Rafiki
Urafiki wa Chesi
Mei 2024


“Urafiki wa Chesi,” Rafiki, Mei 2024, 14–15.

Urafiki wa Chesi

Wangecheza vipi kama hawangeweza kuelewana?

Hadithi hii ilitokea huko Ujerumani.

“Kuna Nuru Moyoni Mwangu!” Matvii anaimba. Mama yake na kaka yake, Tymofii wanaimba pamoja naye. Ilikuwa giza nje ya dirisha la gari. Lakini wimbo ulisaidia kila kitu kuhisi angavu kidogo.

Ulikuwa ni wakati wa kutisha kwa Matvii na familia yake. Walikuwa wanahamia Ujerumani kwa sababu nyumbani kwao hakukuwa salama kabisa. Walisafiri kwa siku mbili, na sasa walikuwa wamekaribia kufika huko. Askofu hapa Ujerumani alikuwa anawaendesha kwa gari hadi mahali ambako wangeishi.

Matvii alikuwa na shukrani kwamba Baba wa Mbinguni alikuwa amewasaidia kufika Ujerumani salama. Lakini alimkumbuka Baba yake. Yeye alimbidi abakie katika nchi yao kwa sababu ya vita. Matvii alikuwa na wasiwasi sana kumhusu yeye.

Askofu aliegesha gari nje ya nyumba. “Karibuni nyumbani kwangu.”

Matvii alitwaa mkoba wake na kuifuata familia yake ndani. Nyumba ilikuwa kimya. Familia ya askofu lazima ilikuwa imeshalala tayari.

“Mnaweza kukaa katika vyumba vya Mats na Lore wakati mnakaa hapa,” askofu alisema.

“Ngoja,” Mama alisema. “Hawahitaji kutuachia vyumba vyao.”

Askofu alitabasamu. “Wanafurahi kufanya hivyo. Tunataka mwendelee kuhisi faraja.”

Mama alikubali kwa kichwa. “Asanteni.”

Asubuhi, Matvii na Tymofii walienda jikoni kwa ajili ya kiamsha kinywa. Askofu alikuwa alikuwa mezani na mvulana na msichana. Hawakuoneka kuwa wakubwa sana kuliko Matvii.

“Hawa ni watoto wangu Mats na Lore” askofu alisema.

“Ni furaha kukutana nanyi,” Tymofii alisema.

Mats na Lore walionekana kukanganyikiwa kidogo.

“Hawaongei lugha yenu,” askofu alisema. “Lakini nina hakika watakuwa marafiki wazuri.”

Matvii alikunja uso. Wangekuwa marafiki vipi kama hawangeweza wao kwa wao kuongeleshana? Alihisi kama nuru aliyokuwa akimba kuhusu usiku uliopita haipo tena.

Baada ya kula, Mats na Lore waliwaonyesha chumba cha michezo. Watoto wawili wadogo walikuwa huko wanacheza na wanasesere. Matvii alidhani walikuwa ni wadogo wa Mats na Lore.

Mats alisema kitu. Ilisikika kama swali, lakini Matvii hakujua kilichosemwa. Mats alikaa kitako na kufungua sanduku la kadi. Alizipanga katika rundo. Kisha yeye na Lore wakatwaa kadi zao. Matvii alitaka kucheza. Lakini hakujua jinsi ya kucheza!

Mats alipanga kadi chini na kumtazama Matvii. Alisema kitu fulani tena.

Matvii alitaka kulia. Hakutaka kuishi Ujerumani kama hangwweza kumwelewa mtu yeyote.

Lore alisema kitu kwa Mats, kisha akakimbia kabatini. Alirudi na kupanga mchezo mpya sakafuni.

Matvii alijua mchezo huu mpya. Vipande vya mbao vilionekana kama vile alivyokuwa navyo nyumbani. Ilikuwa ni chesi! Alikuwa amecheza na Baba kwa masaa mengi. Matvii aliitikia kwa furaha. Alijua jinsi ya kucheza mchezo huu.

Lore alitabasamu sana na kuanza kupanga vipande hivi.

Matvii alisogeza askari wake miraba miwili na alimtazama Lore akisogeza kete yake yenye kichwa cha farasi. Kisha Matvii akasogeza askofu wake kwa shujaa wa Lore Yeye na Tymofii walishangilia. Lore alitoa sauti ya kukata tamaa, lakini alikuwa anatabasamu.

Picha
Watoto wakicheza chesi

Walicheza kwa muda mrefu. Punde wakawa wanacheka. Hawakuelewa maneno ya mmoja na mwingine, lakini bado walikuwa na burudani.

Katika wiki chache zilizofuata, walipata michezo mingine ambayo wote waliijua. Walicheza mpira wa miguu nje pamoja na watoto wengine wa Kijerumani. Matvii alijifunza maneno machache ya Kijerumani pia. Wakati mwingine alifanya makosa, lakini aliendelea kujaribu.

Matvii bado alimkumbuka baba yake na nyumba yao. Lakini alikuwa na furaha kwamba Baba wa Mbinguni alikuwa amemsaidia kupata marafiki wapya.

Picha
PDF ya hadithi

Vielelezo na Hannah Li

  • Wimbo wa Kanisa, na. 227.

Chapisha