Liahona
Wanafunzi wa Shule ya St. Theresa Kujiunga na Seminari na Miujiza Kufuata
Julai 2024


Makala

Wanafunzi wa Shule ya Mt. Theresa Kujiunga na Seminari na Miujiza Kufuata

Mnamo 2018, Shughuli za Kibinadamu za Kanisa la Yesu kristo la Watakatifu wa Siku za mwisho zilifanya maboresho muhimu kwenye majengo na vifaa katika Shule ya Sekondari ya Mt. Theresa iliyoko viunga vya Daggoreti huko Nairobi. Mt. Theresa ni shule ya jamii ambayo wanafunzi wake hutokea katika hali ngumu za jamii ya Kabiria. Sambamba na maboresho ya majengo na vifaa, programu ya Kanisa ya Seminari inayoongozwa na waumini wa Kanisa wa Kigingi cha Nairobi West ilifanyika shuleni hapo. Miujiza imefuatia baada ya hapo.

Mnamo 2018, wanafunzi watatu wa Mt. Theresa walijiunga na Seminari. Idadi ya wanaojiunga imezidi kuongezeka maradufu kuanzia kwenye mwanzo huo mtukufu. Wanafunzi 118 wa Mt. Theresa sasa wamejiunga na Seminari. Katika miaka mitatu iliyopita, wanafunzi 73 wa Seminari wamebatizwa na kuwa waumini wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za mwisho. Wahitimu 12 wa Seminari ya Mt. Theresa wanahudumu misioni kwa sasa, na mhitimu mmoja, Stephen Kemboi, amerejea karibuni baada ya kumaliza misheni yake. Miujiza hii na mingine mingi iliyoshuhudiwa juu ya shule yenyewe na wanafunzi wake ni madhihirisho ya baraka ya kuwa na Seminari kwa wanafunzi wa Shule ya Mt. Theresa.

Mnamo Februari 2019, Rais Russell M. Nelson alitoa mwaliko binafsi wa kushiriki katika Seminari na Chuo. Baraka nyingi kwa wanafunzi wa seminari wa Mt. Theresa huakisi mwaliko wa Rais Nelson. Nabii alisema, “Seminari na chuo vitaongeza uwezo wenu wa kujua mambo ya muhimu sana ambayo mtafanya katika maisha.” Rais Nelson aliweka wazi kwamba kushiriki katika Seminari na Chuo kutawalinda washiriki kutokana na tufani za maisha na kuwasaidia waongeze upendo wao kwa Bwana na wengine. Idadi kubwa ya wanafunzi wa Seminari wa Mt. Theresa ambao wamefanya maagano ya ubatizo, na wale wanaotumikia au kujiandaa kutumikia misioni ni ushuhuda hai wa maneno ya nabii – kwamba upendo kwa Bwana na wengine utaongezeka.

Mzee Chamala, ambaye kwa sasa anatumikia huko misioni ya Uganda Kampala na ni mwongofu kutoka programu ya Seminari ya Mt. Theresa, alishiriki jinsi ambavyo programu ya Seminari imekuwa ngao kwake kutokana na tufani za maisha. “Seminari imenisaidia nipate upendo kwa ajili ya Mungu na shukrani kwa ajili ya amri zake. Nilichojifunza kutoka Seminari kimenikinga kutokana na mazoea ya mila zilizozoeleka huko ninakoishi. Seminari imenipatia mlango wa kutorokea kutokana na uraibu wa madawa ya kulevya na kushiriki katika uvunjaji wa sheria ya Bwana ya usafi wa kimwili kulikozagaa katika jamii yangu. Tunahimizana katika njia sahihi pale tunaposimama pamoja katika mahali patakatifu.” Hivi karibuni mmisionari aliyerejea Stephen Kemboi ni mfano wa matokeo chanya ya programu ya seminari kwenye maisha ya wanafunzi. “Mimi ni mfano hai wa vile Seminari na Chuo inavyoweza kufanya kwenye maisha ya mtu pale tunapopokea na kujifunza kanuni sahihi. Programu inaimarisha shuhuda na chaguzi sahihi zinafanywa.”

Mwalimu na Askofu wa Mt. Theresa Simon Mukeku, wa Kata ya Kabiria, ambaye anasaidia kusimamia programu ya Seminari, alisema kwamba mtazamo wa wanafunzi umebadilika sana kwa wema. Japokuwa wanafunzi wengi hutokea katika hali ngumu za kiuchumi huko Daggoreti pembezoni mwa Nairobi, wanafunzi sasa wanaonyesha tumaini kwa ajili ya siku zijazo. Kwa kuongezea, shule imepata mafanikio makubwa ya kielimu na maboresho katika nidhamu miongoni mwa wanafunzi. Mafanikio haya yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na msaada uliotolewa na Huduma za Kibinadamu za Kanisa. Juhudi za kibinadamu zimebadilisha hali chakavu ya miundombinu ya shule kwa kujenga majengo ya kisasa hivyo kuongeza uwezo wa shule wa kutoa elimu bora. Kutoka ofisi zilizoboreshwa, madarasa mazuri na maabara, maktaba ya kisasa na hivi karibuni programu ya chakula, Huduma za Kibinadamu za Kanisa zimesaidia kuibadili shule.

Kwa muda sasa, wahitimu wa seminari wameonesha njaa ya vitu vya kiroho na hamu yao ya kusimika miguu yao kwa uthabiti kwenye njia ya agano. Ushiriki wao hai katika programu za kanisa na miito zimepelekea kuichonga upya Kata ya Kabiria kuwa sehemu ya mkusanyiko kwa ajili ya vijana wadogo. Kila siku, vijana hawa wadogo hutii wito wa nabii wa kusimama mahali patakatifu. Vijana wadogo hukusanyika kwa ajili ya jioni ya familia nyumbani kila Jumatatu jioni na kushiriki katika madarasa ya Chuo cha Dini angalau mara mbili katika juma.

Mabadiliko ya Shule ya Sekondari ya Mt. Theresa hutoa mfano wa matokeo yafikayo mbali ya Huduma za Kibinadamu za Kanisa. Maisha yameboreshwa na nafsi zimeongolewa. Mafanikio ya Mt. Theresa hutoa walau mfano mmoja tu wa juhudi zilizokamilishwa na zinazokubalika za kanisa likishirikiana na shule ili kuboresha majengo na vifaa na kusaidia ubora wa elimu. Shukrani daima zitabakia katika mioyo ya wanufaika wa matendo haya kama ya Kristo yatolewayo na Kanisa na watakatifu waaminifu wa Sayuni ya Kigingi cha Nairobi West.

Chapisha