2023
Marafiki wa Origami
Mei 2023


“Marafiki wa Origami,” Rafiki, Mei 2023, 30–31.

Marafiki wa Origami

Ni jinsi gani Ari na rafiki zake wangeweza kumsaidia Bi. Franklin?

Hadithi hii ilitokea huko Marekani.

Picha
Wasichana watatu wakimpungia mikono mkutubi

“Muda wa mapumziko!” Mwalimu wa Ari alisema.

Wana darasa wenzake Ari walisimama kwenye mstari kwenda nje kwenye uwanja wa michezo. Lakini Ari na rafiki zake siku zote walikwenda maktaba. Walipenda kuazima vitabu na kufanya kazi za mikono pamoja.

Kristin na Ella walikuwa tayari wanangojea karibu na mlango. Ari alinyakua kitabu chake na rundo la karatasi. Kisha aliongoza njia kuelekea kwenye ukumbi.

“Nategemea kitabu cha The Dragon Keeper’s Secret kimerudishwa!” Ari alisema. “Nimetaka kukiazima kwa muda mrefu.”

Walipofika maktaba, wasichana walimpungia mikono Bi. Franklin, mkutubi wa shule. Siku zote alikuwa akiwapokea kwa tabasamu la furaha. Lakini leo tabasamu lake halikuonekana la bashasha.

Ari alikunja uso alipokuwa akiweka kitabu chake mezani. “Je, Bi. Franklin alionekana kama vile mwenye huzuni kwenu?”

Kristin alijibu kwa kupandisha mabega. “Huenda alikuwa tu na shughuli nyingi.”

“Labda.” Ari alikaa kitako na kutoa kipande cha karatasi. Alikikunja kwa uangalifu, akilainisha mikunjo kwa kidole gumba chake.

“Leo tunatengeneza nini?” Ella aliuliza.

“Vipi kuhusu alamisho?” Ari alisema. “Hizo ni rahisi sana Nitawaonesha.”

Ari amekuwa akijifunza jinsi ya kutengeneza origami. Ilikuwa aina ya sanaa kutoka Japan, iliyofanywa kwa kukunja karatasi kwenye maumbo tofauti tofauti. Ari alijua jinsi ya kutengeneza aina zote za maumbo, na aliwafundisha rafiki zake kile alichojifunza.

Ari aliwaonesha Kristin na Ella jinsi ya kutengeneza kila mkunjo. Punde wote watatu walikuwa na alamisho ndogo ya mraba

Picha
Wasichana watatu wakitengeneza origami

“Inakaa kwenye kona, kama hivi.” Ari alifungua kitabu chake na alipenyeza alamisho kwenye kona ya ukurasa.

“Vizuri!” Kristin alinyakuwa karatasi nyingine. “Ninataka kujaribu mimi mwenyewe.”

Walipokuwa wakifanya kazi, walizungumza kuhusu vitabu walivyokwisha kuvisoma na vile walivyotaka kuvisoma wakati ujao. Ari alimtupia tena jicho Bi. Franklin. Bado alionekana mwenye huzuni kidogo.

Mara Bi. Franklin alisimama kando ya meza yao.

“Mambo, wasichana.” Aliweka kitabu kwenye meza. Kilikuwa kitabu cha the dragon keeper! “Hiki ni kwa ajili yako, Ari. Ninajua umekuwa ukisubiri kukisoma.”

“Asante!” Ari alikiinua.

Bi. Franklin alishusha pumzi. “Mtu fulani alipora gari langu leo. Walichukua vitabu vyangu vyote na muziki wangu wote.”

“Hiyo inatisha!” Kristin alisema.

Bi. Franklin aliwapa tabasamu la huzuni. “Vyema, ni vitu tu. Vitu vinaweza kununuliwa tena. Nafurahi tu kwamba hakuna mtu aliyeumia”

Ari alimwangalia Bi. Franklin akiondoka.

“Natamani tungefanya kitu fulani ili kumsaidia,” Ella alisema.

Ari alitazama alamisho ya origami mikononi mwake. “Labda tunaweza!”

“Kama kipi?” Kristin aliuliza.

Ari alitabasamu. “Njooni nyumbani kwetu baada ya shule. Nina wazo.”

Siku iliyofuata, Ari, Kristin na Ella walikwenda maktaba wakati wa mapumziko yao, kama walivyofanya siku zote. Lakini wakati huu, hawakuleta vitabu tu. Walikuwa na kitu maalumu kwa ajili ya Bi. Franklin.

“Tumetengeneza hivi kwa ajili yako!” Ari alimpa Bi. Franklin mfuko. “Tunajua hatuwezi kurudisha vitu vyote ambavyo viliibwa, lakini tumewaza hivi vinaweza kukufariji.”

Bi. Franklin alitazama ndani ya mfuko. Ulikuwa umejaa alamisho za—origami za samaki, mioyo, vipepeo. Alitoa tabasamu angavu.

“Hii ni ya kupendeza! Asanteni sana.” Alichomoa kipande cha origami kutoka kwenye mfuko. Kilikunjwa kutengeneza kijitabu kidogo. “Ninakwenda kutumia shajara hii ndogo kuandika mawazo yangu yote madogo madogo ya furaha!”

Ari alitabasamu pia. Siku zote angeweza kufanya jambo zuri kwa ajili ya wengine—mkunjo mmoja wa karatasi kwa wakati.

Picha
PDF ya hadithi

Vielelezo na Brian Martin

Chapisha