Mkutano Mkuu
Mwenzi Wetu Daima
Mkutano mkuu wa Oktoba 2023


Mwenzi Wetu Daima

Wewe na mimi tunayo fursa ya kuwa na Roho Mtakatifu kama mwenzi wetu daima.

Wapendwa akina kaka na dada zangu, katika mkutano huu tumebarikiwa kwa mbubujiko wa ufunuo. Watumishi wa Bwana Yesu Kristo wamezungumza na watazungumza maneno ya ukweli, ya kutia moyo, na yenye mwongozo.

Nimeguswa na shuhuda zilizotolewa katika mkutano huu kwamba Bwana huzungumza nasi binafsi kupitia Roho Mtakatifu. Tunaposali na kisha kusikiliza misukumo ya Roho, tunapata utambuzi mkubwa na baraka kuu za kutuongoza kupita siku ngumu zinazoongezeka mbele.

Tumesikia tena onyo la Rais Russell M. Nelson kwamba, “Katika siku zijazo, haitawezekana kunusurika kiroho bila mwongozo, maelekezo, faraja na ushawishi wa mara kwa mara wa Roho Mtakatifu.”1

Onyo hilo la kinabii limenisukuma kutafakari kile ninachoweza kuwafunza watoto wangu, wajukuu na vitukuu kuhusu jinsi ya kuwa na mwongozo huo muhimu katika siku zao ngumu zijazo.

Hivyo, ujumbe huu leo ni barua fupi kwa uzao wangu ambao utawasaidia wakati sipo pamoja nao katika siku za kusisimua zijazo. Ninataka wajue kile nilichokijua ambacho kitawasaidia.

Nimekuja kuelewa vyema zaidi kile ambacho kitahitajika kwao ili wawe na ushawishi wa daima wa Roho Mtakatifu katika siku ambazo wataishi. Na nimehisi kuvutiwa kuzungumza leo juu ya uzoefu wangu binafsi wa kumwalika Roho Mtakatifu, karibu zaidi niwezavyo, ili awe mwenzi wangu daima. Sala yangu ni kwamba niweze kuwahimiza.

Ningeanza kwa kuwafanya wafikirie na wasali kuhusu wana wa Helamani, Nefi na Lehi, na watumishi wengine wa Bwana wakifanya kazi pamoja nao. Walikabiliwa na upinzani mkali. Walikuwa wakitumikia mahali penye uovu na ilibidi wakabiliane na udanganyifu wa kutisha. Ninapata ujasiri, nanyi vivyo hivyo mngeweza, kutokana na aya hii moja kutoka kwenye kumbukumbu ya Helamani:

“Na katika mwaka wa sabini na tisa kulianza kuwa na mzozo mkuu. Lakini ikawa kwamba Nefi na Lehi, na wengi wa ndugu zao ambao walijua kuhusu ukweli wa mafundisho ya dini, wakiwa na mafunuo mengi kila siku, kwa hivyo waliwahubiria watu, mpaka kwamba wakaweka kikomo kwa mzozo wao katika mwaka huo huo.”2

Tukio hili linanipa moyo, na linaweza kuwapa moyo. Wana wa Helamani walifundishwa na kuongozwa na mfululizo wa matukio ya Roho Mtakatifu. Hii inanihakikishia kwamba tunaweza kufundishwa na kujifunza kutoka kwa Roho mstari juu ya mstari, tukipokea kile tunachohitaji, na kisha tunapokuwa tayari, tutapokea zaidi.

Nimetiwa moyo kwa njia hiyo hiyo na maelezo ya Nefi kuombwa kurudi Yerusalemu kwa ajili ya mabamba ya Labani. Mnakumbuka uamuzi alioufanya. Alisema, “Nitaenda na kutenda vitu ambavyo Bwana ameamuru.”3

Uzoefu wa Nefi juu ya Roho Mtakatifu katika jukumu hilo umenipa ujasiri mara nyingi wakati nilipokuwa kwenye majukumu niliyojua yametoka kwa Bwana lakini ambayo yalionekana kupita uzoefu wangu wa nyuma na kupita kile nilichokiona kama uwezo wangu.

