Mkutano Mkuu
Kwenye Njia ya Jukumu Lao
Mkutano mkuu wa Oktoba 2023


14:29

Kwenye Njia ya Jukumu Lao

Ninyi ambao hivi leo mnasonga mbele katika njia ya jukumu lenu ni nguvu ya Kanisa la Mwokozi lililorejeshwa.

Ninaomba kwa dhati msaada wa Roho Mtakatifu wakati huu ninapoelezea upendo wangu, matamanio na shukrani kwa waumini wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho kote ulimwenguni.

Wao wa Mkokoteni wa Mwisho

Mwaka 1947 ilikuwa ni kumbukizi ya miaka 100 ya waanzilishi Watakatifu wa Siku za Mwisho wa mwanzo kuwasili Bonde la Salt Lake. Sherehe nyingi za kumbukizi zilifanywa katika mwaka huo, na shukrani zisizo na idadi zilitolewa kwa wafuasi waliojitoa wa Yesu Kristo ambao walioweka alama ya njia, wakajenga nyumba, wakapanda mazao katika jangwa kame na kuanzisha makazi.

Rais J. Reuben Clark, Mshauri wa Kwanza katika Urais wa Kwanza, alitoa moja ya shukrani inayokumbukwa na ya kugusa sana kwa waanzilishi hawa kwenye mkutano mkuu wa Oktoba 1947.

Katika ujumbe wake, Rais Clark kwa ufupi aliwatambua viongozi ambao waliongoza uhamiaji wa kuelekea magharibi, kama vile Brigham Young, Heber C. Kimball, Wilford Woodruff, Parley P. Pratt na wengine wengi. Hata hivyo, lengo lake kuu lilikuwa siyo kusimulia tena mafanikio ya watu hawa mashuhuri. Bali, alifokasi maneno yake kwenye nafsi tiifu ambazo majina yao hayajulikani wala hayakuwekewa kumbukumbu rasmi kwenye historia ya Kanisa. Kichwa cha somo cha ujumbe wake ni “Wale wa Mkokoteni wa Mwisho.”1

Rais Clark alieleza kwa kina sifa na changamoto za wahamiaji ambao walisafiri katika mkokoteni wa mwisho katika msururu wa mikokoteni ambayo ilivuka nyanda. Aliwasifu mashujaa hawa wasiojulikana na walio sahaulika ambao, siku hata siku, wiki baada ya wiki na mwezi baada ya mwezi, walipigwa na vumbi lililotolewa na mikokoteni yote iliyokuwa mbele yao—na ambao walishinda vikwazo vizito walivyokabiliana navyo njiani.

Rais Clark alitangaza, “Wale wa mkokoteni wa mwisho walisonga mbele, kwa taabu na uchovu, miguu iliyovimba, wakati mwingine nusura wakate tamaa, wakibebwa na imani yao kwamba Mungu aliwapenda, kwamba injili ya urejesho ni ya kweli na kwamba Bwana aliwaongoza na kuwaelekeza Ndugu zao waliokuwa mbele.”2

Alihitimisha ujumbe wake kwa maoni haya ya kugusa: “Kwa nafsi hizi nyenyekevu, hodari katika imani, hodari katika kazi, hodari katika kuishi kwa haki, hodari katika kuchonga urithi wetu wa thamani, kwa unyenyekevu natoa upendo wangu, heshima, unyenyekevu wangu mkuu.”3

Hakuna Huduma Ndogo

Mwaka 1990, Rais Howard W. Hunter, wakati huo akiwa Rais wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili, alitoa ujumbe kuhusu mchango usio na kifani wa waumini wasio na idadi ambao wanahudumu kwa bidii na kwa uaminifu na ambao wanapokea au hawapokei utambuzi au shukrani ya umma.

Rais Hunter alifafanua:

“Ilisemwa [kuhusu Moroni Kapteni mdogo na jasiri]:

“‘Ikiwa watu wote wangekuwa, na wako, na ikiwa daima watakuwa, kama Moroni, tazama, hizo nguvu za jehanamu zingetingishika milele; ndiyo, ibilisi hangekuwa na uwezo juu ya mioyo ya watoto wa watu’ (Alma 48:17).

“Ni pongezi iliyoje kwa mtu maarufu na jasiri. … Mistari miwili baadaye ni kauli kuhusu Helamani na ndugu zake, ambao hawakuwa na jukumu dogo kuliko Moroni, ambayo inasomeka:

“‘Sasa tazama, Helamani na ndugu zake hawakufanya kazi ndogo kwa watu kuliko Moroni’ (Alma 48:19).”

