2023
Cameron Mpiga Piano
Mei 2023


“Cameron Mpiga Piano,” Rafiki, Mei 2023, 40–41.

Cameron Mpiga Piano

Cameron hakujua jinsi ya kupiga, lakini alitaka kusaidia.

Hadithi hii ilitokea huko Marekani.

Picha
Mvulana akifanya mazoezi ya kupiga piano

“Mimi ni mtoto wa Mungu,” Cameron aliimba pamoja na watoto wengine wa Msingi. Cameron alikuwa mzito wa kusikia lakini alipenda kuimba. Na punde tu watakuwa wakiimba katika programu ya Msingi. Mwezi mmoja tu ulikuwa umebakia!

Wakati muda wa kuimba ulipokwisha, Dada Jones alitoa tangazo. “Mpiga piano wetu wa Msingi atahama hivi karibuni. Tungependa baadhi yenu mpige piano kwa ajili ya programu ya Msingi. Nani kati yenu angependa kupiga wimbo mmoja au zaidi?

Cameron alinyoosha mkono wake. Alitaka kusaidia kwenye programu.

Dada Jones aliorodhesha majina ya watoto waliotaka kusaidia. “Emma. Ben. Na Cameron! Sikujua kama unaweza kupiga.” Dada Jones alitabasamu.

Cameron kamwe hakuwahi kuchukua masomo ya piano, lakini alipenda kutengeneza nyimbo kwenye piano nyumbani kwa bibi yake.

“Bado sijajua vizuri sana,” alisema. “Lakini nadhani nitaweza kama nikifanya mazoezi!”

“Asanteni kwa kuwa tayari kuhudumu,” Dada Jones alisema. Aliwapa kila mtoto nyimbo mbili za kupiga.

Cameron alihisi kukimbia kuzunguka ukumbi. Siku zote alitaka kujifunza na sasa alikuwa anakwenda kufanya hivyo!

“Unaonekana mwenye furaha! Kuna chochote kimetokea katika Msingi?” Mama aliuliza walipoingia ndani ya gari baada ya kutoka kanisani.

Cameron alitabasamu. “Ninakwenda kupiga piano kwa ajili ya programu ya Msingi!”

“Ninapenda kwamba unataka kusaidia,” Mama alisema. “Lakini hujui jinsi ya kupiga piano vizuri kiasi cha kutosha kufanya hivyo.”

Cameron aliketi wima. “Ninaweza kujifunza. Nitafanya mazoezi makali sana! Ninaweza kutumia piano ya Bibi.”

“Ni vyema tukaanza, basi!” Mama alisema.

Mama alimsaidia Cameron kumpata mwalimu wa piano. Mwalimu alimwonyesha njia rahisi za kupiga “I Love to See the Temple” na “The Church of Jesus Christ.”

Cameron alifanya mazoezi nyumbani kwa bibi yake mara kwa mara kadiri alivyoweza. Alifanyia mazoezi kila mstari wa nyimbo tena na tena. Alifanya makosa mengi, lakini aliendelea kujaribu na aliendelea kupiga. Hatimaye aliweza kupiga nyimbo zote mbili.

Punde ulikuwa muda kwa programu ya Msingi. “Je, unahisije?” Mama aliuliza.

Cameron alikumbatia kitabu chake cha piano karibu na kifua chake. “Wasi wasi Lakini mwenye furaha pia.”

Picha
Mvulana akipiga piano na watoto wakiimba

Ilipofika zamu yake kupiga, mikono ya Cameron ilitetemeka kidogo. Baba wa Mbinguni, tafadhali nisaidie, alisali akilini mwake. Alivuta pumzi ndefu. Kisha alipiga vizuri kadiri alivyoweza. Watoto wengine waliimba sambamba naye.

Mwisho wa wimbo, alitabasamu. Ilikuwa burudani kweli! Alijua Roho Mtakatifu alikuwa akimsaidia.

Sasa kwa kuwa alikuwa amepiga wimbo mmoja tayari, Cameron alihisi kujiamini zaidi. Alianza wimbo wa pili. Vidole vyake vilitembea kuvuka vibao kama vile alivyokuwa amefanya mazoezi.

Wimbo huu ulikuwa ule aupendao Cameron. Alifikiri kuhusu maneno alipokuwa akipiga. “Ninaamini katika Mwokozi, Yesu Kristo. Nitaliheshimu jina Lake.” Cameron alikuwa amefanya kazi kwa bidii kujifunza nyimbo kwa ajili ya programu.

Pengine kupiga piano ni njia mojawapo ya kushiriki ushuhuda wangu, Cameron aliwaza.

Baada ya programu, Mama alimpa Cameron kumbatio kubwa.

“Ilikuwaje?” alimwuliza.

“Nilikuwa na wasiwasi hapo mwanzo, lakini ilikuwa burudani!” Cameron alisema. Alitaka kuendelea kufanya mazoezi na kujifunza nyimbo nyingi zaidi.

Picha
PDF ya hadithi

Vielelezo na Adam Koford

Chapisha