Mnakumbuka kile Nefi alichokisema kuhusu uzoefu wake: “Na ilikuwa usiku; na nikasababisha kwamba [ndugu zangu] wajifiche nje ya kuta. Na baada ya wao kujificha, mimi, Nefi, nilinyemelea hadi ndani ya mji na nikaelekea hadi nyumba ya Labani.”

Anaendelea kusema, “Niliongozwa na Roho, bila kujua mapema mambo ambayo nilipaswa kufanya.”4

Nimetiwa moyo kwa kujua kwamba Nefi aliongozwa na Roho dakika baada ya dakika usiku wote katika kazi ya Bwana.

Tunahitaji, na utahitaji, wenzi wa daima wa Roho Mtakatifu. Sasa, tunatamani uwepo wake, lakini tunajua kutokana na uzoefu kwamba si rahisi kuupata. Sote tunafikiria na kusema na kufanya vitu katika maisha yetu ya kila siku ambavyo vinaweza kumuudhi Roho.

Hilo linapotokea, kadiri litakavyotokea, tunaweza kuhisi kutokubaliwa na Bwana. Na tunaweza kujaribiwa kuhisi tuko peke yetu. Ni muhimu kukumbuka ahadi ya uhakika tunayoipokea kila wiki pale tunapotubu na kushiriki sakramenti: “ili daima Roho wake apate kuwa pamoja nao.”5

Kama umehisi msukumo wa Roho Mtakatifu leo, unaweza kuuchukua kama ushahidi mzuri kwamba Upatanisho unafanya kazi katika maisha yako.

Kama ambavyo Mzee Jeffrey R. Holland amesema: “Wakati wowote nyakati hizi za hisia yetu ya juu zinapokuja, hatupaswi kusalimu amri kwenye hofu kwamba Mungu ametuacha au kwamba Hasikii maombi yetu. Yeye anatusikia. Yeye anatuona. Yeye anatupenda sisi.”6

Hakikisho hilo limenisaidia. Wakati ninapohisi kuwa mbali na Bwana, wakati majibu ya maombi yangu yanapoonekana kuchelewa, nimejifunza kufuata ushauri wa Rais Nelson wa kupitia upya maisha yangu kwa ajili ya fursa za kutubu. Anatukumbusha, “Toba ya kila siku ndiyo njia ya kuelekea usafi, na usafi huleta nguvu.”7

Ukijikuta unapata shida katika kumhisi Roho Mtakatifu, unaweza kutafakari ikiwa kuna kitu chochote ambacho kwacho unahitaji kutubu na kupokea msamaha.8 Unaweza kuomba kwa imani ili kujua nini cha kufanya ili utakaswe na hivyo ukaribie zaidi kustahili wenzi wa daima wa Roho Mtakatifu.

Ikiwa unataka kupokea wenzi wa Roho Mtakatifu, lazima utake kumpokea kwa sababu sahihi. Kusudi lako lazima liwe kusudi la Bwana. Ikiwa nia zako ni za ubinafsi sana, utapata ugumu kupokea na kuhisi maongozi ya Roho.

Muhimu kwangu na kwako ni kutaka kile ambacho Mwokozi anakitaka. Nia zetu zinahitaji kuongozwa na upendo safi wa Kristo. Sala zetu zinatakiwa kuwa “Vyote nivitakavyo ni vile uvitakavyo. Mapenzi yako yatimizwe.”

Ninajaribu kukumbuka dhabihu ya Mwokozi na upendo Wake kwangu. Kisha, ninaposali kwa Baba wa Mbinguni ili kutoa shukrani, ninahisi upendo na hakikisho kwamba sala zangu zinasikilizwa na kwamba nitapokea kilicho bora zaidi kwangu na kwa wale niwapendao. Inaimarisha ushuhuda wangu.

Kati ya mambo yote ambayo Roho Mtakatifu anashuhudia, la thamani zaidi kwetu ni kwamba Yesu ndiye Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai. Mwokozi aliahidi: “Ajapo huyo Msaidizi, nitakayewapelekea kutoka kwa Baba, huyo Roho wa kweli, atokaye kwa Baba, yeye atanishuhudia.”9

Miaka kadhaa iliyopita, nilipokea simu kutoka kwa mama aliyefadhaika. Aliniambia kwamba binti yake alikuwa amehamia mbali na nyumbani. Alihisi kutokana na mawasiliano ya muda mfupi na binti yake kwamba kuna kitu hakikuwa sawa kabisa. Alinisihi nimsaidie.

