Rafiki
Kuwatembelea Bibi na Babu
Julai 2024


“Kuwatembelea Bibi na Babu,” Rafiki, Julai 2024, 30–31.

Kuwatembelea Bibi na Babu

Ernesto alitaka kushiriki kitu alichojifunza katika darasa la Watoto.

Hadithi hii imetokea huko Indonesia.

Ernesto aliweka shati jingine katika begi lake. Aliangalia kote katika chumba. Ni nini kingine alitakiwa kuchukua? Aliona Kitabu chake cha Mormoni mezani. Hangeweza kukisahau hicho!

Ilikuwa likizo ya majira ya kiangazi. Familia ya Ernesto ilikuwa inaenda kuwatembelea Bibi na Babu. Alikuwa na shauku ya kuwaona bibi na babu.

Picha
Mvulana na wazazi wake wakiwaamkia bibi na babu

Ernesto na familia yake walipofika, babu alimpa kumbatio kubwa. “Nimefurahi sana mmekuja!”

“Tumekukumbuka!” Bibi alitabasamu na kumkumbatia Ernesto pia.

“Nimesubiri sana siku ya leo. Tunapenda kuwatembelea,” Ernesto alisema.

“Twendeni ndani,” alisema Babu. “Bibi anaenda kuwatengenezeeni vyakula vyenu vyote mnavyopendelea.”

Ernesto alitembea kuingia ndani ya nyumba pamoja na Bibi na Babu. Alikuwa mwenye furaha kutumia muda pamoja nao.

Asubuhi iliyofuata, Ernesto aliamka na kukutana na harufu nzuri ya wali ukipikwa. Alimkuta Mama na Bibi wakishughulika jikoni. Aliwabusu wote mashavuni. Kisha alikimbia nje uani.

Baba na babu walikuwa wamekaa wakizungumza nje, na kunywa kutoka katika vikombe.

“ Habari za asubuhi. Je, ungependa kupata chai?” Babu aliinua kikombe chake kwa Ernesto.

Ernesto alikiangalia kikombe kile cha chai na kisha akaangalia kwa babu. Alitaka kushiriki kitu alichojifunza katika darasa la Watoto. “Hapana, asante, Babu” alisema. “Nilijifunza kanisani kwangu kwamba chai, kahawa na tumbaku siyo nzuri kwa miili yetu. Ninataka kufuata kile Yesu ananitaka nifuate.

Baba akatabasamu. “Familia yetu inatii Neno la Hekima, lakini Babu anaamini tofauti, na hilo ni SAWA.”

“Asante kwa kushiriki kitu unachoamini,” Babu alisema kwa Ernesto. “Wewe ni mvulana mzuri. Unaweza ukanywa maji ya moto kama baba yako. Babu akammiminia kikombe cha maji ya moto kutoka kwenye birika.

Ernesto akanywa funda moja. Akahisi furaha ndani kwa kuchagua lililo jema.

Wakati wa chakula cha mchana, Ernesto alikula chakula chake akipendacho. Bibi alitengeneza nasi goreng, chakula cha wali, mayai, nyama na mboga za majani. Ilikuwa tamu sana. Na Ernesto alipenda kuzungumza na Bibi na Babu wakati walipokuwa wakila.

Picha
Sahani ya wali na yai

Jioni, familia walicheza mchezo wa kujificha na kutafutana pamoja. Hata Bibi na Babu walicheza!

“Ninakuona nyuma ya mti, Ernesto!” Baba aliita, huku akimkimbilia. Ernesto alicheka alipokuwa anajaribu kuondoka. Kucheza na familia yake ilikuwa burudani tosha.

Usiku ule, kila mmoja alikaa karibu na Babu wakati alipokuwa akisimulia hadithi. Babu alipomaliza, Ernesto alikumbuka kwamba walikuwa bado hawajasoma maandiko.

Ernesto aliruka. “Nitarudi sasa hivi.”

Alikimbia na kuleta Kitabu chake cha Mormoni. Aliporudi, aliuliza, “Tunaweza kusoma?”

“Nafurahi umekumbuka.” Mama alichukua kitabu kutoka kwa Ernesto na akafungua aya yake aipendayo. Aliisoma kwa sauti. Kisha wote wakapiga magoti chini.

“Mngependa kusali pamoja na sisi?” Ernesto aliwauliza Babu na Bibi zake.

“Ndiyo, itakuwa vizuri,” Bibi alisema. Akapiga magoti karibu na Babu.

Picha
Familia wakisoma Kitabu cha Mormoni pamoja

Baba alisema sala. Alimshukuru Baba wa Mbinguni kwamba walipata muda wa kuwa pamoja kama familia

Baada ya sala, Babu alimpa Ernesto kumbatio. “Ni vyema kwamba familia yako inasali,” alisema. “Ninafurahi unataka kuwa karibu na Mungu. Itaisaidia familia yenu kubaki imara.”

Ernesto alihisi vizuri na mwenye amani moyoni. Alipenda kushiriki imani yake—kitu alichokipenda—pamoja na Bibi na Babu —watu aliowapenda.

Picha
PDF ya hadithi

Vielelezo na Melissa Manwill Kashiwagi

Chapisha