Mkutano Mkuu
Upendo Unazungumzwa Hapa
Mkutano mkuu wa Oktoba 2023


Upendo Unazungumzwa Hapa

Na kila mmoja wetu tujifunze kuzungumza na kusikia upendo Wake hapa, katika mioyo yetu na nyumba zetu, na katika miito yetu ya injili, shughuli, utumishi na huduma.

Watoto wetu wa Msingi wanaimba “Upendo unazungumzwa hapa.”1

Niliwahi kumpa Dada Gong kibweta kidogo. Niliomba iandikwe nukta-nukta, nukta-nukta, nukta-nukta-dashi. Wale wanaofahamu msimbo wa Morse watatambua hizo ni herufi I, I, U. Lakini nilijumuisha msimbo wa pili. Katika Kichina cha Kimandarini, “ai” inamaanisha “upendo.” Hivyo, kukiwa na msimbo wa aina mbili, ujumbe ulikuwa “Nakupenda”. Susan kipenzi, “Ninakupenda.”

Tunazungumza upendo katika lugha nyingi. Naambiwa familia ya binadamu inazungumza lugha hai 7,168.2 Katika Kanisa tunazungumza lugha 575 za msingi, zenye lahaja nyingi. Sisi pia tunawasilisha dhamira, mabadiliko na hisia kupitia sanaa, muziki, ngoma, alama za kimantiki, ishara binafsi na kati ya mtu na mtu.3

Leo, hebu tuzungumze juu ya lugha tatu za upendo wa injili: lugha ya uchangamfu na heshima, lugha ya huduma na dhabihu na lugha ya kuwa sehemu ya agano.

Kwanza, lugha ya injili ya uchangamfu na heshima.

Kwa uchangamfu na heshima, Dada Gong anawauliza watoto na vijana, “Mnajuaje kwamba wazazi wenu na familia zinawapenda?”

Nchini Guatemala, watoto husema, “Wazazi wangu hufanya kazi kwa bidii ili kulisha familia yetu.” Huko Amerika Kaskazini, watoto husema, “Wazazi wangu hunisomea hadithi na kunilaza kitandani usiku.” Katika Nchi Takatifu, watoto husema, “Wazazi wangu huniweka salama.” Nchini Ghana, Afrika Magharibi, watoto husema, “Wazazi wangu hunisaidia kutimiza malengo yangu ya Watoto na Vijana.”

Mtoto mmoja alisema, “Ingawa amechoka sana baada ya kufanya kazi kutwa nzima, mama yangu huja nje ili kucheza nami.” Mama yake alilia aliposikia kwamba dhabihu zake za kila siku ni za muhimu. Binti mdogo alisema, “Ingawa mimi na mama yangu hatukubaliani nyakati fulani, ninamwamini mama yangu.” Mama yake naye alilia.

Wakati mwingine tunahitaji kujua upendo unaozungumzwa hapa unasikika na kuthaminiwa hapa.

Kwa uchangamfu na heshima, sakramenti na mikutano yetu mingine inafokasi kwa Yesu Kristo. Tunazungumza kwa heshima juu ya Upatanisho wa Yesu Kristo, wa binafsi na halisi, sio upatanisho katika dhana tu. Tunaliita Kanisa la Yesu Kristo lililorejeshwa katika jina Lake, Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho. Tunatumia lugha ya staha katika maombi tunapozungumza na Baba wa Mbinguni na heshima ya upendo tunapozungumza sisi kwa sisi. Tunapomtambua Yesu Kristo kama kiini cha maagano ya hekaluni, tunamaanisha kwa uchache “kwenda hekaluni” na zaidi tunamaanisha “kwenda kwa Yesu Kristo katika nyumba ya Bwana.” Kila agano linanong’ona, “Upendo unazungumzwa hapa.”

Waumini wapya wanasema msamiati wa Kanisa mara nyingi unahitaji kufafanuliwa. Tunacheka juu ya wazo la kwamba neno “stake house” (yaani kigingi) lingeweza kumaanisha chakula cha jioni kizuri cha nyama ya ng’ombe; “ward building” (yaani kata) linaweza kumaanisha hospitali; “opening exercises” kungetualika kwenye kushika kichwa, mabega, magoti na vidole kwenye sehemu ya kuegesha magari kanisani. Lakini, tafadhali, tuwe wenye kuelewa na wakarimu tunapojifunza lugha mpya za upendo pamoja. Akiwa bado mgeni kanisani, mwongofu mmoja aliambiwa kuwa sketi zake ni fupi sana. Badala ya kuudhika, alijibu, kwa kweli, “Moyo wangu umeongoka; tafadhali kuweni wavumilivu wakati sketi zangu zikipambana na hilo.”4

Maneno tunayotumia yanaweza kutuleta karibu au kututenganisha na Wakristo na marafiki wengine. Wakati mwingine tunazungumza kuhusu kazi ya ummisionari, kazi ya hekaluni, kazi ya kibinadamu na ustawi katika njia ambazo zinaweza kuwasababisha wengine kuamini kuwa tunafanya kazi hizi peke yetu. Hebu daima tuzungumze kwa upendo na unyenyekevu wa shukrani kwa ajili ya kazi na utukufu na faida ya Mungu, rehema na neema ya Yesu Kristo na dhabihu Yake ya kulipia dhambi.5

Pili, lugha ya injili ya huduma na dhabihu.

