“Mafuriko ya Upendo,” Rafiki, Mei 2023, 26–27.
Mafuriko ya Upendo
“Je, sisi pia tunaweza kuisaidia familia ya Jose?” Marius aliuliza.
Hadithi hii ilitokea huko Ufilipino.
Wakati Marius alipotembea kwenda nyumbani kwake, aliweza kusikia watu wakizungumza ndani. Alichungulia kupitia dirishani.
Najiuliza nani yuko ndani, aliwaza. Mama yake aliishi katika nchi nyingine kwa sababu ya kazi, kwa hiyo kwa kawaida alikuwa ni yeye na Lola (bibi) pekee nyumbani.
Alifungua mlango. Rafiki zake wote walikuwa pale!
“Hongera!” walisema.
“Tulitaka kukushangilia wewe na medali uliyopata kwenye mashindano yako ya Taekwondo,” alisema Jose, rafiki kipenzi wa Marius.
“Ninajivunia juu yako.” Lola alimpa Marius kumbatio kubwa. “Mama yako yupo kwenye simu! Nina hakika atataka kusikia yote kuhusu medali yako.”
Baada ya Marius kumaliza kuzungumza na Mama, yeye na rafiki zake walifurahia sherehe. Walikuwa na burudani kuzungumza na kula chakula kitamu cha Lola.
“Utapenda kwenda kucheza na mimi mchezo wa kutupa tufe kesho?” Jose aliuliza kabla hajaondoka.
“Ndiyo!” Marius alisema.
Usiku ule kabla ya kwenda kulala, Marius alisali. “Baba wa Mbinguni, nakushukuru Wewe kwa kunipa marafiki na familia adhimu kama hawa. Tafadhali mbariki mama yangu wakati yupo mbali sana. Na tafadhali nibariki mimi niburudike kwenye mchezo wa kutupa tufe na Jose kesho.”
Lakini siku ya pili, Marius hakuweza kwenda kwenye kutupa tufe. Mvua kubwa ilinyesha, na kila mmoja ilibidi abaki ndani nyumbani. Marius alikaa nyumbani, akisikiliza mvua ikiponda paa. Alitamani kumwona Jose.
Kwa siku tatu iliendelea kunyesha. Mitaa ilifurika maji. Baadhi ya nyumba katika ujirani wa Marius zilifurika maji pia.
Baadaye Marius alimkuta Lola jikoni. Alikuwa akipika kitu ambacho kilionekana kuwa kitamu sana.
“Unapika nini?” aliuliza.
“Ninapika chakula kwa ajili ya baadhi ya familia katika kata yetu,” alisema. “Nyumba zao zimefurika maji, kwa hiyo askofu aliniomba nisaidie.”
Marius alimfikiria Jose. “Tunaweza kupika chakula kwa ajili ya familia ya Jose? Wanaweza kuhitaji msaada pia.”
“Hilo ni wazo zuri sana,” Lola alisema.
Marius alipika wali na mayai ya kukaanga kwa ajili ya Jose na familia yake. Kisha alimsaidia Lola kufungasha chakula.
Hatimaye mvua ilikoma. Marius na Lola walitembea kwa shida kwenye mitaa kupeleka chakula. Maji yalifika kweye magoti ya Marius!
Walimkuta Jose na familia yake wamesimama nje ya nyumba yao. Jose alikuwa akilia.
Marius alimkumbatia rafiki yake. “Pole kwa nyumba yenu kufurika maji,” alisema. “Yesu anawapenda. Na sisi pia tunawapenda.”
Kwa pamoja Marius na Jose walisaidiana kusafisha vitu vyenye matope ndani ya nyumba ya Jose. Marius aliimba “Mimi ni Mtoto wa Mungu,” walipokuwa wakifanya kazi. Wakati walipopumzika, Marius alimpa Jose chakula alichopika kwa ajili yake.
“Asante kwa kuisaidia familia yangu,” alisema Jose. “Na asante kwa chakula! Ni kitamu sana.”
“Karibu sana,” Marius alisema.
“Je unadhani ungeweza kuniambia zaidi kuhusu Yesu? Na ule wimbo uliokuwa unauimba?” aliuliza Jose.
“Hakika!” Marius alisema. “Ungependa kuja kanisani pamoja na mimi Jumapili? Huko ndiko ninakojifunza kuhusu Yesu. Na tunaweza pia kuimba pamoja.”
“SAWA,” Jose alisema.
Marius alihisi vizuri moyoni. Alifurahi kwamba aliweza kumsaidia Jose na familia yake. Na alikuwa na furaha kwamba aliweza kushiriki injili pia.