Liahona
Kumtegemea Mungu
Julai 2024


Makala

Kumtegemea Mungu

Mnamo 2016, wakati Kigingi cha Brazzaville Jamhuri ya Kongo kilipoanzisha darasa lake la kwanza la kujitegemea, akina dada wengi wa kigingi wa Kikundi Saidizi walijiandikisha. Kozi ya wiki 12 ilitoa kwa akina dada uwezo wa kiuchumi na kuandaa njia ya wao kuwa wenye kujitegemea kiroho. “Kujitawala kimwili na kujitawala kiroho huenda kwa pamoja,” alisema Lucia M. Boyembé, mmoja wa washiriki.

Boyembé, mhitimu wa chuo na mjasiriamali, tayari alikuwa anamiliki biashara ndogo wakati alipoanza kozi ya kujitegemea. Darasa lilimfundisha jinsi ya kujenga msingi imara kwa ajili ya biashara yake pamoja na ujuzi wa utunzaji fedha. Alianza kutunza kumbukumbu tofauti za akaunti binafsi na biashara na kutenga pesa kwa ajili ya akaunti ya kuhifadhi. “Nilipoanza biashara yangu ya kuuza bidhaa za kike, niliwauzia wateja wangu kwa mkopo na hawangenilipa,” Boyembé alisema. Kozi ya kujitegemea ilimfundisha yeye kumuuliza Mungu maswali mahususi kuhusu biashara yake. “Nilisali kwa Mungu kuhusu kile nilichopaswa kufanya, na alinifunulia kwamba nahitaji kulipa zaka yangu.” Boyembé alisema kwamba alipoanza kulipa zaka yake mara kwa mara, wateja wake walianza kulipa mikopo yao na biashara yake ikaanza kustawi. Hatimaye, Boyembé alipokea ushuhuda wa umuhimu wa kiroho na wa kimwili wa sheria ya zaka.

Kama Boyembé, Léonce L’or Tsiba alihisi msukumo wa kujiandikisha kwenye darasa la kujitegemea pale lilipotangazwa. Baba yake alikataa kumsaidia baada ya uongofu wake, na alishinda bila chakula wala malazi kwa muda kabla ya kusaidiwa na askofu wake. Kupitia kozi hii, Tsiba alipata utawala mkubwa wa kimwili na kiroho. “Nilijifunza kumtanguliza Mungu kwanza katika maisha yangu,” Tsiba alisema. “Pia nilidhamiria kulipa zaka yangu, kuitumikia familia yangu, marafiki na jamii yangu.”

Karibu na mwishoni mwa kozi, mmoja wa rafiki za Tsiba alimwambia kuhusu tangazo la kazi na alimpendekezea kwamba atume maombi. Uwoga na dukuduku binafsi vilimfanya Tsiba kusita. Hata hivyo kwa msaada wa mkufunzi wake wa darasa la kujitegemea, askofu wake na washiriki wengine wa darasa, Tsiba alipitia wasifu wake binafsi, akafanyia mazoezi usaili na taratibu akapata ujasiri. Alipotuma maombi yake, aliambiwa kwamba muda wa kutuma umekwisha, lakini aliomba tu kuacha maombi na wasifu wake. Wiki mbili baadaye, Tsiba aliitwa kwa ajili ya usaili na kisha kuajiriwa kweye kazi. Baadaye alisema, “Uzoefu ule ulinifundisha kwamba Mungu atatujalia; Yeye anajua hitaji letu. Yeye anahitaji tu tuwe na imani Kwake.”