“Muujiza wa Jimena Kuhusu Hekalu,” Rafiki, Mei 2023, 36–37.
Muujiza wa Jimena Kuhusu Hekalu
Jimena alikuwa na wasiwasi. Lakini alijua kuwa Bwana angemsaidia.
Hadithi hii ilitokea huko Guatemala.
Jimena aliingia ndani ya gari na kufunga mkanda wa kiti chake. Yeye na wazazi wake walikuwa njiani kuelekea hekaluni. Hii itakuwa mara yake ya kwanza kufanya ubatizo wa hekaluni. Papi alikuwa anakwenda kumbatiza kwa niaba ya baadhi ya mababu zao. Jimena hangeweza kungoja!
Lakini Jimena aliwaza kuhusu kitu fulani ambacho kilimfanya ahisi kushikwa na hofu ndani. “Papi”, alisema, “vipi kuhusu pampu yangu?”
Jimena alikuwa na kisukari daraja la 1. Ili kubaki mwenye afya, siku zote alikuwa akivaa pampu ya insulini ili kusaidia kudhibiti kiwango cha sukari katika damu yake. Kama hakuvaa kifaa hiki kwa muda mrefu, aliugua.
“Je, wataniruhusu nikivae ndani ya hekalu?” Jimena aliuliza. Moyo wake ulikuwa ukidunda kwa kasi. “Vipi kuhusu wakati nitakapoingia ndani ya maji?”
“Itakuwa sawa,” alisema Papi. “Unaweza kuvaa pampu yako mpaka utakapoingia ndani ya maji. Kisha Mamá atakusaidia uivae tena mara tu unapotoka nje ya maji.”
Mamá aliitikia kwa kichwa. “Na kama utaanza kuugua wakati unapofanya ubatizo, mara moja mwambie Papi na unaweza kuacha.” Mamá aliminya mkono wake. “Tutakuwa pamoja nawe muda wote.”
“Sawa,” alisema Jimena. Bado alihisi wasiwasi. Lakini Mamá na Papi walikuwa wamemsaidia ahisi vizuri angalau.
Wakati walipofika, Jimena alishika mikono ya Mamá na Papi walipokuwa wakitembea kuielekea milango ya hekalu. Mara tu alipoingia ndani, Jimena alihisi hisia za upendo na faraja. Alijua Roho Mtakatifu alikuwa akimwambia kwamba Baba wa Mbinguni atamsaidia, japokuwa alikuwa na wasiwasi. Kila kitu kitakuwa SAWA kama Papi alivyosema.
Jimena alibadilisha na kuvaa nguo nyeupe. Kisha Mamá alimsaidia Jimena kuvua pampu yake. “Itakuwa kwa dakika chache tu,” Mamá alisema. Alimkumbatia Jimena.
Jimena aliingia ndani ya maji. Papi alikuwa akimsubiri. Alinyoosha mkono wake na kumsaidia ashuke ngazi.
Papi alisema sala ya ubatizo na alimzamisha Jimena ndani ya maji. Aliporudi juu, Jimena alitabasamu. Kisha walifanya ubatizo mwingine zaidi.
“Je, unahisi vizuri?” Papi alimnong’oneza sikioni.
“Ndiyo!” alisema Jimena.
Papi alimbatiza kwa niaba ya watu wengine zaidi. “Unaweza kufanya zaidi?” Aliuliza tena.
“Ndiyo!” alisema Jimena.
Baada ya ubatizo wa mwisho, Mamá alimsaidia Jimena avae pampu yake na kukagua kiwango cha sukari katika damu ya Jimena. Mamá alitabasamu. Kilikuwa kawaida! Ilikuwa kama vile Jimena hakuivua pampu yake kabisa.
Kufuatia hapo walikwenda ndani ya chumba kidogo. Papi aliweka mikono yake juu ya kichwa cha Jimena. Alimthibitisha kuwa muumini wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho kwa niaba ya watu waliokufa ambao amebatizwa kwa niaba yao. Sasa mababu zake wangeweza kuchagua kujiunga na Kanisa la Yesu Kristo!
Kwenye jioni ya nyumbani wiki iliyofuata, Jimena na wazazi wake walizungumza kuhusu safari yao ya hekaluni. “Hekalu ni nyumba ya Bwana,” alisema Papi. “Tunapokwenda, tunaweza kupata miujiza katika maisha yetu.”
“Aina gani ya miujiza?” aliuliza Pablo, kaka mdogo wa Jimena.
“Nilikuwa na wasiwasi kuvua pampu yangu ya insulini ili niingie ndani ya maji,” alisema Jimena. “Lakini wakati nilipokuwa nafanya ubatizo, sikuhisi kuumwa hata kidogo. Ulikuwa muujiza!” Jimena alitabasamu. “Na ingawa nilikuwa na hofu, Roho Mtakatifu alinisaidia nihisi utulivu. Huo ulikuwa muujiza pia.”