2023
Sala ya Rosi
Mei 2023


“Sala ya Rosi,” Rafiki, Mei 2023, 14–15.

Sala ya Rosi

Rosi alichoshwa na hisia ya kutostahili kuwa wa mahala pale.

Hadithi hii ilitokea huko Marekani.

Msichana akiwa amekaa kwenye kochi akionekana mwenye huzuni wakati mama yake akimkumbatia

Rosi alidondosha begi lake la mgongoni sakafuni. Ndiyo kwanza alikuwa amemaliza siku yake ya pili katika darasa lake jipya. Na haikuwa siku nzuri.

“Kuna tatizo gani?” Mama aliuliza.

Rosi alijibwaga kwenye kochi. “Baadhi ya watoto darasani kwangu walisema mambo mabaya juu yangu,” alisema. “Kuhusu ngozi yangu ya kahawia.”

Hawakuwepo watu wengi shuleni waliokuwa na ngozi yenye rangi kama ya Rosi, kwa hiyo alihisi kama hakustahili kuwa pale. Lakini utani ulimfanya ahisi vibaya mara mia zaidi.

Mama alionekana mwenye wasiwasi. “Nasikitika,” alisema. Alimkumbatia Rosi. “Nitaongea na mwalimu wako kuhusu hilo.”

Lakini siku ya pili shuleni, Rosi alitaniwa tena. Mvulana mmoja darasani kwake alimfanyia mzaha siku nzima.

Rosi alihisi huzuni. Lakini pia alihisi hasira. Wakati mwingine mvulana huyo alipokoswa adabu, Rosi alibishana naye. Lakini hiyo haikumfanya ahisi vizuri.

Siku moja wakati Rosi aliporudi nyumbani kutoka shule, alikimbia moja kwa moja chumbani kwake. Alikuwa amechoka kufanyiwa mzaha. Alichoka kuhisi hastahili kuwa pale. Alifunika uso wake kwa mto na alilia.

Nitafanya nini? aliwaza. Hakutaka kuhisi hivi kwa mwaka wote wa shule.

Rosi alifuta macho yake. Kisha aliangalia juu kwenye sanamu ndogo ya Yesu ambayo ilikuwa juu ya rafu ya vitabu vyake. Mama alikuwa amempa Rosi ili imsaidie kumkumbuka Yesu.

Labda napaswa kusali, aliwaza. Alipiga magoti na kukunja mikono yake.

Msichana akiwa amepiga magoti katika sala

“Baba mpendwa wa Mbinguni,” nina maumivu makali ndani yangu. Wanafunzi wenzangu wamekuwa wakatili kwangu kwa sababu ya ngozi yangu ya kahawia, na inanifanya nihisi vibaya. Tafadhali nisaidie.”

Ilikuwa vizuri kumweleza Baba wa Mbinguni kuhusu hisia zake. Alijua Alikuwa anasikiliza. Alihisi ukunjufu wa moyo na kupendwa, kama vile alikuwa anafunikwa na blanket laini. Alihisi kwamba rangi yake ya ngozi ilikuwa nzuri. Alikuwa mtoto wa Mungu, na Mungu alimpenda.

Wakati Rosi alipomaliza kusali, alikuwa amepata wazo. Labda kulikuwa na mengi zaidi ambayo angeweza kufanya ili kusaidia kwenye shule yake.

Wiki iliyofuata, Rosi na mama yake walizungumza na watu wenye madaraka katika shule kuhusu nini kilikuwa kinatokea katika darasa lake. Rosi aliwatafuta watoto wengine shuleni waliokuwa wanafanyiwa vitendo vya uonevu na alikuwa rafiki yao. Alijaribu kutomjali mvulana aliyekuwa anamfanyia utani. Na kanisani siku ya Jumapili, alishiriki ushuhuda wake kwamba Baba wa Mbinguni alimpenda kila mtu.

Mambo shuleni hayakutengamaa mara moja. Lakini wakati yalipokuwa magumu, Rosi alikumbuka jinsi alivyohisi wakati wa sala yake. Yeye alikuwa mtoto wa Mungu, na Mungu alimpenda. Na kwa sababu alijua hivyo, angeweza kufanya chochote.

PDF ya hadithi

Vielelezo na Shawna J. C. Tenney