Tunapokusanyika tena kanisani kila wiki kuheshimu na kufurahia katika siku ya Sabato, tunaweza kueleza ahadi yetu ya agano la sakramenti kwa Yesu Kristo na kwa kila mmoja wetu kupitia miito yetu katika Kanisa, ushirika, ujamaa na huduma.

Ninapowauliza viongozi wa Kanisa wenyeji kitu gani kinachowasumbua, wote, akina kaka na akina dada husema, “Baadhi ya waumini wetu hawakubali miito ya Kanisa.” Miito ya kumtumikia Bwana na kila mmoja katika Kanisa Lake hutoa fursa ya kuongezeka katika huruma, uwezo na unyenyekevu. Tunapoitwa kwenye wito, tunaweza kupokea mwongozo wa kiungu wa Bwana ili kuwainua na kuwaimarisha wengine na kujiimarisha sisi wenyewe. Bila shaka, mabadiliko ya hali na majira ya maisha yetu vinaweza kuathiri uwezo wetu wa kuhudumu, lakini kamwe si nia yetu. Pamoja na Mfalme Benjamini, tunasema, “Kama ningekuwa nacho ningetoa”6 na kutoa yote tunayoweza kutoa.

Viongozi wa kigingi na kata, tufanye sehemu yetu. Tunapowaita (na kuwapumzisha) akina kaka na akina dada kuhudumu katika Kanisa la Bwana, hebu tafadhali tufanye hivyo kwa heshima na kwa mwongozo wa kiungu. Msaidie kila mmoja ahisi anathaminiwa na kwamba anaweza kufanikiwa. Tafadhali shaurianeni na muwasikilize akina dada viongozi. Na tukumbuke, kama Rais J. Reuben Clark alivyofundisha, katika Kanisa la Bwana tunahudumu mahali tulipoitwa, “mahali ambapo mtu hatafutwi kuitwa wala kukataa kuitwa.”7

Mimi na Dada Gong tulipooana, Mzee David B. Haight alishauri: “Daima shikilia wito Kanisani. Hasa wakati maisha yana shughuli nyingi,” alisema, “unahitaji kuhisi upendo wa Bwana kwa wale unaowahudumia na kwako wewe unapohudumia.” Ninaahidi kwamba upendo unazungumzwa hapa, pale na kila mahali tunapojibu ndiyo kwa viongozi wa Kanisa kumtumikia Bwana katika Kanisa Lake kwa Roho Wake na maagano yetu.

Kanisa la Bwana lililorejeshwa linaweza kuwa kitotoleo kwa jumuiya ya Sayuni. Tunapoabudu, kutumikia, kufurahia na kujifunza upendo Wake pamoja, tunamweka kila mmoja wetu imara katika injili Yake. Tunaweza tusikubaliane kisiasa au katika masuala ya kijamii lakini tukapata maelewano tunapoimba pamoja katika kwaya ya kata. Tunakuza muunganiko na kupambana na unyanyapaa pale tunapotumikia kila mara kwa mioyo yetu katika nyumba za kila mmoja wetu.

Wakati wa matembezi kwa waumini pamoja na marais wa vigingi, ninahisi upendo wa kina kwa waumini katika kila hali. Tulipokuwa tukiendesha gari kupita nyumba za waumini katika kigingi chake, rais mmoja wa kigingi alibainisha kwamba iwe tunaishi katika nyumba yenye bwawa la kuogelea au nyumba yenye sakafu ya udongo, huduma ya Kanisa ni fursa ambayo mara nyingi inajumuisha dhabihu. Na bado, alisema kwa hekima, tunapohudumu na kujitolea katika injili pamoja, tunapata makosa machache na amani kuu. Tunapomruhusu Yeye, Yesu Kristo hutusaidia kuzungumza upendo Wake hapa.

Majira haya ya kiangazi, familia yetu ilikutana na waumini wazuri wa Kanisa na marafiki huko Loughborough na Oxford, Uingereza. Mikusanyiko hii ya maana ilinikumbusha jinsi gani shughuli za kijamii na huduma zinavyoweza kujenga muunganiko mpya na wa kudumu wa injili. Kwa muda fulani nimehisi kwamba, katika sehemu nyingi katika Kanisa, shughuli chache zaidi za kata, bila shaka zilizopangwa na kutekelezwa kwa madhumuni ya injili, zinaweza kutuunganisha pamoja na kwa umoja mkubwa zaidi.