Rais Hunter aliendelea, “Kwa maneno mengine, ijapokua Helamani hakuwa maarufu au aliyesikika kama Moroni, alikuwa kama mtoa huduma sawa; yaani, alikuwa mwenye msaada au muhimu kama Moroni.”4

Rais Hunter kisha alitushauri sote kutokuwa dhaifu kwenye huduma. Alisema: “Kama unahisi kwamba mengi ya yale unayofanya mwaka huu au miaka ijayo hayakufanyi uwe maarufu, jipe moyo. Watu wengi wazuri sana walio wahi kuishi hawakuwa maarufu. Hudumu na ukue, kwa uaminifu na kimya kimya.”5

Kwenye Njia ya Jukumu Lao

Nina shukrani kwa mamilioni ya waumini wa Kanisa ambao hivi leo huja kwa Mwokozi6 na kusonga mbele kwenye njia ya agano katika mikokoteni ya mwisho ya msururu wa mikokoteni yetu ya sasa—na ambao kwa dhati hawafanyi kazi ndogo. Imani yenu thabiti katika Baba wa Mbinguni na Bwana Yesu kristo na maisha yenu yasiyo ya kuigiza, yaliyowekwa wakfu hunivutia niwe mtu na mfuasi mwema zaidi.

Ninawapenda. Ninawatamania. Ninawashukuru. Na ninawapongeza.

Kauli moja katika Kitabu cha Mormoni iliyotolewa na Samweli Mlamani inafupisha hisia zangu kwenu vyema zaidi.

“Sehemu yao kubwa wako kwenye kazi yao, na wanatembea kwa uangalifu mbele ya Mungu, na wanatii amri zake na sheria zake na maamuzi yake. …

“Ndiyo, ninawaambia, kwamba sehemu yao kubwa wanafanya hivi, na wanajaribu kwa bidii bila kuchoka ili walete ndugu zao waliosalia kwenye elimu ya ukweli.”7

Ninaamini kifungu cha maneno “kwenye njia ya jukumu lao” humaanisha akina kaka na akina dada ambao huwatafuta na kukaa kando ya watu walio wapweke katika mikutano ya kanisa na katika matukio mengine tofauti tofauti. Daima huwafariji wale wanaohitaji faraja,8 bila matarajio ya kutambulika au kupewa sifa.

Kifungu cha maneno “kwenye njia ya jukumu lao” humaanisha wanandoa na watoto wanao msaidia mwenza, mzazi au mtoto ambaye anahudumu katika nafasi ya uongozi katika Kanisa lililorejeshwa la Bwana. Ushawishi wao wa kuunga mkono kwa dhati, usio wa kelele na usiotambulika unaleta baraka kwa watu na familia nyingi katika njia ambayo itajulikana kikamilifu katika umilele pekee.

Kifungu cha maneno “kwenye njia ya jukumu lao” humaanisha watu ambao, baada ya kuwa mbali na Mungu, kwa unyenyekevu hurejea‑Kwake tena,9 wakitubu dhambi zao, na kutafuta nguvu ya utakaso na uponyaji ya Upatanisho wa Mwokozi. Kuja kwa Kristo10 kwa kurejea kwenye njia ya agano kutoka kwenye njia za dhambi katika “njia zilizo kataliwa”11 ni muhimu kiroho na ni jitihada njema. Wanaposonga mbele kwa imani na pasipo kuchoka katika kutenda mema, wanaweka msingi wa kazi kuu katika maisha yao binafsi,12 “kwa vizazi vyote na kwa milele yote.”13

Kifungu cha maneno “kwenye njia ya jukumu lao” kinamaanisha watu wema ambao wanatamani kufungiwa nira kwa Mwokozi kupitia maagano na ibada zilizoidhinishwa za injili Yake—lakini wanaweza kuzuiliwa kufanya hivyo kwa vikwazo vilivyo nje ya uwezo wao. Ninakuahidi maumivu yako binafsi yataondolewa na utiifu na uaminifu wako kwa subira kuweka matakwa yako kwa Mungu vitalipwa katika “wakati wa Bwana.”14 “Kulia kunaweza kudumu kwa usiku mmoja, lakini furaha huja asubuhi.”15

Kifungu cha maneno “kwenye njia ya jukumu lao” kinamaanisha watafsiri na wakalimani ulimwenguni kote ambao humtumikia Bwana kwa kuwasaidia marafiki na waumini “wasikie utimilifu wa injili katika ndimi [zao] wenyewe, na katika lugha [zao] wenyewe.”16 Sauti zao, lugha za alama, na nyaraka zilizotafsiriwa hufikisha kweli za milele, na bado wachache wetu huwajua majina yao au kamwe hawajawahi kupewa asante. Kupitia kipawa cha ndimi walichobarikiwa nacho, watafsiri na wakalimani hutumikia kwa bidii, bila ubinafsi na mara nyingi, bila kujulikana ili kuwasaidia watu wapokee zawadi ya kiroho ya imani kupitia kusoma na kusikia neno la Mungu.17

