Mungu wenu.

102 Tazama, ninawaambia, ninayo huduma niliyoiweka kwa ajili ya mtumishi wangu William, na mtumishi wangu Hyrum, na ni kwao peke yao; na acheni mtumishi wangu Joseph akae nyumbani, kwani yeye anahitajiwa. Wanaobaki nitawaonyesha hapo baadaye. Hivyo ndivyo. Amina.

103 Na tena, ninawaambia, kama mtumishi wangu Sidney atanitumikia mimi na kuwa mshauri kwa mtumishi wangu Joseph, acheni asimame na kuja na kusimama katika ofisi ya wito wake, na kujinyenyekeza mwenyewe mbele zangu.

104 Na kama atanitolea matoleo ya kukubalika, na ya shukrani, na kubaki pamoja na watu wangu, tazama, Mimi, Bwana Mungu wenu, nitamponya ili apate kupona; naye ataipaza sauti yake tena milimani, na kuwa msemaji mbele ya uso wangu.

105 Acheni aje na kuiweka familia yake katika maeneo ya jirani na mtumishi wangu Joseph anapoishi.

106 Na katika safari zake zote acheni apaze sauti yake kama vile sauti ya parapanda, na kuwaonya wakazi wa dunia kuikimbia ghadhabu inayokuja.

107 Acheni amsaidie mtumishi wangu Joseph, na pia acheni mtumishi wangu William Law na amsaidie mtumishi wangu Joseph, katika kutengeneza tangazo la dhati kwa wafalme wa dunia, hata kama vile nilivyowaambia hapo awali.

108 Kama mtumishi wangu Sidney atafanya mapenzi yangu, msimwache aipeleke familia yake nchi za mashariki, lakini acheni abadilishe makazi yao, hata kama vile nilivyosema.

109 Tazama, siyo mapenzi yangu kwamba atatafuta kupata usalama na kimbilio nje ya mji ambao nimewachagulia, hata mji wa Nauvoo.

110 Amini ninawaambia, hata sasa, kama ataisikiliza sauti yangu, itakuwa vyema kwake yeye. Hivyo ndivyo. Amina.

111 Na tena, amini ninawaambia, acheni mtumishi wangu Amos Davis alipe hisa mikononi mwa wale ambao nimewateua kujenga nyumba ya kuishi, hata Nyumba ya Nauvoo.

112 Acheni afanye hili kama atapata faida; naye acheni asikilize ushauri wa mtumishi wangu Joseph, na kufanya kazi kwa mikono yake mwenyewe ili apate kuaminiwa na watu.

113 Na atakapojithibitisha mwenyewe kwamba ni mwaminifu katika mambo yote yatakayo aminiwa kwake, ndiyo, hata mambo machache, atafanywa mtawala juu ya mengi;

114 Kwa hiyo mwacheni ajidhili mwenyewe ili apate kukwezwa. Hivyo ndivyo. Amina.

115 Na tena, amini ninawaambia, kama mtumishi wangu Robert D. Foster atatii sauti yangu, acheni ajenge nyumba kwa ajili ya mtumishi wangu Joseph, kulingana na mkataba alioufanya naye, kwa vile mlango utafunguliwa kwake mara kwa mara.

116 Naye acheni atubu upumbavu wake wote, na kujivika hisani; na kuacha kutenda uovu, na kuweka kando maneno yake magumu;

117 Na alipe hisa pia mikononi mwa akidi ya Nyumba ya Nauvoo, kwa ajili yake na kwa ajili ya kizazi chake baada yake, tangu kizazi hadi kizazi;

118 Na asikilize ushauri wa watumishi wangu Joseph, na Hyrum, na William Law, na kwa viongozi ambao nimewaita kuweka msingi wa Sayuni; na itakuwa vyema kwake, milele na milele. Hivyo ndivyo. Amina.

119 Na tena, amini ninawaambia, acheni mtu yeyote asilipe hisa kwa akidi ya Nyumba ya Nauvoo isipokuwa amekuwa muumini katika Kitabu cha Mormoni, na mafunuo niliyoyatoa kwenu, asema Bwana Mungu wenu;

120 Kwani kile kilicho zaidi au pungufu kuliko hii chatoka kwa mwovu, nacho kitashughulikiwa kwa laana na siyo baraka, asema Bwana Mungu wenu. Hivyo ndivyo. Amina.

121 Na tena, amini ninawaambia, acheni akidi ya Nyumba ya Nauvoo walipwe ujira sahihi kwa kazi zao zote wanazozifanya katika kujenga Nyumba ya Nauvoo; na acheni ujira wao uwe kama itakavyokubalika baina yao wenyewe, kulingana na thamani yake.

122 Na acheni kila mtu alipaye hisa abebe sehemu yake ya ujira wao, kama hapana budi, kwa ajili ya kuwasaidia, asema Bwana; vinginevyo, kazi zao zitahesabiwa kama hisa kwao katika nyumba hiyo. Hivyo ndivyo. Amina.

123 Amini ninawaambia, sasa ninatoa kwenu maofisa walio wa Ukuhani wangu, ili ninyi mpate kuzishika funguo zake, hata ukuhani ambao ni kwa mfano wa Melkizedeki, ambao ni kwa mfano wa Mwanangu wa Pekee.