Mwenyekiti mmoja wa kamati na shughuli wa kata analea watu binafsi na jumuiya ya Watakatifu. Shughuli zao zilizopangwa vizuri husaidia kila mtu kuhisi kuthaminiwa, na kualikwa kufanya jukumu linalohitajika. Shughuli kama hizo huunganisha rika na asili, hutengeneza kumbukumbu za kudumu, na zinaweza kufanywa kwa gharama ndogo au bure. Shughuli za kufurahisha za injili pia hualika majirani na marafiki.

Ujamaa na huduma mara nyingi huenda pamoja. Vijana wakubwa wanajua ikiwa kweli ungependa kumjua mtu, basi pakeni rangi mkiwa ngazini bega kwa bega katika mradi wa huduma.

Picha
Vijana watu wazima wakipaka rangi kwenye shughuli ya huduma.

Bila shaka, hakuna mtu binafsi na hakuna familia iliyo kamili. Sote tunahitaji usaidizi ili kuzungumza vyema upendo hapa. “Upendo kamili hutupa hofu nje.”8 Imani, huduma na dhabihu hutuvuta zaidi ya sisi wenyewe karibu na Mwokozi wetu. Kadiri huduma na dhabihu yetu inavyokuwa ya huruma zaidi, aminifu na isiyo na ubinafsi na dhabihu iko ndani Yake, ndivyo tunavyoweza kuanza kuelewa huruma ya kulipia dhambi na neema ya Yesu Kristo kwa ajili yetu.

Na hiyo inatuleta kwenye lugha ya injili ya kuwa sehemu ya agano.

Tunaishi katika ulimwengu wa kujiangalia wenyewe. Mambo mengi ni “Najichagua mimi mwenyewe.” Ni kana kwamba tunaamini tunajua vyema zaidi masilahi yetu binafsi na jinsi ya kuyatatua.

Lakini hatimaye si kweli. Yesu Kristo anawakilisha ukweli huu wenye nguvu usio na mwisho:

“Kwa kuwa mtu atakaye kuiokoa nafsi yake, ataipoteza: na mtu atakayepoteza nafsi yake kwa ajili yangu, ataipata.

“Kwani binadamu ananufaika nini, kama atapata ulimwengu wote, na kupoteza nafsi yake?”9

Yesu Kristo anatoa njia iliyo bora zaidi—mahusiano yaliyojengwa juu ya agano la kiungu, yenye nguvu zaidi kuliko kamba za mauti. Agano la kuwa pamoja na Mungu na kila mmoja wetu linaweza kutuponya na kutakasa mahusiano yetu ya thamani sana. Yeye, anatujua vizuri zaidi na anatupenda kuliko tunavyojijua au kujipenda sisi wenyewe. Kwa ukweli, tunapofanya agano la vyote tulivyo, tunaweza kuwa zaidi ya tulivyo. Nguvu na hekima ya Mungu vinaweza kutubariki kwa kila zawadi nzuri, kwa wakati na njia Yake.

Akili ya uwezo bunifu (AI) imepiga hatua kubwa sana katika tafsiri ya lugha. Zama nyingi zimepita ambapo kompyuta ingeweza kutafsiri usemi usemao “Roho i radhi, lakini mwili ni dhaifu” kuwa “divai ni nzuri, lakini nyama imeharibika.” Cha kushangaza, kurudia mifano mingi ya lugha huifundisha kompyuta lugha vyema zaidi kuliko kuifundisha kompyuta kanuni za sarufi.

Vivyo hivyo, uzoefu wetu wa moja kwa moja, unaojirudia unaweza kuwa njia yetu bora ya kiroho ya kujifunza lugha za injili za upendo na heshima, huduma na dhabihu na kuwa sehemu ya agano.

Kwa hiyo, ni wapi na jinsi gani Yesu Kristo anazungumza nawe kwa upendo?

Wapi na jinsi gani unasikia upendo Wake ukizungumzwa hapa?

Na kila mmoja wetu tujifunze kuzungumza na kusikia upendo Wake hapa, katika mioyo yetu na nyumba zetu, na katika miito yetu ya injili, shughuli, kuhudumu na huduma.

Katika mpango wa Mungu, kila mmoja wetu atapita kutoka katika maisha haya hadi maisha yajayo. Tunapokutana na Bwana, ninawaza kufikiria Yeye akisema, kwa maneno ya mafundisho na ahadi, “Upendo wangu unazungumzwa hapa.” Katika jina takatifu la Yesu Kristo, amina.

Chapisha