Kifungu cha maneno “kwenye njia ya jukumu lao” kinamaanisha wanandoa waaminifu waume na wake ambao huheshimu jukumu la agano lao la kuzaa na kuijaza dunia, na ambao wamebarikiwa kwa nguvu na ustahimilivu wa kukimbizana na watoto wao katika mikutano ya sakramenti. Katika ulimwengu wenye mkanganyiko unaoongezeka uliojaa majanga na vipaumbele hewa, nafsi hizi jasiri hazisikilizi sauti za ulimwengu zinazosisitiza kujijali binafsi; zinaheshimu usafi wa maadili na umuhimu wa maisha katika mpango wa furaha wa Baba wa Mbinguni kwa watoto Wake.

Wanandoa wengi pia huamini katika Mungu wakati matamanio yao mema ya mioyo hayatimii kwa namna na wakati waliotarajia au kupanga. Wao “humngojea Bwana”18 na hawahitaji kwamba Bwana akimbizane na muda wao waliojiwekea. “Maana tangu mwanzo wa ulimwengu watu hawakusikia wala kufahamu kwa masikio, wala jicho lo lote halikuona, Ee Mungu, zaidi yako wewe, ni mambo gani makuu uliyoyaandaa kwa ajili yake yeye akungojae wewe.”19

Kifungu cha maneno “kwenye njia ya jukumu lao” kinamaanisha maelfu na maelfu ya viongozi wa watoto na waalimu wa msingi ambao huwapenda na kuwafundisha watoto wa Kanisa kila Siku ya Sabato.

Fikiria matokeo ya milele ya huduma itolewayo na wafuasi hawa waliojitolea—na baraka kuu zilizoahidiwa kwa wale wanao wahudumia watoto.

“[Yesu] akatwaa mtoto, akamweka katikati yao; na alipomchukua mikononi mwake, aliwaambia,

“Mtu akimpokea mtoto mmoja wa namna hii kwa jina langu, anipokea mimi; na mtu akinipokea mimi, humpokea, si mimi, bali yeye aliyenituma.”20

Kifungu cha maneno “kwenye njia ya jukumu lao” kinamaanisha watoto waliojitoa kuwajali wazazi wao wazee, mama asiye na usingizi akimfariji mtoto mwoga wakati akimlinda kama “simba jike kwenye lango” la nyumba yake,21 waumini wa Kanisa ambao hufika mapema na kuchelewa kutoka ili kupanga na kuondoa viti, na watu wanaoalika familia, marafiki na washirika ili kuja na kuona, kuja na kusaidia, na kuja na kubakia.22

Nimeeleza mifano michache tu niliyochagua ya wafuasi washika maagano na waliojitoa wa Yesu Kristo kama wewe ambao mnasonga mbele “kwenye njia ya jukumu [lenu].” Mamilioni ya mifano ya ziada ya watakatifu wa siku za mwisho ambao hujitoa kwa “mioyo yao yote”23 kwa Mungu wanapatikana katika nyumba ambazo kitovu chake ni Kristo na katika matawi na kata za Kanisa kote ulimwenguni.

Mnapenda na mnahudumu, mnasikiliza na kujifunza, kujali na kufariji, na kufundisha na kushuhudia kwa nguvu ya Roho Mtakatifu. Mnafunga na kuomba mara kwa mara, mnaimarika na kuwa imara katika unyenyekevu, na mnakuwa imara zaidi na zaidi katika imani juu ya Kristo, “hadi nafsi [zenu] zikajazwa na shangwe na faraja, ndiyo, hata kwenye kusafishwa na utakaso wa mioyo [yenu], utakaso ambao huja kwa sababu ya … kumtolea Mungu mioyo [yenu].”24

Ahadi na Ushuhuda

Wao wa mkokoteni wa mwisho, wote ambao hawafanyi kazi ndogo, na nyie ambao hivi leo mnasonga mbele katika njia ya jukumu lenu ni nguvu ya Kanisa la Mwokozi lililorejeshwa. Na kama Bwana alivyoahidi, “enzi zote na tawala, himaya na nguvu, zitafunuliwa na kuwekwa juu ya wote ambao wamestahimili kwa ujasiri mkubwa kwa ajili ya injili ya Yesu Kristo.”25

Kwa shangwe nashuhudia kwamba Baba wa Mbinguni na Mwanaye Mpendwa wako hai, na ahadi Zao ni za kweli, katika jina takatifu la Bwana Yesu Kristo, amina.