Ujumbe wa Urais wa Kwanza
Wenye Haki Wataishi kwa Imani
Rabi na Mtengeneza Sabuni
Kuna hekaya ya kale ya Kiyahudi kuhusu mtengeneza sabuni ambaye hakumwamini Mungu. Siku moja akiwa anatembea na rabi, alisema, “Kuna kitu nisichoweza kukielewa. Tumekuwa na dini kwa maelfu ya miaka. Lakini kila unakoangalia kuna maovu, ufisadi, udanganyifu, udhalimu, maumivu, njaa, na vurugu. Inaonekana kwamba dini haijausaidia ulimwengu kabisa. Hivyo nakuuliza wewe, ina uzuri gani?”
Rabi hakujibu kwa muda bali aliendelea kutembea na mtengeneza sabuni. Hatimaye walikaribia uwanja wa michezo ambapo watoto, wakifunikwa na vumbi, walikuwa wanachezea udongo.
“Kuna kitu sikielewi,” rabi alisema. “Waangalie wale watoto. Tumekuwa na sabuni kwa maelfu ya miaka, na bado wale watoto ni wachafu. Nini uzuri wa sabuni?”
Mtengeneza sabuni akajibu, “Lakini rabi, si sahihi kuilaumu sabuni kwa ajili ya watoto hawa wachafu. Sabuni inabidi itumike kabla haijatimiza malengo yake.”
Rabi yule akatabasamu na akasema, “Kabisa.”
Jinsi Gani Tunapaswa Kuishi?
Mtume Paulo, akimnukuu nabii wa Agano la Kale, alifanya muhtasari ina maana gani mwenye kuamini pale alipoandika, “Mwenye haki ataishi kwa imani” (Warumi 1:17).
Huenda katika maelezo haya rahisi tunaelewa tofauti kati ya dini ambayo ni dhaifu na isiyo jiamini na ile ambayo ina nguvu na inabadilisha maisha.
Lakini ili kuelewa ina maana gani kuishi kwa imani, ni lazima tuelewe imani ni nini.
Imani ni zaidi ya kuamini. Ni kumwamini kabisa Mungu kukiambatana na matendo.
Ni zaidi ya kutamani.
Ni zaidi ya kukaa nyuma, tukiinamisha vichwa vyetu, na kusema tunakubali. Tunaposema “mwenye haki kwa imani ataishi,” tuna maana tunaongozwa na kuelekezwa na imani yetu. Sisi hutenda kwa njia ambayo inaendana na imani yetu—siyo nje ya mawazo yasiyo ya utiifu bali katika kujiamini na upendo wa kweli kwa Mungu wetu na kwa hekima isiyo na thamani Yeye amefunua kwa watoto Wake.
Imani lazima iambatane na matendo; vinginevyo haina maisha (ona Yakobo 2:17). Sio imani kabisa. Haina nguvu ya kumbadilisha hata mtu mmoja, achilia mbali ulimwengu.
Wanaume na wanawake wenye imani wanaamini katika huruma ya Baba yao wa Mbinguni—hata wakati wa mashaka, hata wakati wa wasiwasi na shida wakati wasipoona vizuri au kuelewa vizuri.
Wanaume na wanawake wenye imani wanatembea njia ya ufuasi na kujitahidi kufuata mfano wa Mwokozi wao mpendwa, Yesu Kristo. Imani inatia hamasa na, hakika, inatusukuma kuielekeza mioyo yetu mbinguni na kuwafikia, kuwainua, na kuwabariki wanadamu wenzetu.
Dini bila matendo ni kama sabuni ambayo imebaki kwenye boksi. Inaweza kuwa na umuhimu wa ajabu, lakini kwa uhakika ina nguvu kidogo ya kuleta tofauti hadi itakapotimiza majukumu yake. Injili iliyorejeshwa ya Yesu Kristo ni injili ya matendo. Kanisa la Yesu Kristo linafundisha dini ya kweli kama ujumbe wa matumaini, imani, na hisani, ikijumuisha kuwasaidia wanadamu wenzetu katika njia za kiroho na kimwili.
Miezi michache iliyopita, mke wangu, Harriet, na mimi tulikuwa kwenye safari ya kifamilia pamoja na baadhi ya watoto wetu katika eneo la Mediterania. Tulitembelea baadhi ya makambi ya wakimbizi na kukutana na familia zilizotoka kwenye nchi zenye vita. Watu hawa hawakuwa wa imani yetu, lakini walikuwa kaka na dada zetu na walihitaji msaada wa haraka. Mioyo yetu iliguswa sana wakati tulipoona kwa macho yetu jinsi imani hai ya waumini wetu wa Kanisa ilivyoleta msaada, faraja, na tumaini kwa wenzetu wenye shida, bila kujali dini, taifa, au elimu yao.
Imani ikiunganishwa pamoja na matendo inajaza moyo kwa wema, akili pamoja na hekima na kuelewa, na nafsi pamoja na amani na upendo.
Imani yetu inaweza kubariki na kwa haki ikashawishi wale wanaotuzunguka na sisi wenyewe.
Imani yetu inaweza kuujaza ulimwengu kwa mema na amani.
Imani yetu inaweza kubadilisha chuki kuwa upendo na maadui kuwa marafiki.
Wenye haki, kisha, huishi kwa imani; wanaishi kwa kumwamini Mungu na kutembea katika njia Yake.
Na hiyo ndiyo aina ya imani ambayo inaweza kumbadilisha mtu mmoja mmoja, familia, mataifa, na ulimwengu.