Niligundua ni nani mwalimu wa nyumbani wa binti huyo. Unaweza kugundua kupitia jina hilo kwamba ilikuwa ni kitambo sana. Nilimpigia simu. Alikuwa kijana. Hata hivyo aliniambia kwamba yeye na mwenzi wake wote walikuwa wameamshwa usiku wakiwa na wasiwasi si tu kwa binti huyo bali kwa msukumo kwamba alikuwa karibu kufanya maamuzi ambayo yangeleta huzuni na taabu. Kwa mwongozo huu wa kiungu wa Roho, walikwenda kumwona.

Mwanzoni, hakutaka kuwaambia kuhusu hali yake. Kwa mwongozo wa kiungu, walimsihi atubu na achague njia ambayo Bwana alikuwa ameiweka kwa ajili yake. Kisha binti yule alitambua wakati huo, naamini kwa Roho, kwamba njia pekee ambayo wangeweza kujua kile walichokijua kuhusu maisha yake ilikuwa kutoka kwa Mungu. Mama alikabidhi mahangaiko yake ya upendo kwa Baba wa Mbinguni na Mwokozi. Roho Mtakatifu alikuwa ametumwa kwa wale walimu wa nyumbani kwa sababu walikuwa tayari kumtumikia Bwana. Walikuwa wamefuata ushauri na ahadi inayopatikana katika Mafundisho na Maagano:

“Na moyo wako pia uwe umejaa hisani kwa wanadamu wote, na kwa jamaa ya waaminio, na wema uyapambe mawazo yako bila kukoma; ndipo kujiamini kwako kutakuwa imara katika uwepo wa Mungu; na mafundisho ya ukuhani yatatonatona juu ya roho yako kama umande utokao mbinguni.

“Roho Mtakatifu atakuwa mwenzi wako daima, na fimbo yako ya kifalme fimbo isiyobadilika ya haki na ukweli; na utawala wako utakuwa utawala usio na mwisho, na usio wa njia ya kulazimisha utatiririka kwako milele na milele.”10

Ninashuhudia kwamba Bwana ametimiza ahadi Yake. Roho Mtakatifu anatumwa kwa waumini waaminifu wa agano wa Kanisa la Yesu Kristo. Sasa, uzoefu wako utakuwa wa kipekee, na Roho ataongoza kwa njia inayofaa zaidi kwa imani yako na uwezo wa kupokea ufunuo kwa ajili yako na kwa wale unaowapenda na kuwahudumia. Ninaomba kwa moyo wangu wote kwamba ujasiri wako uweze kukua.

Ninatoa ushahidi wangu kwamba Mungu Baba yu hai. Yeye anakupenda. Anasikia kila sala yako. Yesu Kristo aliomba kwa Baba ili amtume Roho Mtakatifu atuongoze, atufariji na ashuhudie ukweli kwetu. Mungu Baba na Mwanaye Mpendwa walimtokea Joseph Smith kwenye kijisitu cha miti. Nabii Joseph Smith alitafsiri Kitabu cha Mormoni kwa kipawa na uwezo wa Mungu.

Wajumbe wa mbinguni walirejesha funguo za ukuhani. Rais Russell M. Nelson ni nabii wa Mungu kwa ajili ya ulimwengu wote.

Kama shahidi wa Yesu Kristo, ninajua kwamba Yeye yu hai na analiongoza Kanisa Lake. Wewe na mimi tunayo fursa ya kuwa na Roho Mtakatifu kama mwenzi wetu daima na kuwa na kweli hizo zikithibitishwa pale tunapokumbuka na kumpenda Mwokozi, kutubu, na kuomba upendo Wake uwe mioyoni mwetu. Ninaomba kwamba tupate baraka hiyo na wenzi wa Roho Mtakatifu leo na kila siku ya maisha yetu. Ninawapenda. Katika jina takatifu la Yesu Kristo, amina.

Chapisha