124 Kwanza, ninawapa Hyrum Smith kuwa patriaki kwenu ninyi, kushikilia baraka za kufunga za kanisa langu, hata Roho Mtakatifu wa ahadi, ambaye kwake yeye ninyi mmetiwa muhuri hata siku ya ukombozi, ili msiweze kuanguka licha ya kuwa saa ya majaribu yaweza kuja juu yenu.

125 Ninawapa mtumishi wangu Joseph kuwa mzee kiongozi juu ya kanisa langu lote, kuwa mfasiri, mfunuzi, mwonaji, na nabii.

126 Ninampa yeye kuwa washauri wake mtumishi wangu Sidney Rigdon na mtumishi wangu William Law, ili hawa wapate kuunda akidi na Urais wa Kwanza, kupokea mafunuo kwa ajili ya kanisa zima.

127 Ninawapa ninyi mtumishi wangu Brigham Young kuwa rais juu ya baraza la Kumi na Wawili wasafirio;

128 Kumi na Wawili ambao hushikilia funguo za kufungua mamlaka ya ufalme wangu juu ya pande nne za dunia, na baada ya hiyo kupeleka neno langu kwa kila kiumbe.

129 Wao ni Heber C. Kimball, Parley P. Pratt, Orson Pratt, Orson Hyde, William Smith, John Taylor, John E. Page, Wilford Woodruff, Willard Richards, George A. Smith;

130 David Patten nimemchukua kwangu; tazama, ukuhani wake hakuna mtu auondoaye kutoka kwake; lakini, amini ninawaambia, mwingine aweza kuteuliwa kwa wito huo huo.

131 Na tena, ninawaambia, ninawapa baraza kuu, kwa ajili ya jiwe la kona ya Sayuni—

132 Majina yao, Samuel Bent, Henry G. Sherwood, George W. Harris, Charles C. Rich, Thomas Grover, Newel Knight, David Dort, Dunbar Wilson—Seymour Brunson nimemchukua kwangu; hakuna mtu aondoaye ukuhani wake, lakini mwingine aweza kuteuliwa katika ukuhani huo huo badala yake; na amini ninawaambia, acheni mtumishi wangu Aaron Johnson atawazwe kwa wito huu badala yake—David Fullmer, Alpheus Cutler, William Huntington.

133 Na tena, ninawapa Don C. Smith kuwa rais juu ya akidi ya makuhani wakuu;

134 Agizo ambalo limewekwa kwa madhumuni ya kuwapasisha wale ambao watateuliwa kuwa marais wasimamizi au watumishi juu ya vigingi mbalimbali vilivyoenea ngʼambo;

135 Nao waweza kusafiri pia kama wanataka, lakini badala yake wametawazwa kuwa marais wasimamizi; hii ndiyo ofisi ya wito wao, asema Bwana Mungu wenu.

136 Ninampa yeye Amasa Lyman na Noah Packard kuwa washauri, ili wapate kuongoza juu ya akidi ya makuhani wakuu wa kanisa langu, asema Bwana.

137 Na tena, ninawaambia, ninawapa John A. Hicks, Samuel Williams, na Jesse Baker, ukuhani ambao ni kuongoza juu ya akidi ya wazee, akidi ambayo kimewekwa kwa ajili ya wahudumu kudumu; hata hivyo hawa wanaweza kusafiri, lakini hawa wametawazwa kuwa wahudumu wa kudumu kwa kanisa langu, asema Bwana.

138 Na tena, ninawapa Joseph Young, Josiah Butterfield, Daniel Miles, Henry Herriman, Zera Pulsipher, Levi Hancock, James Foster, kuongoza juu ya akidi ya sabini;

139 Akidi ambayo kimewekwa kwa ajili ya wazee wasafirio kutoa ushuhuda wa neno langu ulimwenguni kote, popote baraza kuu lisafirilo, mitume wangu, watakapo watuma kuitengeneza njia mbele za uso wangu.

140 Tofauti kati ya akidi hii na akidi ya wazee ni kwamba moja ni ya kusafiri daima, na ingine ni ya kuongoza juu ya kanisa mara kwa mara; moja ina wajibu wa kuongoza mara kwa mara, na ingine haina wajibu wa kuongoza, asema Bwana Mungu wenu.

141 Na tena, ninawaambia, ninakupeni Vinson Knight, Samuel H. Smith, na Shadrach Roundy, kama ataupokea, kusimamia uaskofu; maarifa juu ya uaskofu uliosemwa yametolewa kwenu katika kitabu cha Mafundisho na Maagano.

142 Na tena, ninawaambia, Samuel Rolfe na washauri wake kwa ajili ya makuhani, na rais wa walimu na washauri wake, na pia rais wa mashemasi na washauri wake, na pia rais wa kigingi na washauri wake.

143 Ofisi zilizoko hapo juu nimezitoa kwenu, na funguo zake, kwa misaada na kwa serikali, kwa kazi ya huduma na kuwakamilisha watakatifu wangu.

144 Na amri ninaitoa kwenu, kwamba lazima mzijaze nafasi hizi zote na kuyathibitisha majina hayo niliyoyataja, au vinginevyo myakatae kwenye mkutano wangu mkuu;

145 Na kwamba tayarisheni vyumba kwa ajili ya ofisi hizi zote katika nyumba yangu wakati mtakapoijenga kwa jina langu, asema Bwana Mungu wenu. Hivyo ndivyo. Amina.